kutokana na kauli hii, jee anamaana kuwa safari hii mwenye kutaka kuwania urais Tanzania kwa kupitia CCM anaweza kuchukua fomu na kugombea pamoja na mkuu huyu au???????
...Ndani ya CCM hakuna kuhodhi madaraka'
Na Reuben Kagaruki
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, amesema ndani ya chama hicho hakuna mwanachama wa kuhodhi madaraka na kuwakumbusha kuwa kila mmoja asishangae wala kuchukia pale anapoona wana CCM wenzake wanajitokeza kugombea nafasi aliyoishikilia sasa.
"Ni haki yao kikatiba, hivyo mtu anapoamua kuitumia asionekane wa ajabu au anafanya hiana, si vizuri kuanza kutafuta mchawi...kama mchawi basi ni Katiba iliyoweka utaratibu wa miaka mitano."
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akihutubia Taifa kupitia wakazi wa mkoa huo wakiwamo wabunge, majaji na viongozi wa CCM ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na wananchi kila mwisho wa mwezi.
Alisema moja ya sifa ya CCM ni kuwapo kwa demokrasia ya ndani ya chama. "Tumeweka utaratibu kuwa kila kiongozi ana umri wa miaka mitano katika uongozi, huo ndio mkataba wake na chama na wanachama...hakuna mwenye hatimiliki ya uongozi wa kudumu kwa nafasi aliyonayo," alisisitiza Rais Kikwete.
Alisema hakuna sababu ya watu waliokuwa wakishikilia nyadhifa ndani ya chama hicho wanapowaona wengine wanataka kugombea na kuanza kuhoji ni kwanini kaja, nani kamtuma.
"Ni dhambi kujengeana chuki kwa sababu hiyo. Najua kila mmoja wetu aliyepo madarakani angependa asipate mpinzani. Lakini, matumaini hayo yasiwe sababu ya watu kuwachukia wale wanaojitokeza kugombea nafasi tunazozishikilia," alisema Rais Kikwete.
Alisema pindi wanapojitokeza ichukuliwe kuwa ni jambo la kawaida kutokea, kwani hayo ndiyo matakwa ya Katiba ya CCM.
"Kununiana na kufanyiana vitendo vya uadui ni kinyume na misingi ya demokrasia ndani ya chama chetu. Nayasema haya kwa sababu nasikia kuna baadhi ya wilaya na mikoa zipo dalili hizo. Nawasihi msifanye hivyo. Tuzingatie maadili ya chama chetu," alisema Rais Kikwete.
Kuhusu kampeni, Rais Kikwete aliwataka wagombea wote kuzingatia kanuni na maadili ndani ya chama. Alisema kati ya mambo muhimu ni kuepuka kampeni chafu za kupakana matope na kuchafuliana majina.
Aliwataka wagombea wajinadi kwa ubora wa sifa zao au kama ni wapambe wanadi ubora na sifa za wagombea wao.
"Katu msifanye vitendo vya kukashifu au kuwapaka matope wagombea wenzenu. Vitendo hivyo vinajenga chuki na mfarakano miongoni mwa wanachama, jambo ambalo halina maslahi kwa chama chetu," alisisitiza Rais Kikwete.
Kuhusu rushwa, alisema ni jambo la hatari kwa kiongozi kupata uongozi kwa njia ya rushwa au kwa kununua kura. Alisema kufanya hivyo ni kitu haramu na ni kudhalilisha heshima ya chama
"Nawasihi wana CCM tusitoe rushwa kupata uongozi na tusipokee rushwa ili kumpigia kura mgombea...uongozi usinunuliwe na kura isiuzwe, uongozi wa CCM upatikane kwa ridhaa ya wanachama kutokana na kutoshelezwa na sifa na ubora wa mwombaji," alisema Rais Kikwete na kuongeza:
"Nawaomba wasimamizi wa uchaguzi na hasa vikao vinavyohusika na uchaguzi, kuhakikisha vitendo vya rushwa na watoa rushwa na wapokea rushwa wanadhibitiwa. Tunatengeneza taratibu nyingine zaidi za kusaidia mapambano hayo."
Pia alikemea tabia ya baadhi ya wagombea au wapambe wao kutaka kushinda kwa kupandia migongo ya wengine. Alisema kuna baadhi wanaotumia majina ya watu wengine kupatia ushindi.
"Wapo wanaodai ati wanagombea kwa kutumwa au kutakiwa na wakubwa fulani...tena wanasema wakubwa wa ngazi za juu. Wapo waliodiriki kunitaja mimi kuwa ndiye ninayehusika. Watu hao ni waongo! Sijamtuma mtu yeyote kugombea, na sina mgombea popote, kwa ngazi yoyote.
"Nawaomba mnaposikia yeyote anasema hivyo, mjue ni mwongo. Mwambieni awaambie sifa zake za kufaa kwa nafasi anayoomba kwani mnamchagua yeye na si huyo anayedai amemtuma," alisema Rais Kikwete.
Aliwakumbusha wagombea kuwa kuna kushinda na kushindwa. Aliwataka watakaoshindwa kuwa tayari kukubali matokeo.
"Tuyachukulie (matokeo) kuwa ndio uamuzi wa watu bila ya kuweka nongwa, kujengeana chuki na kutafuta mchawi. Ndiyo demokrasia ilivyo. Tulizoee jambo hili," alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wanaCCM wasiigeuze siasa ni vita na chuki kama ambavyo wanafanya baadhi ya watani (wapinzani) wao.
Hata hivyo, aliwataka wale wanaodhulumiwa waseme bila kufanya vitendo vya kuleta mgawanyiko au misukosuko ndani ya CCM.
Alisema kiongozi anaweza kutoka kwenye chama chochote, lakini kiongozi bora hawezi kutoka nje ya CCM.
Kuhusu wagombea alisema amefarijika kuona watu wengi wamejitokeza kuomba uongozi. Alisema waombaji ni rika zote, makundi yote katika jamii na wa viwango vyote vya elimu.
source:
http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=3385