Masheikh 25 waanza mchakato wa Kadhi
Na Ummy Muya
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limetangaza kamati ya masheikh 25 watakaofanya kazi na serikali katika mchakato wa kuunda Mahakama ya Kadhi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, kamati hiyo iliundwa baada ya kikao cha pamoja kati ya masheikh na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kilichofanyika hivi karibuni.
Sheikh Lolila alisema kuwa waziri mkuu alipendekeza mchakato wa majadiliano unaohusisha pande mbili za masheikh na serikali uanze na kwamba kamati hiyo itakuwa chini ya Mufti Simba.
Kamati hii inaundwa na jumla ya masheikh maarufu 25 na tayari imeshaanza kazi na ndani yake kuna wanasheria wa Kiislamu, mawakili wa kujitegemea na wataalamu wa fani za jamii, alisema Lolila.
Ratiba ya vikao vya kamati hiyo vitatangazwa mara tu wanakamati watakapokutana na serikali na kuweka mbinu za utekelezaji, alisema.
Masheikh wanaounda kamati hiyo ni Mufti Issa bin Shaaban Simba (mwenyekiti wa kamati), Ustadh Suleiman Lolila (kaimu katibu mkuu -Bakwata), Sheikh Ismail Habib, mjumbe wa baraza la Ulamaa, Sheikh Taufiq Malilo, mjumbe wa baraza la Ulamaa, na mjumbe wa baraza la Ulamaa Sheikh Fereji Hassain.
Wengine kwa mujibu wa Sheikh Lolila ni Sheikh Alhad Mussa, ambaye ni sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Suleiman Kilemile (Islamic Call Society), Sheikh Twaha Bane (Al-Haramain), Ustadh Abdallah Matumla na Sheikh Abdallah Nyasi wa Bakwata.
Wengine ni mwakilishi kutoka Bohora, mwakilishi kutoka Shia, mwakilishi kutoka Sunni, mwakilishi kutoka Masjid Ibaadhi Istiqama Sheikh Mussa Kundecha, Sheikh Juma Pori (Answar Sunna) na Sheikh Abdallah Bawazir (Masjid Kiblaten).
Pia wapo Sheikh Twalib Ahmed (Masjid Maamur), Ustadh Yahya Njama (mwanasheria), Ustadh Issa Maige (mwanasheria), Sheikh Muharam Juma Dogga (Al Haramain), Sheikh Hamid Masoud Jongo (Masjid Manyema), Sheikh Abdallah Ndauga (International Islamic Relief Organisation), Sheikh Abubakar Zubeir (Salafiya) na Ustadh Mohamed Said (Bakwata).
Hivi karibuni baadhi ya Waislamu waliilalamikia serikali baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kutangaza kuwa serikali imeamua kutounda Mahakama ya Kadhi na badala yake itajumuisha sheria za Kadhi kwenye mahakama za kawaida.
Akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2009/10, Chikawe alisema kuwa uamuzi huo wa serikali unatokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tume ya wataalamu waliochambua mapendekezo ya utafiti uliofanywa na Kamati ya Kurekebisha Sheria nchini.
Taasisi kadhaa za Kiislamu zilipinga uamuzi huo na kutishia kufanya maandamano na hata kuinyima kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, madhehebu mengine ya Kikristo yamekuwa yakielezea kuwa hayaoni ubaya wowote kwa Waislamu ila wanachokikataa ni serikali kutumia sehemu za walipakodi nchini kwa ajili ya kuzigharamia.