SoC02 Bei za vyakula na vinywaji katika hoteli zinazotumiwa na wasafiri mikoani si sawa waungwana wenzangu!

Stories of Change - 2022 Competition

cupvich

JF-Expert Member
Aug 2, 2022
408
246
Je, umewahi kusafiri safari ya umbali mrefu mfano kutoka Dar es salaam hadi Mwanza? Safari iliyokulazimu upite sehemu zinazotoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wasafiri ili uweze kupata chochote kitakachopoza njaa yako? Na je ulinunua Chakula au kinywaji? Kama jibu lako ni ndio leo utakuwa shahidi wangu muungwana mwenzangu.

Siku moja nikiwa safarini kutoka Mbeya kuelekea Dar es salaam huku nikiwa na akiba ya tsh elfu tano (5000/=) mfukoni mwangu, Nilisikia kondukta wa basi nililokuwemo akisema " Gari inaingia hotelini, hivyo tunazo dakika kumi za kuchimba dawa na kula" Nilijisikia mwenye furaha kwasababu sikuwa nimekula chochote tokea mwanzo wa safari hivyo nilijua nitapa walau maji. Looo!!!! Niliishiwa na nguvu pale nilipotaka kununua Juisi ya Azam Embe na kuambiwa inauzwa Tsh elfu mbili (2000/=) tofauti na bei ninayoijua ya tsh elfu moja (1000/=), Chipsi za Dar es salaam zinazouzwa tsh elfu mbili mia tano (2500/=) niliambiwa tsh elfu tano (5000/=). Nilivurugwa kabisa pale nilipoenda kununua wali maharage mhudumu akanipakulia vijiko viwili tu na kuniambia nilipie tsh elfu tano (5000/=).

Najua sasa uko pamoja nami Muungwana mwenzangu. Nadhani tutakubaliana wote kwamba Mababu na mabibi zetu waliishi kipindi cha ujamaa ambacho Baba wa taifa mwalimu julius kambarage nyerere alipiga vita Uonevu na Unyonyaji. Vivyo hivyo mimi na wewe tunaishi katika kipindi ambacho wizi, uonevu, na unyonyaji dhidi ya binadamu mwenzako ni kosa kisheria.

Inawezekana vipi Waungwana wenzangu, Bei za chakula na vinywaji katika hoteli zinazotumiwa na wasafiri waliowengi zinakuwa za juu, Hivi hii juisi ya Azam Embe inayouzwa Dar es salaam si ndo ile inayouzwa Tanga?. Hivi kile kipimo cha wali maharage katika hoteli hizo kina thamani ya tsh elfu tano (5000/=)?

Waungwana wenzangu, wasafiri wengi wanaotumia Mabasi kusafiria wengi ni watu wa kipato cha kati na cha chini, lakini pia usafiri wa mabasi umekuwa mahususi sana kwa Wanafunzi pindi wanapokwenda shule za mikoani na kurudi wakati wa likizo, isitoshe ndio usafiri unaopatikana kirahisi pindi mtu anapopata Dharura. Wasafiri Wote hao wanategemea vyakula na vinywaji katika hoteli hizo ambazo zinapandisha bei za Vyakula na vinywaji kila kukicha. Swali kwenu wamiliki na wahudumu katika hoteli hizi, je ni kweli mnatoa huduma au mnafanya unyonyaji uliokatazwa tokea enzi za mwalimu Nyerere?

Muungwana mwenzangu, Ngoja nikupe siri hii, Usione wakati wa Kuchimba dawa.. Muungwana mwenzako amebaki amekaa kwenye siti yake wakati wengine wanashuka. Sio kwamba hana haja au hapendi kukanyaga ardhi ya ugenini, LAHASHA anawaza na kuwazua pale anapokumbuka kuwa anahisi njaa ilihali hata maji ambayo angenunua hana uwezo nayo kutoka na pesa aliyonayo kwasababu amepata safari ya ghafla huwenda ni kutokana na matatizo au Vinginevyo.

Haya achana na bei hizo za chakula na vinywaji kuwa juu, Unakuta hoteli ambayo inatoa huduma ya chakula na vinywaji haina viwango wala ubora wa kukidhi haja za wasafiri. Chakula kinachopatikana ni cha aina moja tena wasafiri wanasubiri kwa muda mrefu bila kupata huduma hii imesababisha abiria wengine kuachwa na magari au wengine kukosa huduma hiyo ya chakula. Sio kwamba wahudumu wa hayo mabasi tunayopanda hawajui, wanajua vizuri sema kwasababu na wao wanapata chochote kutoka katika hoteli hizo ndio maana wanazipenda hata kama hazikidhi vigezo. Muungwana mwenzenu naona jambo hili si sawa kabisa.

Je, serikali yetu inazimulika hoteli hizi?. Nadhani imefika wakati serikali kutusaidia katika Eneo hili kwasababu wasafiri wengi wanategea hoteli hizi ili kuweza kupata chakula na vinywaji na kusafiri kwa amani na salama.Lakini pia Serikali yetu kupitia mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) izimulike hoteli hizi ambazo zinaongezeka kwa kasi ili kuona Kama faida inayopatikana inaenda sambamba na kodi ya serikali inayolipwa. Kama juisi ya tsh 1000/= inauzwa tsh 2000/=, Basi na kodi ya serikali ilipwe kwa ukamilifu wake. Nadhani ipo haja ya Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kuzipitia hoteli hizi nakufanya upya makadirio ya ulipaji wa kodi katika hoteli hizi ili Nchi yetu iweze kupata mapato yake kihalali kwasababu huu ni Uhujumu uchumi. La sivyo Bei halali ya bidhaa itumike ili kuwalinda wasafiri na kuifanya serikali ikusanye mapato halali.

Muungwana mwenzenu, Sikatai wala sipingi kuwa, hoteli hizi zipo katika maeneo ya Kimkakati(strategic areas) lakini kisiwe kigezo cha Kuwakandamiza wasafiri kwasababu tu kwamba wanapita na Kuondoka. Hii si sawa kwa waungwana na kwa Mungu pia. Safari ni sehemu mojawapo ya utalii wa ndani, na watalii ni sisi wenyewe hivyo ni lazima mazingira ya utalii yawe rafiki kwa sisi watalii.

Iwapo hoteli hizi zitaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuuza chakula pamoja na vinywaji kwa bei halali na inayoweza kufikiwa na wasafiri, Wasafiri wengi watapata huduma ya chakula na vinywaji kupitia hoteli hizo. Hii Itasaidia kupunguza usumbufu wanao pata wasafiri wakati wa safari kama vile kuuziwa vyakula vilivyokwisha haribika au kupoa katika vituo vya mabasi, kuacha chechi zao kwa wauzaji wa bidhaa kupitia madirisha ya mabasi lakini pia itapunguza wauzaji wa chakula na vinywaji ndani ya mabasi ambao husababisha usumbufu usio wa lazima.

Mwisho, Muungwana mwenzenu, naamini serikali yetu inayoongozwa na Raisi wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kupitia katika wizara ya Uchukuzi na Usafirishaji itazimulika hoteli hizi ili kuleta mazingira ya Usawa na kuwafanya wasafari kufurahia safari zao wawapo safarini hususan ni katika swala hii la BEI ZA CHAKULA na VINYWAJI katika hoteli hizi.

Ni mimi Muungwana mwenzenu
Mwita Ngutunyi Mohono
S.l.p 237- Rujewa-Mbarali
0762185894/0693531366
 
Eti Sambusa 1000 sambusa haina kichwa wala miguu
Huu wizi mtupu.. nadhani sio sawa. Ila unakuta hakuna namna kama msafiri inakulazimu ununue.

Tafadhari usiache kupiga kura yako katiko andiko hili MWANAJUKWAA.
 
Habari mwana JF.. nikualike kusoma makala hii na kuipigia KURA.
 
Naam karibuni kwa maoni wana JF. na kupigia kura andiko Hili.
 
Back
Top Bottom