Oct 4, 2023
6
12
Utata (Ambiguity) ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Mfano; Kima, kombe, meza, zama, barabara, kanda na katika sentensi "kaka zangu wote wana wake".

SABABU ZA UTATA
(i) Neno kuwa na maana zaidi ya moja mfano; Mbuzi, paa, tupa, pasi, Mswahili n.k.

(ii) Kutozingatia alama za uandishi kama vile mkato, nukta, alama ya kuuliza n.k. Mfaano sentensi zifuatazo zina maana tofauti lakini zote zina maneno yale yale
Baba, John amefika
Baba John, amefika
Baba John amefika.
Baba John amefika?


(iii) Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha. Mfano matumizi ya neno halali.

(iv) Kutozingatia matamushi sahihi ya neno.
Mfano dhana (concept) na zana (Kifaa), Meza(table) meza (Swallow) barabara (Road) barabara (correctly)

(v) Utumiaji wa maneno yenye maana za mafumbo/ lugha ya picha. Mfano: ua, jiko, na mkono wa birika.

(vi) Kuacha baadhi ya maneno. Mfano; Wizi wa silaha umeoongezeka. Hapa inaweza kuwa wizi wa vifaa ambavyo ni silaha umeongezeka au wizi wa kutumia silaha umeoongezeka.

(vii) Matumizi ya vitenzi vyenye kauli ya kutenda au kutendewa
Mfano: Peter ameuawa na simba. Hapa inaweza simba amemuua Peter au Peter amemuua simba au Simba na Peter wameuawa na mtu fulani.

(vii) Kuwapo kwa kiambishi cha kauli ya kutendea (i, e, li na le) Mfano: Ahimidiwe alimpigia Zuwena simu inaweza kuwa:- Ahimidiwe alimpiga Zuwena kwa sababu ya simu au Ahimidiwe alipiga simu kwa niaba ya Zuwena au Ahimidiwe aliwasiliana na Zuwena.

(vii) Kuwapo kwa kiambishi nafsi kiambata A-Wa Mfano:
a) Alisema atakutembelea. Hapa inaweza kuwa mtu huyo atakutembelea wewe au mhusika huyo anakuambia mtu mwingine atakutembelea
b) Baba atawatuma sokoni hapa inaweza kuwa baba atawatuma nyinyi sokoni au baba atawatuma wahusika wengine sokoni

(ix) Matumizi ya baadhi ya viunganishi Mfano:
-a) Nilikuwa na Juma na watoto wake. Hapa inaweza kuwa Juma aliambatana na watoto wake au nilikutana na Juma, kisha nikakutana na watoto wa mtu mwingine.

(x) Matumizi ya baadhi ya vihusishi Mfano:
Juma hapendi kusoma kama Damasi. Hapa inaweza kuwa wote hawapendi kusomaau Juma hapendi kusoma ila Damasi amezidi

(xi) Matumizi ya vimilikishi Mfano:
a) Frenki atajenga kibanda chake. Hapa inaweza kuwa Frenki atajenga kibanda atakachokimiliki yeye au Frenki atajenga kibanda cha mtu mwingine.
b) Mercy alisema atakwenda kwao. Hapa inaweza kuwa mtu fulani atakwenda kwa akina Mercy au Mercy atakwenda kwa mhusika fulani au Mercy atakwenda anakoishi na wazazi wake

(xii) Matumizi ya mzizi “ingine” Mfano:
a) Kingine kimepatikana. Hapa inaweza kuwa kitu kingine zaidi ya hiki kimepatikana au kingine kimepatikana badala ya hiki b) Wengine hawahitajiki. Hapa inaweza kuwa wengine zaidi ya hawa hawahitajiki au wengine baadhi ya hawa hawahitajiki -au wengine badala ya hawa hawahitajiki.

NJINSI YA KUEPUKA UTATA
i) Uteuzi mzuri wa maneno hasa yenye kubeba maana zaidi ya moja

ii) Kuzingatia mkazo tofauti wa sauti kuonesha kwamba neno lipi lipewe uzito zaidi.

iii) Kuzingatia matumizi sahihi ya alama za uandishi katika maandishi kama vile nukta, mkato na alama ya kuuliza.

iv) Kuepuka makosa ya kisarufi na kimantiki yasiyo ya lazima

v) Kuwa makini na matumizi ya maneno yenye maana za picha au mafumbo.

vi) Kutoacha baadhi ya maneno mhimu kwenye sentensi.

#DARASA HURU
Na: Zacharia Emanuel,(Swahili Linguist & Translator)
WhatsApp+255755350165.
 
Back
Top Bottom