Ilani ya Uchaguzi 2005 -2010 ya Chama cha Mapinduzi. said:
Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwamba ardhi wanayomiliki wananchi ni mtaji wao wa msingi wa kutegemewa katika kuwapatia ajira, kuwaondolea umaskini na kuwaletea ustawi wa jamii pale walipo."
Barua ya Wakazi wa Kurasini kwa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(Aione Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)
Mheshimiwa,
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania uliahidi (wakati wa awamu ya tatu) kuwa wananchi wote tuliojenga kwenye maeneo yasiyopimwa hasa mijini tutapimiwa maeneo ya nyumba zetu na kupewa hatimiliki ili kutuwezesha kuweka dhamana ya nyumba zetu tunapotaka mikopo kwenye benki zinazokopesha.
Sisi wananchi wa Kurasini Shimo la Udongo tunakukumbusha ahadi hiyo, na kukuomba SITISHA tafadhali uamuzi wa sisi kuondoshwa kwenye makaazi yetu mpaka pale utakapotoa uamuzi wa mwisho.
Mheshimiwa Rais, mwaka huu (2006), Machi 28 Bungeni Dodoma, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rita Miaki (MB), alikariri ahadi ya kuyatambua maeneo yaliyojengwa bila kupimwa na kuwapa wananchi wanaomiliki leseni za makazi (Residential License).
Kazi ya kuwatambua wakazi waliojenga kwenye maeneo yasiyopimwa imefanyika katika Jiji la Dar es Salaam ambapo jumla ya miliki 210,000 zilitambuliwa na leseni za makazi 20,000 zimetolewa kwa wamiliki wa maeneo hayo," alisema Mheshimiwa Waziri Miaki alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Masolwa Cosmas Masolwa, Mbunge wa Bububu (CCM).
Mheshimiwa Rais, hi kwa nini makazi yasiyopimwa Kurasini yasijumuishwe kwenye mpangiho huo? Sisi watu wa Kurasini tumelikosea nini taifa letu mpaka tulazimishwe kuyaacha makazi yetu, tofauti na ahadi uliyotupa Mheshimiwa Rais? Kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri Mlaki, ni baadhi tu ya nyumba zitakazoondolewa ili kupisha ujenzi wa MIUNDOMBINU kwenye makazi kama yetu kama vile barabara na mifumo ya majitaka au wale waliojenga kwenye maeneo hatari kama vile mabondeni. Hivi Mheshimiwa Rais unayo habari ya mambo haya?
Sababu tunayoambiwa ni "kupisha upanuzi wa bandari". Mheshimiwa Rais, sisi wananchi wa Kurasini haturidhiki na sababu hiyo, kwa vile watakokuja kuchukua maeneo yetu Si Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwa matumizi ya Bandari, bali ni "wawekezaji" ambao wanataka kuwa na "matumizi yanayoelekeana na bandari" hapa Kurasini.
Hili Mheshimiwa Rais lina tofauti ipi na ubaguzi wa rangi ("ethnic cleansing") -- kwamba sisi wazawa hatustahili kuwepo Kurasini? Je, makazi yabinadamu siyo matumizi yanayoelekeana na bandari?
Huku kwenye makazi yetu wanajenga gati namba ngapi? Hata TPA yenyewe ingekuwa ndiyo inahitaji maeneo ya huku Kurasini, bado Si sawa kutumia utaratibu wa kutunyang'anya ardhi uliyorasimisha tutumie, wakati ambapo sera iliyoko ni ya ardhi kuwa na thamani, na kwamba sekta binafsi (ambayo TPA ni mojawapo, au itakuwa hivi karibuni) inatakiwa kutumia nguvu ya soko kujipatia ardhi.
Serikali yako Mheshimiwa Rais ilijitoa kufanya biashara muda sasa. Ni kwa nini tena serikali itutoe kwa nguvu kwenye ardhi, halafu yenyewe ifanye biashara ya kuuza viwanja vyetu kwa 'wawekezaji'? Ikiwa serikali inaona hatuitumii ardhi ipasavyo, ni kwa nini isituagize tutumie kwa matumizi inayoona vyema?
Ulisema Mheshimiwa Rais kwamba uwekezaji siyo lazima uwe ugenisishaji. Hata ilani ya uchaguzi iliyotufanya tukupigie kura inasema "Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwamba ardhi wanayomiliki wananchi ni mtaji wao wa msingi wa kutegemewa katika kuwapatia ajira, kuwaondolea umaskini na kuwaletea ustawi wa jamii pale walipo.
" Ilani hivo inaahidi "Kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kurasimisha ardhi na nyumba zao ili waweze kuzitumia kupata mikopo ya mabenki na miluko mingine ya fedha inayokopesha" ndani ya miaka mitano 2005 - 2010.
Sisi tulipo hapa Kurasini kwa nini tuondolewe, licha ya ahadi zako zote hizo? Kwa mujibu wa sheria za Ardhi, Mheshimiwa Rais unaweza kunyang'anya umiliki wa ardhi "kwa maslahi ya taifa". Je, kutoa umiliki kwa mtu mmoja binafsi, na kuuleta kwa mtu mwingine au taasisi nyingine binafsi, ni maslahi ya taifa?
Je ulituambia tufanye wanachotaka kukifanya hao watu wengine kwenye ardhi hii tukashindwa? Nini nafasi ya MKURABITA, MKUKUTA na mikakati mingineyo ikiwa Si kutuwezesha sisi wananchi kumiliki uchumi na makazi ya nchi yetu?
Au mikakati hiyo ni ya kwenye makaratasi tu? Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri Mlaki, "Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 kifungu Na. 23 Halmashauri nchini zinayo mamlaka ya kutambua wananchi waliojenga nyumba kwenye maeneo yasiyo hatari na kutoa leseni za makazi." Sisi tunaoishi Kurasini hatupo kwenye maeneo ya hatari.
Tunakuomba Mheshimiwa Rais uturasimishie makazi yetu kama ambavyo ulituahidi kwenye ilani ya uchaguzi na kwenye nyaraka za serikali iii tuweze kuendelea kujenga taifa letu.
Kana kwamba uchungu wa kunyang'anywa ardhi yetu Si kitu, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, inatutaka kubomoa nyumba zetu ndani ya siku 14 baada ya kupewa fidia zenye utata kwa hundi ambazo huiva ndani ya siku saba ambapo ni sawa na kwamba tumepewa siku saba za kuondoka katika eneo hilo.
Hata utawala wa Makaburu wa Mrika Kusini katika kilele cha ubaguzi wa rangi haukufanya hivyo! Ikiwa wamachinga walipewa miezi sita kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa, vipi wakazi ambao tumeishi kwa miaka hadi 40 tupewe siku 14 kuondoka wakati tuna familia? Utawezaje kujenga nyumba ya kuishi kwa siku 14?
Maafisa wa Wizara ya Ardhi walituahidi kuwa wangetupa viwanja katika eneo la Kibada kujenga nyumba mpya, fedha za usafiri, fedha za miaka mitatu kwa ajili ya kutuwezesha kupanga nyumba, pamoja na kulipwa fidia kulingana na thamani ya nyumba ya mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna lolote lililokwisha kutekelezwa.
'Fidia' yenyewe ambayo Wizara imelipa inakiuka misingi ya sheria za Ardhi Tanzania, Taaluma ya Tathmini ya Ardhi na haki za binadamu. Nyumba 46 za Kurasini Highway zimethaminiwa, lakini hazikufidiwa ipasavyo: Hamna "valuation reports" malipo yanayotolewa hayaonyeshi unalipwa kwa ajili ya nyumba ipi; hamna uwazi kwenye tathmini wala ripoti; hata viwanja vilivyopimwa vinanyang anywa bila kufuata taratibu; na hamna mchanganuo wa mazingira (EIA) uliofanywa kabla ya mradi huu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kutekelezwa.