article yenyewe ni hii !
Mzimu wa ufisadi waingia upinzani
Habari Zinazoshabihiana
*Mbowe atakiwa akamatwe na Polisi
*Ni kwa deni la sh. bilioni 1.2 NSSF
Na Mwandishi Wetu
MZIMU wa ufisadi unaoendelea kutikisa taasisi na sekta mbalimbali nchini, sasa umeigeukia kambi ya upinzani na kuzua mtafaruku huku baadhi ya viongozi wakitofautiana na kushinikiza wenzao wachukuliwe hatua za kisheria.
Sakata hilo limekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila wiki, kuandika habari ikimhusisha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe na kashfa ya kukopa mamilioni ya fedha katika Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kwamba hajalipa.
Gazeti hilo lilidai, kwamba Bw. Mbowe alikopa fedha hizo mwaka 1990 kwa nia ya kufanya upanuzi wa hoteli yake ya Mbowe, maarufu kama Billcanas, Dar es Salaam.
Likaeleza kuwa kumbukumbu zilizopo zinaonesha kuwa alichukua deni la mkopo huo kwa kutiliana saini kati yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NPF) ambalo baadaye lilibadilishwa jina na kuwa NSSF. Mkopo huo sasa umekua na kufikia zaidi ya sh. milioni 1,200 kutokana na riba inayotokana na deni hilo.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Bw. Paul Kyara, alidai kusikitishwa na kitendo cha kutokamatwa hadi sasa kwa Bw. Mbowe kwa kile alichodai kutolipa fedha hizo, kwani notisi ilishatolewa tangu Desemba 5 mwaka juzi, ikielekeza akamatwe kabla ya Desemba 12, 2006.
Bw. Kyara amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kutoa maelezo kwa nini amri ya Mahakama Kuu ya kukamatwa, Bw. Mbowe haijatekelezwa na kuitaka NSSF iwajibike kwa kile alichodai ni kushindwa kusimamia vizuri fedha za wafanyakazi na wastaafu.
Katika hatua hiyo inayoonesha mvutano miongoni mwa viongozi wa vyama vya upinzani, Bw. Kyara pia alimtaka Bw. Mbowe kuvunja ukimya na kutoa tamko la kwa nini hajisalimishi Polisi na hajalipa deni hilo na kudai kuwa ufisadi wa viongozi wa vyama vya upinzani, unavipunguzia uwezo wa kukemea maovu ya Serikali na chama tawala.
"Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kinapenda kueleza masikitiko yake ya taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari jana (juzi) za kupotea kwa sh. milioni 1,200 za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) zinazotokana na Bw. Freeman Mbowe kukataa kulipa deni alilokopa NSSF tangu wa mwaka 1990," alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza:
"Hapa nchini kumekuwa na upotevu mwingi wa fedha na mwingine unapita bila kuripotiwa na vyombo vya habari, katika hili chama cha SAU kinalitaka Jeshi la Polisi liwaeleze wananchi ni kwa nini linashindwa kuwakamata wahusika licha ya kuwapo notisi ya Mahakama ya kufanya hivyo...tuambiwe kama katika Taifa hili wapo watu wako juu ya sheria hata wakifanya makosa."
Alipotakiwa kujibu swali kwamba hatua yake ya kumshambulia Bw. Mbowe imelenga kudhoofisha nguvu ya kambi ya upinzani, Bw. Kyara alikanusha na kueleza kuwa upinzani si kichaka cha kuficha mafisadi na Bw. Mbowe amekuwa mstari wa mbele katika vita ya kupinga mafisadi, hivyo anapaswa kuwa safi.
Hatua hii inaonekana kugeuza wimbi la tuhuma za ufisadi kutoka kwa viongozi wa Serikali na kuhamia kwa kambi ya upinzani ambayo imekuwa siku zote mstari wa mbele kupasua mabomu yaliyohusu mikataba ya Buzwagi, Richmond na ubadhirifu wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika kambi ya upinzani, CHADEMA ndiyo imekuwa na wabunge waliopigia kelele sana masuala haya akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe na Mbunge wa Karatu, Bw. Willbroad Slaa.