3. MIZUNGU
Kauli ile ya Sheikh kuwa kwa maradhi niliyonayo ni ya bara ilitukatisha tamaa kiasi cha kufanya tusijuwe la kufanya, tukarudi nyumbani kwa ajili ya kupeleka mrejesho na kufikiria kutafuta waganga wa kienyeji.
“Msiende kwa waganga wa kienyeji, nendeni kwanza kwa Shariff mtoto…” hii ilikuwa kauli ya baba baada ya kuona tutapotea njia maana yeye hakuwa mtu wa kufuatilia tabibu za kienyeji ingawaje pia hakuwa mtu wa kusali sana msikitini.
Shariff mtoto wakati huo alikuwa kiitwa Hanssen. Shariff huyu asili yao ni maeneo ya Mkwaja pia ambapo ndipo matatizo yangu yalipoanzia. Hakuwa mtoto kihivyo lakini watu walizoea kumwita hivyo maana alianza huduma za maombezi akiwa kijana mdogo kabisa.
Mashariff kwa mukhtadha wa hapa ni wale watu wanaume ambao wamekirimiwa zawadi na Mwenyezi Mungu ya kuweza kukusudia jambo na likawa. Watu walikuwa wanasema wana ‘makarama’. Wapo mashariff wa aina kuu nne kama sijakosea, wapo wale wa nasaba (kutokea kwenye kizazi cha wajukuu wa Mtume Mohammad, rehema na amani zimfikie), wapo wale wa ucha Mungu (kila mwenye kuitakasa nafsi basi aweza kuwa shariff) na wapo wale wa kukirimiwa tu na Mwenyezi Mungu kupitia mawalii wake. Inasemekana kuna hata kizazi cha paka (nyau / cats) ambao ni mashariff. Ndiyo maana haishauriwi kuwapiga paka hovyo bila sababu ya msingi maana kuna wengine ni uzao huo, wakikusudia baya basi litakupata, na hii imeenda mbali kwa viumbe wengine wengi wataambao, warukao na watembeao. Pia kuna Mashariff ‘jina’. Hawa wamepewa tu jina hilo na wazazi wao ama kujiita wao wenyewe pasi na karama zozote ama kwa kujifanya wana karama za kutibu nk.
(Habari za Mashariff ni pana na linafaa kuwa na uzi wake.)
*************
Siku iliyofuata tulienda kumtafuta Shariff mtoto, lakini hatukumkuta, tulirudi jioni nyumbani kwake ndipo tukamkuta lakini cha ajabu tulimkuta akiwa amelewa pombe aina ya mnazi.
Mnazi ni aina ya pombe igemwayo kutoka kwenye mti wa mnazi kama vile pombe aina ya ulanzi inavyogemwa.
“Njooni kesho asubuhi, muda huu siwezi kufanya kitu…” ilikuwa kauli ya Shariff Hanssen.
Tuliondoka kwa unyonge sana huku tukiwaza kama huduma ya maombezi itafanikiwa kwa hali ya ulevi ule wa pombe.
“Makarama yatamwisha huyu kwa sababu ya ulevi” kaka alisema kwa kulalamika wakati tunarejea nyumbani.
Asubuhi yake tulifika kwa Hanssen mapema ili kuona kitakachoendelea, alitukaribisha kwenye mkeka na baada ya maelezo marefu ya kaka akachukuwa kitabu kidogo akaanza kusoma kiarabu kwa haraka haraka sana kiasi kwamba hata sikuweza kujuwa anasoma kitu gani. Aliendelea kusoma hivyo kwa muda mrefu, kiasha akaingia ndani akaleta ‘chetezo’ na ubani aina tatu tofauti na kendelea kusoma huku akiweka ubani kwenye chetezo chenye moto.
Baadaye akatuamuru tuwe tunaitikia dua kwa kusema ‘amin’, tulitikia dua kwa muda mrefu hatimaye akamaliza.
**********
Hali yangu kiafya ilitulia kiasi cha kama miezi miwili hivi lakini baadaye maruweruwe yakanirudia tena. Nakawa nikilala usiku naona ndoto za kama napaa hivi juu ya ardhi na kuiangalia dunia kama mwewe vile aangaliavyo chini akiwa hewani, siku nyingine naota nipo msituni peke yangu kama nimepotea hivi natafuta njia ya kutokea barabarani, siku nyingine naota nipo mwenye mji wa ajabu wenye miamba ya mawe mengi watu wakiwa wanataabika na hali za huko mie nakuwa nawasaidia nk.
Siku nikiota ndoto za namna hiyo tu, asubuhi yake napata homa kali kiasi cha kushinwa kula vizuri hali iliyopeleka afya yangu kuzidi kudhoofu, lakini pia nikawa kama vile naona yatakayotokea muda ujao japo siyo kwa asilimia mia lakini inakuwa vivyohiyo. Kwa mfano, naweza kulala hata mchana nikaona / kuota kama kutakuwa na msiba jirani, basi kweli haipiti muda tunapata taarifa za msiba na mambo ya ajabu ajabu kama hayo.
Hali yangu iliendelea kuwa mbaya mpaka familia ikaamua nianze kujaribu tiba za kienyeji. Ndipo nilipo pelekwa Mlingotini – Bagamoyo. Tulipitia njia ya kaole kisha kuingia ndani upande wa kulia ndani ndani kabisa kwa kuulizia kwa Mzee wa tiba, mganga maarufu Mlingotini. Nilikuwa kijana barobaro tu wa miaka kumi na mitano hivi kuelekea kumi sita na wala sikuwa nawajuwa wanawake.
Elimu ya sekondari sikuchaguliwa kuendelea na wala wazazi hawakujishughulisha kuhusu mimi kwenda Sekondari, haikuwa kipaumbele sana kwa watu wa ukanda wetu, tulikuwa tunarithi kazi za baba zetu tu.
Baada ya mapokezi ya pale kwa mganga tulisubirishwa na kundi wa wateja wengine wapatao wane hivi pale. Kila mmoja alikuwa anaitwa ndani kwenye kilinge cha Mzee wa tiba.
Ilipowadia zamu yangu niliitwa na kuelekezwa kukaa kwa kunyoosha miguu uelekea upande jua linapo chomozea (mashariki). Mpaka hapo hatukuwa tumesema chochote kwa mganga. Akauliza jina langu na la mama yangu kisha akaanza kusema maneno yasiyoeleweka pale na vimbwanga kibao hatimaye akatikisa kichwa na kutulia.
“Kijana!” aliniita yule mganga, nikatoa tu macho kwa kumuangalia. Yeye akaendelea kusema kwa sauti nzito…
“Kijana, umerogwa!”
“Umehangaika sana bila suluhu lakini hapa sasa umefika!”
Kwa mganga huyu tulienda watu watatu, yani mimi, Kaka mkubwa pamoja na mama yangu mzazi. Ilikuwa ni mwendo mrefu wa kutembea, maana tulivizia basi la MFDC (Mbegani Fisheries Development Centre) lililokuwa likiwapeleka wafanyakazi na familia za wafanyakazi kwenye Chuo cha maendeleo ya uvuvi Mbegani Bagamoyo. Tulishukia mbele kidogo ya kaole na safari ya kutembea kwa miguu ikaanza kuelekea huko kwa Mzee wa Tiba Milingotini ndani ndani.
“Eeee wanatakiwa kuku wawili, jogoo mwekundu na tetea mweusi…” alisema yule mzee wa tiba kwa sauti nzito.
“Eeee kuku wawe wamekomaa kiasi cha kuwa na ukucha mrefu juu ya miguu…” aliendelea.
Mimi na kaka tukawa tunatazamana, lakini mama akawa anasikiliza kwa makini.
“Baba, tumetoka mbali, hao kuku tutawapata wapi na ni hatua kurudi kuwatafuta…” Mama alimsemeza yule mganga.
“Hahahahhaa…. Hahahahaha…” Mganga alicheka kwa sauti nzito kika akasema kuwa kuku watapatikana.
“kuku watapatikana, kuku watapatikana, kuku watapatikana…” sauti ya mganga ikawa inafifia kisha akainamisha kichwa.
Pale kilingeni kulikuwa pia kuna wasaidizi wawili wa mganga, mmoja ni kijana wa kiume na mwingine ni mdada wa makamo ambao wote walikuwa wamevaa kawaida tu isipokuwa mganga mwenyewe alikuwa amevaa kanini nyeusi, kilemba cheupe huku ameshika usinga wenye shanga kadhaa .
Pembeni ya chumba kulikuwa na makopo mengi yaliyo na mizizi iliyosagwa (dawa) na upande mwingine kulikuwa na vibuyu vidogo vidogo kadhaa ambavyo sikujuwa mara moja ndani yake kuna nini. Sehemu nyingine kulikuwa na kitambaa chekundu kilichofunika vitu ambavyo pia sikujuwa ni nini.
Mara yule mzee wa tiba akainua kichwa na kuwauliza wale wasaidizi wake…
“Wamesemaje…?” aliuliza mganga kwa sauti ya kawaida huku akiwaangalia wale wazaidizi wake.
Wakaumueleza kuwa kunatakiwa jogoo na tetea. Basi mganga akawambia yule kijana akachukuwe hao kuku bandani.
Kulikuwa na banda maalumu la kuku wenye rangi moja moja tofauti. Yanai kuku weupe tu, kuku weusi tuu na kuku wekundu tu lakini wote waliweka pamoja.
“Tiba yako kijana itaanza kwa kafara ya kuku hao wawili… hebu nifuateni” alisema yule mganga huku akitoka nje ya kilinge na kwenda eneo la uwazi ambalo kwa dalili zote palikuwa panaonyesha kuwa ni machinjio ya kuku maana kulitapakaa damu za kuku zilizoganda.
Kuku wale walichinjwa kila mmoja kwa wakati wake, baada ya kuku kupapatika na kufa mzee wa tiba alikuwa ‘anatolea macho’ miguu, mabawa, shingo na ueleko wa kuku maana walikuwa wakichinjwa wanaachwa wapapatike hadi wafe.
“Njia imefunga” alisikika mganga akisema baada ya kumchinja yule tetea mweusi.
“Magharibi” aliropoka yule mzee wa tiba, hiyo ni baada ya kumchinja kuku wa pili ambaye ni jogoo.
Basi tukaambiwa tukae nje tusubiri na wale kuku walichukuliwa na yule mdada msaidizi na kutoweka nao upande mwingine wa nyumba.
Mganga aliingia tena kilingeni na kuita wateja wengine waliokuja baada ya sisi.
Tulisubiri pale nje hadi njaa ikaanza kuniuma maana ilikuwa inakaribia saa nane mchana. Mara akaja yule kijana msaidizi wa mganga na kutuita ulekeo wa jamvi safi kwa ajili ya chakula. Kilikuwa chakula maalumu kilichoandaliwa kwa ajili yetu sisi, kulikuwa na ugali, samaki pamoja na vibakuli vitatu vya finyango za kuku.
“Wewe bakuli lako hili” alisema yule kijana huku akinionesha upande wa kukaa.
Wakati nakula ndiyo nikagundua niliwekewa maini, firigizi na miguu ya kuku wakati mama na kaka wao niliona baadaye wakila vipapatio.
Kulikuwa na makundi mengi yanayokula muda huo na mtindo ulikuwa ni huo huo wa vibakuli vibakuli.
Baada ya maakuli, kila mteja alikuwa akiitwa kilingeni na kupewa dawa na maelekezo ya kutumia. Zamu yetu ilipofika mganga akasema, kazi yangu kubwa maana imeegemea magharibi na njia imefunga. Hivyo tujiandae kwa kafara kubwa ya kondoo. Tutafute wenyewe. Ujira wa kazi alisema tuweka kwenye mtungi kiasi chochote ambapo mama alienda kuweka, sikujuwa hata ameweka kiasi gani lakini nilisikia sauti za sarafu zikilia, pia tulilipishwa kuku wawili kwa bei ya sokoni tu.
Hata hivyo nilipewa dawa za kutumia na maelekezo yake. Baadhi ya dawa zilikuwa majani fulani sijapata kuyaona tangia nizaliwe, yanalowekwa kwenye maji ya kuogea kisha kila nikitaka kuoga niliambiwa niwe nachanganyia maji hayo ya majani ya ajabu ajabu, dawa nyingine ilikuwa ya kupaka kama mafuta lakini yalikuwa meusi ti! Yalikuwa kimiminika, unajipaka mwili mzima, kali kupita yote nilipewa mafuta fulani ya kupata nyayoni, viganyani na usoni usiku tu wakati nataka kulala lakini ilikuwa inanuka balaa! Ilikuwa inanuka kuliko mafuta yatumikayo ‘kukarafati’(siyo karabati) vyombo vya baharini kwa sufi na mafuta ‘makasamala’.
**********
Inaendelea