KIKWETE KWENDA UFARANSA NA ITALIA;
Mwandishi WetUu,
HabariLeo; Monday,October 15, 2007 @00:02
RAIS Jakaya Kikwete anaondoka nchini leo kwenda Italia kwa ziara ya kikazi ya siku nane nchini humo na Ufaransa ambako pia ataonana na viongozi mbalimbali akiwamo Papa Benedicto XVI.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema akiwa Italia ambako anakwenda kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Romano Prodi, kesho atashiriki na kuhutubia katika sherehe za Siku ya Chakula Duniani ambazo zimeandaliwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO).
Katika sherehe hizo ambazo hufanyika kila Oktoba 16, mada kuu itakuwa Haki ya Chakula ikisisitiza haki ya msingi ya mwanadamu kupata chakula, haki ambayo Shirika hilo linasema haizingatiwi ingawa kuna zaidi ya watu milioni 850 duniani kote ambao wana tatizo kubwa la ukosefu wa chakula.
Baada ya kuhudhuria sherehe hizo, Rais atakutana na kuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na viongozi wengine.
Keshokutwa atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Prodi wakati Alhamisi atashiriki mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.
Mkutano huo utafanyika Milan ukiwa na lengo la kuwashawishi wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia kufanya biashara na wenzao wa Tanzania na kuwekeza nchini.
Ijumaa Rais Kikwete atakwenda Vatican ambako atakutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedicto XVI .
Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais kukutana na Baba Mtakatifu tangu ashike madaraka ya urais wa Tanzania.
Akiwa Italia, Rais atakuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kimataifa unaowakutanisha viongozi wakuu wa madhehebu mbalimbali ya dini duniani (Interfaith Conference). Mkutano huo umeandaliwa na Jumuiya ya Sant'Egidio na utafanyika Napoli.
Rais amealikwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo kutokana na Tanzania kuwa nchi ya mfano duniani ambako watu wake wanaishi kwa maelewano, ushirikiano na amani bila ya kujali tofauti zao za dini na imani.
Baada ya kuhutubia mkutano huo, Rais atakwenda Ufaransa ambako atahudhuria Mkutano wa 34 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mada kuu katika mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili itakuwa ni Elimu na Maendeleo.
Akiwa Paris, Rais pia anatarajiwa kukutana na Rais Nicolas Sarkozy.
Rais na ujumbe wake wanatarajiwa kurejea nchini Oktoba 24.