Watu wa makabila hayo walibahatika tu kupata elimu enzi ya ukoloni kabla ya watu wa makabila mengine. Ingekuwa ni Waha, Wanyaturu, Wakwere, na wengine walio elimika kuliko makabila mengine enzi hiyo, wangekuwa wanasemwa hivyo pia.
Ni wivu mtupu kuyalaumu makabila hayo.
Hata mimi niliwahi kusikia mara nyingi enzi ya Nyerere na baada ya Mwalimu kuondoka madarakani kwamba aliwazuia watu wa makabila hayo kupata nafasi ya uraisi na sehemu zingine za uongozi nchini. Hakuna uthibitisho Mwalimu alifanya hivyo.
Hakuwaamini kuongoza nchi lakini aliwaamini na maisha yake? Mnamkumbuka yule mlinzi wake mrefu, Mwangota kutoka Kyela, kwa miaka mingi? Tusimsahau daktari wake, Msokile mwingine - samahani Myakyusa - Mwakyusa.
Hili halina uhusiano na usalama wa Mwalimu au wa taifa lakini kati ya wakwe zake ni Mnyakyusa mwingine, Mwamakula. Sidhani hakumwamini kwa sababu alikuwa ni Mnyakyusa. Halafu kulikuwa na Wachaga, Wayakyusa, na Wahaya wengi katika usalama wa taifa enzi ya Mwalimu. Jeshini pia, kulikuwa na maofisa wengi kutoka makabila hayo. Alikuwa na wasi wasi kwamba watampindua? Sikuwahi kusikia.
Na yule aliyegusia hapo juu kuhusu chama kikubwa cha upinzani, si kweli kwamba ni cha Kichaga au ni cha Wachaga. Kimeshinda uchaguzi sehemu zote za Tanzania, pamoja na washindi wake walioibiwa kura katika uchaguzi mkuu uliopita. Pia kuna viongozi katika chama hicho kutoka watu wa makabila mbali mbali. Siyo Wachaga tu.
Ikiwa hatuaminiani kwa sababu ya makabila yetu, nchi yetu itapotea. Mhaya ana haki kuwa raisi wa Tanzania kama Mnyaturu; Mchaga ana haki kuwa raisi wa Jamhuri hii kama Mmakonde; Mnyakyusa ana haki kuwa raisi wa nchi yetu kama Mdigo, Mmatengo, Mzaramo, Mkinga, Mkurya, Mzanaki, Mluguru na kadhalika.