SoC03 Ili Bunge liwe na nguvu ya kuiwajibisha Serikali, Spika wa Bunge asiwe mwanachama ama mshirika wa chama cha siasa na apatikane kwa kura za Wananchi

Stories of Change - 2023 Competition

TheForgotten Genious

JF-Expert Member
Jan 18, 2014
995
1,508
UTANGULIZI.
Bunge ni miongoni mwa vyombo vinavyounda dola,Bunge ndicho chombo kinacho wakilisha wananchi moja kwa moja kwa kuwa kina wabunge ambao wanapatikana kutokana na kura za wananchi.

Bunge ndilo linalotunga sheria kwa niaba ya wananchi,Bunge ndilo linalopitisha maazimio yote ambayo serikali inadhamiria kuyafanya kwa manufaa ya nchi,bunge ndio sauti ya wananchi,serikali inapaswa kufuata maamuzi ya bunge na sio bunge kufuata maamuzi ya serikali kwa kuwa serikali imeundwa na chama cha siasa ambacho kina kanuni na maslahi yake hivyo ni rahisi kwa serikali kusimamia maslahi ya chama kuliko maslahi ya wananchi,kwa mantiki hiyo bunge linapaswa liwe na nguvu kuizidi serikali.

Katiba yetu ibara ya 84 imeeleza wazi namna ambavyo spika wa bunge anapatikana,ambapo mbunge ama mtu yeyote mwenye sifa za kuwa mbunge anaruhusiwa kuomba wazifa wa kuwa spika wa bunge,na kwa mujibu wa katiba yetu hiyo hiyo ibara ya 67 (b),inasema ili mtu ateuliwe kuwa mgombea wa ubunge basi ni sharti awe ni mwanachama wa chama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa,kanuni hii inafaida chache endapo Idadi ya wabunge wa upinzani inakuwa ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wabunge wa chama tawala kitu ambacho ni nadra sana kutokea katika nchi yetu,ambapo ikitokea hivyo itakuwa ni mtihani mgumu kwa serikali kulitawala na kuliamulia bunge na kulifanya dhaifu.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mabunge dhaifu sana Barani Afrika na Afrika mashariki kwa ujumla,sababu kubwa inayofanya bunge liwe dhaifu ni kwamba limekosa meno yakuing’ata serikali na kuisismamia kwa kuwa spika wa bunge,Naibu spika na mwenyekiti wa bunge ambao wote ni zao la chama cha siasa ambacho ni chama dola kitu kinachopelekea serikali kuwa na nguvu ya kuliamulia bunge nini cha kufanya na ndio maana halina ufanisi kitu ambacho ni sawa na kusema kile ambacho serikali inataka kifanyike kiwe kizuri ama kibaya kwa wananchi kitafanyika.

Wengi wetu tunaofuatilia siasa tumeona namna ambavyo spika wa bunge anavyo kuwa upande wa chama chake na serikali na kuwatelekeza wananchi ambao ndio anapaswa kuwatetea tena akijinadi waziwazi kwa madaha na kiburi cha kuwa mwana chama wa chama dola.

Taifa lolote ambalo bunge lake linakosa nguvu ya kuiwajibisha serikali na washirika wake kamwe haliwezi kuendelea na hii ndio sababu ya nchi yetu bado inasuasa kwa miongo takribani 6 sasa.

NINI KIFANYIKE.
Katiba ijayo iwe na kifungu kitakacho elezea namna bora ya kumpata Spika wa bunge,Naibu spika wa bunge ambaye atakuwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa wala hakuwahi kuwa mwanachama ama mshirika wa chama cha siasa,kwa kuwa zoezi la upatikanaji wa katiba mpya ni la kusuasua,basi itungwe sheria ambayo itaeleza namna bora yakupatikana kwa spika wa bunge na naibu wake.

NAMNA WATAKAVYO PATIKANA.
Spika wa bunge na naibu spika
wote wapatikane kupitia uchaguzi mkuu ambapo Tume ya uchaguzi ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ndiyo itakayokuwa na mamlaka kisheria kusimamia zoezi la uchaguzi kama ilivyo kwa chaguzi zingine.

Uchaguzi utafanyika katika kipindi sawa na uchaguzi mkuu,mtu ambaye atakuwa na nia ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi hii ni lazima asiwe mwanachama ama mshirika wa chama chochote cha siasa,na pia awe na uwezo kitaaluma hasa katika masuala ya utawala ama sheria na awe na uwezo kiuchumi,tume itaweka kima cha chini cha fedha ambacho mgombea anapaswa kuwa nacho katika kapindi hicho,atawasilisha taarifa zake katika tume ya uchaguzi itakayoambatana na kiapo cha mahakama kuu akiapa kuthibitisha kwamba si mwanachama wala mshirika wa chama chochote cha siasa, na nakala ya benki ikionesha kiwango cha fedha alicho nacho kwa wakati huo, wote waliowasilisha nyaraka zao wataitwa katika mahojiano ya mchujo ambayo yataongozwa na tume ya uchaguzi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya utawala bora,mdahalo huo iwe ni sharti kuoneshwa mubashara katika luninga ya Taifa na zile ambazo zitakuwa na uwezo wakurusha taarifa hizo halikadhalika katika radio.

Washiriki wote katika mdahalo huo watapigiwa kura na wajumbe wote katika mdahalo huo, na tume itatangaza kura za washiriki wote ambapo wale watatu ama wa tano wajuu (kulingana na idadi ya washiriki) ndio watakaopitishwa kugombea ,nafasi itakayogombewa ni ya Spika wa bunge tu,naibu spika atapatikana kwa kumchukua mshindi wa pili miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi.

Wote waliopita katika mchujo wa tume ndio watakaoshiriki katika uchaguzi mkuu ambapo watalazimika kufanya kampeni nchi nzima katika majimbo yote ya uchaguzi ambapo atapata nafasi ya kuomba kura zake kwa wananchi maana ndio anaotaka kuwawakilishi kuwasimamia wabunge wao.

Kutakuwa na karatasi maalum ya kupigia kura kwa Spika wa bunge ambapo muundo wake utakuwa kama ule wa wagombea wa nafasi nyingine.

Mgombea ataruhusiwa kuwa na mawakala wake wakusimamia zoezi la kuhesabu na kuhakiki kura zake katika kila majimbo ambao mawakala hao watalipwa na tume ya uchaguzi baada ya kuwasilishwa na mgombea kupitia timu yake.

Matokeo ya jumla yatakuwa ni kutoka katika vituo vyote vya kupigia kura katika majimbo yote Ya uchaguzi.

Mshindi atakuwa ni Yule aliyepata kura nyingi zaidi na ndiye atakaye tangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi na ndiye atakaye kuwa spika mteule wa Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mshindi wa pili ndiye atakaye tambuliwa kuwa ndiye Naibu spika wa bunge la Muungano wa Tanzaia.

Spika na naibu spika wataapishwa na Jaji mkuu katika bunge.

FAIDA ZA KUWA NA SPIKA NA NAIBU SPIKA WA BUNGE WALIO CHAGULIWA NA WANANCHI.
  • Ni ngumu kwa spika kuwa sehemu ya serikali na kukandamiza wananchi
  • Inaongeza uwajibikaji na utawala bora kwa maofisa wa serikali kama Mawaziri.
  • Inafanya wabunge wawe na uhuru wa kufanya maamuzi yao pasipo hofu ya vyama vyao.
  • Bunge linakuwa na uhuru wakufanya maamuzi pasipo kuingiliwa na Rais ama serikali.
  • Bunge linakuwa na nguvu ya kuwawajibisha wale wote ambao wameripotiwa na CAG kuhusika katika ubadhirifu
  • Bunge linakuwa na uhuru wa kumuita na kumuhoji Rais kwa niaba ya wananchi.
  • Spika na naibu wanakosa nguvu yakutetea mambo ya kichama na kusimamia matakwa ya wananchi
  • Inakuwa rahisi kwa maoni ya wananchi kusikilizwa na kueshimiwa na serikali.
  • Itaongeza nidhamu na ufanisi wa bunge.
 
Back
Top Bottom