Wakili wa Moyo-29
ILIPOISHIA:
Walikubaliana kuvuka upande wa pili, baada ya watu na baadhi ya magari kujaa ndani ya kivuko safari ya kuelekea Kigamboni ilianza. Kivuko kiliposimama upande wa Kigamboni, watu waliteremka na kuelekea maeneo tofauti ya Kigamboni, Mji mwema mpaka Geza Ulole na kwingineko.
SASA ENDELEA...
Brenda alitangulia baadaye aliliona gari la Hans likija nyuma, hakusimama aliendelea na safari mpaka karibia na kwa kina Mage alisimamisha gari pembeni Hans naye alisimamisha pembeni yake na kuteremka.
Hans na Brenda walikumbatiana na kupeana pole upya huku Brenda akiwa haamini kama Hans amepona.
"Dah! Pole sana."
"Asante."
"Sasa inakuwaje?"
"Fanya hivi, hili gari langu tuliache sehemu salama ili twende na lako tukifika utaingia ndani kwenda kumuita akija utamuingia kwenye gari lako najua atashangaa kuniona lakini nitatumia muda huo kuzungumza naye kisha atarudi ndani mwao na sisi tuondoke."
"Hakuna tatizo."
Hans alilipaki gari lake sehemu ya usalama na kuingia kwenye gari la Brenda hadi nyumbani kwao na Mage. Alipofika alilisimamisha gari pembeni ya geti hakutaka kuliingiza ndani na kuteremka. Mlinzi alishangaa kuliacha gari nje na kumuuliza.
"Da' Brenda mbona huingizi gari ndani?"
"Hapana sikai sana," Brenda alijibu huku akiingia ndani ya geti.
Alitembea kwa mwendo wa kukimbia hadi ndani, alimkuta msichana wa kazi akiondoa vyombo mezani na kumuuliza.
"Mage yupo wapi?"
"Chumbani kwake."
Alikwenda hadi chumbani na kugonga.
"Ingia," sauti ya Mage toka ndani ilisema.
Brenda alisukuma mlango na kuingia ndani, Mage alishtuka kumuona shoga yake muda ule, kwa vile hawakuwa na miadi ya kukutana muda ule wakati mchana wa siku ile walikuwa pamoja na kuachana jioni.
"He! Vipi mbona huku muda huu?" Mage alimshangaa Brenda.
"Shoga hebu twende nje mara moja."
"Kuna nini?"
"Utajua huko, we twende mara moja."
Mage bila kuongeza neno alinyanyuka kitandani na kuongozana na Brenda hadi nje, alishangaa kuona wanatoka nje ya geti. Lakini hakuhoji, alisubiri kuona Brenda kamuitia nini. Alipotoka nje ya geti aliliona gari la Brenda, kwa vile alikuwa akisubiri muda wa kwenda kwa Colin na alichelewa kwenda kutokana na mama yake kutoka alimwambia shoga yake.
"Brenda siwezi kufika mbali namsubiri mama ili niende kwa mume wangu."
"Hata huendi popote twende ndani ya gari."
"Kuna nini?"
"Hebu punguza maswali."
Waliongozana wote hadi kwenye gari.
"Ingia mlango wa nyuma," Brenda alimwambia Mage, naye hakubisha, aliingia.
Ndani ya gari kulikuwa na giza, Brenda baada ya kuingia mbele aliwasha taa na kumfanya Mage ashtuke kumuona Hans.
"Ha! Hans?"
"Ndiyo mimi Mage samahani kwa kukushtukiza."
"Bila samahani, kwanza unaendeleaje?"
"Namshukuru Mungu sijambo kabisa."
"Pole na kufiwa mke na mtoto."
"Asante, pole na wewe kutokana na ulichotendewa na familia yangu."
"Hans achana na hayo yameshapita, nina imani kuna kitu kimekuleta naomba tuzungumze kwa haraka nataka kwenda kwa mume wangu muda si mrefu."
Hans alijikuta akitulia huku maneno yakigoma kutoka mdomoni, Mage alishangaa kuona mpenzi wa zamani akitokwa na machozi. Brenda alitoka nje ya gari na kuwaacha wapenzi ndani ya gari wazungumze yao.
"Jamani nipo nje."
"Hakuna tatizo, usikae mbali natoka sasa hivi," Mage alisema.
Baada ya kutoka, Mage alimuuliza Hans aliyekuwa akitokwa machozi.
"Hans umeniita kuona machozi yako au kuna kitu kingine? Kama ni machozi nimeisha yaona, naomba niende zangu," Mage alizungumza kwa sauti ya upole huku akimtazama usoni Hans.
"Ma..ma..ge," Hans alisema kwa kigugumizi.
"Jina langu."
"Kilichonileta si kuja kukuonesha machozi bali moyo wangu umejaa maumivu makali."
"Najua inauma kupoteza mke na mtoto si kitu cha kawaida yataka moyo wa chuma kuyashinda maumivu yake lakini Mungu siku zote ni mfariji na atakufanya utayasahau yote kisha atakuletea mke mwingine."
"Mage mimi na wewe tuliahidiana nini?"
"Kuoana kuwa mke na mume."
"Baada ya matatizo ya familia yangu nilikueleza nini?"
"Ulisema huwezi kuzaa na yule mwanamke, baadaye utamuacha na kunioa mimi."
"Kwa nini umekubali kuolewa na mwanaume mwingine?"
"Kwa sababu umevunja ahadi yetu."
"Mage nina imani unajua jinsi gani ninavyokupenda?"
"Siyo unavyonipenda bali ulivyokuwa ukinipenda."
"Mage moyo wangu hautachoka kukupenda, nilikueleza nini baada ya kulazimishwa kuoa mwanamke mwingine?"
"Ulisema wakikulazimisha kuoa utajiua."
"Ulinishauri nini?"
"Nilikuwa radhi uoe lakini si kukupoteza maishani, ulichoniahidi ndicho kilinipa moyo na kuwa radhi kukusubiri hata miaka mia. Lakini wewe ndiye ulivunja mkataba na kuamini sina changu na kuamua nami kutafuta wangu japokuwa ilikuwa sawa na kunimezesha mfupa."
"Ndiyo sababu ya mimi kuja kuzungumza na wewe, baada ya kunisikiliza uamuzi utakaoutoa hapa sitapingana nao hata kama utaniumiza."
"Haya niambie hicho kilichokuleta."
Hans alianza kuzungumza kwa sauti ya chini yenye kisikika huku machozi yakiweka michirizi kwenye mashavu. Mazungumzo yalikuwa ‘off air' ambayo hayakutakiwa mtu yeyote kusikia zaidi ya watu wawili tu. Hans alimaliza kuzungumza huku machozi na kamasi zikimtoka chapachapa.
Itaendelea...........