BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 422
- 1,049
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila
Viongozi mbalimbali wametembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi ambalo pia linajulikana kama Daraja la JP Magufuli, leo Jumapili Aprili 23, 2023.
Daraja hilo linapatikana Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, bado lipo kwenye hatua ya ujenzi. Hivi ndivyo viongozi walivyozungumza baada ya kufika eneo la tukio.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima:
Katika Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna vitu viwili vinavyoweza kuwa katika vivutio, navyo ni Uwanja wa Ndege wa Mwanza na Daraja la JP Magufuli (Daraja la Kigongo - Busisi).
Ukishuka Mwanza ukaja Busisi na kutumia saa zaidi ya tatu kuvuka ni rahisi kuahirisha kufanya utalii, lakini uwepo wa daraja hili utasaidia kurahisisha mawasiliano na hata utalii utaongezeka.
Kamati ya Ulinzi na Usalama tulikuwa tunafuatilia, kulikuwa na udokozi wakati ujenzi ukiendelea, mtu anaona anawaibia Wachina kumbe anawaibia Watanzania wenzake.
Michezo hiyo ilikuwa inafanywa, tumefinya na tumeshatuma salamu kwa kuwa vifaa vilikuwa vinaibiwa na kupelekwa Usagara, Sengerema au Buhongwa.
Tukimkuta mtu ambaye ana vifaa vinavyotokana na mradi tutafunga duka na hatafanya tena biashara Mwanza na tutamfungulia kesi ya uhujumu uchumi kisha atatueleza anaoshirikiana nao.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja:
Nampongeza Rais Dkt. Samia anavyoendelea kufungua fursa mbalimbali ikiwemo daraja hilo, ukanda huu wa Ziwa Victoria tunatamani utalii uzidi kukua.
Utalii wa Ukanda wa Kaskazini ni kama umejaa kwa kuwa watalii wengi wanaenda huko, lakini tuna vivutio vingi Ukanda huu wa Ziwa pia, hivyo lengo la mradi hii kama ya daraja ni kufungua uwekezaji na kutengeneza mazingira ya utalii.
Tunataka watalii wanapokuja Nchini wazunguke huku na huku badala ya kuegemea upande mmoja.
Ukanda wa Ziwa tuna vivutio vingi kama ilivyo Ukanda wa Kaskazini, miundombinu ikikamilika kama barabara na daraja kutakuwa na ongezeko la Watalii na haya uchumi utakua kwa kuwa kutakuwa na mzunguko wa fedha.
Sekta ya Utalii inachangia pato kubwa Serikalini takribani 18% hadi 21%, kuna ajira na uwekezaji, pia watu wanaburudika.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila:
Daraja hili lina umuhimu kwa Watu wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa jumla, mfano kufika Mwanza kwenda Geita au Sengerema ilikuwa ni lazima uzunguke hadi Kahama, hivyo Daraja la Busisi litarahisisha mzunguko wote huo.
Daraja hili litaunganisha watu wa Mwanza, Geita, Kagera na Nchi jirani ya Uganda, kwa huo ukaribu utatumia muda mfupi kwenda nchi nyingine zinazotuzunguka kama Rwanda.
Watu walikuwa wanatumia vivuko na mitumbwi na wanachukua zaidi ya saa mbili hadi nne huku kukiwa na msongamano, lakini daraja hili litawahisisha na kupunguza muda, wanaweza kutumia dakika tano kuvuka.
Daraja hili lilianza kujengwa Mwaka 2020 baada ya mkataba kusainiwa Mwaka 2019 na hatua ya ujenzi imefikia 72%.
Makubaliano ya mkataba ni kuwa linatakiwa kukamilika Februari 25, 2024 kulingana na makubaliano yaliyopo, kuhusu kasi ya Mkandarasi tunaridhishwa nayo.
TANROADS tunasimama kwa niaba ya Serikali katika mradi huu na sisi ndio tunaosaini mikataba na kusimamia mchakato wote ili kuhakikisha ubora unafikiwa kama ulivyopangwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya:
Tumefanya kazi kubwa katika Mkoa wa Mwanza kwenye Wilaya ya Sengerema na Misungwi, ambapo tumesaini mkatana wa ujenzi wa Kivuko cha Buyagu-Mbarika ambacho hakikuwepo kabisa Ziwa Victoria.
Hayo ni maeneo yanayotazamana lakini hakukuwa na kivuko, lakini kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kukaonekana kuna umuhimu huo.
Baada ya kusikia kilio cha wananchi Rais Dtk. Samia akatoa maelekezo ya ujenzi wa kivuko kitakachokuwa na uwezo wakubeba wananchi 100 na tani 50 na kitajengwa na mkandarasi mzawa Songoro Marine.
Aidha, tumefanya ziara ya kushtukiza kuja kutazama maendeleo ya Daraja la Busisi lenye urefu wa Kilometa 3 ambalo linapita kwenye maji.
Hili ni moja ya madaraja marefu Afrika, taarifa ya Wakandarasi na msimamizi ni kuwa mradi utakamilika Februari 2024, fedha inayotumika ni ya Tanzania na bahati nzuri hakuna deni ambalo mkandarasi anaidai Serikali.
Likikamilika linatarajiwa kugharimu Tsh. Bilioni 716, faida ya uwepo wa daraja hili ni kama lango la kuingilia Mwanza.
Daraja limezingatia viwango vya juu, linaweza kuwa imara kwa zaidi ya miaka 100.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja
Meneja wa TANROADS Mwanza, Mhandisi Pascal Ambrose:
Mbali na araja la Busisi pia kuna mradi mingine kadhaa, mfano kuna barabara yenye takribani Kilometa 150 kutoka Mwananga hadi Kahama.
Usanifu umeshakamilika kuanzia Mwaka 2017, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Pia kuna usanifu tumeufanya wa barabara kutoka Mwanza hadi Nyanguge kuelekea mpakani na Simiyu.
Ili kupunguza msongamano kipande cha Mwanza hadi Nyanguge usanifu umefanyika wa njia nne.