Upasuaji wa kwanza bila kufungua kifua wafanyika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
JKCI yaanza kutoa huduma ya kibingwa kuweka 'valve' kwenye moyo bila kufanya upasuaji wa kifua

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza rasmi kutoa huduma ya kibingwa ya Uwekaji wa mlango wa moyo (valve) kupitia tundu dogo bila upasuaji wa kifua (Transcatheter aortic valve implantation- TAVI).

Akizungumza na wadau mbele ya vyombo vya habari Desemba 14, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa huduma hiyo kwa mara ya kwanza imefanyika nchini kwa kuhusisha wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na madaktari Bingwa kutokea hospitali ya Myhart Starcare Hospital nchini India, ambapo wagonjwa watatu amesema kuwa wamefanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri.

"Leo taasisi yetu ya moyo imefanya jambo kubwa sana kwa kubadilisha valve ya moyo kwa wagonjwa watu wazima ambao kwa kawaida ukiwafanyia upasuaji wa moyo wanapata shida kubwa wengine hata kupoteza maisha." amesema Dkt. Peter Kisenge

Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa kuna watu wengi nchini wenye changamoto ya aina hiyo, ambapo amedai kuwa baadhi yao awali walikuwa wakiwaelekeza kwenda Nchi za nje ili kupata huduma hizo.

"Wagonjwa wanye shida hiyo nchini wapo wengi ambao valve zao za moyo zimeziba, tulikuwa wengine tunawapeleka India na sehemu mbalimbali hili waweze kuokoka maisha yao familia zao zilikuwa zinateseka."amesema Dkt. Peter Kisenge

Akieleza kuhusu huduma hiyo amesema kuwa kwa Afrika ni Nchi chache ambazo zinatoa huduma ya TAVI ambapo ametolea mfano baadhi ya mataifa hayo kuwa ni pamoja na Afrika ya Kusini na Morocco, hata hivyo amedai kuwa katika tathimini aliyoifanya kuhusu huduma hiyo kwenye hospitali za Serikali kwa Afrika amebaini Tanzania kupitia JKCI ni hospitali ya kwanza ya Serikali kutoa huduma hiyo.

"Hakuna hospitali ya Serikali yoyote ya Afrika ambayo inatoa huduma hii, kwahiyo sisi ni wakwanza tumetengeneza hiyo historia na tunamshukuru Mh. Rais kwa kutuwezesha kuanza kutoa hii huduma," amesema

Aidha Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amesema kuwa jambo hilo ni matokeo ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kukuza huduma za kibingwa nchini.

"Uwekezaji kwenye sekta ya Afya ni jambo muhimu sana kwenye Nchi yoyote, ni muhimu kwa mtu mmoja mmoja lakini pia kwa maendeleo ya Taifa, ukiwa na Taifa la wagonjwa usitarajie kuwa na maendeleo hata kama una rasilimali kiasi gani au hata kama una mipango kiasi gani," amesema Dkt. John Jingu.

Akieleza juu ya uwekezaji huo amesema "Kwa mwaka wa fedha huu 2023 uwekezaji ambao umewekwa kwenye sekta ya afya kwa ujumla ni zaidi ya Tilioni 7 ni uwekezaji mkubwa, lakini linalohusiana shughuli yetu ya leo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Bilioni tano kwa ajili ya kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi na moja ya taasisi zilizonufaika na uwekezaji huu ni taasisi ya JKCI."

Kwa upande wa Hospitali ya Myhart Starcare ambao wameshirikiana na wataalamu wa ndani kufanikisha suala hilo kupitia Mkurugenzi Mkuu, Asishkumar Mandalax amepongeza jitihada za Serikali kuwekeza kwenye huduma za kibingwa hususani vifaa ambavyo vinavyotumika kufanikisha huduma hiyo kutolewa.

Amesema kuwa vifaa hivyo vina ubora ambao unawezesha huduma hiyo vitawezesha huduma hiyo kufanyika vizuri, ambapo amedai kuwa hilo amelishuhdia katika mchakato wa wagonjwa waliopatiwa huduma hiyo kwenye taasisi hiyo.

Kufuatia huduma hiyo kuanza kutolewa nchini imeelezwa kuwa itasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa ambao walikuwa wakifanyiwa upasuaji muda mrefu na kukaa hospitilini hapo wakiuguza vidonda, ambapo kwa sasa mgonjwa anaweza kupatiwa huduma hiyo ndani ya muda mfupi kwa siku mbili au tatu akaruhusiwa kuondoka.

Hata hivyo Dkt. Peter Kisenge ametoa ombi kwa Serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu mipya ya majengo, ambapo amedai kuwa kwa sasa wanapokea wagonjwa wengi hata kutoka nje ya Nchi huku akieleza kuwa kuanza kutolewa kwa huduma hiyo ya kibingwa kutachochea zaidi ongezeko la wagonjwa hivyo suala la miundombinu muhimu, katika hoja hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Afya amepokea ombi hilo na kuahidi kulifanyia kazi kwa wakati sambamba na ombi la baadhi ya madawa kujumuishwa kwenye bima ya afya ya NHIF.
 
Kwa gharama hiyo, ndugu zangu wa hali ya chini mkae tu pembeni. Waacheni matajiri watibiwe. Au mkubali tu kuendelea na utaratibu wa zamani wa kupasuana vifua.
 
Back
Top Bottom