Ni kweli sheria haitambui uchawi?
Na Majaliwa Mohamed.
Posted Date::12/13/2007
Katika jamii nyingi duniani hasa za kiafrika, imani za kichawi zimejikita na kuota mizizi kiasi cha baadhi ya jamii au wanajamii fulani kutukuza imani hizo wakiamini ni sehemu ya mila zao.
Na pia katika jamii hizo zenye imani ya uchawi, imedhihirika ili uwe maarufu na mwenye kuheshimiwa katika jamii hiyo husika, uwezo wako katika kumiliki na pia kutumia nguvu zinazoaminika ni za kichawi huwa ni kigezo kikuu na muhimu.
Kwa maneno mengine ni kuwa heshima na ukubwa wa mtu hupimwa kwa kuangalia uwezo wake wa kichawi alionao.
Zaidi katika jamii za aina hii, watu wake huamini kuwa kwa mafanikio katika maisha, hutokana na jitihada katika matumizi ya nguvu za kichawi, hii hujumuisha kuhusisha kuhusisha imani hizo katika nyanja mbalimbali za maisha kama vile biashara, elimu, kazi, michezo na hata uongozi (siasa).
Lakini ni ukweli usiofichika kuwa kuna baadhi ya watu ambao hutumia nguvu za kichawi kudhuru wenzao katika miili yao au hata katika mali zao.
Kimsingi katika sheria, kumdhuru mtu kwa makusudi kwa namna yoyote ile ni kosa chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Sasa je, utambuzi huu wa sheria juu ya makosa yanayohusu kumdhuru mtu katika mwili wake, hufika hata kwa makosa kama hayo yanayoaminika kutendeka kwa njia ya kichawi?
Swali hili litatusaidia kutambua kama mashitaka au malalamiko yanayohusiana na uchawi yanapokelewa au kutambulika na sheria.
Ni siku za hivi karibuni tu katika maeneo ya kanda ya ziwa , hasa katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza, kulizuka mfululizo wa matukio ya mauaji yanayofanywa zidi ya vikongwe kwa imani kuwa vikongwe hao walikuwa na nguvu za kichawi wanazozitumia kuwadhuru watu wengine.
Baada ya uchunguzi rasharasha, sababu zilizoelezwa kuchochea mauaji hayo ni ukweli kuwa hata ukiamua kumchukulia hatua za kisheria mtu unayeamini kuwa ndiye mchawi wako, haitosaidia kitu kutokana na ukweli kuwa serikali au sheria haitambui uchawi.
Hivyo wauaji waliamini hata wakiwapelekwa katika vyombo vya dola, bibi vizee hao ambao ndio hasa waathirika katika mauaji hayo, wataachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi kuthibitisha malalamiko yao ya uchawi.
Kwa mujibu wa sheria ya uchawi ya mwaka 1920 toleo la 18, sheria imejidhihirisha kutambua baadhi ya makosa yanayotokana na imani za kichawi, hii ni pamoja na mtu kutengeneza au kumiliki vifaa vinavyoaminika kuwa ni zana za kichawi.
Kwa mashitaka kama haya huwa ni utata katika kuyaendesha hasa kwa upande wa mashitaka ambao ndio wenye jukumu la kuthibitisha madai hayo zidi ya mshitakiwa.
Hii inatokana na ukweli kuwa ni vigumu kuthibitisha kuwa vitu au vifaa alivyokutwa navyo mshitakiwa ni kweli vinanguvu inayoaminiwa kuwa ni ya kichawi.
Katika hili pia kuna wanaharakati wengine hujenga hoja kuwa iweje sheria imuadhibu mtu kwa kosa la kudhania tu.
Ukweli ni kuwa ni vigumu kama siyo haiwezekani kabisa kuthibitisha uwezo wa nguvu za kichawi wa vitu husika mbele ya mahakama.
Lakini kwa upande mwingine vifaa ambavyo hudhaniwa ni vya kichawi hujieleza vyenyewe kutokana na asili yake na hasa baada ya mshitakiwa kushindwa kujitetea kwa kueleza matumizi ya vifaa hiyo na jinsi alivyovipata.
Hii inatokana na ukweli kuwa mara kadhaa imetokea watu kukamatwa na viungo vya binaadamu kama vile sehemu za siri za watoto wadogo na vingine vinavyofanana na hivyo.
Na hili pia si rahisi kuthibitisha kuwa viungo hivyo vina nguvu za kichawi. Endapo upande wa mashitaka ukiweza kuthibitisha kuwa vifaa hivyo vina nguvu au inaaminika kuwa na nguvu za kichawi, mtuhumiwa atashitakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria hii ya uchawi, lakini pia mshitakiwa anaweza kufunguliwa kosa lingine kwa kukutwa na viungo vya binaadamu chini ya sheria ya makosa ya jinai.
Kosa jingine na ambalo ni maarufu sana linalotambuliwa na sheria ya uchawi ni lile la kutishia watu kuwaumiza au kuwadhuru kwa kutumia nguvu za kichawi.
Kutishia katika sheria ni kosa hata pasipo kuhusisha imani ya kichawi. Japo ni agharabu kutokea, lakini imetokea mara kadhaa baadhi ya wanafamilia wa familia moja au mtaani kutishiana kulogana kutokana na uhasama uliopo kati yao.
Vitisho vya kichawi ni kosa kwa mujibu wa sheria hii ya uchawi, kosa hili linaweza kufanywa aidha kwa maneno ya mdomo au maandishi. Vitisho peke yake vinatosha kuthibitisha kosa hilo.
Vitisho hivi vinaweza kuwa vya kuondoa maisha ya mtu, yaani kifo, kumbebesha ugonjwa au kumdhuru vinginevyo kwa nguvu za kichawi, na adhabu ambayo imewekwa na sheria hii juu ya kosa hili ni kifungo kisichopungua miaka saba, lakini pia mahakama ina nguvu ya kisheria kubadilisha adhabu hii pindi ikiona inafaa kufanya hivyo.