Mimi ninajua kuwa mwanamke akisimama kwenye nafasi yake amepewa "mamlaka" ya kujenga ndoa yake.
Ukisoma (Mithali 14:1)-
Kila mwanamke aliye na "hekima"hujenga nyumba yake, Bali aliye "mpumbavu" huibomoa kwa mikono yake mwenyewe".
Mara nyingi napenda sana kumkumbusha mwali wangu kwamba "ACHUNGE SANA ULIMI WAKE" kwani maneno yanaweza kuleta uharibifu na maumivu zaidi ya fimbo, kisu, jiwe, bunduki au hata bomu.
Maneno yanaweza kuleta madhara na majeraha ambayo sio rahisi kuyaponya.
Maneno yanaweza kusababisha vifo. Ukisoma katika Mithali 18:21 neno linasema; “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi."
Maneno tunayosema kwa ulimi bila kujali ni mazuri au mabaya, yanachoma. Katika Mithali 12:18 neno linasema; “Kuna anenaye bila kufikiri kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya." Maneno yakinenwa kwa kukurupuka, bila kufikiri hata kama hayakunenwa kwa lengo la kuumiza huchoma kama upanga. Kinyume chake maneno yakinenwa kwa busara na hekima huponya na kutia moyo.