Mwandishi Wetu
HII ni ndoto yangu. Ndoto hii niliiota siku nilipoamua kumrejea Mungu wangu wa kweli ambaye hakuna asiyemjua duniani, chini ya ardhi, juu ya ardhi hata angani.
Jina la Mungu wangu ni siri kuu. Ni siri ya siri kuu zote za dunia hii. Hivyo nimeona ni vyema nikawasimulia na wananchi wenzangu ili tujifunze yaliyowahi kuwatokea wenzetu waliotutangulia na kuona kama tutapata somo.
Kwa bahati mbaya au tuseme makusudi, Kaisari alipokuwa akishindana na wadogo zake juu ya urithi wa himaya yao Julius Mroma Augustus Kaizer (JMK), aliwadanganya Warumi kuwa angewatoa kwenye mateso yaliyokuwa yamefanywa na Kaisari Brutus Wilfrem Mkirene (BWM), aliyekuwa amemtangulia.
Wakati wa kampeni hizo za mwaka 2005 (KK), alitoa ahadi lukuki zinazoingia na kutoingia akilini. Katika ahadi zake zote, moja kuu iliwamotisha na kuwashawishi warumi hadi wakamchagua kwa kura nyingi. Ahadi hii si nyingine ni ile ya kuwapeleka Kanaani kwenye nchi ya maziwa na asali.
Warumi (Waisraeli) kwa mtazamo wa Kaisari, walikuwa utumwani Misri (BWM). Utumwa huu waweza kuelezwa kama ubabe, wizi, uzushi, kulindana, rushwa, matusi, unyang'au na mengine mengi kama hayo.
Kwa kuwa kwao Misri kwenye kiu na njaa, aliwaahidi kuwa atawapeleka Kanaani kwa msisitizo.
Aliwaahidi kuwavusha kwenye Bahari ya Sham (rushwa, wizi, ubadhirifu, kujuana, uzembe, umaskini, maradhi, ujinga na jinamizi lote la madhira kama hayo).
Warumi walidanganyika na kupewa matumaini hadi wakafikia kukufuru kwa kumlinganisha huyu Musa (Kaisari) wao wa bandia na Nabii yule (Julius Karneillo Nemesis au kwa kifupi JKN).
Ndimi zilianza kuwawasha wakikamia kugida maziwa na kumung'unya asali na manna (mafanikio, ukuaji wa uchumi, kuondoa rushwa, kurekebisha zoezi zima la uwekezaji na madhambi mengi yaliyokuwa yametamalaki).
Hamadi! Kumbe maskini Warumi hawakujua lugha za mafumbo tena ya kinyumenyume. Hawakujua na saa nyingine hawatajua wala kukengeuka kuwa walichochagua ni sawa na zile siku arobaini za Mwana wa Adam kujaribiwa na shetani!
Hawakujua kuwa walikuwa wakiandaliwa kutiwa mijeledi, kunyweshwa siki na hatimaye kusulubiwa. Na hii ingefanyika kwa kufungwa kamba na kuswagwa kama ngombe apelekwaye machinjioni.
Hakuchi hakuchi sasa kuchele. Matarajio yote kama tofali la barafu yalimomonyoka yasiache lau tuta!
Badala ya kuanza msafara kuelekea Kanaani na kuiacha Misri, kwa jeuri mpya na nguvu mpya na staili mpya, walichapa mguu kuelekea Misri kusini kwenye maeneo ya Ismailia na Aswan wakajenge mapiramidi mengine makubwa kuliko yale ya Giza (kutamalaki vitendo vya rushwa na wizi, kulindana kimtandao katika himaya ya Rumi wakati ule).
Amini usiamini firauni wa jana alianza kuonekana mzuri kuliko Musa bandia huyu na nduguye Haruni Losarius.
Hata wale wazee wa Mayahudi waliokuwa na busara waligeuzwa majuha watupu tena wa kujikomba kwa Musa Farao.
Waisraeli walipoomba samaki walitupiwa nyoka, wanaomba maji wananyweshwa usaha, wanaomba mkate wanapewa mawe! Anayebisha aangalie washauri wa Musa bin Bandia.
Angalia yanayojiri kwa sasa. Si kingine zaidi ya mapigo zaidi ya mia ya ndui, ukoma na magonjwa mengine hatari kuliko hata UKIMWI. alinungunika Mrumi mmoja baada ya kuona mambo si mambo.
Kulitokea ukoma na ndui na Musa, yaani Kaisari aliamua kujivua kushughulikia magonjwa kama haya akidai aliyeyasambaza ni mtangulizi wake.
Pili, kulizuka majipu na ngwengwe ya kuuzwa Roma kwa Magiriki na misafara ya wafanyabiashara wa Kiasia.
Pia kilizuka kifua kikuu cha Rumi kuingia mikataba ya vito vyake na magonjwa mengine ya zinaa kama vile kujuana, na dini mpya iliyoitwa webnization.
Mambo yalienda yakijirudia na kuongezeka. Kwani kulizuka na kashfa ya kununuliwa punda feki wa Musa kwa bei ya kulangua. Hata pesa ya Rumi kipindi kile ilianza kushuka thamani.
Iliporomoka kama inaharisha huku Kaisari akiwaambia Warumi Mambo poa.
Kwa upande mwingine Musa aliwaarika kina Delila wakachukua marimba, mabanjo, nyuta na kayamba zao kuwapumbaza Waisraeli ili waisahau ahadi kuu na agano kuu la kupelekwa Kanaani.
Angekuwa na uwezo angewaita hata wazaburi watumbuize Waisraeli ili waendelee kulala na kunajisiwa.
Taratibu ilianza kujitokeza tabia ya kujitengenezea sanamu ya ndama ifananayo na Musa na kuanza kuisujudia! Hasira za Mimi niko ambaye niko lazima zitawaangamiza Waisraeli.
Hebu zitazame dalili zote. Bahati mbaya wamejaa makahaba kila kona. Wako hata karibu na lilipowekwa agano kule Jerusalem (Roma hii ni kama Dodoma kwetu).
Walikuwamo hata kwenye madhabahu ya Bwana (wakuu wa mikoa na wilaya za Rumi).
Hata makuhani (viongozi wa dini), waandishi (vyombo vya habari), Mafarisayo (wasomi) na Masadukayo (watu maarufu) walinyweshwa kikombe hiki cha usaliti na uovu kiasi cha kuwa kwenye kundi moja na Firauni (Kaisari) mpya ambaye aliingia akiwa amejivika sura ya Musa.
Waisraeli badala ya kupelekwa Kanaani walikoahidiwa, wamewekwa rehani mikononi mwa Wagiriki majambazi (Waasiria) na kila aina ya utumwa.
Lile hekalu takatifu la Mungu (Ikulu ya Roma), taratibu liligeuka kuwa pango la wevi na watafuta ngawira. Hali iliharibika tangu alipoondoka nabii yule.
Hadithi hii ni ndefu mno. Leo tuishie hapa tukiwasalimia ndugu zetu waliopo kule Kaperanaum, Kahama ,Kaisaria, Mtwara, Krete, Tanga, Samalia, Mbeya, Galilaya, Biharamulo, Bethlehemu, Dumila, Idumea na Korintho.
Ni wenu Muisraeli aliyemo safarini kuelekea utumwani kusini mwa Misri.
Muhimu mtahadhali pigo hilo jipya la UKIMWI wa kiuchumi kutoka Asia Minor.
mmsemahovyo@yahoo.com Simu:0713260071
Source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/1/31/makala4.php