AKWEPA KUKAA JUKWAA KUU,
WENGI WAMZIKA REGIA Juma Mtanda na Shakila Nyerere, Ifakara KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa, jana alimkwepa tena Rais Jakaya Kikwete safari hii ikiwa katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipangalala.
Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao Dk Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34 akiwa nyuma ya Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, Dk Slaa hakuwahi kukutana na mkuu huyo wa nchi ana kwa ana. Katika hafla ya kutangazwa matokeo ya urais iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Dk Slaa hakuhudhuria tofauti na ilivyokuwa kwa waliokuwa wagombea wenzake wote.
Jana, Dk Slaa tofauti na viongozi wenzake wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, hakutaka kujiweka katika mazingira ambayo yangemkutanisha na Rais Kikwete katika mazishi hayo. Nyumba kulikofanyika shughuli za awali za mazishi, waandalizi waliandaa majukwaa mawili, moja maalum kwa ajili ya wabunge huku jingine likiwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu ambalo alikaa Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe. Mbali ya kukaa viongozi hao, kulikuwa na nafasi ambayo ilikuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya Rais.
Mbali ya nafasi hiyo, pia kulikuwa na kiti ambacho ilitegemewa kwamba Dk Slaa angekalia. Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alikikwepa na kwenda kujichanganya katika jukwaa la wabunge na kiti hicho kubaki bila ya kuwa na mtu. Hata hivyo, Rais Kikwete hakuweza kufika nyumbani hadi mwili wa marehemu Regia ulipopelekwa katika Viwanya vya Viungani ambako uliagwa na mamia ya waombolezaji. Uwanjani hapo nako kulikuwa na majukwaa mawili.
Kama ilivyokuwa nyumbani, jukwaa moja lilikuwa la wabunge na jingine la viongozi wa ngazi za juu lakini bado, Dk Slaa alilikwepa jukwaa hilo ambalo Rais alitarajiwa kuwa angefikia. Rais hakuweza kufika Viungani pia. [Rais Jakaya Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema) Regia Mtema wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Ipangalala Ifakara mkoani Morogoro jana.
Picha na Juma Mtanda] Rais Jakaya Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema) Regia Mtema wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Ipangalala Ifakara mkoani Morogoro jana.
Picha na Juma Mtanda Baadaye wakiwa eneo la mazishi, Rais Kikwete alifika na kushiriki tukio hilo na kisha kusalimiana na wabunge mbalimbali na viongozi waliokuwa wamefika akiwemo Mbowe, Mbunge wa Rombo Joseph Selasini, Zitto na viongozi wengine lakini Dk Slaa hakuonekana.
Ilitegemewa kuwa tukio hilo la msiba lingewaleta wanasiasa hao lakini hadi Rais Kikwete alipoondoka hakuna mahali ambako walisalimiana. Mbali ya tukio hilo, hata katika hafla mbalimbali ambazo viongozi wa Chadema wamekuwa wakialikwa ikiwemo Ikulu, Dk Slaa hakuwahi kuhudhuria.
Novemba mwaka jana viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, walifanya mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu ya Dar es Salaam kujadili suala la Katiba Mpya, lakini Dk Slaa hakuhudhuria.