SoC02 "Ulevi" wa mafanikio ya baba na madhara yake kwenye uwajibikaji wa familia

Stories of Change - 2022 Competition

Idrissou02

JF-Expert Member
Jul 31, 2018
354
643
Imeandikwa na : IDRISSOU02
Mdau wa JF.



images (9).jpeg

Picha na Sema Tanzania

Hakika kila mtu anatamani mafanikio. Hata yule mtu mwenye mafanikio tiari, bado anatamani awe na mafanikio zaidi. Kutamani maisha yaliyo bora zaidi ndio kichochezi kikubwa kinachofanya watu waendelee kupambana usiku na mchana. Je, unaweza kumudu angalau milo mitatu kwa siku kwa kujitegema? Vipi kujivalisha na kuwavalisha uwapendao nguo nzuri ? Vipi kuzunguka sehemu mbalimbali unazozipenda na watu wako wa muhiimu? Maswali hayo na mengine mengi zaidi juu ya maisha yako, yanaweza kukupa mwangaza wa kuona kama umefikia mafanikio ama la. Jambo la muhimu kabisa la kuzingatia hapa ni kwamba hatimae ukifikia mafanikio yako ya kidunia basi hayapaswi kutia doa uwajibikaji wako kwa familia.

Ugumu wa maisha halisia ya mtu anapotoka yanachangia kwa kiasi kikubwa jinsi atakavyokuwa anaishi baada ya kuonja mafanikio. Mabadiliko haya yanaweza yasiambatane na nia mbaya bali ushamba wa kuyaendea maisha ambayo alikua anayatazama tu kwa macho ambao unaweza kuleta madhara makubwa mno ambayo hakuyadhamiria. Watu wametoka mbali bana, kuanzia kutembea kilomita 7 kwenda shule kwa viatu visivyokuwa na sakafu na soksi zilizochora ramani ya Africa alafu kurudi nyumbani na uchovu lakini bado kazi rundo nzima zinakusubiri mpaka kufikia leo hii ambapo siku nzima unatembea si zaidi ya mita 100 huku mwendo mwingine wote ukiutumia juu ya chombo chenye magurudumu manne. Naam, inavutia sana tena mpaka unafaa kuwa "motivesheno spika" lakini hiki kisiwe chanzo cha familia yako kupitia kipindi kigumu kwasababu ya ulevi wa mafanikio.

5a64ed6142f15d29711fcbd9d4d35f3e(1).png

Picha na Capital News

Mungu si athumani na siku zote ndiye anayechagua wa kumpa na kumnyima. Ulifika mjini kwa nia ya kubadilisha maisha yako, angalau na wewe upeleke mkono mdomoni kwa jasho lako mwenyewe na uishi kwa uhuru unaoutaka. Matarajio yakawa zaidi ya ulivowaza, mungu akakubariki kwelikweli ukawa una maisha ambayo pengine ungeambiwa ungekuja kuyaishi miaka mitano iliyopita ungekataa kata kata; tena ingewezekana ungezua ugomvi kwa kuona kama vile mtu anakudhihaki. Ukapata "koneksheni" nzuri ya watu, madili mengi mazuri yalikuja upande wako; ulevi wa mafanikio ukaanza kukuingia kidogo kidogo ukawa malaya wa kupindukia. Eeeeh bana itakuaje uache kutafuna viumbe ambavyo ulikuwa ukivitamani sana alafu uwezo wa kuvipata ulikuwa huna? Paukwa pakawa, ukatumbukia kwenye maisha ya ndoa, ukiwa bado hujaumaliza ushamba wako wa ulevi wa mafanikio.

Kuna kitu ambacho pengine wazazi wengi hawajakifahamu. Kuchukua muda wa kutosha kukaa na familia yako kuna maana kubwa sana. Inakuaje baba upo bize mpaka wikiendi wakati siku za kazi wewe unaondoka nyumbani mwiko wa jogoo na kurudi milio ya popo? Ushamba wa mafanikio unakufanya uzurure viwanja mbalimbali, kila chocho maarufu hutaki ikukose, watoto wako wanakuona kwa manati; unategemea mapenzi mazito kweli kutoka kwa wanao. Inawezekana ndio sababu ya kesi za watoto kuua wazazi wao ili kurithi mali zimekua nyingi mno, maana mtoto hana mapenzi kwa mzazi. Kwanini usitumie mafanikio uliyoyapata kuipa maisha bora familia yako yote, na hapa maisha bora hayamaanishi kuacha hela ya matumizi tu nyumbani kila siku bali kuwa sehemu ya familia yako. Familia yako usiifanye kama sehemu tu ya makato ya kipato chako kama makato ya NSSF ama NHIF. Unakuta mtoto anakuja kuishi na baba ake tiari baba ameshastaafu amezeeka, baba hajui tabia za mwanae na mtoto nae ameshakua mtu mzima anaona uwepo wa baba nyumbani ni kama vile mzigo au mtu baki aliyekuja kuingilia maisha ya nyumbani; unategemea nini hapo.

Kunywa pombe sio tatizo kubwa, tatizo baba unarudi nyumbani umelewa chakari unaanza kusababisha mizozano na mkeo ambae tiari ana pengo la kuziba la baba kutokana na kutokuepo kwako kana kwamba yeye ni mjane alafu bado hapahapo ana jukumu la kuwa mama, tabu tupu. Uwajibikaji sifuri ambapo hata kufuatilia maendeleo ya watoto wako na kumpendezesha mke wako imekua si jukumu lako tena wakati unatengeneza fedha nzuri tu.

629467185f343fb4352e0879909899e2.png

Picha na Healthline

Kwako sasa ndugu wamekua ni watu wasumbufu. Yawezekana kweli kuna baadhi ya ndugu ni wasumbufu na hawana nia njema lakini isiwe sababu ya wewe kujitenga na kuwapa pointi za kukuongelea vibaya. Madhara yake hayatoishia kwako tu, yatatembea mpaka kuathiri uhusiano wa watoto wako na ndugu wengine ambao ni wema tu na mngeweza kushirikiana kwenye mambo kadhaa mazuri. Ushawahi kuona ndugu ambao wazazi wao wamezaliwa tumbo moja lakini hawapatani kisa tu mababa zao walikua hawaelewani. Chungeni sana wababa, vitendo vyenu vinawatengenezea vikwazo na maisha magumu watoto wenu.

Kabla sijamaliza siwezi kuacha kuzungumzia jambo hili ambalo baadhi yenu wasomaji mtakua mmeshakua mashahidi. Wewe mwanaume mthamini sana mkeo, mthamini sana mkeo ambaye anakulelea vizuri watoto wako japo anaweza akawa ana mapungufu machache. Pengo lake ni kubwa mno siku akija kuondoka ama kufariki, haki ya mungu utatambua maana ya wanaosema thamani ya ulichonacho utakiona kipindi hauna tena. Hatakama una michepuko yako uko nje inakupa raha zaidi ya mkeo, heshima na uwajibikaji wako kwa mkeo na familia ubaki imara vilevile lasivyo utatengenza madhara yatakayodumu kwenye kizazi chako chote. Wangapi ambao walitoa talaka kwa pupa na kusababisha watoto wao waishi na mama wa kambo ambao pia walikuja kuwaacha kwa kuona bora angebaki na aliyekua mkewe wa kwanza? Tuwe makini mno na masuala ya familia, uamuzi wako mdogo unaweza kupindua mueleko mzima wa familia.

View attachment 2311978
Picha na Mtanzania

Siku zote muda wa kubadilika upo ni wewe tu kuamua. Ewe baba au mwanaume ambae anatarajia kuwa baba siku moja zingatia uwajibikaji lasivyo usimchukue binti wa mtu na kwenda kumfanya aone maisha machungu kwasababu yako. Ewe mama au mke wa baba ambae sio mwajibikaji, ufahamu kwamba kila mtu anahitaji nafasi nyingine kujirekebisha. Mpe nafasi nyingine baba wa familia yako ajirekebishe pengine mungu atamjaalia hekima kupitia nafasi uliyompatia. Alamsiki.

images (10).jpeg
 
Hii ni kwa wazazi wote, ajabu amekuwa akishambuliwa baba tu!!
Una maana nzuri kwamba hii inawahusu wazazi wote lakini kwenye jamii yetu baba ndiye ana jukumu la kuihudumia familia upande wa fedha. Unakuta hatakama mama ana kazi nzuri bado huduma kubwa ambayo inaitaji fedha anakuwa nayo baba. Nadharia hii imemfanya mtoto wa kiume kuanzia akiwa mdogo anachakarika na kupambana ili aje kuwa na uwezo wa kuhudumia familia baadae, nadharia ambayo haipo kwa akina mama wengi ambao ukikuta wanahangaika basi imewabidi kwasababu ya mazingira fulani.
 
Wadau tuendelee kutoa maoni yetu juu ya mada hii ili kupaza sauti dhidi ya wababa wa namna hii. Madhara kwenye familia ni makubwa mno.
 
Mfumo wa maisha ya watanzania kiutamaduni unamtaka baba afanye kazi kubwa sana kulea na kutunza familia. Andiko lako ni zuri sana ila limeegemea baba ambaye anafanya kazi na kisha kustarehe na michepuko na pombe. Binafsi siko hivyo ila bado naangukia kwenye kundi la watafutaji ambao mwisho wa siku tunakosa muda na familia

Sio tu kwa kuwa nakaa baa hapana ni mfanyakazi na pia nina biashara muda mrefu natumia kupambana ili niwe na mafanikio zaidi. Kuna kipindi nashindwa kubalance familia na kazi zangu. Nashindwa kusimamia watoto kiasi kwamba naona kabisa mama ndio kila kitu kwao licha ya kuwatimizia mahitaji yote

Utamaduni wa kumfanya baba kuwa ndio kila kitu unatutesa sana wanaume. Pia unasababisha watoto kuwachukia baba zao at the end of the day
 
Mfumo wa maisha ya watanzania kiutamaduni unamtaka baba afanye kazi kubwa sana kulea na kutunza familia. Andiko lako ni zuri sana ila limeegemea baba ambaye anafanya kazi na kisha kustarehe na michepuko na pombe. Binafsi siko hivyo ila bado naangukia kwenye kundi la watafutaji ambao mwisho wa siku tunakosa muda na familia

Sio tu kwa kuwa nakaa baa hapana ni mfanyakazi na pia nina biashara muda mrefu natumia kupambana ili niwe na mafanikio zaidi. Kuna kipindi nashindwa kubalance familia na kazi zangu. Nashindwa kusimamia watoto kiasi kwamba naona kabisa mama ndio kila kitu kwao licha ya kuwatimizia mahitaji yote

Utamaduni wa kumfanya baba kuwa ndio kila kitu unatutesa sana wanaume. Pia unasababisha watoto kuwachukia baba zao at the end of the day
Upo sahihi kabisa mkuu, ndio maana watu wanaoongoza kwa kuathirika na msongo duniani ni wanaume
 
Back
Top Bottom