WAKILI WA MOYO-45
ILIPOISHIA:
Juzi tulikuja huku na Mage kuvunja uchumba wetu ambao ulinishtua sana na kuumiza moyo wangu japokuwa haikuwa hoteli hii, lakini ni hukuhuku Bagamoyo.
SASA ENDELEA
Lakini leo nimezaliwa upya kwa kulipata penzi la kweli ambalo naamini nilitaka kulipoteza, haya ni machozi ya uchungu na furaha.
Nafurahi kusikia hivyo, lakini moyo wangu bado haujaamini kama tayari wewe ni wangu.
Kwa nini Cecy?
Naogopa Mage anaweza kurudi na wewe kunitosa, nitaumia mara mbili kwa vile nimeonja utamu wa mapenzi naweza kufa kwa presha kama utafanya hivyo, Cecy alisema kwa sauti ya kulalamika.
Cecy unataka kuamini vipi wakati penzi langu lilikuwa wazi mbele ya mama yangu.
Mama yako alikuitia nini pembeni?
Tulikuwa na yetu wala haikuhusiana na sisi, Colin alitengeneza uongo ili kuendeleza furaha ya siku ile.
Mmh! Nilikuwa na wasiwasi labda chokoraa nimeingia kwenye nyumba ya malkia, Cecy alitania utani wenye ukweli.
Hapana wewe ndiye malkia wangu.
Nashukuru kusikia hivyo, Cecy alimkumbatia mpenzi wake kwa furaha bila kujua palichimbika mpaka yeye kuwa pamoja muda ule.
***Mage na Hans waliwasili katika ardhi ya Tanzania katika Jiji la Dar na ndege ya Shirika la Afrika Kusini. Nje ya uwanja wa ndege walisubiriwa na gari la kifahari aina ya Land Cruiser V8 nyeusi. Baada ya ndege kutua waliteremka na kwenda moja kwa moja ndani ya gari lililokuwa likiwasubiri na kuingia.
Gari liliondoka kuelekea Mikocheni anapoishi Hans, njiani Mage alikuwa na furaha ya ajabu kurudi mikononi kwa mpezi wake mwanaume wa maisha yake. Baada gari kuingizwa ndani na kusimama, Hans alizunguka upande wa pili na kumfungulia Mage mlango na kumkaribisha.
Karibu utamu wangu.
Asante raha zangu.
Walishikana mikono na kuingia ndani, mapokezi ya familia ya Hans yalikuwa tofauti na siku za nyuma, waliufurahia ugeni wa Mage huku wadogo zake wakimwita wifi na shemeji na wazazi wakimwita mkwe.
Ilikuwa ni faraja kubwa moyoni kwa Mage, aliona sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano kukubalika katika familia ile.
Moyoni alijilaumu kukubali kuolewa na Colin kumbe ahadi ya kuvumilia ili ndoto yao ya muda mrefu waliyoahidiana kutenganishwa na kifo ilikuwa njiani. Familia haikuwa na tatizo tena kuingilia uamuzi wa mtoto wao kwa vile chaguo lao ni la Mungu, hawakuwa na jinsi.
Baada ya mapokezi mazuri katika familia ya mpenzi wake, Mage na Hans walielekea Kigamboni nyumbani kwa kina Mage ili kujitambulisha rasmi kwa mzazi wake.
Walipofika Kigamboni, Mage alimkaribisha Hans nyumbani kwao.
Karibu mume wangu.
Asante mke wangu.
Walishikana mikono na kuingia ndani kwa mwendo wa mahaba, sebuleni walimkuta mama Mage. Mage alimuachia mkono Hans na kumkimbilia mama yake na kumkumbatia.
Waaawoo mama.
Mage mwanangu karibu mama.
Asante mama.
Mage alichukua nafasi ile kumtambulisha Hans.
Mama leo nimemleta mume wangu chaguo la moyo wangu.
Nimemuona, karibu baba, mama Mage alisema kwa sauti ya unyonge.
Asante mama.
Mama mbona unaonekana mnyonge, unaumwa? Mage alimuuliza mama yake.
Walaa mwili umechoka tu.
Mama Mage alinyanyuka na kuelekea chumbani kuwapisha, alipoondoka eneo la sebule alimwita mwanaye.
Mage mama njoo mara moja.
Nakuja mama, kabla ya kuondoka alimuaga mpenzi wake.
Mpenzi nakuja.
Hakuna tatizo msikilize mama.
Mage alimbusu shavuni Hans na kuchepua mwendo kwenda kumsikiliza mama yake.
Abee mama.
Njoo chumbani.
Waliongozana hadi chumbani, walipofika mama yake alisimama na kumwambia Mage akae kwenye kochi, baada ya kukaa alimgeukia na kumwita.
Mage.
Abee mama.
Hivi ndiyo umeamua kunivua nguo?
Kukuvua nguo! Kivipi mama.
Kwa hiyo hutaki kuolewa na Colin?
Mamaaa! Mbona hilo tuliisha limaliza, si nimekueleza ukweli wangu na Colin anajua kila kitu. Sasa swali kama hilo linatoka wapi?
Mage kwa nini unalamba matapishi yako?
Mama Hans si matapishi ni chakula kilichowekwa kwenye hot port, nimekipakuwa bado kina moto. Unajua jinsi gani nilivyoteseka baada ya Hans kulazimishwa kuoa mwanamke mwingine. Ni wewe uliniambia niwe na subira sasa leo karudi mikononi mwangu unaniuliza hivyo.
Kama ungekuwa huna mchumba nisingekuuliza lakini wewe tayari umeshakuwa mchumba wa mtu tena upo kwenye hatua za mwisho za ndoa.
Mama wewe ndiye unayekuza mambo, Colin tumesha malizana na sasa hivi tunatoka nyumbani kwao Hans ambako sikuamini kama wangenipokea kama malkia. Yaani mama nimefurahi kukubalika katika familia ya mpenzi wangu.
Mwanangu siku zote mkataa pema pabaya panamwita.
Mamaa maombi gani hayo?
Nakuambia utamkumbuka Colin, ipo siku Hans atakukimbia na kurudi kwa Colin utambembeleza ukitembea kwa magoti, kibaya ukute ameoa mwanangu utakuja jutia uamuzi wako, mama alitoa tahadhari.
Mama kuwa na Hans sitajuta katika maisha yangu ni chaguo sahihi la moyo wangu.
Mmh! Sawa.
Kuonesha Hans hataki kunichezea, wiki ijayo barua inakuja na baada ya majibu maandalizi ya harusi yanaanza mara moja. Kinachotakiwa vikao vya harusi visogezwe mbele ili michango ya harusi yangu na Colin iwe yangu na Hans. Hapo nina imani hakuna kitakacho haribika.
Sawa, siwezi kukuingilia kwa vile umeamua mwenyewe, ila kila aliyae hushika kichwa chake.
Mama hiyo misemo, ninachoshukuru nimepata tiba ya moyo wangu, kuna lingine?