Ebu tujikumbushe kidogo hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Bungeni tarehe 30 Desemba, 2005 kuhusu Rushwa (ufisadi):
"Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake. Tutajitahidi kuongeza mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya Serikali hasa katika manunuzi na mikataba. Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa, hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi na Mahakama. Lakini yote hayo ni bure iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo. Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi.
Katika harakati za kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na Serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji. Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta utajiri.
Kadhalika, hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali. Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi yako ya utumishi au uongozi wa umma kujipatia manufaa ya kujitajirisha au kujilimbikizia mali.
Jambo hili ndilo linalokera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote lakini miezi michache tu baada ya kupata cheo anakuwa tajiri mkubwa. Ona majumba ya fahari, ona madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na kadhalika. Wananchi wanayo haki kuhoji, na wanayo haki kupata majibu. Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane. Nataka Tume ya Maadili ya Viongozi isione haya kutuuliza jinsi tulivyozipata mali tunazosema tunazo. Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo kama tatizo lenu ni hilo".
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete...ulisema mwenyewe....sasa tunataka majibu sahihi ni akina nani hao wanaorejesha hizo pesa na kwanini hadi sasa hawapo Keko au Segerea...ulituambia mwenyewe kwamba tunayo haki ya kuhoji...sasa twambie tuwajue wezi wetu ni akina nani?