Kizaazaa Tarime (Tanzania Daima)
na Joseph Senga, Tarime
MAZISHI ya aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, yameingia dosari baada ya kuahirishwa kutokana na shinikizo la wananchi kutaka uchunguzi mwingine ufanyike kubaini chanzo cha kifo chake.
Familia ya Wangwe ilikubali matakwa ya waombolezaji waliotaka kufanyika upya kwa uchunguzi huo kwa madai ya kutokuwa na imani na uchunguzi wa awali.
Hali hiyo ilimlazimu kaka wa marehemu Profesa Samwel Wangwe, kutoa taarifa rasmi ya familia kukubali kuahirisha mazishi hayo hadi leo.
Wangwe ambaye alikuwa akisikika kwa shida kutokana na kelele za vurugu za waombelezaji hao, alisema wameamua kuahirisha ili kupisha uchunguzi wa kifamilia ufanyike leo.
"Naomba tusikilizane, kwa niaba ya familia, mazishi yameahirishwa leo mpaka hapo uchunguzi wa mwili wa marehemu kipenzi chenu utakapofanyika kesho (leo), ili kuondoa haya manung'uniko yaliyopo," alisema.
Alisema wamefikia uamuzi huo ili kuepuka baadaye kuja kufukua mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Alisema sheria za nchi hii zinatoa ruhusu kwa familia kufanya uchunguzi kwa mara ya pili kama haijaridhishwa na matokeo, na uchunguzi huo utafanyika chini ya mtaalamu wa kujitegemea pamoja na shuhuda wa serikali.
‘Uchunguzi huu ni kwa ajili ya kujiridhisha lakini pia atakuwepo shuhuda wa serikali, na baada ya hapo ndipo tutafanya taratibu za mazishi," alisema Wangwe.
Naye Waziri wa Kilimo na Chakula Stephen Wasira, alisema serikali haina kipingamizi juu ya uchunguzi wa kifo cha Wangwe.
Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema tangu awali aliweka wazi kuwa kuna haja ya kufanyika uchunguzi huru juu ya kifo cha Wangwe.
Alisema kifo hicho kimezua maswali mengi miongoni mwa jamii, hivyo njia pekee ni kufanyika kwa uchunguzi utakaoweza kuwaridhisha wana familia na Watanzania kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, John Mnyika, alisema CHADEMA inaungana na familia ya marehemu kutaka kufanyika kwa uchunguzi kwa mara ya pili.
Alisema utata wa kifo cha Wangwe umewafanya CHADEMA kumwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, kutaka kufanyika kwa uchunguzi.
Pamoja na kaka wa marehemu huyo kuueleza umma uliohudhuria mazishi hayo, bado alikuwa na wakati mgumu, kwani wananchi hawakutaka kumsikiliza zaidi ya kupaza sauti kutaka uchunguzi huo ufanyike upya na matokeo yatangazwe hadharani kabla ya mazishi.
Wakati hatua hiyo inafikiwa, maandalizi ya mazishi hayo, ikiwa ni pamoja na kaburi na mfuniko wa zege uliokuwa utumike kufunika kaburi hilo, vilikuwa tayari, na kusubiri kumalizika kwa ibada.
Hata hivyo hasira za waombolezaji hao, zilibadilika na kuwa furaha pale alipowasili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Mbowe aliwasili nyumbani kwa marehemu, majira ya saa 7:30 mchana, akitokea Dar es Salaam kupitia Musoma kwa ndege ya kukodi.
Kana kwamba wananchi hao walikuwa wamemsubiri afike ili waanze kueleza dukuduku lao, walimpokea kwa shangwe na nderemo huku wengine wakisema ndiye shujaa pekee aliyebaki.
"Umebaki wewe tu Mbowe, kamanda wetu, wametuondolea mbunge wetu, tunataka watuambie, nani kamuua, vinginevyo watuue na sisi," walisikika baadhi ya vijana.
Aidha, katika kile kilichoonekana kumlinda Mbowe, vijana hao walimsindikiza hadi katika meza kuu ambako alijumuika na viongozi wengine.
Baada ya Mbowe kuketi katika meza kuu, na hatimaye mwongozaji wa shughuli za mazishi alipoanza kutaka kueleza ratiba ya mazishi, vijana hao waliisogelea meza kuu huku wakiangua vilio na miluzi, wakitaka waelezwe mbunge wao yuko wapi na mambo mengine.
Sakata hilo halikuishia hapo, vijana hao walizidi kuongezeka sehemu ilipokuwa meza kuu, wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wakiwa na hamaki ya kutomsikiliza kiongozi yeyote, hata wale waliowafahamu kutoka kijijini hapo.
Hali ilipozidi kuwa mbaya, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliamua kupanda juu ya meza na kuanza kuwaomba vijana hao watulie ili shughuli ianze.
Kusimama huko kwa Zitto kulionekana kuwa suluhisho la kadhia hiyo, kwani walimshangilia na kunyamaza.
Zitto alitoa ombi kwa vijana hao kumsikiliza msemaji wa familia, Profesa Wange kuhusu utaratibu wa mazishi.
Hata hivyo Profesa Wangwe hakufika mbali, kelele zilianza tena kwa kumtaka asizungumze chochote mpaka hapo watakapojua chanzo cha kifo cha kipenzi chao, Chacha Wangwe.
Baada ya kaka huyo wa marehemu kushindwa kuendelea na utaratibu huo, ilikuja ajenda ya pili, nayo ni kufanyika kwa uchunguzi.
Ajenda hiyo ilitolewa ufafanuzi na Zitto Kabwe kuwa familia imeridhia kufanyika kwa uchunguzi tena wa kifo cha marehemu Chacha Wangwe na ndipo kelele za mayowe ya kukubaliana naye zilipolipuka.
"Uchunguzi wa kina utafanyika, wananchi msiwe na hofu hata kidogo, utahusisha pande zote zinazohusika, na endepo itabainika kuwa kifo chake kilikuwa na mkono wa mtu, tutahakikisha haki inatendeka na taarifa zitatolewa kwa uwazi," alifafanua Zitto.
Ufafanuzi huo wa Zitto, uliwafanya waombolezaji hao kutulia na kumwezesha Wangwe kuendelea na hotuba yake.
Kwa mara nyingine, Wangwe alisema familia imekubali ombi la kufanyika upya kwa uchunguzi huo leo, na taarifa yake kutangazwa hadharani kabla ya mazishi.
Baada ya maelezo ya Profesa Wangwe, ambayo hata hivyo hayakusikika vizuri kutokana na kelele za watu, ndipo Zitto Kabwe alipolazimika kurudia tena kupanda mezani, kujaribu kuwatuliza.
Hali ilizidi kuwa tete, kwani watu walipoanza kutawanyika kukazuka vurugu za kurushiana mawe.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya watu kutafuta njia ili kunusuru maisha yao huku wangine waliotoka salama wakishukuru kwa kunusurika katika vurugu hizo.
Waombolezaji hao, walianza kurushiana mawe wenyewe kwa wenyewe, hali iliyohatarisha maisha ya baadhi yao.
Baadhi ya watu waliozungumza na Tanzania Daima, walisema kuna uwezekano mkubwa wa watu wachache kujitokeza katika mazishi hayo leo, kwa kuhofia vurugu.
Hadi watu walipotawanyika katika eneo hilo, chakula na vinywaji vilikuwa tayari, lakini hakuna mtu aliyevitumia.
Baadhi ya viongozi, hususan wale wanaotoka Mkoa wa Mara, hawakwenda mbali, akiwamo Wasira, walirejea katika eneo la tukio na kufanyiwa mahojiano na vyombo vya habari, ambapo waliezea kusikitishwa kwao na tukio hilo.