Hadithi: Wakili wa moyo

mizambwa

JF-Expert Member
Oct 8, 2008
4,422
1,790
WAKILI WA MOYO...SEHEMU YA 1

Maumivu ya moyo hayana msaidizi na moyo wa kupenda hauna subira, kilichojificha moyoni huwa sawa na mfungwa asiye na kosa lakini hajui kujitetea. Siku zote anayependa kama muhusika hajui kama anapendwa huwa mateso ya kujitakia.

Cecilia msichana alinayetoka katika familia ya maskini anampenda Colin mvulana aliye katika familia ya kitajiri mwenye mchumba anayetaka kufunga naye ndoa. Anajikuta akiumia kila akimuona, pamoja na kuonekana jambo hilo kama maji kupanda mlima lakini msichana Cecy anauapia moyo wake kuwa atauwekea wakili na kuweza kushinda kesi ya maumivu ya mapenzi.

Je, atafanikiwa? Kuyajua yote ungana tena na mtunzi mahiri katika hadithi tamu ya mapenzi ili upate uhondo mwanzo mwisho.
TWENDE KAZI.....

Mama Cecy alishangaa kumuona mwanaye amerudi mapema huku sinia likiwa limejaa ndizi. alimalizia kupuliza moto wa kuni kisha alitoka jikoni huku akifuta machozi kwa upande wa khanga kutokana na moshi wa kuni kumuingia machoni. Alimtazama binti yake aliyekuwa amekaa chini huku ameshika tamaa na machozi kumtoka.

"Cecy nini tena mama?" alimuuliza huku akimsogelea.
"Mama hata nashindwa kujielewa sijui ni kwa nini inakuwa hivi?" alisema huku akiondoka mkono shavuni bila kufuta machozi.

"Una lingine au ni lilelile za siku zote?"

"Kuna lingine lipi mama yangu! Hata sijui kwa nini nimejiingiza kwenye mateso ya kumpenda Colin mtu ambaye hayajui mapenzi yangu kwake."

"Lakini kwa nini mwanangu unapenda kuota ndoto za mchana, wewe na Colin wapi na wapi kama mbigu na ardhi."

"Najua mama utasema hivyo lakini katika mapenzi hakuna kitu kama hivyo, nakuapia kwa Mungu Colin atakuwa mume wangu wa ndoa."

"Cecy mwanangu hebu achana na kujishugulisha na masuala ya mapenzi, hebu jiangalie ulivyo na alivyo Colin. Kwanza mwenzako hand same."

"Hata mimi beutiful girl," Cecy alijibu kwa kujiamini huku akinyanyuka na kujishika mkono kiunoni kujionesha kuwa ni mrembo.

"Mwenzio ana elimu ya chuo kikuu wewe darasa la saba la kufeli, mwenzako anatoka kwenye familia ya kitajiri wewe pangu pakavu tia mchuzi. Kingine ambacho kinafanya usiweze kabisa kumpa ni kuwa Colin ana mchumba na mipango ya harusi ipo karibuni sasa huyo Colin yupi wa kukuona?"

"Mama nina uhakika kwa asilimia mia Colin kunioa," Cecy alisema kwa kujiamini.

"Wee mtoto una wazimu? Au kuna mganga kakudanganya, maana siku hizi ushirikina hauna mtoto wala mzee."

"Mama katu mapenzi sitayaendelea kwa mganga, ila nitayapigania kwa nguvu zote."

"Kipi hasa kinakupa jeuri ya kusema hivyo?"

"Ipo siku nitakwambia lakini amini ndoa ya Colin na Mage haipo ila mimi ndiye mke wake."

"He he he heee, usinichekeshe miye, kwa nini unasema hivyo?" mama Cecy alicheka mpaka machozi yakamtoka.

"Mage hampenzi Colin."

"We umejuaje?"

"Ni historia ndefu mama."

Cecy alianza kumuhadithia mama yake sababu ya kuamini siku moja Colin atakuwa mpenzi japokuwa hajawahi kumtamkia kitu kama hicho hata siku moja.

Alianza toka siku ya kwanza kumuona Colin, Mage msichana aliyetoka katika familia ya kimaskini elimu yake ya dalasa la saba shuleni alikuwa mmoja wa wasichana wabuluza mkia.
Baada ya kufeli kwenye mtihani wa mwisho aliamua kufanya biashara ya ndizi kwa kupita mtaani kuuza. Japokuwa alikuwa maskini lakini alijipenda sana.

Baada ya kuuuza ndizi siku za mwanzo alinunua nguo nzuri ambazo alizivaa kila alipozunguka mkaani kuuza ndizi zake. Kitu kilichopelekea apendwe na wateja wengi kutokana na umalidadi wake na heshima kwa wote akiwemo mama Colin ambaye alikuwa mnunuzi wake mkubwa.

Nyumba ya mama Colin ilikuwa ndiyo iliyokuwa ikinunua ndizi nyingi kitu kilichomfanya Cecy aongeze mtaji. Mama Colin alitokea kumpenda sana na kumwita mkwe.

Siku moja alipitisha ndizi kama kawaida bila kujua kama nyumba ile ina kijana mzuri aliyekuwa nje amerudi baada ya kumaliza masomo yake. Baada ya kufika nje ya geti alibonyeza kengele na mlinzi alimfungulia mlango na kuingia ndani.

"Mwambie mama mkwe leo nimeleta ndizi za ukweli," alimwambia mlinzi aliyekuwa amemzoea sana.

"Mamkweee," Cecy alipaza sauti kama kawaida yake kila alipofika.

Mara alitoka mama Colin akiwa katika muonekano wa mtoko.
"Ha! Ma mkwe safari ya wapi tena?"

"Nampeleka mchumba wako mjini."

"Muongo, yupo wapi?"

Siku zote Cecy alipokuwa akipeleka ndizi alitaniwa na mama Colin kwa kuitwa mkwe japokuwa hakuwahi kumuona huyo mwanaume. Kila siku alikuwa na hamu ya kumuona japokuwa alikuwa akitaniwa.
"Jana usiku na ndege."

"Waawooo," Cecy aliruka juu kama anamfahamu.

Ghafla alinyamaza baada ya kumuona mvulana mzuri tenamtanashati akitoka ndani. Alibakia kama kapigwa shoti ya umeme kwa jinsi alivyosimama kwa mshangao kidole mdomoni.
"Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?" mama Colin alitania.

"Nimemuona mzuri," Colin alisema huku akimtazama Cecy aliyekuwa bado amesimama.

"Cecy umemuona Colin?"

"Ndi..ndi..yo," Cecy alipatwa na aibu na kushindwa kuzungumza.

"Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini."

"Sawa mkwe."

Mama Colin alifungua pochi na kutoa noti ya elfu tano na kumpatia Cecy, wakati huo Colin alikuwa akilisimamisha gari pembeni ya mama yake. Mama Colin alifungua mlango wa gari wa nyuma na kuingia.
"Bai mchumba," Colin alimuaga Cecy aliyekuwa ameingiwa aibu.

"Bai," Cecy alisema huku akiangalia pembeni.

Geti lilifunguliwa na gari lilitoka nje kuelekea mjini na kumuacha Cecy akitoa ndizi kwa msichana wa kazi kisha alitoka na kuendelea kufanya biashara kama kawaida.
****
Safari ya mama Colin na mwanaye ilikuwa kwenda nyumbani kwao Mage msichana aliyemchagua kuwa mke wa mwanaye. Alimuona siku moja alipokuwa na mama yake walipokutana na shoga yake Super Market, wakati akiwa katika manunuzi ya bidhaa muhimu.

"Ha! Shoga za siku?" Mama Colin alimsemesha mama Mage.

"Nzuri shoga, za kupotezana?"

"Mmh! Nzuri, vipi Colin bado hajarudi?"

"Anarudi mwezi kesho mwishoni."

"Shikamoo," Mage alimwamkia mama Colin.

"Marahaba, hujambo mama?"

"Sijambo."

"Monika, binti yako?" mama Colin alimuuliza shoga yake.

"Ndiyo amemaliza chuo kikuu Mlimani anasubiri ajira."

"Nimempenda sana, unafaa kuwa mke wa Colin."

"Tena wataendana wasomi kwa wasomi," mama Mage aliunga mkono.

"Anaitwa nani?"

"Mage," Mage alijibu mwenyewe.

Tokea siku ile wakawa wakiwasiliana hata kutembelea huku wakisubiri muda wa Colin kurudi toka masomoni ili wapange mipango ya ndoa. Mama Colin alimpenda sana Mage kwa umbile lake nzuri na heshima aliyoionesha siku zote kwake. Naye mama Mage alifurahi mwanaye kuolewa na Colin kutokana na kumfahamu vizuri.

Siku Colin aliyofika hakutaka kuwajulisha, kesho yake alimpeleka nyumbani kwao Mage bila taarifa ili wafanye surprise. Familia ya kina Mage ilikuwa ikikaa Kigamboni walikwenda hadi kwao na kupiga honi nje ya geti. Wakati wote huo Colin alikuwa hajui anakwenda wapi.
Baada ya geti kufunguliwa Colin aliliingiza gari ndani na kwenda kulipaki kwenye maegesho. Mama Mage alitoka nje baada ya kusikia gari likingia ndani na kujiuliza nani amekwenda kwake bila taarifa. Alishtuka kumuona mama Colin akiteremka kwenye gari.

"Waawooo jamani, ha! Colin siamini jamani karibu mwanangu," alikuwa akimfuata mama Colin kumkumbatia lakini aligeuza baada ya kumuona Colin na kwenda kumkumbatia.


Itaendelea...............
 
WAKILI WA MOYO.... SEHEMU YA 2
ILIPOISHIA:
Tangu siku ile wakawa wakiwasiliana hata kutembeleana huku wakisubiri muda wa Colin kurudi kutoka masomoni ili wafanye mipango ya ndoa. Mama Colin alimpenda sana Mage kwa umbile lake nzuri na heshima aliyoionesha siku zote kwake. Naye mama Mage alifurahi mwanaye kuolewa na Colin kutokana na kumfahamu vizuri.

Siku Colin aliyofika hakutaka kuwajulisha, kesho yake alimpeleka Mage nyumbani kwao bila taarifa ili wafanye ‘surprise'. Familia ya akina Mage ilikuwa ikikaa Kigamboni, walikwenda hadi kwao na kupiga honi nje ya geti. Wakati wote huo, Colin alikuwa hajui anakwenda wapi.

Baada ya geti kufunguliwa, Colin aliliingiza gari ndani na kwenda kulipaki kwenye maegesho. Mama Mage alitoka nje baada ya kusikia gari likingia ndani na kujiuliza nani amekwenda kwake bila taarifa. Alishtuka kumuona mama Colin akiteremka kwenye gari.

"Waawooo jamani, ha! Colin siamini jamani karibu mwanangu," alikuwa akimfuata mama Colin kumkumbatia lakini aligeuza baada ya kumuona Colin na kwenda kumkumbatia.
SASA ENDELEA...


Colin alijikuta akishangaa baada ya kuteremka kwenye gari na kujiuliza pale ni wapi na yule aliyemfurahia na kumkumbatia ni nani.
"Asante, shikamoo."

" Marahaba karibu sana mwanangu," mama Mage alisema kwa furaha huku amemshika mabegani Colin na kumtazama.
Aliwapokea wageni na kuingia nao ndani sebuleni, baada ya kukaa alimwita Mage kwa sauti.

"Mageee."

"Abee mama," sauti ya Mage ilitoka chumbani.

" Njoo mara moja."

"Nakuja."

Mage alikuja mbio bila kujua anaitiwa nini, alipofika alishtuka kumuona mama Colin.
"Ha! Mamamkwe."

"Nimejaa tele," mama Colin alijibu kwa tabasamu pana.

"Shikamoo."

"Marahaba."

"Mambo?" Mage alimsabahi Colin bila kumjua.

"Poa za hapa?"

"Nzuri," Mage alijibu huku akishtuka na kujiuliza yule kama ndiye Colin. Ili kupata uhakika, aliomba msamaha na kutoka mara moja.

"Jamani samahanini nakuja mara moja."

"Bila samahani," alijibu mama Colin.

Alichepua mwendo na kwenda upande wa vyumba huku akimwambia mama yake.
"Mama njoo mara moja."

"Jamani samahanini nakuja mara moja."

"Hakuna tatizo," mama Colin alijibu.

Baada ya mama Mage kuondoka kumfuata mwanaye, mama Colin alimsemesha mwanaye kwa sauti ya chini.
"Mchumba unamuonaje?"

"Yupo vizuri."

"Umempenda?"

"Sana."

"Nimefurahi kuona chaguo langu umelikubali."

"Unajua kuchagua."

Mama Mage baada ya kufika kwa mwanaye aliyekuwa amesimama upande wa vyumba, mambo yakawa hivi;
"Vipi?" alimuuliza mwanaye.

"Safi, eti mama yule si ni Colin?"

"Ndiyo."

"Mamaaa! Kwa nini hukuniambia mapema nijiandae, anaweza kuniona sijipendi."

"Walaa mbona umependeza, vipi umempenda?"

"Ndiyo," Mage alikubali huku akinyanyua kichwa.

"Basi turudi."

"Naona aibu ngoja nikaoge na kubadili nguo."

Mama Mage aliwarudia wageni wake ili kuwapatia kinywaji kabla ya kuanza mazungumzo.
***
Mage, msichana mwenye elimu ya chuo aliyekuwa na shahada ya Uhusiano, baada ya kuachana na mama yake alikwenda chumbani kwake ili kujiandaa kuonana na wageni. Kwanza, alikwenda kuoga kisha alibadili nguo ambayo aliamini ni sahihi kwa ajili ya kumpokea mgeni wake.

Alijipulizia manukato ya bei mbaya aliyonunuliwa na baba yake alipokwenda Ufaransa kikazi. Alisimama mbele ya kioo kikubwa cha ndani na kujitazama kisha kujigeuza kila pembe. Baada ya kuridhika na gauni alilovaa alikisogelea kioo na kujitazama jinsi Mungu alivyomuumba kwa uzani unaolingana, alijikuta akitokwa machozi.

Aligundua kuna mapungufu kichwani mwake, alikwenda mpaka kwenye ‘dresing table' na kukaa kwenye kiti kidogo kisha alivuta droo na kutoa wanja. Alipaka wanja mwembamba ulioongeza uzuri wa sura yake.
Alichukua hereni ndogo na kuvaa kisha alichukua cheni yake ndogo ya dhahabu na kuivaa, kidani chenye jina lake kilikaa kwenye mfereji wa matiti yaliyojaa na kumfanya apendeze zaidi.
Mage aliamini mpaka pale alikuwa amekamilika kwenda mbele ya wageni wake ambao walikuja mahususi kwa ajili yake.

Alikwenda kwenye kabati na kutoa kiatu cha kisigino kifupi cha rangi ya machungwa kilichoendana na rinda la chini la gauni lake alilovaa lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na weupe kwa mbali.
Hakika Mage alikuwa amependeza kama malkia aliyekuwa tayari kuonana na mfalme. Alitembea kwa madaha kutoka chumbani kwake kuelekea sebuleni palipokuwa na wageni.

Harufu ya manukato yake ilitangulia kabla yake. Colin na mama yake waligeuza macho kuangalia upande wa chumba na kukutana na Mage aliyetokeza akiwa amependeza maradufu na awali alivyokuwa.
Moyo wa Colin ulipasuka vipande na kuwa hoi kwa uzuri wa Mage, msichana chaguo la mama yake. Alijikuta akijiuliza kwa hali ile, mama yake ni mwanamke, amejua kuchagua binti mrembo kama yule, je, angekuwa mwanaume angekuwa na uwezo gani wa kuchagua wanawake warembo?
Mama Colin alitulia kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme hata kupepesa macho alishindwa kutokana na uzuri wa Mage, mkwewe mtarajiwa.

"Wageni karibuni sana, huyu mnayemuona ndiye Magreth halisi."

"Asante. Tunashukuru kukutambua," Colin alijitahidi kuitikia japo mwili ulipoteza ujasiri wa kiume baada ya kuingiwa baridi la mshtuko.
"Mama zangu samahanini namuomba mgeni
wangu," Mage alisema huku akisogea kwa Colin na kumshika mkono.
Colin alinyanyuka na kukiacha kinywaji chake juu ya meza ndogo, lakini Mage alikichukua na kukishika mkono wa kushoto huku wa kulia akimshika mkono Colin na kuondoka naye kuelekea nyuma ya nyumba kwenye bustani.

Walivyokuwa wakitembea, wazazi wao waliwasindikiza kwa macho mpaka walivyopotea kwenye macho yao. Waligeuka na kutazamana kisha walitabasamu.

"Yaani walivyopendeza nilitamani leo ndiyo iwe siku ya ‘send-off' ya mwanangu," mama Mage alisema kwa hisia kali.

"Kila kitu kina wakati wake, kilichonifurahisha mimi ni jinsi walivyoonekana kupendana. Wasiwasi wangu huenda Mage asingempenda Colin."

"Isingekuwa rahisi, Colin ni mmoja wa vijana wazuri ambao Mungu kawajalia. Nitajivunia kuwa na mkwe kama yeye, nitatembea kifua mbele."

Upande wa pili, Mage alimpeleka Colin mpaka kwenye bustani.
"Karibu kwenye kiti mgeni wangu," Mage alimkaribisha kwenye kiti cha uvivu na meza ndogo katikati ya kuwekea vinywaji. Mage kabla ya kukaa alikumbuka amesahau kinywaji chake.

"Sorry Colin nakuja nimesahau kinywaji changu," Mage alisema huku akigeuka ili arudi ndani.

"Mage," Colin alimwita Mage aliyeanza kwenda ndani.

"Abee," Mage alitikia huku akigeuka kumsikiliza Colin.

"Kinywaji hiki kinatutosha."

"Mbona kidogo, hakitutoshi."

"Kinatutosha, kwangu wewe ni zaidi ya kinywaji."

"Colin nimefurahi kufahamu hilo."

Mage alirudi na kukaa pembeni mwa Colin. Baada ya kukaa, Colin alibeba glasi iliyokuwa na kinywaji na kumnywesha Mage ambaye alisogeza mdomo kuipokea.

Itaendelea baadaye.......
 
WAKILI WA MOYO - SEHEMU YA 3



Upande wa pili Mage alimpeleka Colin mpaka kwenye bustani.
"Karibu kwenye kiti mgeni wangu," Mage alimkaribisha kwenye kiti cha uvivu na meza ndogo katikati ya kuwekea vinywaji. Mage kabla ya kukaa alikumbuka amesahau kinywaji chake.
"Sorry Colin, nakuja nimesahau kinywaji changu," Mage alisema huku akigeuka ili arudi ndani.
"Mage," Colin alimwita Mage aliyeanza kwenda ndani.
"Abee," Mage alitikia huku akigeuka kumsikiliza Colin.
"Kinywaji hiki kinatutosha."
"Mbona kidogo hakitutoshi."
"Kinatutosha, kwangu wewe ni zaidi ya kinywaji."
"Colin nimefurahi kusikia hivyo."
Mage alirudi na kukaa pembeni ya Colin, baada ya kukaa Colin alibeba glasi iliyokuwa na kinywaji na kumnywesha Mage ambaye alisogeza mdomo kuipokea.
SASA ENDELEA...

Baada ya kumeza funda la juisi, alimumunya midomo yake mipana na kusema:

"Colin, leo ni siku yetu ya kwanza kuonana lakini umenifanya nikuone mwenyeji katika moyo wangu. Nasikia fahari kuwa mkeo," Mage huku akimtazama kwa macho yake makubwa kidogo yaliyoongezwa uzuri na wanja aliojipaka.

"Nashukuru kwa hilo," Colin alijibu huku akiachia tabasamu pana.

"Lakini nina wasiwasi mmoja ambao umekuwa ukisumbua moyo wangu na kuukosesha amani," Mage alisema huku uso wake ukionesha huzuni.

"Wasiwasi wa nini Mage?"

Colin aliuliza huku akijiweka vizuri kitini na kuiweka glasi ya juisi juu ya meza kisha alipeleka mkono kwenye nywele fupi za kipilipili na kuzichezea, kitu kilichomfanya Mage asisimke.

"Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda."

"Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.
"Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza," Colin alisema huku amemshika mabegani Mage na kumtazama usoni kwa jicho la huruma.

"Vitu gani hivyo Colin?" Mage aliuliza huku akijitahidi kuyatoa macho nje kama anaweza kuyaona maneno kwa macho.

"Kila umbile na sura niliyoiwaza ambayo niliamini huenda mojawapo itakuwa yako, imekuwa kinyume kabisa."

"Mmh! Colin, kwa nini?"

"Mage we' ni mzuri wa wazuri, mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako," Colin alisema akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza anamaanisha.

"Siamini, Colin siamini," Mage alisema akiwa amemshika kifuani Colin huku machozi yakimtoka.

"Mage huamini nini?"

"Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako," Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.

"Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu unavyochukua uhai wa mtu ghafla."

"Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani," Mage alisema huku akijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.

"Kwa nini mpenzi?"

"Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu."

"Sijakuelewa mpenzi."

"Umeweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji. Boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung'olewa jino bila ganzi."

"Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema."

"Nami nakuahidi kuwa mke mwema."

Baada ya hapo mazungumzo yaliendelea kila mmoja kutaka kumjua mwenzake kiundani mpaka muda ulipofika wa kuondoka.
Colin akiwa mtu mwenye furaha na mama yake, waliondoka na kuwaacha Mage na mama yake nje baada ya kuwasindikiza wageni. Walirudi ndani mtu na mama yake wakishikana mikono.
Walipoingia ndani, Mage alimuuliza swali mama yake.

"Mama, kweli Colin atanioa?" alimuuliza huku akimkazia macho.

"Mbona umeniuliza hivyo, kwani mmezungumza nini?"

"Amenihakikishia atanioa."

"Sasa wasiwasi wako nini?"

"Mama anaweza kuwa na mwanamke mwingine na kuniacha njia panda kama alivyofanya Hans. Najiona nimefanya haraka sana kumkubali Colin bila kujua historia yake. Safari hii sitakubali kuumizwa mara mbili, lazima nitaua tu," Mage alisema kwa hisia kali.

"Kwa hiyo ukigundua Colin ana mwanamke mwingine utamuua?"

"Siwezi kumuua Colin bali mwanamke wake."

"Lakini Hans alikuwa akikupenda tatizo wazazi wake ndiyo waliomchagulia mwanamke mwingine."

"Mama, Hans hakuwa ananipenda ni muongo mkubwa."

"Kwa nini?"

"Alisema anamuoa yule mwanamke kuwafurahisha wazazi wake tu, ila hatakaa naye muda mrefu atamuacha. Lakini mwezi jana nilikutana na yule mwanamke akiwa mjamzito."

"Ndiyo basi tena, nawe umepata wako tena kijana mzuri msomi mwenzako," mama Mage alisema huku akijenga tabasamu.

"Mama bado inaniuma sana, niliutoa mwili wangu kwa Hans kwa kujua ndiye atakayekuwa mume wangu. Mama simjui mwanaume yeyote zaidi yake.

"Nilijitunza kwa ajili yake matokeo yake alinidanganya ataachana na yule mwanamke aliyelazimishwa kuoa.

"Mama, nilimuamini lakini mwezi ulioisha nilijikuta nikimchukia Hans zaidi ya mauti baada ya kumuona yule mwanamke wake ni mjamzito. Imeniuma sana mama, nakuahidi sitamsamehe Hans na sitakubali kuchezewa tena na Colin, nitakufa mimi au yeye," alisema Mage

"Mage mwanangu, ya Hans tuliyazungumza tukayamaliza. Hili lingine kabisa."

"Mama hujui kiasi gani nilivyoumia Hans kuoa, lakini alinituliza na kusema kuwa ataachana na mpenzi wake ili anioe. Lakini nilichokiona niliwaza mbali sana mama.

"Leo nakupa siri niliyoificha moyoni."


Itaendelea...................
 
WAKILI WA MOYO - 4


"Nilimuamini lakini mwezi ulioisha nilijikuta nikimchukia Hans baada ya kumuona yule mwanamke mjamzito. Imeniuma sana mama nakuahidi sitamsamehe Hans na sitakubali kuchezewa tena na Colin nitakufa mimi au yeye," Mage alibadili uzuri wake wote ulipotea alikuwa kama akipigana na mtu.
"Mage mwanangu, ya Hans tuliyazungumza tukayamaliza."
"Mama hujui kiasi gani nilivyoumizwa na Hans kuoa, lakini alinituliza na kusema kuwa ataachana na mpenzi wake ili anioe. Lakini nilichokiona niliwaza mbali sana mama."
SASA ENDELEA...

"Leo nakupa siri niliyoificha moyoni, siku niliyokutana na mke wa Hans mjamzito, nilinunua vidonge na pombe kali ambavyo nilipanga kunywa usiku ili asubuhi ukiamka ukute maiti.

"Usiku ulipoingia niliandaa vitu vyote kwa ajili ya kuutoa uhai wangu, kabla ya kufanya tendo lile nilikumbuka kauli ya profesa mmoja wakati tupo chuoni, kuwa thamani yangu haipo kwa mtu mmoja bali ya ulimwengu mzima kwa hiyo nisipoteze uhai wangu kwa kosa la makusudi bali niitazame thamani yangu mbele ya jamii.

"Mama nililia sana na kuchukua vitu vyote na kwenda kuvitupa. Huwezi kuamini nilimchukia Hans kama kifo. Ujio wa Colin umenishtua na kuona kama maumivu mengine yanakuja."

"Mage mwanangu naiamini familia ya kina Colin uzuri mama yake kakuchagua."

"Mama! Ngoja tuone."

Mage alisema huku akielekea chumbani kwake.

***
Cecy baada ya kufanya biashara yake, iliisha mapema na kurudi nyumbani akiwa mwenye furaha. Mama yake alijua furaha ile ni kwa ajili kumaliza bishara mapema, kumbe sivyo. Usiku ulipoingia aliwahi kula, baada ya kuoga alipanda kitandani mapema.

Kitendo kile kilimshtua mama yake na kuamini mwanaye labda anaumwa. Mama Cecy baada ya kumaliza kazi zake, alimfuata mwanaye chumbani na kumkuta akiwa amejilaza chali mikono ameilalia kwa nyuma.

Mpaka anaingia chumbani, Cecy alikuwa ametulia macho kayaelekeza juu. Mama yake alitulia akimuangalia na kumuona mwanaye yupo katika lindi la mawazo, jambo ambalo halikuwa la kawaida kuliona kwa mwanaye.

Baada ya muda, alimuona akitabasamu na kujikuta akitazama juu labda kuna kitu mwanaye anakitazama na kumfurahisha, lakini hakuona kitu. Alijiuliza kipi kilichomfanya mwanaye awahi kitandani kisha kutulia akitazama juu na kutabasamu?

Baada ya kutabasamu alimuona akishika mikono kifuani na kusema kwa sauti ya chini ambayo mama yake aliisikia.

"Cecy mimi, mmh! Sijui?"

Baada ya kusema vile aligeukia ukutani na kumpa mgongo mama yake aliyekuwa amesimama mlangoni bila kumuona.

"Cecy..Cecy," mama yake alimwita.

"A..a..bee," Cecy aliitikia huku akigeuka kumtazama mama yake na kumshangaa kumuona amesimama mlangoni.

"Vipi mama?" alimuuliza bila kunyanyuka zaidi ya kujigeuza.

"Unajua leo sikuelewi kabisa."

"Kivipi?" Cecy alijibu huku akikaa kitako.

"Umewahi kupanda kitandani si kawaida yako, nimefika muda nimekuona ukitazama juu na kutabasamu peke yako. Kisha unazungumza peke yako, una nini leo mwanangu?"

"Mama nipo kawaida, siku hazilingani."
"Kipi kilichokupa furaha leo?"

"Mama nawaza kama siku moja nitaweza kuolewa na mwanaume mzuri mwenye uwezo tena mwenye mapenzi ya dhati, nitafurahi sana."

"Utapata tu mwanangu, Mungu hawezi kutunyima vyote."

"Asante mama yangu kwa kunipa moyo."

"Lakini huna tatizo lolote?"

"Sina mama yangu."

"Haya mwanangu usiku mwema."

"Na wewe pia mama yangu."

Mama Cecy aliondoka na kurudi chumbani kwake kulala na kumuacha mwanaye akirudi kujilaza kama mwanzo macho yake yakiangalia juu.
Alijikuta akikumbuka kauli y
a mama Colin baada ya Colin kutoka ndani; mwanaume mzuri ambaye alikuwa na kila sababu ya kujivunia kama akiwa mumewe au mpenzi wake.
Alikumbuka jinsi alivyoshtuka baada ya kumuona Colin. Kauli ya mama Colin ilijirudia kichwani mwake.

"Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?"

"Nimemuona mzuri."

"Cecy umemuona Colin?"

"Ndi..ndi..yo," Cecy alikumbuka alikipata kigugumizi na kuugua ugonjwa wa mapenzi ghafla.

"Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini."

"Sawa mkwe."

Cecy alijiuliza kauli ile ya mama Colin ilikuwa na ukweli gani kutokana na kuona kuolewa na Colin sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.

"Mbona sielewi, kweli Colin atanioa au ananitania, mbona hakukataa mbele ya mama yake? Kwa nini mama yake aendelee kuniita mkwe?" Cecy alijiuliza bila kupata jibu la moja kwa moja. Lakini wasiwasi wake ikawa kwenye hali zao yeye muuza ndizi anazurura mitaani na mwenzake mtoto wa kitajiri.

"Watakuwa wananitania," alisema kwa sauti ya kukata tamaa na kugeukia ukutani kuutafuta usingizi.
Usiku ulikuwa mrefu kwake baada ya kushtuka katikati ya usingizi kutokana na ndoto aliyoota akiwa na Colin ndani ya gari yeye akiwa anafundishwa kuendesha na baada ya hapo walikwenda ufukweni kupumzika. Wakiwa wamejilaza ufukweni, Cecy alitembeza mikono yake kwenye kifua cha Colin kilichojaa kimazoezi na vinyweleo vingi ‘garden love.' Upepo mwanana wa bahari uliwapepea.

Badala yake alishtuka na kujiona yupo kitandani peke yake, mapigo ya moyo yalimwenda mbio na kijasho chembamba kilimtoka. Alikaa kitandani na kujiuliza ndoto ile ina maana gani?

Aliwasha taa na kukaa kitandani mkono shavuni akijitahidi kujua ndoto ile ilikuwa na maana gani. Mama yake aliyeshtuka usingizi, naye alishtuka kuona taa inawaka, alijiuliza usiku ule Cecy alikuwa akifanya nini.
Alinyanyuka taratibu na kwenda chumbani kwa mwanaye. Kwa vile chumba hakikuwa na mlango zaidi ya pazia la kitenge kichakavu, alipofika alifunua taratibu na kuangalia ndani.

Alimkuta mwanaye amekaa kitandani mkono shavuni. Alitulia kwa muda bila kumsemesha na kutaka kujua mwisho wake nini. Baada ya muda kidogo, Cecy alizima taa na kujilaza kitandani.


Ndoto hiyo ilikuwa na maana gani? Itaendelea............
 
WAKILI WA MOYO - 5


Alinyanyuka taratibu na kwenda chumbani kwa mwanaye. Kwa vile chumba hakikuwa na mlango zaidi ya pazia ya kitenge kichakavu, alipofika alifunua taratibu na kuangalia ndani.

Alimkuta mwanaye amekaa kitandani mkono shavuni. Alitulia kwa muda bila kumsemesha na kutaka kujua mwisho wake nini. Baada ya muda kidogo, Cecy alizima taa na kujilaza kitandani.
SASA ENDELEA...

Mama yake aliendelea kusimama mlangoni kwa muda huku akiwa na maswali na hali ya mwanaye toka jana yake. Aliamua kurudi chumbani kwake na kupanga kumuuliza siku ya pili kwa kumbana sana ili ajue sababu ya kuwa katika hali ile ambayo kwake ilikuwa ngeni.
***
Colin akiwa chumbani kwake amejilaza kitandani, aliukumbuka uzuri wa Mage msichana aliyeonekana mwelewa lakini mwenye jeraha la mapenzi. Sifa zake za elimu ya juu pia urembo na ucheshi ni vitu vilivyomteka kimwili na kiakili.

Moyoni alijiapiza kumpenda Mage kwa moyo wake wote, aliiona familia bora mbele yake yeye akiwa baba, Mage mama na watoto wao wawili wa kike na kiume.

Siku zote alipanga kuzaa watoto wachache ambao angewamudu kuwahudumia kimalazi na elimu. Hakupenda kuwa na familia kubwa japokuwa wao walizaliwa sita, lakini yeye alitaka watoto wawili wakizidi basi wanne.

Alitaka ndoa yake ifanyike haraka ili kujipanga kwa maisha mapya. Wazo lake la kuanzisha kampuni aliliona litakwenda vizuri kama Mage mwanamke mwenye shahada ya uhusiano akiwa mkewe ambaye angesaidia kampuni yake kukua na kutanuka.

Moyoni alimshukuru mama yake kuwa na jicho la tatu kumtafutia mwanamke ambaye hakuwa tofauti na samaki anayekaa kwenye maji marefu kwani bila kuwa na chombo madhubuti huwezi kumpata.
Alijikuta akiyakumbuka maneno mawili ya Mage ambayo yaliuumiza moyo wake na kuamini ana deni kubwa kwa msichana yule:

"Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako," Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.
Baada ya kumhakikishia anampenda kwa dhati, alimpa mtihani ambao Colin aliamini anauweza kwa vile hakuwa mwanaume kigeugeu.

" Colin umeweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung'olewa jino bila ganzi."

Baada ya kuyakumbuka maneno ya Mage, Colin alijiapiza kuwa tiba ya maumivu aliyoyapata siku za nyuma. Aliamini maumivu yale yalikuwa na sababu ya kuwakutanisha ili wajenge familia bora. Usingizi mororo ulimpitia huku akitabasamu.
***
Asubuhi Cecy aliamka kama kawaida na kwenda kwenye gulio kununua ndizi za kuuza. Mama yake aliposhtuka alikuta ameshatoka muda. Baada ya kupata ndizi alirudi nyumbani na kuzipanga kwenye beseni kisha alikwenda kuoga na kutafuta nguo nzuri ambayo aliiteua kwa ajili ya kanisani tu.
Hakutoka kama siku nyingine anazokwenda kwenye biashara. Alitumia muda mwingi kujipamba zaidi ya siku ya Jumapili akienda kanisani.

Baada ya kuhakikisha amependeza sana, alitoka kwa ajili ya kwenda kuuza ndizi. Mama yake alishtuka kumuona mwanaye kwenye hali ile aliingiwa wasiwasi labda mwanaye ana safari nyingine si kwenda kufanya biashara.

"Cecy safari ya wapi?"

"Kwenye biashara mama."

"Kwenye biashara! Ndiyo uvae vizuri hivi?"

"Basi tu leo nimeamua."

"Si kweli toka jana sikuelewi kabisa, sasa nimeanza kupata mwanga."

"Mwanga gani mama?" Cecy alishtuka.

"Si bure lazima utakuwa umepata mwanaume, Cecy angalia mwanangu, we bado mdogo usijishughulishe na wanaume mwisho wake mbaya."

"Mamaaa!" Cecy alimshangaa mama yake.

"Unashangaa nini, ndiyo maana eti unatamani kuolewa kumbe una mwanaume," mama Cecy alizungumza ameshika pua.

"Maama...mama kwa nini unanihukumu bila kosa?" Cecy alimlalamikia mama yake.

"Huna kosa, haya endelea ukiniletea tumbo hapa utatafuta mbeleko ya kunibebea."

"Mama yangu sijawaza kufanya hivyo, japokuwa nami napenda siku moja niolewe na mwanaume mwenye mapenzi ya dhati si kuanza mapenzi kihuni."

"Haya kipi kilichokufanya uvae nguo ya kanisani kwenda kuuzia ndizi na kujipamba kupita kiasi?"

"Mama nikueleze mara ngapi siku hazilingani."

"Mmh! Haya biashara njema."

"Asante mama."

Cecy alibeba ndizi zake na kuelekea kwenye biashara zake. Hakutaka kupita popote mpaka kwa mama Colin ndipo alipopanga kuanzia biashara yake kwa siku ile. Alipofika kama kawaida alibofya kengele na mlinzi alimfungulia.

"Ha! Cecy mbona umependeza hivyo?" mlinzi alimshangaa Cecy.

"Mbona kawaida yangu," Cecy alisema huku akiingia ndani ya geti, aliweka ndizi chini na kumwita mama Colin kwa sauti ya juu.

"Mamkweee nimeshafika."

Colin ndiye aliyetoka kufuata ndizi kutokana na wasichana wa kazi kuwa na majukumu mengine. Macho yake yalishtuka kumuona Cecy.

"Ha! Mchumba ni wewe?"

"Ndiyo mpe...," Cecy hakumalizia aliingia kigugumizi.

"Karibu sana."

"Asante."

Colin alinunua ndizi na kumlipa fedha yake.

"Mama mkwe yupo wapi?"

"Anatoka sasa hivi."

Mara alitoka mama Colin, Cecy baada ya kumuona alimsalimia kwa kuchuchumaa chini kuonesha heshima.


Itaendelea..............
 
WAKILI WA MOYO - 6


Colin ndiye aliyetoka kufuata ndizi kutokana na wasichana wa kazi kuwa na majukumu mengine. Macho yake yalishtuka kumuona Cecy.
"Ha! Mchumba ni wewe?"
"Ndiyo mpe...," Cecy hakumalizia, aliingia kigugumizi.
"Karibu sana."

"Asante."
Colin alinunua ndizi na kumlipa fedha yake.
"Mama mkwe yupo wapi?"
"Anatoka sasa hivi."
Mara alitoka mama Colin, Cecy baada ya kumuona alimsalimia kwa kuchuchumaa kuonesha heshima.
SASA ENDELEA...

"Shikamoo mkwe."

"Marahaba mkwe wangu, hujambo?"

"Sijambo."

"Nyumbani?"

"Wanakusalimia."

"Mkwe una safari nyingine?" mama Colin alimuuliza Cecy.

"Kwa nini mama mkwe?"

"Umependeza sana."

"Hapana nipo kwenye biashara, mwanamke kujipenda bwana," Cecy alisema kwa pozi.

"Hongera, nina wasiwasi mwanangu anaweza kuibiwa."

"Walaa, Colin mpenzi nipo kwa ajili yako na wewe ndiye utakuwa mwanaume wangu wa kwanza."

"Muongo! Usimdanganye mwanangu," mama Colin alisema.

"Kweli ma'mkwe."

"Mchumba umenifurahisha sana, kesho ukija nitakupa zawadi," Colin alisema.

"Zawadi gani?"

"Utaiona hiyo kesho."

"Mmh! Asante."

"Unakubali tu, hujui zawadi gani?" mama Colin alitania.

"Yoyote atakayonipa, zawadi haipangwi."

Baada ya manunuzi, Cecy aliondoka kuendelea na biashara zake. Colin na mama yake walirudi ndani, baada ya kuweka ndizi jikoni alirudi sebuleni alipokuwa amekaa mama yake.
Alipofika alikaa pembeni ya mama yake aliyekuwa yupo bize na simu. Baada ya kuachana na simu, Colin alimuuliza mama yake: "Mama unajua Cecy ni mzuri?"

"Ni kweli mwanangu, Cecy ni binti mzuri sana," mama yake alimuunga mkono.

"Tena anajipenda, ana tofauti na wasichana wengi wanaofanya biashara kama yake. Hali ile anauza ndizi yupo vile, akifanya kazi za ofisini itakuwaje?" Colin alisema huku akimtazama mama yake aliyejenga tabasamu kutokana na maneno ya mwanaye.

"Ni kweli, ndicho kitu kilichonifanya nipende kununua biashara yake. Toka nimfahamu, sijawahi kumuona mchafu."

"Sasa kipi kilichokufanya umwite mkwe?" Colin alimuuliza mama yake akiwa amemkazia macho.

"Nilitokea kumpenda sana binti yule na kutamani awe mkwe wangu lakini alikosa sifa muhimu."

"Zipi mama?"

"Kwanza elimu yake darasa la saba tena la kufeli, pia anatoka katika familia ya kimaskini."

"Tabia yake?"

"Kwa kweli binti yule ana tabia nzuri sana, ila tatizo ni hilo. Kama angekuwa na sifa angalau ya elimu ya kidato cha sita au chuo kama Mage, basi yeye ndiye alikuwa chaguo langu la kwanza."

"Kweli mama, Cecy ni mzuri, lazima nikusifie. Unajua kuchagua wasichana wazuri."

"Nataka mwanangu mwanamke utakayemuoa basi moyo wako utabasamu kila ukimuona."

"Nashukuru kwa hilo mzazi wangu."
***
Kama kawaida, Cecy baada ya biashara zake, usiku aliwahi kuoga na kula kisha kuwahi kitandani. Alitaka kupata muda wa kuyatafakari yote aliyokutana nayo mchana. Mama yake hakutaka kupoteza wakati, alimfuata na kumwita ili ajibiwe maswali yanayomsumbua mwanaye.

"Cecy."

"Abee mama."

"Tabia gani uliyoanzisha, ukimaliza kula unawahi kitandani?"

"Mama kazi ya kuzurura na ndizi inachosha."

"Umeanza leo?"

"Mama siku hazilingani."

"Hebu njoo."

Cecy kwa mara ya kwanza alimuona mama yake anamsumbua kwa kumnyanyua kitandani wakati yeye alitaka kuzama kwenye dunia nyingine ya kufikirika, yenye raha zisizo na kikomo.
Alitoka ndani akiwa amekunja uso kitu ambacho mama yake alikigundua na kumuonya:
"Tabia ya kukasirika nikikuita imeanza lini?"

"Mama nimechoka."

"Hata ukichoka hujawahi kunikunjia uso, hebu njoo hapa."

Cecy alikaa kwenye kigoda pembeni mwa mama yake huku ajitahidi kuficha hasira alizokuwa nazo.
"Umepata mwanaume?" mama yake alimuuliza kwa sauti kavu.

"Hapana mama."

"Cecy, mi mtu mzima nimeona jua kabla yako, wasichana wakipata wanaume hujenga kiburi na kujiona wapo sawa hata na wakubwa zao."

"Haki ya Mungu sijapata mwanaume."

Mama yake alimweleza yote aliyoyaona kwa mwanaye usiku wa kuamkia siku ile.
"Haya bisha, ninakusingizia?"

"Najua utasema hivyo, lakini mama sina mwanaume ila kuna mtihani moyoni mwangu wenye majibu tata."

"Mtihani gani?"

Cecy alimuelezea ukaribu wake na mama Colin wa kuwa mteja mzuri wa ndizi zake na tabia ya kumwita mkwe mpaka siku aliporudi Colin kutoka Ulaya na kutambulishwa kama mchumba'ke.

"Sasa hapo kipi kinakutatiza?" mama yake alimuuliza baada ya kumsikiliza.

"Mama sielewi kama kweli mama Colin amenichagua niwe mchumba wa mwanaye."

"Mwanangu kumbe ndicho kinachokuchanganya?"

"Ndiyo mama yangu, hakuna kingine. Sijawahi kupenda wala simjui mwanaume lakini nimetokea kumpenda sana Colin na kutamani awe mume wangu."

"Umesema ametoka Ulaya kusoma, sasa akuoe wewe mbumbumbu ambaye hata darasa la saba limekushinda?"

"Mama elimu haina mwisho, naweza kujiendeleza najua tatizo labda kuzungumza kingereza."

"Sasa hicho kingereza utakijulia wapi?"

"Zipo shule nitajifunza, nitajua."

"Nataka nikuambie mwanangu, mama Colin kukuita mkwe ni kukutania tu, siku zote matajiri huwapeleka watoto wao kusoma Ulaya ili wawaoe watoto wa matajiri wenzao tena wasomi.


Itaendelea.............
 
WAKILI WA MOYO - 7


"Mama elimu haina mwisho, naweza kujiendeleza, najua tatizo labda kuzungumza kingereza."
"Sasa hicho kingereza utakijulia wapi?"
"Zipo shule, nitajifunza, nitajua."

"Nataka nikuambie mwanangu, mama Colin kukuita mkwe ni kukutania tu, siku zote matajiri huwapeleka watoto wao kusoma Ulaya ili wawaoe watoto wa matajiri wenzao tena wasomi. Sasa wewe pangu pakavu wapi na wapi?"
SASA ENDELEA...

"Sawa mama, lakini naamini ipo siku maji yatapanda mlima."

"Hizo ni ndoto za mchana."

"Sawa mama, ipo siku utakubali ndoto za mchana huwa zina ukweli."

"Mwanangu naomba uachane na mawazo hayo, muda ukifika Mungu atakupa mume mzuri mwenye mapezi na wewe."

"Asante mama yangu."

"Haya kalale mwanangu."

"Haya mama usiku mwema."

"Na kwako pia."

Cecy aliagana na mama yake na kurudi chumbani kwake kulala. Alipofika chumbani alizima taa na kujilaza kitandani. Hakukubaliana na mama yake, akili yake kubwa ilikuwa kwenye zawadi aliyoahidiwa na Colin.

Alijiuliza ni zawadi gani anayotaka kumpa ambayo hakuweza kumpa siku ile mpaka asubiri siku ya pili? Alijikuta akiuona usiku ukienda taratibu sana, hamu yake kukuche upesi ili akaione zawadi aliyoahidiwa na Colin.
***
Mage, pamoja na kukubali kuolewa na Colin, bado alikuwa na kovu moyoni mwake la kutendwa na mtu aliyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua, Hans. Mwanaume aliyemuingia kwenye ulimwengu wa mapenzi.

Wasiwasi wake mkubwa kwa Colin ni kuwa na mpenzi mwingine ambaye ametoka naye mbali na mwisho kuwa kama Hans na kuumizwa kwa mara ya pili kitu ambacho hakutaka kijirudie.

Hakuwa tayari kuliona lile na alikuwa tayari kulipigania penzi lake kwa nguvu zake zote.
Wazo la peke yake liliisumbua akili yake, alihitaji msaada wa mtu wa karibu.

Mtu muhimu katika maisha yake alikuwa ni shoga yake Brenda ambaye aliamini anaweza kumsaidia juu ya uamuzi wake wa ghafla wa kumkabidhi moyo wake Colin bila kumchunguza.

Akiwa amejilaza kitandani alichukua simu yake na kumpigia Brenda, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.

"Vipi shoga, kulikoni mpaka leo ukapiga simu, badala ya kutumia njia ya Whats App au Twiter?"

"Shoga si la kulizungumzia kwenye mtandao, hili ni la uso kwa macho."

"Mmh! Una nini tena shoga?" Brenda alishtuka.

"Kwanza upo wapi?"

"Nimerudi muda si mrefu natoka kufuatilia ile ishu."

"Sasa naomba basi nikupitie tukakae ufukweni tuzungumze vizuri."

"Hakuna tatizo."

"Basi nakuja sasa hivi."

"Poa."

Mage alikata simu na kwenda kubadili nguo, kwa vile alikuwa ametoka kuoga muda si mrefu, hakuwa na haja ya kwenda kuoga tena. Baada ya kuchagua nguo nzuri iliyompendeza alitoka kuelekea nje. Mama yake aliyekuwa sebuleni alishangazwa na mwanaye kutoka bila taarifa.

"Mage safari ya wapi?"

"Ufukweni mama."

"Kufanya nini?"

"Mama akili yangu bado haipo vizuri ngoja nikaipoze kwa kuangalia maji."

"Brenda mwanangu kumbuka sasa hivi wewe ni mchumba wa mtu, japokuwa hujavalishwa pete. Hiki huwa ni kipindi kibaya sana kwa msichana kwani anatakiwa kutulia.

Unaweza kuharibu kila kitu na matokeo yake useme umerogwa."

"Mama hujui kiasi gani nilivyo na msogo wa mawazo juu ya uamuzi wangu wa haraka wa kumkubali Colin.
Katika mapenzi yangu na Hans sikuwaza kama kuna siku tutakuwa mbalimbali. Hivyo nimekuwa muoga sana, mama naona kama nimefanya uamuzi wa ghafla sana."

"Katika penzi lenu na Hans kuna kosa mlifanya ambalo nina imani kwa Colin limekuwa wazi sana."

"Kosa gani mama?"

"Penzi lenu lilitawaliwa na usiri na mambo mengi mlifanya kwa siri bila wazazi wa kujua."

"Mamaa! Wadogo zake wote wananitambua."

"Wazazi wake?"

"Ndiyo tulikuwa katika harakati za kutambulishana likatokea la kupatiwa mchumba," Mage alisema kwa sauti ya masikitiko.

"Umeona! Pengine kama mngekuwa wawazi yote yasingetokea, sasa hivi ungekuwa mke wa Hans."

"Mamaa! Usinikumbushe, kutaja ndoa yangu na Hans moyo unaniuma. Nampenda Colin lakini hawezi kumfikia Hans, kwake nilikuwa kama kipofu niliyebahatika kufumbua macho mara moja na kitu cha kwanza na mwisho kukiona kilikuwa ni yeye."

"Ndiyo hivyo ukificha moto kwa kuufunika na shuka, moshi utakuumbua. Penzi mlilifanya la siri ndoa ya mwanamke mwingine imekuumiza."

"Basi mama inatosha, niache nikapunguze mawazo ufukweni."

"Kwa nini usimfuate mwenziyo ili mwende pamoja, kufanya hivyo unaonesha jinsi gani unavyomuhitaji kama mumeo."

"Mama siku za kutoka na Colin zipo, leo nina mazungumzo na Brenda."

"Haya ila punguza mawazo, Mungu kasikia kilio chako umempata mwanaume wa haja, anamzidi kila kitu Hans."

"Kwa macho ni rahisi kusema hivyo, macho huwa yanaona lakini moyo ndiyo wenye jukumu la kuchagua ulichokipenda. Colin anaweza kuwa na umbile na sura nzuri lakini akawa hana mapenzi kama Hans."

"Mmh! Huyu Hans kakuchanganya sana mwanangu, ina maana akiachana na mkewe upo tayari kuolewa?"

"Mkewe angekuwa hajazaa ningekubali, lakini alichonifanyia Mungu anajua. Sasa hivi namchukia Hans kuliko kifo."

"Basi mwanangu muwahi Brenda."

"Sawa mama."

Mage alitoka hadi nje na kuchukua gari aina ya Toyota Harrier Lexus na kuelekea Oysterbay kwa shoga yake Brenda.
Alimkuta akiwa tayari amejiandaa, hakuwa na haja ya kuingiza gari ndani kwani alimkuta tayari yupo getini.

Baada ya Brenda kuingia ndani ya gari, Mage aliliondoa bila kusema kitu. Shogaye aligundua mabadiliko kwenye uso wa rafiki yake.

"Shoga kuna usalama?"

"Kiasi."

Mage alijibu kwa mkato bila kumtazama shoga yake huku akifunga breki katika foleni ndogo kwenye taa za Daraja la Salenda. Baada ya taa kuruhusu, aliondoa gari, Brenda hakubandua uso wake kwenye uso wa Mage na kugundua michirizi ya machozi kitu kilichomshtua sana.

"Shoga kulikoni?"

Mage alijikuta akipaki gari pembeni na kuanza kulia kilio cha chinichini. Brenda alishtuka sana na kumsogelea shoga yake aliyekuwa amelalia usukani huku akilia.


Tukutane...........
 
WAKILI WA MOYO - 8



Mage alijikuta akipaki gari pembeni na kuanza kulia kilio cha chinichini. Brenda alishtuka sana na kumsogelea shoga yake aliyekuwa amelalia usukani huku akilia.
SASA ENDELEA...


"Mage nini tena shoga si umesema tukazungumzie ufukweni?"

"Ni kweli, lakini inauma sana."

"Sawa, hebu twende huko tukayaongea yote."

"Papara ya mapenzi itaendelea kunitesa, hata sijui kwa nini nimeshindwa kujikontroo," Cecy alisema akiwa bado ameinama kwenye usukani.

"Jamani Mage, nani kakutenda tena?"

"Shoga hebu njoo uendeshe gari naweza kugonga maana kichwa changu hakipo sawa."

Brenda alizunguka upande wa pili na kuingia kwenye gari na kuliondoa kuelekea Kigamboni. Baada ya kusubiri pantoni Kivukoni kwa robo saa, walivuka upande wa pili.

"Twende ufukwe gani?" Brenda alimuuliza baada ya kutoka nje ya geti.

"Yoyote ile," Cecy alijibu akiwa amejilaza kwenye kiti ilichokilaza kwa nyuma.

"Mikadi panafaa?" Brenda alimuuliza huku akimtazama.

"Popote utapopaona panafaa."

Brenda alipaki kwenye maduka na kununua vitu vya kutafuna wakiwa ufukweni kisha aliendesha gari hadi ufukwe wa Mikadi. Waliteremka na kuelekea upande wa bahari.
Hali ya hewa ilikuwa ya kawaida, jua lilikuwa limefichwa kwenye mawingu huku upepo wa bahari ukipepea bila kuwa na kero kwa mtu aliyekuwa ufukweni.

Kwa vile ilikuwa katikati ya wiki, watu walikuwa wa kuhesabu ufukweni. Walitafuta sehemu nzuri na kutandika khanga na kukaa juu yake, kila mmoja alinyoosha miguu kuelekea baharini.
Baada ya utulivu wa muda huku kimya kikitawala, Brenda alikuwa wa kwanza kuuvunja ukimya ule kwa kumsemesha shoga yake aliyekuwa ametuliza macho yakitazama baharini.

"Mage."

"Abee."

"Hebu nitoe tongotongo, najiona kama nipo gizani na sauti ya upande wa pili ikiomba msaada bila kumuona mwenye tatizo. Siku zote tumekuwa watu tunaotegemeana kwenye matatizo yetu. Najua umeniita ili tusaidiane mawazo.

"Naomba unieleze tatizo lako, siku zote tunajua machozi si ufumbuzi wa tatizo zaidi ya kupambana nalo na kulitatua. Basi naomba unieleze kinachokusibu," Brenda alisema kwa sauti ya kubembeleza.

"Brenda, nimekuwa nikikurupuka mara nyingi katika suala la mapenzi kitu ambacho kimekuwa kikinihukumu siku zote," Mage alisema huku akimtazama Brenda.

"Mage mara ngapi umekurupuka? Suala la Hans pale ulikurupuka nini, ikiwa wote mlikuwa mkipendana tatizo wazazi wake?"
"Alichonitenda Hans hukijui?" Mage alimuuliza Brenda huku akimkazia macho.

"Mage nilikueleza toka siku ya kwanza, kitu kama kile hakiwezekanani. Hawawezi kulala pamoja kufanya mapenzi bila kinga ujauzito usipatikane."

"Hans alinihakikishia hawezi kuzaa na yule mwanamke, kitu ambacho tungekifanya tukioana ili tuanze kutafuta mtoto pamoja."

"Inawezekana alipanga vile, lakini imetokea bahati mbaya. Lakini nilikueleza mapema kuhusu mategemeo yako kwa Hans baada ya kuoa kuwa usimtegemee kabisa, lakini ulinibishia."

"Brenda, unajua kiasi gani nilivyokuwa nampenda Hans?"

"Hilo lipo wazi, lakini ndiyo hivyo tena, kitu gani kingine kilichokufanya mpaka ukawa kwenye hali hii tofauti na la Hans?" Brenda alimuuliza Mage huku akimkazia macho.
Mage alimueleza kila kitu toka walipokutana kwa mara ya kwanza na mama Colin na kumwita mkwe kwa kujua anamtania mpaka siku alipomfanyia ‘surprise' ya kuletewa mwanaume nyumbani kwao.

"He! Makubwa, mbona kama umegeuzwa mbuzi hata bila ridhaa yako?" Brenda alihoji huku akigeuka kumtazama Mage usoni.

"Si kwamba sikutaarifiwa bali niliona kama utani, lakini kumbe yule mama alikuwa hatanii."

"Ehe, baada ya kuletwa ikawaje?"

"Yaani hata sijielewi, baada ya kumuona nikawa nimevurugwa mtoto wa kike."

"Mtume!" Brenda alisema huku akimtazama shoga yake kwa jicho la huruma.

Mage alimueleza kila kilichoendelea baada ya kumuona Colin.

"Mmh! Basi inaonekana Colin ni kitu cha haja?"

"Kwa kitu? Kitu hasa! Colin Mungu kajua kumtengeneza mwanaume yule. Yaani mpole na mstaarabu hadi raha," Mage alisema huku akijishika kifuani na kufumba macho.

"Sasa tatizo nini?"

"Najiona nimejirahisi mapema sana bila kuijua historia yake."

"Lakini si amekuhakikishia kuwa yupo tayari kukuoa?"

"Ndiyo, lakini mvulana mzuri kama yule lazima atakuwa na mpenzi tu. Mimi kumkubali nitakuwa naingilia penzi la mtu. Huoni kumkubali Colin ni sawa na kuyatafuta maumivu mengine?"

"Lakini bado hamjavishana pete ya uchumba, una nafasi ya kumchunguza, kwani mmesha duu?"

"Bado."

"Kumbe! Sasa tatizo nini?"

"Hata kama bado, najua nimechelewa kwa vile Colin maisha ya Tanzania hajaishi sana. Kuna vitu aliniambia vimenichanganya sana."

"Vitu gani?"

"Nilimweleza jinsi nilivyoumizwa na mapenzi na kumweleza najitupa tena ndani ya dimwi la huba bila kujua kina chake. Kuwa yeye ni boya la kuniokoa bila hivyo nitakufa maji."

"Akasemaje?"

"Alinieleza ananipenda zaidi ya kupenda huku akinithibitishia kuwa yeye ndiye tiba sahihi ya maumivu ya moyo wangu. Nilimweleza huenda hanipendi bali ananitamani na baada ya kuufaidi mwili wangu anikimbie."

"Akajibu nini?"

"Brenda, Colin alizungumza kwa taratibu na kunihakikishia ananipenda sana, nakumbuka baadhi ya mazungumzo yetu baada ya kumbana na maswali, nilimwambia:

"Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda?"
Colin alinijibu: Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.

"Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza," Colin alisema huku amenishika mabegani na kunitazama usoni kwa jicho la huruma.

Nilimuuliza: " Vitu gani hivyo Colin?" niliuliza huku nikijitahidi kuyatoa macho nje kama naweza kuyaona maneno atakayoniambia kwa macho.

Colin alinijibu: " Kila mtu anapenda kuwa na mwenza mwenye sura anayoiwaza ambayo huamini huenda ikawa sahihi, nami niliitengeneza yako niwezavyo. Lakini imekuwa kinyume kabisa," Colin aliniambia huku akiachia tabasamu ambalo lilivunja nguzo za moyo wangu.

Nilijitahidi kumuuliza: `'Mmh! Colin, kwa nini?"


Itaendelea................
 
WAKILI WA MOYO - 10



"Vitu gani hivyo Colin?" niliuliza huku nikijitahidi kuyatoa macho nje kama naweza kuyaona maneno atakayoniambia kwa macho.
Colin alinijibu: "Kila mtu anapenda kuwa na mwenza mwenye sura anayoiwaza ambayo huamini huenda moja wapo, nami niliitengeneza yako niwezavyo. Lakini imekuwa kinyume kabisa," Colin aliniambia huku akiachia tabasamu ambalo lilivunja nguzo za moyo wangu.
Nilijitahidi kumuuliza: "Mmh! Colin, kwa nini?"
SASA ENDELEA...


Nilimuuliza, nililazimisha tabasamu. Alinijibu: Mage we ni mzuri wa wazuri mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako," Colin alisema huku akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza hatanii.

Huku moyo wangu ukiwa umetawaliwa na tabasamu, nilimwambia: ''Siamini, Colin siamini," nilisema huku mikono nikijishika kifua changu na machozi yakinitoka.

"Mage huamini nini?" Colin aliniuliza kwa uso wa huruma.

"Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako," nilisema huku machozi yakinitoka na kuweka michirizi kwenye mashavu yangu.

"Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu linavyochukuwa uhai wa mtu ghafla," kila kauli ya Colin ilizidi kuusambaratisha moyo wangu.

"Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani?" nilijisemea huku nikijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.

"Kwa nini mpenzi?" Aliniuliza huku akinitazama kwa huruma kitu ambacho sikuwahi kukiona kwa Hans pamoja na kumpenda kote.

"Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu," nilimweleza nilivyokuwa radhi kuwa mateka wa penzi lake.

"Sijakuelewa mpenzi?" Colin aliniuliza.

"Umeweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji, boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung'olewa jino bila ganzi," nilimtahadharisha Colin.

"Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema," Colin aliniahidi japokuwa sikujua aliyosema yanatoka moyoni au mdomoni.

"Nami nakuahidi kuwa mke mwema," nami nilimuahidi kutoka moyoni mwangu.

Baada ya Brenda kumsikiliza kwa muda shogaye, alisema:

"Mmh! Mbona kila kitu kipo wazi, tatizo nini?"

"Wasiwasi wangu anaweza kuwa na mtu wake."

"Anaweza kuwa naye lakini si wa malengo ya kuwa mke na mume, kwani picha yake unayo?"

"Ndiyo, tulipiga siku ile tena alilazimisha yeye."

Mage alisema huku akifungua simu yake upande wa picha. Baada ya kuijaza kwenye kioo cha simu, alimuonesha Brenda.

Shoga yake alishtuka kumuona mwanaume mzuri akiwa na Mage katika pozi tofauti za mahaba.

"Mage! Colin ni mwanaume mzuri sana, mlivyokaa kama mke na mume sijui picha za ndoa yenu zitakuwaje?"

"Nina wasiwasi nimekurupuka sana katika kumkubali."

"Walaa, mapenzi shoga yangu hayana fomula, mnaweza kukutana hivi na penzi lenu likadumu milele, lakini mnaweza kuandaana mwisho mkawa maadui wakubwa kama unavyomuona Hans."

"Umeonae! Yaani sasa hivi sitaki kumuona wala kusikia jina lake."

"Nina imani hili litakwenda vizuri kwa vile hata mzazi wake amekupenda pia familia zenu zinafahamiana na zinapendana."

Wakiwa katikati ya mazungumzo, simu ya Mage iliita, namba ilikuwa ngeni. Aliiangalia kwa muda bila kuipokea.

"Mbona hupokei?" Brenda alihoji.

"Hata sijui ni nani, inawezekana ni Hans, niliapa sitapokea simu yake."

"Hebu pokea hujui anataka kukuambia nini?"

"Hana cha kuniambia."

Wakati huo simu ilikuwa imekatika, baada ya muda uliingia ujumbe mfupi wa maneno. Mage aliufungua na kuusoma:
Najua upo bize na mambo ya mchana, ushikapo simu naomba unipigie. Moyo wangu upo taabuni mpaka nisikie sauti yako.

It's me Colin.

Mage baada ya kusoma ujumbe ule alipiga kelele huku akishika kifua.

"Mungu wangu!"

"Nini tena mbona unanitisha?" Brenda alishtuka.

"Mungu wangu! Kumbe alikuwa Colin," Mage alisema huku akishika kifua.

"Mmh! Ina maana huna namba yake?"

"Sina."

"Ina maana mlipokutana hamkupeana namba za simu?"

"Hatukupeana, wote tulichanganyikiwa."

"Basi mpigie."

"Duh! Sijui atanielewaje?" Mage aliingia wasiwasi.

"Mage akuelewe kivipi?" Brenda alimshangaa rafiki yake.

"Ataona kama ninaringa au siyo muaminifu!"

"Hawezi kwa vile leo ndiyo siku yake ya kwanza kukupigia."

"Mmh! Ngoja nijaribu."

Mage alichukua simu na kumpigia Colin, iliita kwa muda bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara nne lakini haikupokelewa kitu kilichomnyima raha Mage.

"Brenda lazima Colin atakuwa amekasirika, siwezi kupiga mara nne bila kupokelewa."

"Mage acha kujipa presha, yeye ndiye aliyekuambia umpigie huenda simu ipo mbali, akiona missed calls lazima atakupigia."

Mara simu iliita, Mage aliipokea haraka akihofia kumuudhi mpenzi wake huyo mpya.
"Haloo mpenzi," Mage alisema kwa kujichetua.

"Mage siamini kama leo umeweza kurudisha moyo wako chini. Mage unajua sitampenda mwanamke yeyote chini ya jua zaidi yako na hilo unajua. Amini mpango wangu wa kukuoa upo palepale na utaamini baada ya muda mfupi nakupenda Mage."

Mage alishtuka baada ya kuisikia sauti ya Hans.

"Hansiii! Umetumwa? Hebu achana na mimi wewe mume wa mtu nami si muda mrefu nitakuwa mke wa mtu kwa hiyo tuheshimiane."

"Ma..Mage ...u.. usi..fanye hivyo bado nakuhitaji...m..mpe.."

Mage alikata simu na kuizima kabisa.

"Vipi tena?" Brenda alishtuka.

"Si huyu mshenzi."
"Nani, Hans?"

"Ndiyo," Mage alijibu huku uso ameukunja kwa hasira.

"Unakosea, we msikilize na kumueleza ukweli kuwa nawe umepata wako."

"Sina muda huo, najua bado ana ndoto za kuendelea kunifanya chombo cha starehe."

"Vipi kuwasiliana na Colin?"

"Naomba nitumie simu yako kumpigia."

"Namba unaikumbuka?"



Itaendelea wiki ijayo.
 
WAKILI WA MOYO - 11



"Ndiyo," Mage alijibu huku uso ameukunja kwa hasira.

"Unakosea we msikilize na kumueleza ukweli kuwa nawe umempata wako."

"Sina muda huo, najua bado ana ndoto za kuendelea kunifanya chombo cha starehe."

"Vipi kuwasiliana na Colin?"

"Naomba nitumie simu yako kumpigia."

"Namba unaikumbuka?"

PATA UHONDO KAMILI....

"Nitawasha kwa muda ili ninakiri namba kisha nazima."

Mage alipowasha, simu iliingia, alishindwa kujua ni ya nani kati ya Colin na Hans kwa vile hakuzifahamu namba zao.

"Simu ya nani?"

"Sijajua."

"Pokea."

Mage alipokea akiwa hajiamini.

"Haloo."

"Haloo my sweet," Mage alichelewa kujibu ili kuichunguza ile sauti.

"Haloo Mage," sauti ya upande wa pili ilisema baada ya Mage kukaa kimya.

"Colin?" Mage aliuliza bila kujiamini.

"Naam mpenzi," Colin aliitikia.

"Oops," Mage alishusha pumzi baada ya kujua ni Colin.

"Vipi mbona umeshusha pumzi nzito?" Colin aliuliza.

"Yaani nilikuwa nakuwaza hasa baada ya kupata ujumbe wako na kupiga bila kupokelewa mwenzio presha juu." Mage alitengeneza uongo unaofanana na kweli.

"Upo wapi mpenzi?"

"Nipo ufukweni na shoga yangu."

"Kweli sweet?"

"Msalimie basi Brenda," Mage asema huku akimpa simu Brenda.

Brenda aliipokea na kusema:

"Haloo shemu."

"Haloo, habari Brenda?"

"Nzuri tu, yaani nina hamu ya kukuona."

"Mtaniona wapi nanyi wachoyo, mmenikimbia."

"Hapana shemu tukiwa na mazungumzo, mara nyingi huwa tunakuja sehemu hii kuzungumza."

"Hakuna tatizo shemu, nipe Mage."

Brenda alimpa simu Mage ambaye alizungumza kwa uchangamfu.

"Niambie my adorable."

"Kesho birthday yangu."

"Waaa woo! Itafanyikia wapi?"

"Nyumbani saa moja usiku."

"Kesho nitakuletea zawadi nzuuri."

"Nitafurahi sana, nikuacheni muendelee na mazungumzo, mengi tutazungumza kesho."

"Asante mpenzi nimefurahi sana kusikia sauti yako."

"Hunishindi mimi."

***

Usiku ulikuwa mrefu kwa Cecy, alitamani siku ya pili ifike haraka ili akaijue hiyo zawadi aliyoahidiwa na Colin. Alijikuta akipinduka kitandani, usingizi ulikimbia kabisa.

Kutokana na kukosa usingizi akiwazia zawadi, alijikuta akichelewa kuamka kitu ambacho kilimfanya akose njozi nzuri.

Kwa vile shida yake ilikuwa kufika kwa kina Colin akachukue zawadi, ilibidi anunue ndizi nzuri kwa wenzake ambao kwake hazikuwa na faida kwa vile angekwenda kuuza kwa bei ileile.

Hakuchukua ndizi nyingi, alirudi hadi nyumbani. Baada ya kuoga na kujipamba na kuhakikisha amependeza, alibeba ndizi zake na kuelekea kwa mama Colin huku akijiuliza, Colin anataka kumpa zawadi gani?

Kama kawaida alipofika kwenye mlango wa geti alibonyeza kengele, mlinzi alimfungulia na kuingia ndani.

"Mmh! Cecy muuza ndizi unapendeza kuliko mfanyakazi wa ofisini!" Mlinzi alimshangaa Cecy kila siku kupendeza na kuonesha uzuri wake.

"John acha ushamba nani alikuambia muuza ndizi anatakiwa kuwa mchafu?"

"Pamoja na hayo, wee umezidi."

"Kwa hiyo ulitakaje?"

"Walaa, nakupongeza tu."

"Asante."

"Ila mama ametoka sasa hivi, umechelewa kama dakika mbili."

"Na..na Colin?" Cecy alishtuka.

"Ye yupo."

"Ooh! Afadhali!"

Cecy alisema huku akishusha pumzi ndefu kitu kilichomshangaza mlinzi.

"Mbona umeshusha pumzi?"

"John, mbona una maswali mengi kwani we ni polisi?" Cecy alimjia juu mlinzi.

"Basi Cecy nisamehe."

Cecy alisogea kwenye mlango wa kuingilia nyumba kubwa.

Aliweka beseni la ndizi chini na kuita kwa sauti.

"Ndiziii."

Colin alitoka mlangoni akiwa amebeba mfuko mkubwa kidogo mkononi. Cecy alipomuona alijikuta akipoteza kujiamini na mapigo ya moyo kwenda mbio.

"Karibu mchumba," Colin alimkaribisha huku akitabasamu.

"Asante."

Colin alisogea hadi kwenye beseni na kuchagua ndizi.

"Mbona leo ndizi kidogo?"

"Chukua zote, nilichelewa kuamka."

"Ooh! Pole."

Baada ya kuchukua ndizi aliingianazo ndani huku akiacha mfuko wake pembeni ya Cecy. Cecy alimsindikiza kwa macho huku moyo wake ukiendelea kuteseka juu ya Colin.

Aliutazama mfuko ulioonekana una vitu ndani, alijiuliza ni wake? Na kama ni wake, kuna zawadi gani? Lakini hakujua kama ndiyo wake. Baada ya muda alitokeza tena Colin akiwa kwenye tabasamu.

"Mmh! Mchumba samahani nilisahau kukusifia, umependeza."

"Asante," Cecy alijibu huku akiwa ametawaliwa na aibu.

"Jana nilikuahidi nini?" Colin alimuuliza Cecy.

"Zawadi."

Colin alichukua mfuko na kumpa, Cecy aliupokea kwa kupiga magoti kwa heshima mpaka chini.

"Asante mpe...M..chumba," Cecy aliingia kigugumizi.

"Usijali, sasa ni hivi...leo jioni nitakuwa na sherehe ndogo ya kuzaliwa kwangu."

"Waaaooo, hongera mchumba."

"Asante, naomba kila kilichomo ndani ya mfuko huu, uvae leo kwenye sherehe yangu sawa mchumba?"

"Sawa."

Colin alimpa elfu ishirini, Cecy alishtuka kwa vile ilikuwa nyingi tofauti na malipo ya siku zote ya shilingi elfu tano.

"Colin mbona nyingi?"

"Usiwe na wasi chukua zote."

"Asante, kwa hiyo sherehe inaanza saa ngapi?"

"Saa moja usiku, ukikosa utaniudhi."

"Jamani si usiku?"

"Kodi gari."

"Basi nitakuja."

Cecy aliondoka na kumuacha Colin akimsindikiza kwa macho. Wakati Cecy akiwa getini, Colin alikuwa ghorofani akimtazama. Aligundua Cecy ni mzuri kuliko Mage lakini alikosa vigezo kutokana na hali ya maisha kuwa ya sayansi na tekinolojia inayomtaka kila mtu kuwa na elimu ili kukabiliana na kasi yake bila hivyo lazima ikuache.

Wakati Cecy anatoka alipishana getini na Mage aliyekuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8. Colin aliyekuwa ghorofani alishtuka kuona gari la kifahari likiingia nyumbani kwao.


Je sherehe itakuwaje? Fuatilia .............
 
Back
Top Bottom