SoC01 Tozo mpya zinauma, lakini zinaweza kuwauma CCM,upinzani ukasongesha

Stories of Change - 2021 Competition

NnkoJR

New Member
Jul 17, 2021
1
0
ALHAMISI ya Julai 15, 2021 inaweza kuwa moja ya siku yenye kumbukumbu ya kuchosha akili za mamilioni ya Watanzania, ambao simu imekuwa tegemeo lao la kufanya miamala ili kufanikisha shughuli mbalimbali za kibinafsi na hata maendeleo yao.

Hii ni kutokana na kuanza kutekelezwa rasmi kwa tozo mpya ya Serikali kwa wanaofanya miamala kwa njia ya simu iwe kwa kutuma au kutoa fedha.

Vilio vimekuwa si mijini tu, bali pia huko vijijini. Wengi wanataja makato hayo kama njia ya kuwaumiza na kudidimiza uchumi wao.
airtel tz.jpg

Viwango vya makato kwa hisani ya Airtel Tanzania

Hii inamaanisha kuwa, wale wote ambao wanatuma na kupokea fedha, kwa sasa kilio chao ni kimoja yaani makato makubwa ambayo wanakumbana nayo katika miamala wanayoifanya, huku wengine wakidai tozo hizo mpya za Serikali ni sawa na uporaji au unyang'anyi ambao unaweza kufanywa kwa mtu bila mategemeo yake.

Utekelezaji wa mfumo huo mpya ulianza ikiwa ni siku mbili tu, baada ya kampuni za simu za mikononi kuanza kuwatumia ujumbe mfupi wateja kuwajulisha kuhusiana na kuanza rasmi kutekeleza kwa ukataji wa tozo hizo.

Mfumo huu kwa Watanzania wengi, umeibua hofu kubwa si kwa sababu hawataki kuwa sehemu ya kukatwa asilimia fulani ya fedha kuchangia maendeleo yao, bali ni kwa namna ambavyo makato yamekuwa makubwa kuliko ada za awali.

Aidha, hofu hiyo inakuja kutokana na gharama zake kuonekana kuwa mzigo kwa wengi na hasa wakati ambako kunashuhudiwa kupanda kwa gharama nyingine za maisha kulikosababishwa na ongezeko la kodi katika nishati ya mafuta ya Petroli na Diezeli ambayo kila lita moja imeongezewa shilingi 100 ili kusaidia shughuli za maendeleo hususani miradi ya barabara.

Hii kodi ya uzalendo ambayo inaanzia shilingi 10 hadi shilingi 10,000 kulingana na ukubwa wa muamala isipoangaliwa upya haraka inaweza kuleta changamoto kubwa katika uchumi, kwani pia itapunguza matumizi ya huduma hiyo hivyo kushusha mchango wake kwenye uchumi wa nchi.

Tumeona namna ambavyo, kabla ya kodi ya uzalendo, wateja wa Airtel Money walikuwa wanakatwa shilingi 350 tu ndani ya mtandao kutuma shilingi 15,000 lakini sasa wanalipa shilingi 960 na walikuwa wanakatwa shilingi 550 kwenda mtandao mwingine, lakini imepanda mpaka shilingi 1,160 ambapo watakapotaka kutoa fedha hizo watalipia shilingi 2,010 badala ya shilingi 1,400 ya mwanzo. Hii inamaanisha ndani ya muala wa shilingi elfu 15 unakatwa zaidi ya shilingi 3,000 kiwango ambacho ni kikubwa mno.

Vile vile kwa wateja wa Mpesa, kutuma shilingi 15,000 kwenda kwa mteja asiyesajiliwa, makato ni shilingi 970 kutoka shilingi 360 wakati ikigharimu mtu shilingi 2,820 kwa mteja asiyesajiliwa kutoka shilingi 2,210 ambayo inajumuisha na tozo ya Serikali.
mpesa.jpg

Viwango vya makato kwa hisani ya Vodacom Tanzania

Wakati huo huo, kwenda mitandao mingine, kiasi hicho kitalipiwa shilingi 1,160 kutoka shilingi 550 iliyokuwapo na watakaopelekwa kwenye akaunti zao za benki watakatwa shilingi 1,810 badala ya shilingi 1,200 iliyokuwapo. Kutoa kiasi hicho iwe kwa wakala au ATM wanakatwa shilingi 2,060 kutoka shilingi 1,450. Vivyo hivyo katika mitandao mingine ikiwemo Halotel, Tigo Pesa na nyinginezo.

Ukiangalia ukokotoaji wa tozo hizo utaona kuwa, mtu aliyekuwa akipokea fedha kiasi cha shilingi laki moja kutoka kwa wakala alikuwa akikatwa kiasi cha elfu tatu na mia sita, sasa atakuwa akikatwa jumla ya shilingi elfu sita na miamoja na kiwango hicho kinazidi kupanda kadri muamala wa fedha unavyoongezeka.

Lakini jambo linaloonekana kuwaumiza Watanzania zaidi ni lile la makato hayo kufanyika zaidi ya mara mbili, yaani mtumaji na mtumiwaji popote alipo nchini.

Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa imezoeleka hapo nyuma wakati ambapo makato ya fedha yaliyokuwa yakifanyika kwa mpokeaji wa fedha pekee, lakini sasa tozo hiyo inawagusa wote.

Wengi wanaoelezea kuhusiana na tozo hizo bila kujali itikadi ya chama chake, wote wanaonekana kuwa na misimamo inayouwiana, kwani wote kwa pamoja walia kwa pamoja.

Aidha, tozo hizo zinaonekana kuzidisha wasiwasi kwa Watanzania wanaohofia si tu uwezekano wa kupanda kwa gharama za maisha bali pengine kuanguka katika shughuli zao kutokana kuwabana watu wa kipato cha aina yoyote ile nchini.

Hatua hiyo ya serikali si tu inaacha hofu kwa watumiaji wa huduma za simu za mikononi, lakini pia inaibua wasiwasi mwingine juu ya mwelekeo wa baadae wa mitandao ya simu, kwani maamuzi ya wananchi yanaweza kuwafanya waendelee kutoa huduma au kusitisha kwa ajili ya kutafuta njia rahisi ya kufanya miamalai yao.

Tozo mpya kwa namna moja au nyingine zinatarajiwa kuleta athari za moja kwa moja kwa mamilioni ya wananchi ambao walikuwa wanatumia njia hiyo kurahisisha kupatiwa huduma mbalimbali na hata kusaidia ndugu zao.

Katika miaka ya hivi karibuni kiwango cha matumizi ya simu za mikononi kimekuwa kikiongezeka na ongezeko hilo linashuhudiwa pia katika maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme imeanza kuimarika, huku hadi ifikapo 2024 Serikali ikitarajia nishati hiyo iwe imevifikia vijiji vyote nchini.
tigo.jpg

Ni wazi kuwa, kuwepo kwa kodi hiyo pengine kukawa ni pigo kubwa kwa wananchi hao wa vijijini ambako huduma za simu za mikononi kwao si jambo la anasa bali ni nyenzo muhumu inayotumika kuendesha maisha kama vile kusaka masoko ya mazao yao katika maeneo mbalimbali.

Ujio wa tozo mpya, unaonyesha baadhi ya mapungufu kwa wataalamu wetu wanaohusika na masuala ya kiuchumi, kwani inadhirisha wazi kuwa, hawakufanya utafiti mzuri kuona ni kwa namna gani hii miamala ya simu imekuwa ikitumika zaidi kuliko ile ya kibenki.

Ni ukweli kwamba, soko la benki nchini Tanzania linaonekana kuyumba kwa sababu wengi wametumia njia ya simu za mkononi kufanya malipo au huduma nyingine, hii ikiwa ni huduma rahisi na ya haraka, na ilichangiwa na huko nyuma tozo za benki zikiwa kubwa na masharti mengi ambayo yalikuwa kikwazo kwa watumiaji wa chini.

Kwa haraka haraka unaweza kubaini kuwa, miamala ya simu hapa nchini inatumiwa na kundi kubwa la watu wenye vipato vidogo (maskini) ambao unaweza kusema wapo mstari wa umaskini wa dola tano au chini ya dola kumi unaotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Huduma za miamala ya simu zimewarahisishia Watanzania wengi kupata huduma za haraka, mfano ni rahisi kumtumia ndugu yako hata shilingi 3000 huko kijijini akanunulie dawa au sukari ndani ya dakika moja kuliko ungemwambia asubirie benki, huku wakati mwingine akiwa hajui au hana akaunti benki, kwa kuwa hata kiwango hicho kwa haraka kukipata benki ni vigumu, lakini kwa simu ni mara moja.

Ikizingatiwa kuwa, hata benki nyingi kwa sasa zipo maeneo ya mijini, lakini wakala wa huduma za fedha kupitia simu za mikononi wanapatikana kila kona ya nchi.

Hii inamanisha nini? Watanzania wanakwenda kuchangia utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022 ambayo imeainisha maeneo mbalimbali ya vipaumbele kwa mwaka wa fedha iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Mwigulu Nchemba mwezi Juni 10, 2021 bungeni jijini Dodoma huku baadhi ya vipaumbele vikitegemea makato ya tozo hizo wakiwa na manung'uniko, lakini Mheshimiwa Waziri Nchemba atarajie kwamba, yeye na wabunge wenzake ambao kwa asilimia zaidi ya 90 wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekipalia makaa chama hicho tawala.

Kila mmoja wetu anatambua kuwa, tozo mpya zinauma, lakini zinaweza kuwauma Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi ujao mwaka 2025,upinzani ukasongesha kwa kuwa wameandaliwa mazingira mazuri ya kuwa na hoja ya msingi ya kuwasemea kwa wananchi ambao kila mmoja ameguswa na jambo hili.

Hakuna, Mtanzania ambaye anakataa kukatwa hizo tozo, lakini makato yangefanyika kwa kiwango ambacho hakitamuathiri mtu yeyote, kwani mfano ukikatwa shilingi 10 kwenye elfu moja na shilingi 100 kwa elfu kumi au 500 kwa elfu hamsini, kwa ajili ya kodi ya uzalendo haiwezi kusaidia kufaninikisha malengo?

Ikumbukwe kuwa, wakati akizungumza kwenye kipindi cha 360 cha kituo cha Clouds TV, Julai 12, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema, hiyo sio tu ni kodi, "bali tunatunisha mfuko wa mshikamano. Tutachangia kupitia makato ya simu,”alisema, huku akiongeza kuwa,

Iitakuwa ni aibu kwa miradi ya maendeleo kukwama kwa kuwa Serikali imeshindwa kukusanya kodi.“Kuna mambo hayapaswi kuwepo. Haitakiwi kuona kijiji hakina barabara inayopitika muda wote na tunabeba wagonjwa juujuu. Mbona tunaweza miito ya simu na kukatwa hela nyingi tu kwa nini isiwe kutunisha mfuko wa mshikamano

Licha ya hiyo kuwa ni bajeti yake ya kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 -2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Bajeti ikiwa imejielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali, huku ikiwa na mambo mazuri ambayo yalipongezwa awali, kupitia tozo hizi, zimeonekana kuipunguzia alama za juu bajeti hiyo yenye malengo mazuri.

Kila mmoja wetu alisikia, kuhusiana na vipaumbele vilivyoainishwa katika maeneo matano ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22,maeneo hayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

Waziri Mwigulu alieleza kuwa ili kuwa na uchumi shindani na shirikishi, Serikali itajielekeza katika kugharamia miradi ambayo itajikita katika kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa, kusimamia utulivu wa viashiria vya uchumi kwa ujumla.

Alifafanua kuwa, wamekusudia kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji,kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara za kufungua fursa za kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kupunguza msongamano mijini na barabara za vijijini, madaraja, usafiri wa majini na angani, mageuzi ya TEHAMA pamoja na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali, nishati, bandari na viwanja vya ndege. Lakini ni wazi kuwa, kilichobaki sasa ni wao kuuamua kuendelea kuchukua tozo au kuendelea kuwajengea mazingira mazuri wapinzani ili waweze kushika usukani uchaguzi ujao.
 
Back
Top Bottom