Watu 335 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo kwa siku mbili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
Watu 335 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwenye kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt.Tulizo Shemu alisema matibabu hayo ya tiba mkoba yajulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yalifanyika maalumu kwaajili ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Picha no. 1.jpg

Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jane Mathew akimpima kiwango cha sukari kwenye damu mtoto aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.

Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema katika kambi hiyo watu waliowaona walitoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam na wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu pamoja na matatizo mengine ya moyo.

“Nusu ya watu tuliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wengine walikuwa na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu ya moyo kuziba, mafuta mengi kwenye mishipa ya damu, maumivu ya kifua, shida za valvu, shida ya mfumo wa umeme wa moyo pia tumewaona watoto waliokuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa kwenye mpangilio wake”,.

“Tuliowakuta na shida za moyo na wengine waliokuwa na shida mbalimbali za mwili kama vile masikio, mifupa, ngozi, macho tumewapeleka katika kliniki zetu kwaajili ya matibabu kwani katika hospitali hii licha ya kutibu moyo tunatibu pia magonjwa mengine pia wengine tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)”, alisema Dkt. Shemu.

Picha no. 5.jpg

Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) makao makuu na Hospitali ya Dar Group wakichukuwa taarifa za wananchi waliofika katika Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana.

Dkt. Shemu alisema kambi za aina hiyo zitakuwa zinafanyika mara kwa mara katika Hospitali hiyo kwani kwa kufanya hivyo wananchi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani watafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Kwa upande wao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kuomba iwe endelevu ili watu wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Picha no.4.jpg

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Janeth Mmari na Husna Faraji wakitoa ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo na lishe bora kwa wananchi waliofika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.



Tatu Hassan mkazi wa Shinganya alisema aliona katika TV tangazo la kufanyika kwa matibabu hayo na kuchukuwa hatua ya kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Ninaishukuru Serikali kwa kutuangalia wananchi wanyonge wenye kipato cha chini na kutufikishia huduma hii ya matibabu ya kibingwa. Nimefika hapa nimefanyiwa vipimo, nimepewa ushauri na dawa za kwenda kutumia mwezi mmoja kwani mimi ninatatizo la shinikizo la juu la damu ambalo limepelekea moyo wangu kutanuka”, alisema Tatu.

“Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu wanapoona matangazo ya upimaji wa magonjwa mbalimbali wasipuuze wawahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu mapema kuliko kusubiri hadi waumwe ndipo waende kutibiwa”, alisema Richard John mkazi wa Tegeta.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwa kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Hadi sasa wameshatoa huduma hiyo katika mikoa 12 na kuona watu 7196 ambapo 847 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo.
 
Back
Top Bottom