Na Mbasha Asenga
RAFIKI yangu mmoja raia wa Kenya alinisimulia siasa za Wasomali kwamba pamoja na kujitia vichwa maji, kuna kitu kimoja tu kinawafanya wawe na suluhu ya muda katika mapambano yao.
Alisema kwa kawaida wakati wababe wa vita wakiwa wanaendesha ubabe wao wakipambana kwa kutumia kila aina ya silaha, kuna wakati huweka chini silaha zao, wakati huo si mwingine isipokuwa ni wa kupokea shehena ya mirungi.
Kwamba mzigo wa mirungi ukiingia mjini, Wasomali wanasahau tofauti zao, wanagawana kwanza mirungi kila mmoja anaondoka na hapo mapambano huanza upya.
Hakuna ubishi kwamba Wasomali wanapenda mirungi, huitafuna kwa bidii kubwa. Sina uhakika juu ya madhara yake katika mfumo wa chakula mwilini, lakini ni ukweli usiopingika kuwa watu hawa wamekuwa mateka wa mirungi. Huu ni ulevi mbaya kwa wasomali wengi.
Pamoja na ujeuri wa Wasomali na tamaa yao ya kuonyeshana ubabe katika vita, ulevi wa mirungi ni moja ya vitu vinavyowashawishi kusitisha vita japo kwa muda.
Ulevi huu wa Wasomali unafanana na hamu ya kutaka madaraka kwa wale wanaoitwa wapambanaji na watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM.
Kwa muonekano wa nje, tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani imejipambanua katika makundi makuu mawili; moja ni kundi la wapinga dhuluma, wizi, unyanganyi na aina zote za matendo ya ukingeukaji wa maadili ya kiuongozi na utumishi. Hawa ni wapambana dhidi ya ufisadi.
Mbili, ni kundi la watu waliokuwa wanatuhumiwa kwa kila uchafu; wameitwa chanzo cha njaa, umasikini na masaibu yote ya Watanzania. Wameitwa watu walafi, wanaopenda kujilimbikizia mali kwa njia za hila, na kwa ujumla wao ni watu wasiokuwa na huruma na kudumaa kwa maendeleo ya nchi kwani wao ndiyo kiini cha kudumaa huko.
Katika mazingira ya kawaida, makundi haya hayana tofauti na makundi ya wababe wa vita wa Kisomali kwa maana ya uhasama uliojijenga baina yao. Makundi haya ndani ya CCM yamepambana kwa takribani miaka mitatu, kila mmoja likitaka kuangamiza jingine. Mbinu sahihi na chafu zimetumika kumalizana.
Katika mapambano yao makundi haya yalijijengea uhasama wa kweli, chuki isiyoelezeka, lakini kwa mashangao wa wengi hivi karibuni waliweka tofauti zao pembeni kama vile Wasomali wanaosubiri kugawana shehena ya mirungi. Kwa Wasomali inajulikana, lakini kwa hawa wenzetu imekuwa ni vigumu kujua ni kitu gani hasa kiliwapa suluhu hiyo.
Kwa Wasomali suluhu ni mirungi, kwa makundi ya CCM ni uchaguzi. Kwa maneno mengine, wanasiasa wa CCM wanaweza kuweka rehani chochote; utu wao, hadhi yao, hisia za wananchi, matarajio ya wapigakura wao na hata imani ya umma kwao ili mradi tu wawe na uhakika walau wa kukubalika kuteuliwa kushiriki uchaguzi mkuu.
Kwa hali hii si jambo la kushangaza tena kusikia kwamba Wasomali wana kitu kinachowagusa kwa undani sana kiasi cha kutundika bunduki zao; kiasi cha kusahau ubabe wao japo kwa kitambo kidogo tu, kwani hata makundi mengine kama hapa nchini wana vitu vinavyofanana na hivyo.
Kwa Wasomali watu wanawashangaa, huku wakisahau kwamba hata ndani ya CCM makundi yake ambayo ni hasimu kwa maana ya neno hilo, yana ulevi wake mkali kama wa mirungi.
Yaani Wasomali wanapokuwa hawaelewi kitu wakati wanakosa mirungi, makundi ndani ya CCM hata kama yalikuwa na hoja gani za kimsingi dhidi ya kundi jingine?
Hata kama kundi moja lilikuwa limejikita kwenye hoja gani ya kukomboa wananchi, kutetea haki zao na kujitoa kwa nguvu zao zote kuendesha mapambano hayo, inapokuwa sasa ni kuamua juu ya uchaguzi, tofauti zao zinazikwa hapo hapo, tena kwa mbwembwe za ajabu kutaka kuusadilisha umma kwamba kazi imekamilika na kilichobakia ni umaliziaji tu.
Ulevi ni hali ya mtu kupoteza fahamu zake, aghalabu mlevi hufanya vitu ambavyo asilani hasingevifanya akiwa na akili timamu, ulevi humjengea mtu ujasiri wa kitambo, lakini nguvu ya ulevi ikimwacha, basi hujikuta katika sononeko kubwa la moyo; majuto makubwa na pengine kujilaumu ambako hakurejeshi kwa hali yoyote ile hali ya awali.
Ndiyo maana hadi leo wiki kadhaa sasa baada ya makundi ndani ya CCM kuonyesha wanavyolewa uchaguzi, kuthibitisha kwa kauli, mawazo na matendo halisi kwamba kwao hapendwi mtu ila ulevi uchaguzi, wengine tungali tunajiliza hivi baada ya Oktoba mwaka huu, wakishachaguana na kurejea bungeni, nani atathubutu kunyanyua kinywa chake na kutamba kwamba eti yeye ni mpambanaji dhidi ya maovu?
Je, nini sasa kitazuia hukumu ya umma kwa makundi yote hata ndani ya chama hiki kwamba wao ni ndugu mmoja, baba mmoja na mama mmoja, wao ni waumini wa kusaka madaraka ya wananchi, wapo tayari kuhadaa kwa njia zozote, lakini asilani si watetezi wa kweli wa hoja wanazojaribu kuzibeba kwa njia ya kuigiza.
Katika hali ya kawaida ilitarajiwa kwamba katika harakati za kuelekea uchaguzi ndipo makundi haya yachujane, kwamba wale wanaojipambanua ni watetezi wa wananchi, wenye uchungu na nchi hii wangejitwika hoja yao ili sasa umma uwaunge mkono kwenye sanduku la kura, lakini walichofanya wamegeuka na kukumbatiana na wenzao, katika dini moja na imani moja ya kuchaguana huku wakiuacha umma kwenye machungu na mashaka makubwa.
Kama kweli makundi haya hasimu ya CCM yameweza kufuta tofauti zao hata kama ni kwa kitambo kidogo tu ni uthibitisho kwamba wananchi kama wanataka ukombozi basi watasubiri sana , hakika hautaletwa na hawa wanaojitia kuwakilisha maslahi ya wananchi kwa sasa.
Kwa mara nyingine tena makundi ya CCM yamethibitisha kwa undani sana jinsi yanavyofungamana, kwao makundi ni igizo la muda kabla ya uchaguzi, uchaguzi ukiwadia ambao ndiyo ngazi muhumu kutafuta majemedari wa kuongoza mapambano ya ukombozi wa kweli wote ni wamoja, waugizaji na walaji, hawana nia wana sababu ya kukomboa nchi.
Kwa hili wamefanana na wale Wasomali wanaoweka chini bunduki za rashasha, jeuri na ubabe wote ili tu wagawane mirungi, kwa CCM wanatupa tunu ya uadilifu, uchapakazi, utumikiaji wa umma na ujemedari wa ukombozi kwa sababu tu ya kupata fursa ya kuchaguliwa kuwania madaraka ndani ya mchakato wa chama.
Source: MwanaHalisi