Uchambuzi wa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi Bandari Tanzania na DP WORLD

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Utangulizi
Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari za Bahari na Maziwa Makuu ya Tanzania, unaletwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kuridhiwa.

Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding- MoU) Mnamo tarehe 28 Februari, 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority [TPA]) iliingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding [MoU]) na Kampuni ya DP World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai (the Emirate of Dubai). Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors).

Kusainiwa kwa Mkataba (Intergovernmental Agreement-IGA) Mkataba huu ulisainiwa na Serikali zote mbili mnamo tarehe 25 Oktoba, 2022. Ibara ya 25 ya Mkataba inaelekeza kuwa baada ya

kusainiwa Mkataba huu, shughuli za awali za utekelezaji wa mradi (early project activities) zitaanza kufanyika. Shughuli hizo ni kama vile upembuzi yakinifu, kufanya tathmini ya kimazingira na kijamii ya mradi huu (environmental and social due diligence), kujenga barabara za kuwezesha kufika eneo la mradi, nk.

Aidha, mchakato wa kuridhia Mkataba utaanza ndani ya siku thelathini (30) mara tu baada ya kusainiwa Mkataba. Lengo ni kuyafanya masharti ya Mkataba kuzibana pande husika chini ya Sheria za Kimataifa (to make this a binding obligation of each State Party under the International Law). Kutokana na masharti hayo, Mkataba umeletwa Bungeni ili ujadiliwe na hatimaye upate kuridhiwa kwa Azimio la Bunge.

Uchambuzi wa Mkataba​

Mkataba unaanza na Masharti ya Utangulizi (Preamble). Aidha, Mkataba una Sehemu Nne zenye jumla ya Ibara 31. Sehemu ya I ni Tafsiri, Ufafanuzi na Mawanda ya Mkataba. Sehemu ya II inahusu Wajibu wa Jumla, Sehemu ya III inahusu Usimamizi wa Masuala ya Kikodi, na Sehemu ya IV ni Masharti ya Mwisho. Mwishoni mwa Mkataba kuna Viambatisho (Appendices), ambavyo ni; maelezo ya maeneo ya ushirikiano (Areas of Cooperation) na Hati za kutoa Mamlaka ya kutenda kwa niaba ya Serikali zote mbili (Instrument of Full Powers).

SEHEMU YA I- TAFSIRI, UFAFANUZI NA MAWANDA (DEFINITIONS, INTERPRETATION AND SCOPE)
Ibara ya 1 (Definition and Interpretation)

Ibara ya 1 inatoa tafsiri na ufafanuzi wa misamiati na maneno mbalimbali yaliyotumika katika Mkataba huu.

SEHEMU YA II- WAJIBU WA JUMLA (GENERAL OBLIGATIONS)
Ibara ya 2 (Objective of the Agreement)

Ibara ya 2 inafafanua lengo la Mkataba (Objective of the Agreement), ambalo ni kuweka mfumo wa kisheria katika maeneo ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors).

Aidha, maeneo mengine ya ushirikiano ni katika kujenga uwezo (capacity building), kuhaulisha maarifa, ujuzi, na teknolojia (transfer of knowledge, skills and technology), kuimarisha taasisi za elimu na kusaidia upatikanaji wa masoko.

Ibara ya 3 (Cooperation)
Ibara ya 3 inaelekeza pande zote mbili kushirikiana kwa lengo la kuweka na kudumisha mazingira muhimu na yanayofaa kuweza kutekeleza shughuli za mradi huu. Wawakilishi wa kila Serikali watakutana kwa nia njema wakati wowote unaofaa na mara nyingi kadiri inavyowezekana, kwa malengo ya kujadiliana na kuingia mikataba mingine kadiri itakavyoonekana inafaa kwa Serikali zote mbili, kwa lengo la kuidhinisha, kuwezesha na kusaidia utekelezaji wa shughuli za mradi.

Serikali husika zitaunda Kamati ya Ushauri (IGA Consultative Committee) kwa ajili ya kuratibu shughuli za pande zote mbili katika utekelezaji wa Mkataba. Aidha, Ibara inaekeza juu ya kufanyika kwa upekuzi kuhusu mwenendo wa shughuli za mradi na masuala ya ubadilishanaji wa taarifa na utunzaji wa siri.

Ibara ya 4 (Scope of Co-operation and Implementing Entities) Ibara ya 4 inaweka mawanda ya ushirikiano na taasisi za utekelezaji (scope of co-operation and implementing entities). Mawanda ya Mkataba huu ni kuwezesha utekelezaji katika maeneo ya ushirikiano kama ilivyoainishwa katika Kiambatisho 1 (Appendix

1
).
Maboresho katika bandari ya Dar es salaam yatafanyika kwa awamu mbili.

Awamu ya kwanza ni kuendeleza, kusimamia na kuendesha magati ya bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni; gati la RoRo, magati namba 1-4 ya kutunzia mizigo, magati namba 5-7 ya kutunzia makontena na gati la abiria litakaloendeshwa na TPA. Aidha katika awamu hii itaendelezwa, kusimamiwa na kuendeshwa bandari kavu ya Kwala ya kutunzia makontena na bandari kavu ya Kurasini. Pia kuendeleza, kusimamia na kuendesha gati mpya ya RoRo ya kutunzia makontena, kuhamishia yadi ya RoRo kwenye eneo la EPZA na kujenga ghorofa la kuwezesha kuhifadhi magari mengi kwa wakati mmoja (multi storey car park), na kuboresha yadi ya RoRo kuwa yadi ya kuhifadhia mizigo na makontena.

Katika awamu hii, itawekwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA inayohitajika na TPA kwa ajili ya kutoa huduma bora na zenye ufanisi wa kuridhisha na kwa uwazi kwa Watanzania na wadau, katika uendeshaji wa bandari za Tanzania.

Aidha, katika awamu ya kwanza, itawekwa mifumo bora na ya kisasa ya utoaji huduma za meli katika bandari ya Dar es Salaam, na mwisho Kampuni ya DPW itatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA, ili waweze kumudu kuendesha mifumo itakayowekwa.

Awamu ya pili itahusu kuendeleza maeneo ya maegesho na kuhifadhi mizigo (logists platforms), maeneo mahsusi ya kiuchumi (special economic zones), kuendeleza hifadhi ya viwanda, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa maendeleo ya kibiashara na kanda za kibiashara zinazohudumia nchi zisizokuwa na bandari (landlocked countries) za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika. Aidha awamu hii itahusika na maboresho kwa kupanua au kuongeza bandari za bahari na maziwa makuu, na kuongeza mtandao wa kufanya biashara kati ya Tanzania na nchi zisizokuwa na bandari.

Ibara ya 5 (Rights to Develop, Manage or Operate)
Ibara ya 5 inatoa haki za kipekee (exclusive rights) kwa Kampuni ya DPW yenyewe moja kwa moja au kupitia kampuni washirika (Affliates), za kuendeleza, kusimamia na kuendesha miradi kama ilivyoainishwa kwenye Kiambatisho 1 (Awamu ya Kwanza).

Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa TPA haitapokea maombi mengine kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa katika Kiambatisho 1, Awamu ya Kwanza, mpaka hapo mazungumzo kati ya TPA na DPW yatakapokuwa yamesitishwa, au baada ya kupita kipindi cha miezi 12 baada ya kusainiwa Mkataba huu.

Ibara ya 6 (Relevant Government Consents and Approvals) Ibara ya 6 inaelekeza Serikali ya Tanzania, kwa kuzingatia sheria za nchi, kuhakikisha inatoa kwa Kampuni ya DPW, vibali, haki ya matumizi ya ardhi, nafuu au motisha za kiuwekezaji na misamaha ya kikodi, ili iweze kutekeleza kwa ufanisi shughuli za mradi.

Ibara ya 7 (Project Authorisations)
Ibara ya 7 inaielekeza Serikali ya Tanzania kutoa au kuhuisha kwa wakati, vibali vinavyotakiwa kutolewa au kuhuishwa kwa ajili

ya Kampuni ya DPW na au TPA, ili kuwezesha utekelezaji kwa wakati miradi iliyoainishwa.

Ibara ya 8 (Land Rights)
Ibara ya 8 inaitaka Serikali ya Tanzania kutoa haki za kupata na kutumia ardhi (Land Rights) kwa kampuni ya DPW ili iweze kuingia na kutumia ardhi kwa madhumuni ya utekelezaji wa miradi. Serikali italinda haki za ardhi zilizotolewa kwa Kampuni kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Serikali ya Tanzania itachukua kila hatua inayostahili kwa mujibu sheria za nchi, kuhakikisha kuwa haki za ardhi katika mradi zinalindwa muda wote na kwamba mradi hautaathiriwa na ujenzi wa miundombinu kupita eneo la mradi au mendelezo yoyote jirani na eneo la mradi.

Ibara ya 9 (Investment Incentives)
Kutokana na mawanda mapana ya uwekezaji huu na ufanisi au manufaa yanayotegemewa kijamii na kiuchumi, Serikali zote mbili zinakubaliana kuwa Serikali ya Tanzania itatoa motisha za kiuwekezaji (investment incentives) kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Ibara ya 10 (Confidentiality)
Ibara ya 10 inazitaka Serikali zote mbili kutotoa taarifa ya siri inayohusu Mkataba huu, kwa mtu yeyote na kwasababu zozote zile, pale ambapo imekubaliwa kuwa taarifa hiyo ni ya siri na nyeti kibiashara kwa pande zote, isipokuwa taarifa hizo zinaweza kutolewa kwa kibali cha maandishi kutoka kwa DPW na TPA.

Ibara ya 11 (Non-Discriminatory Treatment)
Ibara ya 11 inazuia ubaguzi kwenye kutoza tozo, kodi na ushuru. Mkataba huu unazitaka mamlaka husika nchini Tanzania kutoza kodi, tozo na ushuru kwa kampuni ya DPW, shughuli za mradi au watu (ikiwa ni pamoja na watoa huduma), kwa kuzingatia sheria zilizopo. Sheria husika zitumike kwa nia njema, kwa uwazi na kwa namna ambayo ni ya haki bila kuleta ubaguzi.

Ibara ya 12 (Safety and Security)
Ibara ya 12 inahusu masuala ya Ulinzi na Usalama. Pande zote mbili zinakubaliana kuwa ulinzi na usalama ni jambo la kipaumble katika shughuli za mradi, ikiwa ni pamoja na ardhi inayotumika kwenye mradi, mifumo, watu, bidhaa na vifaa vilivyowekwa juu au chini ya ardhi ya mradi au maeneo ya mradi au vilivyofungwa kwenye eneo la mradi au eneo la shughuli za mradi katika mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali ya Tanzania itaingia Mikataba na Kampuni ya DP World ili:
Kuweka mfumo wa wazi wa majukumu na utendaji wa Serikali kuhusu ulinzi na usalama,
Kufafanua maeneo ya utekelezaji ulinzi na usalama wa Mradi ambayo Kampuni ya Mradi itawajibika,
Kuweka masharti yanayoitaka Serikali husika na Kampuni ya Mradi kushauriana, kushirikiana na kufanya uratibu kuhusu kuendeleza na kutekeleza masuala yote ya ulinzi na usalama wa Mradi.

Ibara ya 13 (Local Content, Employment and Corporate Social Responsibilty)​

Ibara ya 13 ni juu ya masuala ya ushirikishaji wa wazawa katika mradi, ajira na uwajibikaji wa Kampuni katika jamii (Local

Content, Employment and Corporate Social Responsibility). Masuala hayo yanatakiwa kupewa kipaumbele katika mikataba itakayoingiwa katika utekelezaji wa mradi huu.

Kampuni ya DPW itazingatia kutoa ajira kwa watanzania na kuwapa mafunzo, kuheshimu ajira zilizokuwepo. Aidha katika suala la kuwashirikisha wazawa (local content) inasisitizwa kipaumbele kitolewe kwa taasisi za ndani na watu katika ununuzi wa bidhaa, kazi, huduma za ushauri elekezi na zisizokuwa za ushauri elekezi (consultancy and non-consultancy services), pale ambapo taasisi hizo zipo na zinakidhi vigezo vinavyotakiwa.

Ibara ya 14 (Expropriation)
Ibara ya 14 inazuia utaifishaji wa mali za Kampuni (expropriation). Tanzania haitataifisha mali zozote za Kampuni zinazohusiana na mradi, ikiwa ni pamoja na mifumo, mali, hisa, mikopo, nk.

Endapo Serikali itaamua kutaifisha mali za Kampuni; itafanya hivyo kwa manufaa ya umma kwa kuzingatia taratibu za kisheria, na si kwa sababu za kiubaguzi. Inaelekezwa kuwa malipo ya fidia stahiki na ya kuridhisha yafanyike mapema kwa watu wote watakaoathiriwa na utaifishaji huo.

Ibara ya 15 (Environmental, Occupation Health, Social and Safety Standards)​

Ibara ya 15 inazielekeza pande zote mbili za Mkataba kuzingatia masuala ya mazingira na vigezo vya usalama na afya mahali pa kazi (Environmental, Occupational Health, Social and Safety Standards).

Utekelezaji wa mradi utazingati sheria za Tanzania pamoja na za Kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na vigezo vya usalama wa afya mahali pa kazi. Kampuni itazingatia viwango vya Kimataifa katika kuzuia uchafuzi wa mazingira baharini (International Standards for the Prevention of Marine Pollution at Sea).

Ibara ya 16 (Technical Standards)
Ibara ya 16 inafafanua kuhusu viwango vya kiufundi (technical standards) katika kutekeleza shughuli za mradi. Mkataba unazitaka DPW na TPA kuzingatia viwango vya Kimataifa vya kiufundi katika kusanifu, kukuza, kujenga, kuendesha, kuendeleza, kukarabati, kubadilisha, kupanua au kuongeza ukubwa wa miundombinu na uendeshaji wa mradi kwa ujumla. DPW na TPA zitashauriana mara kwa mara kuhusu viwango vya kiufundi vinavyotakiwa.

Ibara ya 17 (Labour Rights)
Ibara ya 17 inahusu haki za wafanyakazi (labour rights) ambazo zinatakiwa kuzingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa mradi, kwa kuzingatia masuala ya mazingira na viwango bora vya usalama wa afya mahali pa kazi na kwa kuzingatia vigezo vya hali ya juu vya Haki za Binadamu.

SEHEMU YA III- USIMAMIZI WA MASUALA YA KIKODI (FISCAL REGIME)
Ibara ya 18 (Taxes, Duties and Other Charges)

Pande zote katika Mkataba zinakubaliana kuwa utozaji kodi, tozo na ushuru utazingatia masharti ya sheria za Tanzania. Masuala ya motisha za kiuwekezaji yatakuwa kama itakavyokubaliwa katika mikataba mingine ya utekelezaji mradi itakayoingiwa kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW au washirika wake (Host

Government Agreements- HGA). Misamaha ya kodi na nafuu nyingine za kiuwekezaji itatolewa kwa kuzingatia sheria za Tanzania au itakavyokubalika katika mikataba mingine ya utekelezaji mradi.

SEHEMU YA IV- MASHARTI YA MWISHO (FINAL PROVISIONS)
Ibara ya 19 (State Succession)

Ibara ya 19 ni juu ya Serikali kurithi Mkataba (State Succession). Endapo kutatokea mabadiliko yanayotokana na Serikali mojawapo katika Mkataba huu kurithiwa na Serikali nyingine, kwa kuzingatia mahusiano ya kimataifa kuhusu mipaka ya eneo lote au sehemu yake, Serikali mrithi itahesabika kuwa imerithi Mkataba huu kutokea tarehe ya mabadiliko yaliyofanyika. Serikali mrithi itaijulisha Serikali nyingine juu ya nia yake ya kuwa sehemu ya Mkataba huu.

Ibara ya 20 (Dispute Settlement)
Upande wowote wa Mkataba unaweza kuleta mgogoro wa Kimkataba ili uweze kusuluhishwa kwa njia za kidiplomasia au kufikishwa kwenye Kamati ya Ushauri ya IGA kwa usuluhishi. Makubaliano yoyote yanayohusu usuluhishi wa mgogoro yatakuwa kwa njia ya maandishi.

Endapo mgogoro hautatatuliwa kwa njia ya kidiplomasia au kupitia Kamati ya Ushauri ya IGA ndani ya siku 90, upande wowote katika mgogoro unaweza kuujulisha upande mwingine kuwa mgogoro bado unaendelea kuwepo (a Declared Dispute exists). Hivyo mgogoro utafikishwa kwenye Baraza la Usuluhishi, chini ya Sheria za Usuluhishi za Kamisheni ya Umoja wa Mataifa juu ya Sheria zinazohusika na Biashara za Kimataifa (UNICITRAL Arbitration Rules).

Baraza la Usuluhishi litakaa Jijini Johannesburg, Jamhuri ya Afrika Kusini. Lugha ya usuluhishi itakuwa ni ya Kiingereza, na tuzo itatolewa kwa maandishi ikionesha sababu za uamuzi uliotolewa.

Ibara ya 21 (Governing Law)
Ibara ya 21 inafafanua sheria zitakazotumika katika Mkataba huu kuwa ni sheria za mfumo wa nchi ya Uingereza (English/ Common Law) zinazotumiwa na Nchi za Jumuiya ya Madola. Mikataba mingine ya utekelezaji mradi kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW au washirika wake itakuwa kwa sheria za Tanzania.

Ibara ya 22 (Subsequent Amendment)
Ibara ya 22 inaeleza kuwa Mkataba huu unaweza kufanyiwa marekebisho wakati wowote kwa maandishi, kwa makubaliano ya pande zote mbili. Marekebisho hayo lazima yawekwe saini na kuridhiwa na Serikali zote mbili katika Mkataba huu.

Ibara ya 23 (Duration and Termination)
Ibara ya 23 ni kuhusu Ukomo na Usitishaji wa Mkataba. Ukomo wa Mkataba ni mpaka hapo shughuli za mradi zitakapokuwa zimekamilika au kukamilika kwa mikataba kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW au washirika wake (HGA) na mikataba mingine ya utekelezaji mradi; na endapo kuna mgogoro, ukomo wa Mkataba utakuwa pale ambapo usuluhishi umefanyika.

Uvunjaji wa Mkataba huu utafanyika kwa ridhaa ya pande zote mbili. Ridhaa au idhini ya kuvunja Mkataba haitazuliwa na upande mmoja bila kutoa sababu za msingi.
Serikali husika katika Mkataba huu hazitakuwa na haki ya kuvunja Mkataba, kujitoa, kuahirisha au kusitisha Mkataba katika

mazingira yoyote yale, ikiwa ni pamoja na mazingira ya uvunjaji mkubwa wa masharti ya Mkataba huu (material breach), mabadiliko ya msingi katika mazingira ya utekelezaji Mkataba, mgogoro mkubwa wa kidiplomasia, au sababu zozote zile zinazotambulika katika sheria za kimataifa. Bila kuathiri yaliyoelezwa hapo juu, mgogoro wowote kati ya Serikali husika katika Mkataba kuhusu mazingira tajwa hapo juu, utashughulikiwa kwa mujibu wa matakwa ya Ibara ya 20 ya Mkataba huu.

Ibara ya 24 (Reservation, Language and Appendices)
Ibara ya 24 inaeleza kuhusu masharti ambayo hayatatumika au hayatakubaliwa na Serikali katika Mkataba huu (Reservations). Aidha kuna maelezo kuhusu lugha itakayotumika na viambatisho vya Mkataba (Language and Appendices).

Mpaka wakati wa kusaini Mkataba huu, hakuna Serikali yoyote iliyoonesha kutokukubaliana na masharti ya Mkataba huu. Aidha, viambatisho vyote na Nyongeza za Mkataba (addendum) ambavyo vitakuwa vikisainiwa na pande zote husika mara kwa mara, vitakuwa sehemu ya Mkataba huu. Lugha ya Mkataba ni Kiingereza.

Ibara ya 25 (Entry into Force)
Ibara hii inaweka masharti ya kuanza kutumika kwa Mkataba huu (entry into force). Ibara inaeleza kuwa, mara tu baada ya kusainiwa Mkataba huu, shughuli za awali za mradi (Early Project activities) zitaanza kutekelezwa. Shughuli hizo ni kama vile upembuzi yakinifu, kufanya tathmini ya kimazingira na kijamii ya mradi (environmental and social due diligence), kujenga barabara za kuwezesha kufika eneo la mradi, nk. Shughuli hizi zinaweza kuanza kufanywa na Kampuni ya DPW au kwa niaba yake

zikafanywa na kampuni washirika, kwa kuzingatia sheria za Tanzania. Aidha, Mkataba unazitaka Serikali husika, ndani ya siku thelathini (30) baada ya kusainiwa Mkataba, kuanza mchakato wa kuridhia Mkataba huu.

Mkataba utaanza kutumika rasmi pale ambapo Serikali zote mbili zitafanya makabidhiano ya Hati za Uridhiaji Mkataba, chini ya sheria za nchi husika.

Ibara ya 26 (Transposition of the IGA into National Law)
Ibara ya 26 inaweka utaratibu wa kuhaulisha masharti ya Mkataba huu katika Sheria za nchi (Transposition of the IGA into National Law). Serikali za nchi husika zitafanya jitihada za mapema kufanya masharti ya Mkataba huu na Mikataba mingine kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW, zinahaulishwa katika sheria za nchi husika.

Ibara ya 27 (Entry into Force Relationship between this Agreement and Other International and Domestic Obligations in the State Parties)​

Ibara ya 27 inaweka masharti kwamba, pale ambapo Mkataba huu utaanza kutumika rasmi, Serikali yeyote katika Mkataba huu haitaingia au kuwa sehemu ya makubaliano ya ndani ya nchi au ya kimataifa, au kuwajibika au kulazimika kisheria kutekeleza sheria yoyote ya ndani ya nchi au ya kimataifa, kanuni au makubaliano ambayo yatakuwa ni kinyume na utekelezaji wa Mkataba huu au Mikataba kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW au kampuni nyingine washirika.

Ibara ya 28 (Competencies of the State Parties and their Signatories)
Katika Ibara ya 28, kila nchi inatoa uthibitisho kwamba utekelezaji wa masharti ya Mkataba huu unafanyika kwa mamlaka yaliyotolewa na Serikali za nchi husika. Aidha, inathibitishwa kwamba Mkataba huu umetiwa saini na mamlaka za umma zenye uwezo wa kisheria, zilizopewa mamlaka na idhini ya kufanya hivyo, kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na sheria za nchi husika, ili kuingia makubaliano haya ya kimataifa kwa niaba ya Serikali.

Ibara ya 29 (Performance and Observance of the IGA and Other related Agreements and Support for Project Activities) Ibara ya 29 inaweka masharti kwa kila Serikali husika kuhakikisha inatekeleza wajibu wake chini ya Mkataba huu na mikataba mingine inayohusu shughuli za mradi. Kwa kutumia mamlaka yake halali kisheria, kila Serikali itahakikisha kuwa mamlaka zake za nchi zinatekeleza kwa namna inayofaa na kuridhisha, majukumu ya Serikali katika Mkataba huu na mikataba mingine iliyosainiwa kati ya Tanzania na Kampuni ya DPW kuhusu mradi huu.

Ibara ya 30 (Stabilization)
Ibara ya 30 inaweka masharti ya kuwa na uthabiti, uimara na uhakika wa kutoyumbisha Mkataba huu (Stabilization). Serikali za nchi husika zinakubaliana kuwa mazingira ya kisheria na kimkataba kuhusu mradi huu yatakuwa ya uthabiti na ya kuridhisha kwa Serikali zote mbili na Kampuni ya DPW. Taarifa zote kuhusu uthabiti wa Mkataba zitakubaliwa kati ya Kampuni ya DPW au Kampuni husika ya mradi na TPA. Aidha masharti ya uthabiti wa Mkataba yatawekwa katika Mikataba mingine itakayoingiwa kati ya Tanzania na Kampuni ya mradi (HGAs).

Katika Tarehe ya kusainiwa Mkataba wa IGA itatumika kama rejea ya tarehe ya uthabiti katika kufanya mabadiliko yoyote ya Kisheria au mabadiliko ya kikodi yanayoweza kuathiri miradi husika.

Ibara ya 31​

Ibara ya 31 inafafanua kuwa Serikali zote mbili zitabadilishana Mkataba na Hati zote za Uridhiaji Mkataba huu.

Uzoefu na Ufanisi wa Kampuni ya DPW katika Uwekezaji kwenye Miundombinu ya Bandari za Barani Afrika​

Kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya DP World1, Kampuni hii imewekeza kwenye miundombinu ya bandari mbalimbali duniani (ports and terminals), huduma za meli (marine services), maeneo maalum ya kiuchumi (economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors). Kampuni ina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ikiendeleza na kufanya maboresho ya miundombinu ya bandari barani Afrika. Baadhi ya bandari hizo ni kama:
DP World Luanda. Kampuni ya DPW imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 190 katika bandari ya Luanda nchini Angola. Uwekezaji huu umechochea ukuaji wa uchumi wa nchi ya Angola na kuifanya kuwa kitovu cha biashara (trade hub) katika pwani ya magharibi ya Ukanda wote wa Kusini mwa Afrika.

Dakar (Senegal). Kampuni ya DP World imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya kuboresha na kupanua bandari ya Dakar nchini Senegal. Uwekezaji huu umeongeza mapato ya bandari kwa asilimia 20 na kupunguza muda wa kusubiri mizigo, kutoka masaa 35 hadi sifuri.

Sokhna (Egypt). Misri ni mzalishaji mkubwa wa sukari barani Afrika, ikizalisha kiasi cha tani milioni 2.6 kila mwaka. Kampuni ya DP World imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 520 katika maboresho ya miundombinu ya bandari ya Sokhna, hususan katika eneo la maegesho ya mizigo na kuongeza tija katika mnyororo wa usambazaji wa sukari barani Afrika (chain supply). Maboresho hayo yameifanya bandari ya Sokhna kuwa lango kuu (primary gateway) la biashara katika eneo la Bahari Nyekundu (Red Sea). Uwekezaji huu umeongeza mapato ya nchi ya Misri, kuongeza kasi ya utoaji mizigo bandarini na hivyo kupunguza gharama.

Berbera (Somaliland). Kampuni ya DP World imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 442 katika kupanua bandari ya Berbera ya nchini Somalia. Upanuzi huu unategemea kuchochea biashara na hivyo kuongeza mapato ya ndani ya nchi ya Somalia (gross domestic product- GDP) kwa asilimia 27. Aidha maboresho hayo yatachochea ukuaji wa biashara katika Ukanda wa Pembe ya Afrika (Horn of Africa) kwa asilimia 75 ifikapo 2035.

Djibout. Mwaka 2008, Kampuni ya DP World iliingia Mkataba na Jamhuri ya Djibout wa miaka thelathini (30) kuendesha bandari ya Dorahel (Dorahel Container Terminal-DCT). Hata hivyo, mwaka 2014, kulitokea mgogoro kutokana na madai kwamba Kampuni ilitoa rushwa kwa mkuu wa Mamlaka ya Bandari wa wakati huo na hivyo kusababisha kuwepo Mkataba wenye masharti yanayoipendelea Kampuni ya DP World. Serikali ya Djibout kwa kuona kuwa Mkataba huo ni tishio kwa mamlaka ya nchi (sovereignty of the state) na tishio kwa uchumi wa nchi (economic independence), iliamua mnamo tarehe 22 Februari, 2018 kuvunja huo Mkataba na kuichukua bandari ya Djibout.

Manufaa ya Mkataba kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania​

Kwa mujibu wa mapendekezo ya kuridhia Mkataba huu yaliyowasilishwa na Serikali, kuridhiwa kwa Mkataba huu kutakuwa na manufaa yafuatayo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:

Kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na uwekezaji mkubwa na ongezeko la shehena ya mizigo itakayopitia bandari ya Dar es Salaam.

Kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandarini nchini.

Kuongezeka kwa pato la taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari.

Kuongezeka tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikijengwa na Serikali kama vile:

Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway-SGR),
ujenzi wa meli za mizigo katika maziwa makuu, na Mradi wa Lango la Bahari la Bandari ya Dar es Salaam
(Dar es Salaam Maritime Gateway Project- DMGP).

Kuchagiza na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi (multiple effect) zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, mifugo, uvuvi, biashara na usafirishaji na hivyo kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla.

Maoni na Ushauri​

Kutokana na uchambuzi tuliofanya hapo juu, ni maoni na ushauri wetu kuwa, Bunge lipate ufafanuzi kutoka Serikalini katika maeneo machache yafuatayo:-

Ibara ya 25 (1) inaeleza kuwa kuna shughuli za awali za mradi (Early Project Activities) zitaanza kufanyika mapema baada ya kusainiwa Mkataba. Shughuli za awali za mradi zitafanyika kabla ya Bunge kuridhia Mkataba na kabla ya Mkataba kuanza kutumika rasmi kwa mabadilishano ya Hati za Uridhiaji kati ya Serikali zote mbili.

Shughuli za awali za mradi zimetafsiriwa katika Ibara ya 1 kuwa ni kufanya upembuzi yakinifu pamoja na kufanya tathmini ya kimazingira na kijamii ya mradi huu (environmental and social due diligence), kujenga barabara za muda kuwezesha kufika eneo la mradi, n.k.

Tunashauri Serikali itoe ufafanuzi katika eneo hili, ambapo shughuli za Mradi zinaanza kabla ya Mkataba kuridhiwa na Bunge.

Ibara ya 20 kuhusu usuluhishi wa migogoro kufanyika Afrika Kusini na kwa kutumia Sheria za Usuluhishi za Kamisheni ya Umoja wa Mataifa juu ya Sheria zinazohusika na Biashara za Kimataifa (UNICITRAL Arbitration Rules), ni kinyume na maelekezo ya kifungu cha 11 cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Rasilimali na Maliasili ya Mwaka 2017 (The Natural Wealth and Resources [Permanent Sovereignty] Act, 2017).

Sheria tajwa inaelekeza kuwa mgogoro wowote unaotokana na matumizi ya rasilimali na maliasili za nchi hautatatuliwa katika mahakama na mabaraza ya nchi za nje, bali utatatuliwa na vyombo vya sheria vya Tanzania na kwa kutumia sheria za Tanzania.

Ibara ya 23 (4) kuhusu kusitisha Mkataba, inaeleza bayana kuwa Serikali husika katika Mkataba hazitakuwa na haki ya kuvunja Mkataba (denounce), kujitoa (withdraw from), kuahirisha (suspend) au kusitisha (terminate) Mkataba katika mazingira yoyote, ikiwa ni pamoja na mazingira ya uvunjaji mkubwa wa masharti ya Mkataba huu (material

breach), mabadiliko ya msingi katika mazingira ya utekelezaji Mkataba (fundamental change of circumstances), mgogoro mkubwa wa kidiplomasia (severance of diplomatic or consular relations), au sabau zozote zile zinazotambulika katika sheria za kimataifa.

Masharti ya Ibara hii yanatakiwa kufafanuliwa na Serikali.

Muda wa utekelezaji Mkataba huu haujawekwa bayana, bali Ibara ya 23
inasema kuwa ukomo wa Mkataba huu ni mpaka hapo shughuli za mradi huu zitakapokuwa zimekamilika. Serikali iombwe kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili la ukomo wa Mkataba.

Ibara ya 27 inaweka masharti kwamba, pale ambapo Mkataba huu utaanza kutumika rasmi, Serikali yeyote katika Mkataba huu haitaingia au kuwa sehemu ya makubaliano ya ndani ya nchi au ya kimataifa wakati wa utekelezaji wa Mkataba.

Serikali iombwe kutoa ufafanuzi wa Ibara hii. Mkataba huu haujaweka muda wa ukomo, hivyo Serikali haitakuwa na nafasi ya kuingia makubaliano mengine kuhusu kuendeleza au kuboresha na kuendesha bandari zake.

Ibara ya 30 inaweka masharti ya kuwa na uthabiti, uimara na uhakika wa kutoyumbisha Mkataba huu (Stabilization). Eneo hili lipate ufafanuzi wa Serikali. Kwa kuzingatia kuwa Mkataba huu hauna muda wa ukomo. Hivyo, kuna mazingira sheria zitahitaji kufanyiwa mabadiliko kulingana na wakati, ambapo mabadiliko hayo yanaweza kuathiri masharti ya Mkataba huu na kuchukuliwa kuwa ni kuyumbisha Mkataba huu.

Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mamlaka ya kusaini mMkataba huu yametolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hata hivyo, kwa upande wa Serikali ya Dubai haijawekwa wazi. Tunashauri Serikali itoe ufafanuzi kuhusu mamlaka ya kusaini Mkataba huu kwa upande wa Serikali ya Dubai.

Tunaomba kuwasilisha.

Imeandaliwa na Sekretariati ya Bunge​


Habari zaidi, soma:
  1. Sakata la DP WORLD: Rais Samia asema Serikali itatafuta mbia wa kuiendesha bandari ya Dar, sasa kuchangia robo tatu ya bajeti ya nchi
 

Attachments

  • UCHAMBUZI WA SEKRETARIET (1)_230606_231229_230612_000251.pdf
    190.8 KB · Views: 18
Bado suala la muda wa mkataba ni dhahiri. Hapa ndipo ulipo ushenzi wa mwanzo kabisa wa mkataba huu.

Jambo jingine ni hilo kwamba hata sheria za nchi zikibadilika, huu mkataba unabakia kama ulivyo.

Mkataba huu, kwa kutokuwa na muda maalum, ni sawa Tanzania imeamua kuiuza sehemu ya ardhi ya Tanganyika kwa Dubai. Ina maana maeneo ya bandari yatakuwa yanamilikiwa na waarabu milele.

Mgeni yeyote mpangaji hawezi kuwa na mkataba wa upangaji usio na kikomo. Kwa nini isitamkwe, labda ni mkataba wa miaka 15, ambao utakuwa na nafasi ya kuhuishwa baada ya muda wa mkataba, kuliko huu usio na kikomo?

Kwa nini tuanzie na bandari mama badala ya kuanza na bandari ndogo kama vile bandari ya Zanzibar? Bandari mama, kukiwa na mgogoro, nchi itaathirika sana. Mataifa mengine, hasa yaliyoendelea, hayajawahi kuipa DP bandari mama kuiendesha. Hao siyo wajinga kufanya hivyo.
 
1. kwanza mkataba unakinzana na sheria ya rasilimali ya mwaka 2017, inayotaka disputes za uwekezaji katika rasilimali za Taifa ziamuliwe nchini

2. Mkataba mama umesema wazi hakuna KUJITOA katika mkataba hata itokee kitu gani, kwa hiyo Hii ngoma ni MILELE labda mfalme atuonee huruma

3. Mkataba MAMA umesema wazi kuwa SERIKALI HAITOKATAA Kurenew mikataba midogomidogo ijayo pindi Mwekezaji atakapotaka kurenew

Kiufupi Bandari imekabidhiwa kwa Mwekezaji, na Kufanikiwa kwetu kutatokana na Huruma yake asitupige, Hatuna namna ya Kumchomoa!
 
Mkataba huu, kwa kutokuwa na muda maalum, ni sawa Tanzania imeamua kuiuza sehemu ya ardhi ya Tanganyika kwa Dubai. Ina maana maeneo ya bandari yatakuwa yanamilikiwa na waarabu milele.

Mgeni yeyote mpangaji hawezi kuwa na mkataba wa upangaji usio na kikomo. Kwa nini isitamkwe, labda ni mkataba wa miaka 15, ambao utakuwa na nafasi ya kuhuishwa baada ya muda wa mkataba, kuliko huu usio na kikomo?

Kwa nini tuanzie na bandari mama badala ya kuanza na bandari ndogo kama vile bandari ya Zanzibar?
Mimi sitowi commenst kuhusu mkataba huu, bali kusu wewe mchangiaji wewe.
1. Bandari ya Zanzibar ndiyo Bandari Mama katika Afrika ya Mashahriki. ila kwa sasa ni ndogo tuu.
2. Watanganyika walipoandika mkataba wa Mungano na Zanzibar hawakuweka Mashariti wala kikomo cha Muungano ,bali waliimeza Zanzibar kwa kuweka ibara hii (iii),''Katiba ya Tanganyika itakuwa ndiyo katiba ya Jamuhuri ya Muungano baada ya kufanyiwa Marekebisho machache fulani fulani ili kuingiza Ukubwa wa nchi ya zanzibar na kuitambua SMZ iwe ni sehemu ya katiba hito.''
3. Kila anayesimama kulalamika kuhusu Muungano huchezea kichapo au kumalizwa kisiasa. MUUNGANO WETU hauna terms OF AGREEMENTS za kubadili wala kutoka wala FOMULA YA MIGAWANYO YA MADARAKA NA RASILIMALI. kila kitu kimefanywa ni cha muungano na muungano ni Tanganyika. IT IS ABAD CONTRACT.

Sasa leo wanadai mkataba huu uchanganue kila kitu,wakihofia maslah yao, well and good SISI WAZANZIBARI JE? MASLAHI YA NCHI YETU MBONA MUNATUWEKEA KAUZIBE?
 
Tumemsikia Rostam Aziz, tumemsikia mohamed dewji, bila shaka ni kwa niaba ya matajiri wakubwa. Wengi tunapiga kelele wapo wanasema ni njaa na wivu. Matajiri wezi na dhulumati wa umma siku zote watasema mnawaonea wivu.
Hivi rostam azizi akisema serikali ilijitoa kwenye biashara hajui biashara ni kitu gani? Hivi serikali kutoza kodi na ushuru tangu lini ni biashara kama sio kupotosha. Kuna vitu havifai kukodisha au kwa mtu au watu binafsi maana ndio nchi yenyewe. Hivi unaweza kukodisha mkoa mmojawapo wa nchi kwa kampuni binafsi tena ya kigeni? Je unaweza kukodisha mbuga zote za wanyama nchini? Au unaweza kukodisha mlima kilimanjaro. Tena ukodishaji wenyewe kuiondolea nguvu ya kuhoji au kutaka kuvunja mkataba serikali?
Hong kong china ilikodishwa kwa waingereza wakiwa tayari wameikamata na china ikiwa dhaifu kwa masharti ambapo iligeuzwa koloni kwa zaidi ya miaka 100. Ni hadi china ilivyoimarika wakaweza irejesha kwa kuitishia uingereza wataichukua kwa nguvu pasipo maelewano.
Tulisema tunataka maendeleo lakini sio kwa gharama ya uhuru wetu. Samia tuliona tangu mwanzo akijidai urafiki na wafanya biashara kuzidi maslahi ya umma.
Watanzania hawataki. Lazima akubali kwamba urithi wake kuongoza ukiisha ajue fikra zake kiuongozi hazifai tuagane. Hakuchaguliwa na wananchi kwa hivyo asitake kuleta mageuzi kiuchumi kinyume na mtangulizi wake. Mageuzi ambayo wala kimsingi hayazingatii itikadi ya chama chake chama cha mapinduzi (CCM)
 
Back
Top Bottom