Serikali yatoa masharti mapya HakiElimu
chanzo:-Mwananchi
WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema serikali itaondoa amri walizopewa taasisi isiyo ya kiserikali ya HakiElimu kuhusu matangazo na machapisho yao kwa makubaliano kuwa taasisi hiyo itazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Mwandishi wa Waziri Mkuu, Said Nguba, alimkariri Lowassa akiyasema hayo jana baada ya kikao alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma, kufuatia maombi ya taasisi hiyo inayojishughulisha na masuala ya elimu ya kutaka kuonana naye.
Alisema kwamba licha ya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, taasisi hiyo katika matangazo na machapisho yao pia izingatie heshima na utu wa Watanzania katika kujiletea maendeleo hayo.
Mazungumzo hayo ambayo yalikuwa ya kindugu na kirafiki yalitawaliwa na dhana kwamba nchi ni yetu sote na tusaidiane kupata maisha bora kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wao HakiElimu, hawakuwa tayari jana kuzungumza chochote kilichotokana na mkutano huo, wakisubiri kwanza serikali itoe taarifa yake kwanza, jambo linaloashiria kuwa huenda hakukuwa na maelewano, na mahusiano baina yao bado ni ya kuwindana mithiri ya paka na panya.
Taarifa ya Nguba kwa gazeti hili ilileza kuwa ilikubaliwa katika mkutano kuwa katika kufuata sheria, kanuni na taratibu, kwa mfano, ili kusambaza shuleni vitabu vya kuelimisha, makala mbalimbali au katika kufanya utafiti kuhusu elimu, HakiElimu inabidi kwanza kupata kibali cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katika utoaji wa matangazo kwenye televisheni, redio na magazeti HakiElimu inabidi ihakikishe kuwa kunakuwepo na uwiano wa maudhui yaliyomo kwenye matangazo yenyewe.
Ilikubaliwa pia kuwepo na mawasiliano ya kutosha baina ya maofisa wa serikali na HakiElimu ili kufanikisha utekelezaji wa lengo la kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta; Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Joseph Mungai na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Dk Emmanuel Nchimbi.
Kwa upande wa HakiElimu waliohudhuria ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Elieshi Lema, Mjumbe wa Bodi, Jenerali Ulimwengu na mwanachama wa taasisi hiyo Helen Kijo-Bisimba na Mkurungenzi Mtendaji, Rakesh Rajani.
Serikali ilitoa amri (Government Notice No. 373) ya tarehe 11 Novemba mwaka 2005 ikipiga marufuku HakiElimu kutoa, pamoja na mambo mengine, matangazo yote ambayo yalionekana yanakwenda kinyume na maslahi ya jamii.
Katika hatua nyingine, Irene Lipende anaripoti kuwa,
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET), umetoa tamko la kupinga hatua ya serikali kuzuia kutangazwa kwa machapisho na matangazo ya HakiElimu katika vyombo vya habari kwa madai kuwa yanaharibu taswira ya elimu nchini.
Tamko hilo lililotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TenMet, Antoine Gizenga, jijini Dar es Salaam, jana liliitetea taasisi ya Hakielimu kuwa ina lengo la kuhumiza utawala bora na uwajibikaji katia sekta ya elimu.
Alisema kuzuiwa taasisi hiyo kufanyakazi zake, ni sawa na ukandamizwaji wa haki za uhuru wa kujieleza na usambazaji wa habari ambazo wananchi wamehakikishiwa katika katiba ya nchi na kutozingatiwa kwa kanuni za utawala wa kidemokrasia.
Maisha ya umma, ushiriki wa umma na nguvu ya umma ndiyo msingi hasa wa utwala wa demokrasia. Zaidi ya hayo mojawapo ya majukumu ya asasi za kiraia yaliyokubaliwa katika MMEM ni kukusanya na kusambaza taarifa za elimu kutoka na kwenda mashukleni, katika jamii, serikali na wadau wengine alisema Gizenga
Alisema katika nchi za kidemokrasia majukumu ya asasi za kiraia ni pamoja na kuchambua mapungufu yaliyomo katika sera za serikali na utekelezaji wake ili kurekebishana na kujenga nchi kwa pamoja.
Katika hatua nyingine asasi zisizo za kiserikali za TEN/MET na Policy Forum, zimelaani hatua ya serikali ya kulifungia shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu kutoa matangazo na machapisho zikisema kuwa, inatishia uwepo wa asasi hizo nchini.
Mbali na hilo, asasi hizo zimesema hatua hiyo pia inalenga kukandamiza uhuru wa kujieleza na usambazaji wa habari, pia inaonyesha namna serikali isivyokuwa tayari kukubaliana na fikra kinzani, kutokuzingatia kanuni za utawala wa kidemokrasia na kupunguza fursa ya kushiriki kwa asasi za kiraia katika maendeleo ya sekta ya elimu na sekta nyingine nchini.
Hayo yamo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na asasi hizo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TEN/MET, Antoine Gizenga na Mratibu wa Policy Forum, Getrude Mugizi, ilieleza kuwa wanachama wa asasi hizo wameguswa na kushangazwa na hatua iliyochukuliwa na serikali dhidi ya HakiElimu ambayo ni mwanachama wa asasi hizo.
"Kwa ufahamu wetu, kazi ya HakiElimu ambayo kwayo imesajiliwa, inalenga katika utawala na uwajibikaji, haki za binadamu, demokrasia na haki za kijamii...kuzuiliwa kwa HakiElimu ni sawa na kugandamizwa kwa uhuru wa kujieleza na usambazaji wa habari, ambao wananchi wamehakikishiwa katika katiba yetu," ilieleza taarifa hiyo.
Wakati asasi hizo zikieleza hayo, Chama cha Wananchi (CUF) nacho kimesema kimesikitishwa na hatua ya serikali ya kuizuia HakiElimu kuzungumzia mipango yoyote inayohusiana na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).
Taarifa ya CUF kwa vyombo habari iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wake wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma, Mbaralah Maharagande, imeielezea hatua hiyo ya serikali dhidi ya HakiElimu kuwa ni ya uvunjaji wa katiba ya nchi inayotoa uhuru na haki kwa kila raia kutoa maoni na kupewa taarifa.
CUF, kimesema hatua hiyo pia inathibitisha ukweli kuhusu madai dhidi ya serikali ya kutaka kuvibana vyombo vya habari kupitia rasimu ya muswada wake wa habari na imelenga kukwepa utekelezajiwa nidhamu ya uwajibikaji pale inapokosolewa