GAZETI MAJIRA
::Habari za Tanzania Jumamosi Des 22, 2007
Sina taarifa ya Balali kujiuzulu-Meghji
Habari Zinazoshabihiana
Gavana Daudi Balali ajiuzulu 21.12.2007 [Soma]
Balali: Kushuka thamani ya shilingi hakutaathiri uchumi 27.10.2006 [Soma]
Na Rehema Mohamed
WIZARA ya Fedha imesema haina taarifa rasmi za kujiuzulu kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daudi Balali.
Jana baadhi ya magazeti yalinukuu barua ya Bw. Balali kwa Rais Jakaya Kikwete, akiomba kujiuzulu wadhifa huo akiwa Boston, Marekani alikolazwa kwa miezi mitatu sasa baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Akizungumza jana baada ya kuzindua Bodi ya Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT), Waziri wa Fedha, Bibi Zakia Meghji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hana taarifa hizo ila alizisoma magazetini.
Waziri Meghji alisema mpaka sasa hajapokea barua yoyote ya kujiuzulu kutoka kwa Gavana Balali.
"Mimi Waziri wa Fedha sina taarifa hiyo, kwa kawaida katika ofisi yetu na hata nyingine, mtu akitaka kuchukua hatua hiyo kuna utaratibu wa kuandikiana barua.
"Mimi ofisini kwangu sikuletewa na sina barua hiyo, subirini ripoti ya Mkurugenzi wiki ijayo," alisema Bibi Meghji.
Kuhusu kubadilishwa kwa Gavana huyo kutokana na matatizo yake ya kiafya, Bibi Meghji alisema Wizara yake haijazungumzia juu ya suala hilo.
Akijibu swali kuhusu ugonjwa na tuhuma zake ndani ya BoT, alisema hana uhakika na hilo, ila anachojua anaumwa na yuko Marekani kwa matibabu.
Magazeti ya jana yalieleza kwamba kujiuzulu kwa Gavana Balali kumekuja huku ripoti ya tuhuma za ufisadi ndani ya BoT ikiwa imeshakabidhiwa kwa Rais Kikwete na inapitiwa.
Uchunguzi huo uliagizwa na Serikali ili kubaini kama kulikuwa na ubadhirifu ndani ya BoT hususan kuhusu ujenzi wa majengo mawili 'twin tower 'ya benki hiyo.
Ulifanywa kupitia kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo kampuni binafsi ya Uingereza ya Ernst & Young, iliufanya na kuwasilisha ripoti yake kwa Rais.
Uchunguzi huo ulitokana na shinikizo kutoka kambi ya upinzani kupitia Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbrod Slaa, baada ya kutangaza ilichokiita orodha ya mafisadi, huku akimtaja Bw. Balali kuhusika na ubadhirifu ndani ya BoT.
Tuma kwa Rafiki Nakala inayochapika