SoC01 Hii ndio mbinu pekee ya kuokoa Mfumo wa Elimu Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Jul 13, 2021
23
24
Shule ya msingi niliyosoma zaidi ya miaka kumi na tano iliyopita inajipambanua kwa kaulimbiu isemayo “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA”. Nakumbuka vyema jinsi ambavyo kaulimbiu hii ilifanywa kuwa sehemu ya maisha ya kila mwanafunzi pale shuleni. Mwalimu alikuwa akiingia darasani kufundisha wanafunzi wote tunasimama kwa pamoja kisha kiongozi wa darasa (monita) anaanzisha salamu kwa kutamka “Elimu ni ufunguo wa maisha” kisha wote tunaitikia “Shikamoo mwalimu”, ukikutana na mzazi yeyote maeneo ya shule ilikuwa ni lazima umsalimie kwa maneno “Elimu ni ufunguo wa maisha, shikamoo baba/mama”.

Kwa muda wa miaka saba niliyotumia kusoma shuleni pale, maisha yangu yalijengwa katika kuamini kuwa ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA. Ni ukweli ambao mimi binafsi niliendelea kuuamini bila kuhoji undani wake hadi namaliza elimu yangu ya chuo kikuu pale Dodoma (UDOM). Kutokana na maendeleo ya teknolojia duniani, mabadiliko katika mfumo wa maisha na uhuru wa fikra ndani ya jamii nadhani ipo haja ya kuhoji mantiki na ufafanuzi wa kaulimbiu hii ambayo bado inaendelea kutumiwa na taasisi nyingi za elimu nchini na duniani kwa ujumla.

Baadhi ya maswali magumu ya kujiuliza ni kama vile; kama elimu ni ufunguo wa maisha, kufuli la maisha ni nini? Mbona walio na elimu hiyo hawaonekani kama watu waliofunguliwa maisha? Mbona Elimu imegeuka na kuwa karakana la kuua vipaji vya watoto wetu? Je, funguo tunazopewa na huyu Elimu si za bandia kweli? Kama si za bandia kwanini hazifungui maisha kwa wasomi wengi? Kwanini leo hii tabaka lenye manung’uniko mengi na yasiyokwisha ndani ya jamii ni tabaka la wasomi? Baada ya kuupata ufunguo huu uitwao Elimu, nani mwenye jukumu la kutuonyesha makufuri yalipo ili tufungue?

Ukifuatilia historia ya wazee wetu wa zamani utagundua walikuwa na mfumo imara sana wa kurithishana maaarifa au kwa lugha ya kisasa "elimu" ambao ulivurugwa na kusambaratishwa na ujio wa mtu mweupe barani Afrika.

Wazee wetu waligawana ujuzi na fani mbalimbali kulingana na KOO zao (specialization of labour). Ilifahamika wazi kabisa kwamba koo flani ni ya waimbaji, koo hii ni ya wataalam wa afya, koo ile ni ya wafua vyuma, koo ile ni ya wawindaji nakadhalika. Ukoo wa wataalam wa afya/madaktari ulitegemewa na kijiji kizima na uliendeleza utaalam wao kwa kurithishana kutoka kizazi hadi kizazi. Mtoto mdogo aliweza kuingia msituni na kukutajia kila mmea na matumizi yake katika afya ya binadamu. Ukoo wa wanamuziki ulitegemewa katika sherehe zote za kifalme kijijini pale. Mtoto mdogo aliweza kucheza marimba na kupiga ngoma katika namna ambayo mtu mwingine asiye mwanamuziki asingeweza kufanya hivyo. Ukoo wa kisiasa uliendelea kuzalisha wanasiasa. Kama babu alikuwa Mfalme basi baba atakuwa mfalme na hatimaye sisi watoto tutakuwa wafalme na hakukuwa na ubaya wowote katika hilo.

Ukitazama MFUMO wa ELIMU wa dunia ya leo utagundua ulichota busara hizo kutoka katika mfumo wa elimu wa mababu zetu. Bahati mbaya ni kwamba ulichota busara hizo kimakosa na kuacha mambo mengi ya msingi.

Hebu tutazame kwa mfano MFUMO wa ELIMU katika sekta ya Afya ya binadamu hapa Tanzania na duniani kote. Miongoni mwa masharti ya msingi ya kuanzisha Chuo au shule ya kutoa mafunzo ya Afya ya binadamu nchini Tanzania ni uwepo wa Hospitali au Kituo cha Afya kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Huwezi kupewa kibali cha kutoa shahada ya udaktari wa binadamu kama chuo chako hakina hospitali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Ndio maana kitivo cha tiba cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimejengewa hospitali kubwa ya Benjamin Mkapa, ndio maana Chuo Cha Tiba Muhimbili kinatumia hospitali ya Taifa Muhimbili, ndio maana Chuo cha Tiba Bugando kinatumia Hospitali ya Rufaa Bugando nakadhalika.

Jambo la pili la kufurahisha katika sekta ya afya ni kwamba walimu au wakufunzi wa wanafunzi katika vyuo hivyo vya afya ni madaktari pia katika hospitali hizo za vyuo. Hivyo, mwanafunzi wa kozi ya udaktari anafundishwa na daktari kamili, sio mhitimu wa fani ya udaktari. Daktari anatoka kujibu wagonjwa anaingia darasani kufundisha. Jambo la tatu katika sekta ya Afya ni kwamba wanafunzi wanatumia muda mwingi katika mafunzo kwa vitendo kuliko darasani. Hii ni kwa sababu wanaenda mtaani kushughulika na “uhai” wa binadamu, hivyo wanapikwa vyema na wahadhiri wao ambao pia ni madaktari kamili. Wataalamu wanaozaliswa pale hupelekwa moja kwa moja katika mahospitali ya mikoa, wilaya na vituo vya afya kuhudumia wananchi.

Ukitazama MFUMO wa ELIMU unaotumika katika sekta nyingine za kitaaluma ni tofauti kabisa na ule unaotumika katika sekta ya afya! Utagundua Chuo Kikuu kilekile cha Dodoma kinatoa ELIMU katika fani nyingine mbalimbali lakini kila mwaka kinazalisha wanasheria butu, wahasibu mamluki na wahandisi kanjanja!

Kama ni sharti la msingi kwa chuo kinachotoa mafunzo ya tiba ya afya ya binadamu kuwa na hospitali au kituo cha afya kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, kwanini lisiwe sharti la msingi kwa chuo kinachotoa mafunzo ya uanasheria kuwa na kampuni za uwakili zinazomilikiwa na chuo husika? Hii itasaidia vijana wetu kufundishwa na mawakili au mahakimu kama ambavyo wale wa fani ya udaktari wanavyofundishwa na madaktari kuliko ilivyo sasa ambapo vyuo huishia kuajiri wataalam wenye ufaulu mzuri wa masomo ya sheria hata kama hawajawahi kupanda kizimbani kutoa utetezi wa kisheria. Ni raha iliyoje kufundishwa na mwalimu ambaye baada ya kipindi anaingia mahakamani kusuluhisha kesi za wananchi! Huyu anaijua dunia vizuri kuliko yule wa nadharia. Huyu ni mwalimu mzuri wa vitendo kuliko yule mwenye ufaulu mzuri pekee.

Kama ni sharti la msingi kwa chuo kinachotoa mafunzo ya tiba ya afya ya binadamu kuwa na hospitali au kituo cha afya kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, kwanini lisiwe sharti la msingi kwa chuo kinachotoa kozi za masuala ya utawala katika biashara na usimamizi wa fedha kumiliki taasisi za fedha kama mabenki? Tazama namna wahitimu wa fani za usimamizi wa fedha walivyo butu mitaani! Hawang’ati, wameduwaa wamejikunyata, wanatia huruma! Wanaanzaje kuwa na makali ilhali walimu wao hawajawahi kumiliki hata duka la mangi mtaani lakini ndio wanaowafundisha mbinu za kujiajiri! Wanaachaje kujikunyata ilhali wanaenda mafunzo kwa vitendo wakiwa mwaka wa pili tena kipindi cha likizo na wakifika kwenye mabenki ya biashara wanaishia kupewa kitengo cha Huduma kwa wateja! Nani amkabidhi benki yake afanyie mazoezi kwa vitendo?

Shule ya biashara ya pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inashindwa vipi kumiliki taasisi yake ya fedha ambayo mbali na kutumika kama kitegauchumi cha Chuo, pia itatumika kama karakana la kunolea wanafunzi wake. Pale watajifunza mbinu za biashara, watawekeza mitaji yao midogomidogo na hata kukopeshwa na kudhaminiwa na Chuo husika pindi wamalizapo mafunzo na kutaka kujiajiri. Kitivo cha biashara cha Chuo Kikuu Mzumbe kinashindwa vipi kufungua taasisi yake ya ukaguzi na usimamizi wa masuala ya fedha (Auditing firm)? Ni raha iliyoje kufundishwa na mwalimu ambaye pia ni mkaguzi wa fedha anayetumia ujuzi wake mtaani kuliko ilivyo sasa ambapo vyuo huishia kuajiri wahadhiri waliojaa nadharia vichwani! Wahadhiri wanaodhani kumfelisha mwanafunzi mitihani ndio ubora wa mhadhiri!

Tukibadili MFUMO wetu wa ELIMU na kufanana na mfumo uliopo katika sekta ya ya afya ya binadamu tutaanza kuona matokeo chanya na ya haraka. Tuko makini sana katika kupika wataalam wetu wa afya ya binadamu kwa sababu tunajua wanaenda kushughulika na uhai wa binadamu moja kwa moja lakini tunakosa umakini huo katika kupika wataalamu wa siasa kwa kudhani siasa haijeruhi kumbe tunajidanganya. Vyuo vya mafunzo ya Muziki sharti viwe na lebo za muziki, studio za muziki na viwe na uwezo wa kuwasimamia wanamuziki wanaozalishwa na vyuo vyao. Vyuo vya uhandisi nchini sharti viwe na shughuli za kihandisi. Kitivo cha Uhandisi wa majengo cha Chuo Kikuu cha Ardhi kinashindwa vipi kumiliki kampuni za usimamizi wa majengo achilia mbali ufyatuaji matofali au utengenezaji vigae?

Kama mababu zetu walirithishana ujuzi na fani kulingana na KOO zao. Ni wajibu wa Vyuo vyetu kurithishana ujuzi na fani kulingana na maarifa yao. Kama ambavyo mababu walikuwa karakana la kuzalisha wataalam ndivyo ambavyo vyuo vyetu vinapaswa kuwa makarakana ya kuzalisha wabobezi.

Mfumo wa elimu wa mababu zetu ulikuwa na matokeo ya haraka sana. Mtoto mdogo alietoka katika KOO ya wataalam wa afya alikuwa na uwezo wa kukuzungusha msituni na kukutajia kila aina ya mti na matumizi yake katika tiba. Mfumo wa elimu wa sasa unatia kizunguzungu, kijana anatumia miaka 7 shule ya msingi, miaka 6 shule ya sekondari na baadae miaka 3 hadi mitano Chuo Kikuu na mingine miwili hadi mitano kwa elimu ya uzamivu lakini mzee mzima huyu aliehitimu shahada ya uzamivu katika biashara ukimkabidhi Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) hajui aanzie wapi!

Tukiamua inawezekana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom