Shibuda aitikisa CCM
na Edward Kinabo
Source: Tanzania daima
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinakusudia kumpitisha Rais Jakaya Kikwete, kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, licha ya katiba na kanuni za chama hicho kutoa uhuru kwa mwanachama yeyote, mwenye sifa zinazostahili kuwania kiti hicho.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati, katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Msekwa akihojiwa katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, alitoa msimamo huo wa chama chake baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusiana na hatua ya Mbunge wa CCM, Jimbo la Maswa, John Shibuda, kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2010, kupitia chama hicho.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa na kuchagua maneno ya kutumia, Msekwa alisema katiba, kanuni na taratibu za CCM zinaruhusu mtu kutangaza nia yake ya kutaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi serikalini.
Alisema Shibuda hajakosea kutangaza nia yake mapema kwa sababu katiba ya CCM haikuweka muda ni lini mhusika atangaze nia yake ya kugombea, ila kinachokatazwa ni kuanza kampeni mapema.
"Katiba yetu haikatazi mtu kutangaza nia yake ya kutaka kugombea na haikuweka muda wa kutangaza nia hiyo. Kwa hiyo yeye ametangaza nia yake … ni sawa. Ila kinachokatazwa ni kuanza kampeni mapema …hiyo ni sawa na sheria ya uchaguzi. Hairuhusu kufanya kampeni kabla ya wakati. Kusema kwamba mimi nitagombea ubunge, udiwani au urais, kanuni hazikatazi," alisema.
Msekwa aliendelea kusema kuwa, pamoja na katiba ya CCM kuruhusu mwanachama kutumia haki na uhuru wake wa kutaka kugombea nafasi yoyote, ikiwemo urais, chama hicho kina utaratibu wake wa ndani uliozoeleka lakini ulio nje ya kanuni, wa kumwachia rais aliye madarakani agombee na kumalizia kipindi chake cha pili, kwa kuwa muda wa ukomo wa urais ni vipindi viwili.
Alisema CCM inakusudia kumpitisha tena Rais Kikwete awanie kiti hicho kwa awamu ya pili, kwa kuwa hadi sasa amefanya kazi nzuri sana ya kuboresha maisha ya wananchi, kwa hiyo itampa nafasi nyingine ya kuomba ridhaa ya wananchi, kama ilivyofanya kwa Rais aliyepita, Benjamin Mkapa.
"Lakini tukiachana na hilo la katiba na kanuni za chama chetu, sisi tuna utaratibu wetu wa ndani ya chama…hii si kanuni, ni utaratibu wetu, ni mazoea. Kwamba kwa kuwa kikomo cha urais ni miaka 10, basi sisi huwa tunamwacha rais aliye madarakani, hasa rais mwenyewe anapokuwa amefanya kazi nzuri, kama Rais Kikwete alivyoboresha maisha ya wananchi, …huwa tunamchagua rais huyo aliye madarakani, agombee urais mara ya pili. Na hivyo ndivyo tunavyokusudia kufanya kwa Rais Kikwete…amefanya kazi nzuri sana," alisema.
Kwa hiyo kama kuna mwenye nia ya kugombea urais kupitia CCM, hakatazwi…lakini kwa kuzingatia mazoea yetu, tunakusudia kumchagua Rais Kikwete. Na haya si maoni yangu binafsi kama ulivyoniuliza…huu ni utaratibu wetu, ndiyo mazoea yetu katika chama," alisema Msekwa.
Naye, Chiligati akizungumza kwa njia ya simu kuhusu suala hilo, alisema Katiba ya CCM haikatazi mwanachama mwenye sifa, kuwania uongozi au kutangaza nia yake ya kutaka kufanya hivyo, isipokuwa inakataza watu kuanza kampeni mapema.
Hata hivyo, kama alivyosema Msekwa, Chiligati pia alisema japo Katiba ya CCM inasema hivyo, bado chama hicho kina utaratibu wake wa kumpa rais aliye madarakani vipindi viwili vya uongozi, kama hajafanya kosa lolote kubwa.
"Kwa hiyo katiba yetu inasema hivyo, japo ndani ya chama chetu tuna utaratibu wetu wa kumwachia rais aliye madarakani apitishwe kugombea urais mara ya pili ili amalizie vipindi vyake vyote viwili. Lakini huo ni utaratibu wetu wa ndani tu…lakini Bwana Kinabo (Mwandishi wetu), wanachopaswa kufahamu walio nje ni kwamba Katiba ya CCM inatoa uhuru kwa mwanachama yeyote yule kugombea wadhifa wowote ule anaotaka," alisema Chiligati.
Katika hatua nyingine, Chiligati alijibu shutuma zilizoelekezwa kwake na kwa Yusufu Makamba, kuhusu kulimbikiziwa vyeo vingi na Rais Kikwete, hata kuelemewa na kukosa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Chiligati alisema, habari hizo amezisoma katika magazeti tu, lakini shutuma za wabunge hao, watazijadili ndani ya vikao vyao vya chama.
Hata hivyo Chiligati, aliwataka wabunge hao wanaomwona kuwa hana ufanisi kuelewa kuwa yeye (Chiligati), kama walivyo binadamu wote, hajakamilika.
"Hayo nimeyasoma kwenye gazeti tu, tutalizungumza hilo kwenye vikao vyetu vya chama. Sina lolote la kusema…ee wanasema sina ufanisi, nilikuwa China wakati wa kampeni za Tarime. Lakini hakuna binadamu aliyekamilika," alisema Chiligati.
Awali katika mahojiano na Msekwa kuhusu shutuma zilizotolewa na wabunge hao ambazo pia zinamgusa Rais Kikwete, Msekwa alisema Rais Kikwete hakufanya kosa lolote katika uteuzi huo kwani alizingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya CCM, ambazo zote, moja kama Rais na nyingine kama Mwenyekiti wa CCM, zinampa mamlaka ya kuteua viongozi anawaona wanafaa.
Alisema tofauti iliyopo ni kwamba, kwa mujibu wa katiba ya nchi, rais anapaswa kuteua waziri kutoka miongoni mwa wabunge, na kwa mujibu wa Katiba ya CCM, rais huku akiwa ni Mwenyekiti wa CCM, ana mamlaka ya kuteua Katibu Mkuu wa chama lakini uteuzi huo lazima uthibitishwe na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).
Alisisitiza kuwa Rais Kikwete kumteua Makamba kuwa Katibu Mkuu wa CCM na wakati huo huo kuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, hakufanya kosa wala hajakosa busara kufanya hivyo.
Alisema hata Rais wa kwanza, Baba wa Taifa, hayati, Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kumteua Oscar Kambona kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na wakati huo huo alikuwa ndiye Katibu Mkuu wa kwanza wa Chama cha TANU, kabla ya kuzaliwa CCM, mwaka 1977.
Hata hivyo alisema, Mwalimu alitumia busara kumteua Kambona kushikilia nyadhifa zote hizo kwa sababu majukumu ya uwaziri wa Tawala za Mikoa kwa wakati huo, yalikuwa yakiendana sana na majukumu ya Katibu Mkuu wa TANU.
Msekwa aliwataka, Zambi na Mpesya, kujenga hoja za kutaka kuwe na sera ya Rais au Mwenyekiti wa CCM, kuwekewa mpaka katika uteuzi wake ili awe anateua mtu mmoja kushikilia wadhifa mmoja tu, badala ya wabunge hao kuendelea kulalamika tu kupitia vyombo vya habari.
"Wao wasilalamike tu kwenu …kwenye vyombo vya habari. Haitawasaidia…wajenge hoja kwenye vikao halali vya chama kwamba sisi tunapendekeza kuwe na policy (sera) inayomshinikiza Rais au Mwenyekiti wa chama (CCM) kuteua mtu mmoja kushikilia cheo kimoja tu, kwamba mtu mmoja asilimbikiziwe vyeo vingi kama wanavyosema, iwe ni ‘one man, one position policy' (iwe ni sera mtu mmoja cheo kimoja). Kwa hiyo wajenge hoja ya kutaka kubadilisha taratibu. Nasisitiza tena, hizi ndizo taratibu zetu," alisema Msekwa.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani katika Jimbo la Tarime na Kata ya Tarime Mjini, ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilishinda, kumekuwa na mjadala mzito ndani ya chama hicho, ambapo baadhi ya wabunge wa chama hicho wameripotiwa mara kadhaa wakimtaka Katibu Mkuu wao, Yusufu Makamba, ajiuzulu.
Aidha, katika hali inayoonyesha kutoridhishwa na uongozi wa Rais Kikwete, mmoja wa wabunge wa chama hicho wa Jimbo la Maswa, John Shibuda, wiki iliyopita alitangaza nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2010, kupitia chama hicho.
source tanzania daima
My take;
Jamani hawa watu wanatuona madanganyika mazuzu eh?? Nashindwa hata kufikiria kama huyu mzee anajua anachokiongea.
Hebu mwenye data tunaomba atuorodheshee kazi nzuri sana alizozifanya huyu anayetajwa hapa jamani jamvini