Tafsiri na uchambuzi Mkataba wa Bandari Tanzania na Dubai

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,329
33,138
Mohammed bin Rashid meets president of Tanzania at Expo 2020 Dubai.jpg
MKATABA NDIO HUO KWA LUGHA YA KISWAHILI USOME NA UELEWE.
TAFSIRI NA UCHAMBUZI MKATABA WA BANDARI TANZANIA NA DUBAI.


UTANGULIZI; Februari 28, 2022, Rais Samia alipokwenda UAE kuhudhuria Maonesho ya Dubai 2020, ilisainiwa hati ya makubaliano (MoU), baina ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DPW.

Ufafanuzi; DPW ni kampuni ya kimataifa ya oparesheni za bandari, huduma za usafiri wa maji, usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (logistics). DPW wamejikita pia kwenye huduma za free trade zones.

DPW ni kampuni tanzu ya Dubai World ambayo ipo chini ya Dubai Inc. Mmiliki wake ni Serikali ya Dubai. DPW inafanya kazi chini ya Shirika la Bandari na Forodha Dubai (PCFC).

DPW ilianzishwa mwaka 2005 baada ya Kampuni ya Dubai Ports International (DP1), kuungana na Mamlaka ya Bandari Dubai. Mwaka 2006, DPW iliinunua kampuni kongwe ya usafiri wa maji na logistics, P&O, ya Uingereza.

Ununuzi wa P&O, uliiwezesha DPW kukua na kutanuka kwa kasi kubwa ndani ya muda mfupi. Hivi sasa, DPW inafanya kazi zake kwenye bandari takriban 80 duniani.

DPW ipo Canada na UK, imejitanua China na India, ina-opareti Ujerumani, Ufaransa, Saudi Arabia, Misri, Ubelgiji, Afrika Kusini, Msumbiji, Senegal na nchi nyingine nyingi duniani.

Turejee utangulizi; MoU iliyosainiwa Februari 2022 na mazungumzo baina ya Rais Samia na mtawala wa Dubai, vimezingatiwa.

Mkataba ulisainiwa Oktoba 25, 2022, kwa kuzingatia matamanio yaliyomo ndani ya MoU, kuhusu kuendeleza au kuboresha na kusimamia miundombinu ya kimkakati kwenye bandari za bahari na maziwa Tanzania.

Utanguliza unaeleza pia kuwa mkataba umezingatia miradi ya Reli ya Standard Gauge (SGR) na Lango la Bahari Dar es Salaam (DMGP).

Ufafanuzi; Serikali inajenga SGR kwa USD 10.04 bilioni (Sh24 trilioni). Imetumia USD 357 milioni (Sh846.5 bilioni) kugharamia DMGP. Sh818.5 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia mwaka 2017 na Sh28 bilioni ni ruzuku kutoka UK.

Imeelezwa kwenye utangulizi kuwa Serikali inataka kuona inapata matokeo mazuri kupitia miradi ya SGR na DMGP, hivyo ushirikiano na DPW ni njia ya kuyaelekea.

Katika utangulizi huo, inaelezwa pia kilichoitamanisha Serikali ya Tanzania ni mageuzi ya huduma ya sekta ya usafiri wa maji ambayo Dubai imeyafanya na kukuza pato la taifa (GDP) kwa asilimia kubwa. Mageuzi hayo Dubai yamefanywa na DPW.

Imeandikwa pia kuwa mkataba huo umezingatia makubaliano mbalimbali ya miradi baina ya nchi na nchi (state parties), kupitia mikataba ya nchi na wawekezaji wa kimataifa, yaani Host Government Agreement (HGA).

MADHUMUNI YA MKATABA

Ibara ya kwanza ni tafsiri ya misamiati na misemo iliyotumika.

Ibara ya pili ni Madhumuni ya Mkataba kwamba ni kuyafunga kisheria maeneo ya ushirikiano kwa ajili ya kukuza, kuboresha, kusimamia na kuendesha bandari za bahari na maziwa, kanda maalum za kiuchumi, maegesho ya logistics, korido za biashara na miundombinu ya kimkakati kwenye bandari.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni kujengana uwezo, maarifa, ujuzi, teknolojia, vilevile kuimarisha vyuo vya mafunzo na kusaidia mbinu za masoko.

USHIRIKIANO

Ibara ya tatu inazungumzia ushirikiano utakavyokuwa. Vipengele vitatu vimeainishwa.

1. Utekelezaji wa mradi; imeandikwa kuwa pande mbili za mkataba, kila upande unapaswa kuweka na kudumisha mazingira bora na muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi.

Imeandikwa kuwa wawakilishi wa pande zote mbili watakutana mara kwa mara kadiri itakavyowezekana kwa ajili ya kujadiliana na kuingia makubaliano mengine ikionekana inafaa, lengo likiwa kuwezesha utekelezaji wa shughuli za mradi.

2. Kamati ya mashauriano; ni mkataba baina ya serikali mbili, yaani Intergovernmental Agreement (IGA). Imebainishwa kuwa itaundwa Kamati ya Mashauriano ya IGA, ambayo ndio itakuwa na wajibu wa kuratibu shughuli za pande zote za kimkataba. Kamati hiyo ya mashauriano itakuwa inaripoti kwa Katibu Mkuu Uchukuzi.

Kamati ya mashauriano ya IGA, itaundwa na wawakilishi wenye sifa kutoka pande zote za mkataba. Muundo wa kamati hiyo na jinsi itakavyofanya kazi zake, itatokana na hadidu za rejea zitakazokubaliwa na kila upande.

3. Ukaguzi na taarifa; Pande zote zitakubaliana kupitia Mikataba wa Utekelezaji wa Miradi (HGA) na makubaliano mengine ye miradi, juu ya masuala ya ukaguzi unaohusu utekelezaji wa shughuli za miradi. Kila upande utahakikisha kuna mazingira bora ya kupeana taarifa, na siri yoyote haipaswi kuvuja.

WIGO WA USHIRIKIANO NA VYOMBO VYA UTEKELEZAJI

Ibara ya nne, inaeleza wigo wa Mkataba ambao ni kuwezesha utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano ambayo yameainishwa kwenye Kiambatanisho 1 kama ifuatavyo;

1. Kuendeleza, kusimamia na kuendesha gati la kushusha magari kisasa, yaani RoRo (Gati 0), gati kuu la mizigo (Gati 1 hadi 4) na gati la makontena (Gati 5 mpaka 7), Bandari ya Dar es Salaam.

2. Kuendeleza eneo la kushusha mizigo na la abiria, Bandari ya Dar es Salaam. Magati haya yataendeshwa na TPA.

3. Kuendeleza, kusimamia na kuendesha eneo maalum la bandari ya nchi kavu, Kwala, Pwani na Kurasini.

4. Kuendeleza, kusimamia na kuendesha kituo kipya cha makotena kwenye magati ya RoRo na gati kuu la mizigo, kuanzisha yadi ya RoRo EPZA (Ubungo), kwa kujenga egesho la magari la ghorofa (multistorey), vilevile kuboresha yadi ya RoRo, gati kuu la mizigo na makontena, Bandari ya Dar es Salaam.

5. Kutoa mfumo wa kisasa wa Tehama unaotakiwa na TPA ili kuwapa wadau wa Tanzania ufanisi ulio bora na wenye kuonekana katika uendeshaji wa bandari zote Tanzania.

6. Kuifanya Bandari ya Dar es Salaam itoe huduma za usafiri wa maji za kiwango cha dunia.

7. DPW itatoa mafunzo na kuwaendeleza wafanyakazi wa TPA ili wao wenyewe waweze kuendesha mtandao wa bandari na kwa udhibiti wao.

Hiyo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji, ya pili ni hii;

1. Kuendeleza mifumo ya logistics, maeneo maalum kiuchumi, maeneo ya viwanda na miundombinu mingine kwa ajili ya logistics ili kuwezesha ukuaji na maendeleo ya biashara pamoja na huduma ya usafirishaji kwa nchi zisizo na bahari, Mashariki na Kusini ya Afrika.

2. Maendeleo, usimamizi na uendeshaji wa bandari za nyongeza baharini au kwenye maziwa kwa kuziboresha na kuziendeleza, vilevile muunganiko na biashara kati ya Tanzania na nchi inazoungana nazo kwa barabara, kama itakavyopendekezwa na TPA, na kukubaliwa na DPW.

Ukiacha hayo maeneo ya ushirikiano, ibara ya nne, kipengele cha pili, inataka Tanzania iijulishe Dubai fursa nyingine zitokanazo na bandari, freezones na sekta ya logistics ili Dubai au taasisi za Dubai, zivutiwe na kutuma maombi ya kuwekeza.

Kipengele cha mwisho ibara ya nne, kinaeleza kuwa DPW ndio watakuwa na wajibu kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya shughuli za miradi.

HAKI YA KUENDELEZA, KUSIMAMIA NA KUENDESHA

Ibara ya tano, kuhusu maeneo ya ushirikiano, kama yalivyoorodheshwa kwenye appendix 1, awamu ya kwanza, DPW wana haki ya kipekee ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha miradi husika.

Utekelezaji wa mipango kwa ajili ya maendeleo ya miradi lazima uendane na makubaliano ya mradi husika, haki ya kutumia ardhi na HGA. Hii ni kwa kila mradi.

Baada ya kusaini makubaliano (haya), DPW ndio watapaswa kuandaa na kuwasilisha maombi ya kutekeleza miradi kwenye maeneo ya ushirikiano.

Kipengele cha nne, ibara ya 5, kinataka mkazo wa upendeleo wa utekelezaji wa miradi husika.

Serikali ya Tanzania inatakiwa ihakikishe TPA haipokei maombi mengine (nje ya DPW) kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyomo kwenye appendix 1 (awamu ya kwanza), kutoka siku ambayo makubaliano haya yamesainiwa. Labda mkataba uwe umesitishwa au kimepita kipindi cha miezi 12 kutoka siku ya kusaini mkataba huu.

IDHINI YA SERIKALI NA RUHUSA

Ibara ya sita, inataka Serikali ya Tanzania kuhakikisha inatoa idhini, ruhusa, haki ya kutumia ardhi, motisha ya uwekezaji na misamaha ya kodi inayotakiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hii ni kwa mujibu wa sheria.

Kipengele cha pili cha ibara ya sita, kinazuia miradi iliyotolewa mapendekezo na DPW, kuingiliwa na mtu au mamlaka ya tatu, vinginevyo kuingiliwa huko kuwe ni muhimu kwa sababu za ulinzi na usalama zitakazoeleweka kwa pande zote mbili.

IDHINI YA MIRADI

Ibara ya saba, Serikali inatakiwa ndani ya wakati mwafaka, itoe, iruhusu, idumishe au ihuishe idhini zote kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi. Na Serikali ya Tanzania inapaswa kutambua kuwa idhini hizo katika muda mwafaka ni muhimu kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa miradi.

Idhini ikishatolewa, hakuna idhini inayohusiana na mradi wowote husika, itabatilishwa, itabadilishwa, itaboreshwa, au itakayofeli kuhuishwa au kutanuliwa na Serikali ya Tanzania, au mamlaka ya nchi inayohusika au wakala, pasipo kufanya mashauriano na Shirika la Bandari na Forodha la Dubai (PCFC).

HAKI YA ARDHI

Ibara ya nane, Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha DPW wanapata ardhi na kuidhinisha matumizi kwa kila mradi. Serikali inatakiwa kutunza umiliki huo wa ardhi. Vilevile kulinda haki hiyo ya ardhi kisheria na kiutaratibu kwa ajili ya DPW.

Wajibu wa Serikali ya Tanzania kwa jumla ni kuhakikisha ardhi inapatikana, isiwe na migogoro na kusiwe na muingiliano kipindi chote cha utekelezaji wa miradi.

MOTISHA YA UWEKEZAJI

Ibara ya tisa, pande zote mbili zinapaswa kukubaliana kuwa uwekezaji wa DPW una thamani kubwa ambayo italeta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii, hivyo inahitaji kupata motisha.

Pande zote zimekubaliana kuwa motisha zitatolewa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo Tanzania na zitakazokuwemo kwenye HGA na makubaliano ya mradi.

USIRI

Ibara ya 10, inataka usiri. Taarifa za makubaliano na majadiliano baina ya pande zote mbili, hazitakiwi kutoka au kutumika upande mwingine.

MATENDO YA KIBAGUZI

Ibara ya 11, inataka kodi, ushuru na tozo nyingine zinazohusu utekelezaji wa miradi, ziwe kwa mujibu wa sheria ya fedha Tanzania. Vilevile utekelezaji wa sheria na udhibiti, viwe kwa nia njema, uwazi, usawa na pasipo ubaguzi.

ULINZI NA USALAMA

Ibara ya 12, inaeleza kuwa pande zote zinakubaliana kuwa suala la ulinzi na usalama halina mjadala. Uwekezaji wote utatekelezwa kwa muongozo wa usalama wa nchi. Kila mradi wa DPW, kupitia HGA, na utekelezaji wake lazima uzingatie ulinzi na usalama wa nchi.

MAUDHUI YA NDANI, AJIRA NA USHIRIKI WA WAJIBU WA KIJAMII

Ibara ya 13, Miradi inapaswa kuwa na mpango wa kutambua na kuendeleza maudhui ya ndani. Ajira zinapaswa kutolewa kwa Watanzania (raia wa Tanzania).

Taasisi na watu binafsi wa Tanzania, wanapaswa kupewa kipaumbele katika kila fursa iliyopo kwenye kila mradi. Ikiwa wana vigezo na wamesajiliwa.

DPW wanapaswa kuwasilisha mpango wa ajira na mafunzo kwa ajili ya Watanzania.

DPW watatakiwa kuwezesha vyuo vya Tanzania vinavyotoa mafunzo ya huduma za usafiri wa maji, na kuweka wazi mipango ya utafiti, maendeleo na mabadilishano ya teknolojia.

TPA watapaswa kusimamia utelekezaji wa maudhui ya ndani. Hii ni kwa mujibu wa tafsiri ya ibara ya 13, kipengele namba tatu.

UZUIAJI WA MALI

Ibara ya 14, kipengele cha kwanza, inaeleza kuwa kwa kusaini mkataba huu, Serikali haitaruhusiwa kuzuia au kutaifisha mali, hisa au mikopo ya kampuni yenye kutekeleza mradi. Na kama itabidi Serikali kutaifisha au kuzuia mali, basi ifuate mchakato wa kisheria, kusiwe na ubaguzi.

VIWANGO VYA MAZINGIRA, AFYA KAZINI, KIJAMII NA USALAMA

Ibara ya 15, inaeleza kuwa pande zote zinakubaliana kufuata sheria za Tanzania na viwango vya kimataifa vya Mazingira, Afya Kazini, Kijamii na Usalama (EOHSS). Utekelezaji wa miradi utaendana na viwango vya kimataifa vya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira baharini, ikiwemo IMO na MARPOL.

VIWANGO VYA UTAALAMU

Ibara ya 16, DPW na TPA watashirikiana na kupeana taarifa kuhusu viwango vya utaalamu wakati wa utekelezaji wa miradi.

HAKI ZA WAFANYAKAZI

Ibara ya 17, haki za wafanyakazi zitalindwa kwa mujibu wa EOHSS na viwango vya kimataifa vya Haki za Binadamu.

KODI, USHURU NA TOZO

Hii ni sehemu ya tatu ya mkataba ambayo inatambulisha Mamlaka ya Kifedha (Fiscal Regime). Ibara ya 18, inaeleza kuwa kodi, ushuru, tozo, motisha ya uwekezaji na misamaha ya kodi, utekelezaji wake utakuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

MABADILIKO YA DOLA

Sehemu ya nne ya mkataba, inaeleza Masharti ya Mwisho (Final Provisions). Hii ni ibara ya 19, tafsiri yake ni kuwa dola ya Tanzania ikibadilika au ikirithiwa, mrithi ataendelea kuwa sehemu ya Mkataba huu.

Niiweke sawa, mathalan, Jumuiya ya Afrika Mashariki inaamuliwa kuwa nchi au serikali moja, hivyo Tanzania inakoma kuwa nchi au majukumu ya kiserikali yanachukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashari. Sharti la ibara hiyo ni kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa sehemu ya mkataba huu.

UTATUZI WA MIGOGORO

Ibara ya 20, inaeleza utatuzi wa migogoro. Njia ya kwanza ni Suluhu ya Kiungwana (Amicable Settlement), mwafaka ukikosekana kidiplomasia ndani ya siku 90 au kupitia Kamati ya Mashauriano ya IGA, upande mmoja utaueleza mwingine kuwa mgogoro unaendelea.

Hatua itakayofuata ni kesi na uamuzi (Arbitration), imeelezwa kwenye kipengele cha pili, ibara ya 20. Imeandikwa kuwa Arbitration itashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Usuluhishi za Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za Biashara Kimataifa (UNCITRAL).

Upande mmoja utawasilisha shauri kwa mwenzake kwa maandishi. Kila upande utateua mwakilishi mmoja ili awe mjumbe Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (Arbitration Tribunal). Wajumbe hao wawili, watateua Mwenyekiti ambaye hapaswi kuwa Mtanzania wala raia wa UAE.

Vikao vyote vya Arbitration vitafanyika Johannesburg, Afrika Kusini. Lugha itakayotumika kuendesha kesi ni Kiingereza. Uamuzi utatolewa kwa maandishi na utafafanua sababu za uamuzi wa baraza.

Kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Tribunal, endapo upande mmoja utashindwa kutekeleza ndani ya siku 30, upande mwingine utapeleka maombi kwa Katibu Mkuu wa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA), The Hague, Uholanzi, aweze kusimamia uteuzi ndani ya siku 30.

SHERIA INAYOONGOZA

Ibara ya 21, inaeleza kuwa mkataba huu utaongozwa kwa mujibu wa Sheria ya Uingereza, wakati Mikataba ya Utekelezaji wa Miradi (HGAs) itasimamiwa na sheria za Tanzania.

MAREKEBISHO YA MKATABA

Ibara ya 22, inatoa ruhusa kufanya mabadiliko ya Mkataba huu wakati wowote, lakini kwa sharti la pande zote kukubaliana kwa maandishi na kusainiwa na pande zote.

MUDA NA USITISHAJI

Ibara ya 23, inaeleza kuwa Mkataba huu utakuwa hai mpaka litokee jambo moja kati haya yafuatayo; 1. Kukoma jumla kwa shughuli zote za mradi. 2. Kuisha muda kwa mikataba yote ya miradi (HGAs) na makubaliano mengine yote ya miradi.

Ikitokea mkataba wa utekelezaji wa mradi (HGA), umesitishwa kabla ya muda wake, Mkataba huu utaendelea kuwa hai kwa muda na kwa kiasi ambacho upande mmoja au kampuni ya utekelezaji wa mradi itaomba ili kudai haki yoyote, kulinda masilahi yoyote yaliyo hatarini au kuibua taratibu ambazo zitasababisha kusitishwa kwa HGA.

Usitishwaji au kuisha muda wa HGA, hakutakiwi kuathiri haki za kimsingi, madeni au fidia za kila upande chini ya HGA husika au makubaliano mengine yoyote ya mradi, yatakayotokana na Mkataba huu.

Mkataba huu utasitishwa kwa idhini ya pande zote mbili, na hiyo idhini lazima iwe na msingi.

Kipengele cha nne, ibara ya 23, inaeleza kuwa pande zote mbili hazipaswi kushutumiana hadharani, kujiengua, kusimamisha au kusitisha Mkataba kwa mazingira yoyote, hata kama kuna upande utakiuka mkataba, kutatokea mabadiliko makubwa ya kimazingira au kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Tatizo lolote ambalo upande mmoja utaona linatosha kuvunja mkataba, utekelezaji wake lazima ufuate masharti ya ibara ya 20 ya Mkataba huu (rejea ibara ya 20).

ANGALIZO, LUGHA NA VIAMBATANISHO

Ibara ya 24, inaeleza kuwa hakuna upande uliotoa angalizo (tahadhari) kuelekea kusaini Mkataba. Lugha ya mawasiliano wakati wote wa utekelezaji wa Mkataba ni Kiingereza.

UHALALISHAJI WA MKATABA

Ibara ya 25, inaeleza wajibu wa kila upande, kuhakikisha Mkataba unafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na za kimataifa.

KUWEZESHA IGA KUINGIA KWENYE SHERIA ZA NCHI

Ibara ya 26, Mkataba huu ni makubaliano baina ya serikali mbili (IGA). Sasa wajibu wa kila upande ni kuhakikisha makubaliano haya, pamoja na mikataba ya miradi (HGA), vilevile makubaliano mengine ya miradi, kwa pamoja yanaingia kwenye sheria za kila nchi husika.

UHALALISHAJI KATI YA MKATABA HUU NA WAJIBU MWINGINE WA KIMATAIFA NA KITAIFA

Ibara ya 27, kila upande unawasilisha na kuthibitisha kwamba Mkataba huu hautakuwa sehemu ya makubaliano yoyote ya kitaifa na kimataifa, ambayo yatakuwa yanakinzana na Mkataba huu, Mkataba wa Utekelezaji wa Miradi (HGA) na makubaliano mengine ya miradi.

MAMLAKA YA WATIA SAINI

Ibara ya 28, kila upande unawakilisha na kuthibitisha kuwa yaliyomo kwenye Mkataba yapo ndani ya mamlaka ya serikali yake na waliosaini wana idhini ya kisheria kufanya hivyo.

UFANISI NA UANGALIZI WA IGA, MAKUBALIANO MENGINE NA KUWEZESHA SHUGHULI ZA MIRADI


Ibara ya 29, kila upande unatakiwa kutekeleza wajibu wake kwenye Mkataba huu, HGA na makubaliano mengine ya miradi. Kila upande utahakikisha mamlaka zake zinatimiza wajibu unaotakiwa kwenye Mkataba huu na HGA.

UIMARISHAJI

Ibara ya 30, pande zote zinakubaliana kwamba sheria na mazingira ya kimkataba yenye kuhusu miradi, vitaimarishwa kwa namna ambayo itaridhisha pande zote na kampuni itakayotekeleza mradi. Taarifa za uimarishaji huo zitakubaliwa baina ya DPW, kampuni ya mradi na TPA, na sharti ziakisi HGA.

MABADILISHANO YA MAKUBALIANO

Ibara ya 31, inaonesha kuwa mkataba huu umesainiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa na mwakilishi wa Dubai, Ahmed Mahboob Musabih.

Ipo pia saini ya Rais Samia Suluhu Hassan, akimpa idhini Prof Mbarawa kusaini, vilevile saini ya Mtawala wa Dubai ikimwidhinisha Musabih.

HITIMISHO

Ukiusoma mkataba wote kwa utulivu, ukiwa sober, utabaini kuwa huu ni "Mkataba Mwavuli" - "An Umbrella Contract." Kwamba ndani ya Mkataba huu au Makubaliano haya (ukipenda kuita hivyo), kuna mikataba mingine na makubaliano mengi ambayo TPA itasaini na DPW.

Ukiusoma mkataba wote kwa mtindo wa "mstari na mstari" - "between the lines", huoni kitisho cha nchi kuuzwa. Huu Mkataba ni mwavuli tu. Soma between the lines, hakuna hata silabi yenye kuashiria bandari inauzwa.

Mahali tatizo linaweza kuwepo ni kwenye mikataba ya utekelezaji wa miradi (HGAs) na makubaliano mengine. Ibara ya tano, kipengele cha tatu, inaonesha kuwa baada ya Mkataba huu kusainiwa, kinachofuata ni DPW kuandika mapendekezo na kuyawasilisha TPA, kisha wanakubaliana na kusaini mkataba.

Awamu ya kwanza ya ushirikiano, imeainisha maeneo saba. Hivyo DPW na TPA, wataingia mikataba mingine saba au zaidi kwa ajili ya utekelezaji. Hapa ndipo kwenye tatizo. TPA na DPW watakapojifungia, watasaini mikataba yenye sura ipi? Uadilifu utakuwaje?

Mkataba wote huoni fedha. Ibara ya nne, kipengele cha tano, kinaonesha DPW ndio watahusika na uwekaji fedha kwenye miradi. Hakuna ufafanuzi zaidi. Hivyo, mikataba ya utekelezaji wa miradi, ndio itakuwa na uchambuzi wa kina kuhusu fedha. Bila shaka, kama ni rushwa, zitakuwa huko. Umakini unapaswa kuelekezwa huko.

Mkataba ni wa miaka 100? Si kweli. Hakuna mahali panasema hivyo. Je, ni mkataba wa maisha? La hasha! Ibara ya 20 imeeleza jinsi mchakato wa kuachana unapaswa kutekelezwa. Lazima sheria na taratibu zifuatwe. Sio kihuni wala kibabe.

Binafsi nimependa mwamko wa kuhoji kuhusu Mkataba huu na wasiwasi juu yake. Hii nchi ni mali ya Watanzania, sharti kuwa macho kuhoji ili wajukuu wasirithi mapanki na mabua.

Sasa, tuhoji mikataba ya miradi (HGAs), huko ndiko kwenye pesa, na kama kuuziana nchi labda ni huko ndiko DPW na TPA watatutenda. Mkataba huu ni mwavuli ambao hauna kitisho chochote.

KAZI KWETU WANA DIASPORA KWA MAONI NA USHAURI.
 
Back
Top Bottom