[TD="bgcolor: #ffffff"] MAHAKAMA ya wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na mume wa zamani wa Josephine Mushumbusi, Eminiel Mahimbo, baada ya kubaini kuwa haikuwa na msingi wowote kisheria.
Josephine Mushumbuzi kwa sasa ni mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Mahimbo alikata rufaa kupinga hukumu ya mahakama ya mwanzo Sinza ambayo ilivunja ndoa hiyo.
Rufaa hiyo ilifutwa jana na Hakimu Aniseth Wambura ambaye alisema kuwa mahakama hiyo inakubaliana na hukumu iliyotolewa na mahakama ya mwanzo.
Alisema mahakama inakubaliana na hukumu hiyo iliyotolewa Aprili mwaka jana katika kesi ya madai ya talaka iliyofunguliwa na Josephine anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Philemon Mutakyamilwa.
Katika uamuzi wake huo, mahakama hiyo ilitangaza kuwa hakukuwa na ndoa baina ya watu hao kwa sababu Mahimbo hakuwa mwaminifu katika ndoa yake na alikuwa akimtesa mkewe.
Baada ya mahakama yangu kusikiliza hoja za mwomba rufaa na mjibu rufaa, mahakama hii imefikia uamuzi wa kukubali hoja za Josephine kwamba kwa tabia ya kutokuwa mwaminifu hapakuwepo na ndoa baina yao, hivyo hukumu ya mahakama ya mwanzo Sinza ilikuwa sahihi, alisema Hakimu Wambura.
Akizungumza na Tanzania Daima jana baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Mutakyamilwa alisema amefurahishwa na hukumu hiyo kwani mahakama imetenda haki kwa sababu kesi hiyo ilikuwa na msukumo wa kisiasa uliokuwa na lengo la kumchafulia jina mteja wake, Josephine.