Wakili wa moyo 43
ILIPOISHIA:
Colin alipewa kiti ili amsubiri Cecy aliyekwenda ndani kubadili nguo, alitoka amejifunga upande wa khanga na kutoka kuelekea bafuni kuoga. SASA ENDELEA
Colin alimsindikiza kwa macho baada ya kupata nafasi ya kuliona umbile la Cecy katika vazi la khanga,rangi adimu
isiyochanganywa madawa ya ngozi. Aliamini chaguo la kwanza la mama yake lilikuwa sahihi,alijua ni wakati wa mama yake kuamini chaguo la pili halikuwa sahihi
bali tamaa ya macho ndiyo iliyompoteza. Cecy baada ya kumaliza kuoga alirudi ndani na kubadili nguo kwa kujipamba kwa vazi la kitenge lililompendeza, alionekanamwanamke wa Kiafrika hasa.
Alisimama mbele ya Colin na kutabasamu. Colin tunaweza kwenda. Duh! Colin alisema akiwa haamini.
Ndiye mimi Cecy,mwafrika asilimia mia moja ninayejivunia rangi yangu nyeusi. Basi mama inatosha, Colin alisema huku akinyanyuka na kumshika mkono. Mama tunaomba tukukimbie, Colin alimuaga mama Cecy.
Haya baba,Mungu awatangulie mfike salama. Amina. Walishikana mikono na kutoka nje kuelekea kwenye gari,mama Cecy aliwasindikiza kwa macho na kunyanyua mikono juu na kurudi
kuomba dua yake ya Colin kumuoa mwanaye ili roho itulie. Hakuteremsha jicho mpaka gari lilipopotea machoni mwake. Ndani ya gari,Cecy moyo wake ulikuwa na furaha nusu kwa vile aliamini lazima Colin atumie nguvu nyingi kupigania penzi lao
bila hivyo hakuna mapenzi kwa vile mama yake alishajenga uadui mapema. Alionekana mtu mwenye mawazo mengi kitu kilichomfanya Colin amshtue. Vipi mpenzi?
Colin bado moyo wangu una wasiwasi. Wa nini? Jinsi mama yako atakavyonipokea. Ondoa wasi kila kitu niachie mimi.
Colin alisimamisha gari mbele ya geti na kupiga honi,mlango ulifunguliwa na kuliingiza gari ndani. Alizunguka upande wa pili
na kumfungulia Cecy na kumshika mkono kuteremka kwenye gari kwa heshima kisha alielekea naye ndani. Walitembea taratibu kama mtu na mkewe, angetokea mtu na kuwaona angejua ni wapenzi wa muda mrefu wanaopendana sana.
Walipofika mlango wa kuingia sebuleni,Colin alisema kwa sauti ya unyenyekevu: Karibu malkia wangu. Asante mfalme wangu, Cecy naye alijibu kwa unyenyekevu.
Sauti zile zilimfanya mama Colin aliyekuwa ameinama akisoma biblia kunyanyua macho na kumuona mwanaye na msichana mrembo
ambaye aliamini ndiye aliyeondoka muda mfupi uliopita. Shikamoo mamkwe! Cecy alimsalimia mama Colin kwa unyenyekevu huku akipiga magoti ya heshima. Marahaba mama,karibu.
Asante, Cecy alijibu huku akinyanyuka na kumfuata Colin aliyekuwa amesimama pembeni yake na kumshika mkono.
Colin alimuongoza Cecy mpaka kwenye sofa na kumkaribisha tena: Karibu. Asante, Cecy alijibu huku akikaa.
Unatumia kinywaji gani? Chochote utakachonichagulia mfalme wangu. Colin si ungemwita dada wa kazi awahudumie, mama Colin aliingilia kati. Hapana huyu ni mgeni wangu,kila kitu chake nitafanya mimi.
Mmh! Haya. Muda wote mama Colin alikuwa bado hajaipata picha ya yule msichana mrembo, alituliza macho kwa wizi ndipo alipogundua kuwa ni
Cecy,msichana muuza ndizi. Alikunja uso kwa hasira na kuamini kabisa lile si chaguo sahihi kwa mwanaye bali ni papara ya kuachwa na Mage.
Alinyanyuka na kuelekea chumbani kwake, alipotoka eneo la sebule alimwita Colin. Colin. Naam mama. Njoo mara moja.
Nakuja, Colin alisema huku akimuwekea juisi Cecy kwenye glasi na kunywa kidogo kisha kumkaribisha. Karibu malkia wangu. Asante mfalme wangu.
Samahani namsikiliza mama mara moja. Nenda mpenzi kamsikilize mama.
Colin alimfuata mama yake kwenye korido alipokuwa amesimama,alimsogelea karibu na kumuuliza: Unasemaje maana ulivyotoka kama kuna kitu? Yule nani? aliuliza huku akinyoosha kidole sebuleni.
Mke wangu mtarajiwa,chaguo sahihi la moyo wangu. Colin
Colin una tatizo gani? Wanawake wote wameisha mpaka umfuate huyu maskini mbumbumbu asiyejua kitu. Mwanangu tuna fedha,
tunaweza kumuoa msichana yeyote mzuri mwenye elimu yake kwa fedha yoyote na popote duniani. Mama naomba kwa hili usizungumze chochote uniache kabisa,umetafuta mwanamke ambaye leo katuvua nguo kwa vile ulimfuata
msomi mwenye uwezo. Lakini suala la Mage bado tulikuwa tunalishughulikia,lilikuwa halijafika mwisho. Hivi leo Mage aje na mama yake wakikute
kinyago hiki kuna ndoa kweli? Penzi langu na Mage liliishia Bagamoyo. Lakini bado wazazi hatujabariki uamuzi wenu.
Mama si uamuzi wetu bali wa Mage, kasema ukweli ana mtu anayempenda tatizo lipo wapi? Basi Cecy si chaguo langu. Mama mimi ni mwanao,umenizaa na kunilea na kunifundisha kila kitu,lakini suala la kumpenda mtu ni matakwa ya moyo wangu.
Nilikukubalia kwa Mage kwa vile ni mzazi wangu zoezi lako lilifeli sasa huu ni muda wangu. Lakini siyo kwa Cecy. Mama Cecy ni zaidi ya mwanamke ndiye mwenye nafasi moyoni mwangu zaidi ya hapo sitakuwa na mwanamke mwingine.
Colin,Cecy umemjulia wapi kama siyo mimi? Basi hili ndilo chaguo lako lililokuwa sahihi hujui tu.
Nilikuwa namtania tu lakini si kwa ajili ya kuwa mkeo. Basi imekuwa hivyo bila kutegemea. Basi mimi simtaki.
Kwa hiyo unatafuta aibu nyingine? Colin alisema huku akifungua simu upande wa picha na kumuonesha mama yake.
Itaendelea