JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 3,232
- 7,627
Sheikh Ponda Issa Ponda akizungumza na Wanahabari, Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Mei 6, 2026.
View: https://www.youtube.com/watch?v=1fog9mpal5Q
UTANGULIZI
Baada ya Tume ya Jaji Mohamed Othman Chande, kukabidhi vitabu vya ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 23 April, 2026 Ikulu ya Dar
Dar es Salaam, Shura ya Maimamu, tulijipa muda ili tuweze kuipitia kwa umakini hotuba ya uwasilishaji ya Jaji Chande, na kufanya tafakuri ya kina juu ya mustakbali wa ustawi wa nchi yetu kisiasa, kiuchumi, kijamii na katika nyanja ya usalama wa wananchi, mali zao na taifa kwa ujumla.
Pia katika muda huo tulipitia na kusikiliza maoni ya watu kadhaa wakiwemo wanazuoni na Asasi mbalimbali za kiraia. Miongoni mwa hizo ni Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDASA, Tamko la pamoja la Asasi 14 za kiraia na taasisi za watetezi wa haki za binaadamu ikiwemo LHRC, THRDC, TLS, CSL, AGEN, TRAFO, Twaweza EA, nk…Tumestafidi maoni mazuri na ya kizalendo waliyoyatoa. Tunatumia fursa hii kuwaunga mkono na kuwapongeza. Aidha pia tunavipongeza Vyama makini vya siasa nchini kwa misimamo waliyoitoa.
MAZINGIRA YA TUKIO
Oktoba 29, 2025, Tanzania ilifanya Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu na mauwaji makubwa hasa kwa raia wa kawaida. Katika hotuba ya Jaji Chande anasema: “Tume inatambua kuwa vifo vimeacha pengo kubwa katika familia na jamii na kuathiri kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa. Madhara yaliyotokea yamesababisha baadhi ya familia kupoteza tegemeo lao kuu na hivyo kuziweka katika hali ya utegemezi wa kiuchumi na kijamii”.1
Siku zilizofuata mauaji ya kiholela yaliendelea huku kukiwa na amri ya wananchi kukatazwa kutoka majumba mwao. Shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kutoruhusiwa. Vyombo vya usafiri pia vilizuiliwa kusafirisha wananchi kutoka sehemu moja hadi nyingine.
1 Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba, 2025, Uk.29.
Mtandao wa internet ulizimwa nchi nzima. Vyombo vya usalama na majeshi vilitawanywa maeneo mbalimbali ya kila kona ya nchi. Hali hiyo ilisababisha maumivu na madhara makubwa kwa wananchi. Wengi wa raia walipata majeraha makubwa na ulemavu wa kudumu.
KUUNDWA TUME YA JAJI CHANDE
Baada ya kutokea hali tuliyoileza kwa ufupi hapo nyuma, watanzania wengi walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan ashirikishe wadau ili iundwe Tume huru itakayochunguza matukio hayo makubwa yaliyopelekea vurugu na umwagaji wa damu mkubwa. Shura ya Maimamu ni miongozi mwa Taasisi hizo zilizotoa wito huo.
Hata hivyo Rais hakupokea maombi hayo na badala yake tarehe 18/11/2025, aliunde Tume yake mwenyewe na kuitangaza Tarehe 20/11/2025. Alimteuwa Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Mohamed Othman Chande, kuwa Mwenyekiti wa chombo hicho. Pia aliteuwa wajumbe 7, wenye wasifu unaoonyesha utaalamu, ujuzi, uzoefu katika utumishi wa serikali. Rais pia aliipa Tume hiyo, hadidu rejea zinazo waonesha kile wanachotakiwa kukifanya katika jukumu walilopewa.
Kwa sababu ya Rais kutozingatia ombi la kuundwa Tume huru na badala yake akaundwa Tume ya serikali, Asasi kadhaa na wananchi wengi walitoa matamko ya kutoikubali Tume hiyo. Miongoni mwa Asasi hizo ni Shura ya Maimamu Tanzania.
Asasi na wananchi hao waliamini itakuwa vigumu kwa tume hiyo kubaini ukweli, kuuweka bayana, kutoa mapendekezo ya uwajibikaji na marekebisho makubwa. Ugumu huo unakuja kwa sababu miongoni mwa wanao tuhumiwa kwa mauwaji yaliyotokea Oktoba 29, ni vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinapokea amri kutoka kwa Rais (aliyeunda Tume). Pia baadhi ya wajumbe wake ni viongozi wakuu wastaafu wa vyombo vya ulinzi na Usalama.
Kwa sababu ya umuhimu wa Tume Huru na nyingine, Shura ya Maimamu Tanzania tulitamka kutoikubali Tume hiyo pamoja na kazi zake. Na huo ndio msimamo wetu mpaka leo.
Aidha Waraka huu unaojadili mukhtasari wa Ripoti ya Tume ya Jaji Chande aliyoitoa tarehe 23 April, 2026, mbele ya Rais Samia, kama tukio muhimu lililotokea katika jamii linalopaswa kujadiliwa na kutoa ushauri.
MTAZAMO WA KIISLAMU
Mtazamo wa Shura ya Maimamu katika yaliyojiri Oktoba 29, 2025, ni wa Kiislamu. Kwa hiyo tunalazimika kuweka nukta chache za mtazamo huo katika Waraka huu.
Mambo tutakayoyagusia
• Umuhimu wa Mahusiano mema.
• Adabu ya Kutofautiana.
• Makemeo ya vurugu na uharibifu.
• Umuhimu wa uadilifu.
• Makatazo ya kuuwa nafsi bila ya Hukumu halali.
• Umuhimu wa Suluhu linapotokea tatizo.
Mahusiano
Mwenyezi Mungu (SW), ndiye aliyeumba nchi zote na kuwaweka watu wake. Kupitia Mitume na Vitabu vyake Vitakatifu amewaamrisha waishi kama ndugu. “Enyi watu Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu”. (49:13). Pamoja na tofauti za kabila, rangi, Imani, kipato, madaraka, lakini tunatakiwa tuishi kwa usawa katika mataifa yetu.
Adabu
Watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kidini au maisha. Uislamu unasisitiza kuheshimiana, uvumilivu na kutendeana haki. Qur’an Tukufu imekataza dharau: “Wala msitukanane wala kuitana kwa majina mabaya…”. (49:11). Baada ya tukio la Oktoba 29, 2025, kumekua na matusi na kashfa nyingi kutoka kwa pande zinazotofatiana. Na bado zinaendelea. Watu wamekwenda mbali zaidi kwa kutengeneza hata video za kughushi zinazolenga kuvunjiana heshma. Sisi Shura ya Maimau kama viongozi wa dini tunawakumbusha watanzania kuacha mwendo huo kwa sababu ni makosa kijamii, kiutamaduni, kisheria na ni makosa makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu (SW). Lengo la mijadala liweze kufikia ukweli.
Uharibifu
Mwenyezi Mungu amekemea suala la uharibifu wa mambo yote muhimu. “Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa…”. (7:56). Kwa mtazamo wa Kiislamu ni makosa kuharibu Mali.
Uadilifu
Mwenyzi Mungu anasema: Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao Ushahidi…ijapokuwa ni kwaajili ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu”. “Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwaajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekee kutofanya uadilifu”. (4:135/5:8)
Tarehe 23 April, 2026, Jaji Mohamed Othman Chande Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliwasilisha vitabu vya ripoti yake kwa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wakati Jaji Chande akisoma hotuba ya kuwasilisha, akili na masikio ya watu wengi vilikua katika kusikia mambo makubwa mawili:
1. Taarifa ya wale waliofanya mandamano.
2. Taarifa ya wale waliouwa Wananchi/Raia.
Katika lile la mwanzo watu walikua wakitafakari atasema nini kuhusu waandamanaji, walifanya hivyo kwa sababu gani, walitumwa na nani na atasema kama kitendo chao kilikua halali au Jinai. Na la pili atasema nini kuhusu walio uwa watu, walipewa amri na nani ya kuuwa, na atasema kama waliuwa kwa mujibu wa sheria au walitenda Jinai.
Watu walitarajia hivyo kwa kuzingatia hadidu rejea namba moja waliyopewa na Rais: “Kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha ghasia zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na siku chache zilizofuata”.2
Kwa wale waliotuhumiwa kufanya maandamano na au vurugu, alisema walikua na nia ya kuvuruga amani. Akasema walitumwa na watu waliokua nje ya uwanja wa maandamano.
Aliorodhesha kauli alizosema zilitumiwa kuamsha vurugu. Kisha akasema walibeba silaha na akataja aina zake. Miongoni mwa hizo ni mawe, mapanga, mikuki, visu, roto, nondo, sululu, fimbo, rungu, kombeo, vibiriti, vilipuzi, manati na bunduki.
Aidha alisema walipata mafunzo makhsusi kambini, na walilipwa fedha. Na mwisho akasema hayakua maandamano bali vurugu zilizoambatana na uvunjifu wa amani.
Akielezea jinsi walivyofikia katika hukumu hiyo, alisema yeye na wenzake walitumia Mikataba ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Afrika ya Mashariki na sheria za Tanzania, kupima uhalali wa maandamano hayo na ndipo walipo baini jinai hiyo.
2 Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba, 2025, Uk.5.
Katika tukio kubwa la pili la mauwaji, Jaji Chande hakufanya kama alivyofanya kwa waandamanaji. Hakutaja nani waliouwa watu. Hakutaja wauwaji walitumwa na nani. Hakufafanua athari ya kauli za viongozi wa dola zilizokuwa zikitolewa wakati wote wa kuelekea siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, za kuvitaka vyombo vya dola na majeshi vikae mkao wa mapambano.
Hakutafsiri vitendo vilivyokua vinafanywa na wale maafisa wa Vyombo vya dola na usalama, ambao katika picha mbalimbali za video wanaonekana wakiwa katika sare rasmi za jeshi la polisi na wengine wakiwa hawana sare waliobeba bunduki wakiwashambulia raia wasio na silaha. Hakutaja aina zote za silaha walizotumia, magari waliyotumia, vyombo vya angani, vifaa vya mawasiliano na aina za mauwaji waliyofanya.
Mwisho ilitarajiwa kama alivyofanya kwa waandamanaji kuyapima mauwaji hayo kwa mujibu wa Mikataba ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, mikataba ya Afrika ya Mashariki na Katiba ya Tanzania. Na hatimaye akasema kama mauwaji hayo yalikua halali au jinai.
Izingatiwe mauwaji yaligawanyika sehemu mbili kubwa: Kuna watu waliouliwa katika medani ya vurugu, na kuna watu wengi waliouliwa katika makazi yao kama ambavyo hotuba ya Jaji Chande inavyosema:
“Tume ilipokea kutoka kwa waathirika na mashahidi kuhusu watu kupigwa risasi, kujeruhiwa na kuuawa katika maeneo ambayo hayakuwa na ghasia au vurugu. Kuna madai ya watu kupigwa risasi kwenye makazi yao ikiwa ni pamoja na ndani ya nyumba au sebuleni na ndani ya maduka”.3
Ni wazi tukio hili ni kubwa kuliko la mwanzo. Lilihitaja uchambuzi wa kina kuliko vurugu au Maandamano. Kwa ufupi katika nukta hii ya Uadilifu hapakua na udilifu katika kuchunguza na kutoa taarifa ya matukio hayo mawili.
Mauwaji
Uislamu umekataza kabisa kumuua mtu asiyekua na hatia. Hata yule aliyeua mtu hatauliwa mpaka tuhuma ithibitishwe na kuhukumiwa na Mahakama: “Yoyote atakaye muua mtu bila ya (yeye kuua), mtu au kufanya ufisadi katika ardhi, basi ni kama amewaua watu wote…”. (5:52). Kwa mafundisho ya Uislamu haruhusiwi mtu kupanga na kumuua mtu hata kama mtu huyo ni muhujumu uchumi alietajwa wazi katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG.
3 Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba, 2025, Uk.30.
Suluhu
Mwenyezi Mungu anaelekeza pale inapotokea pande mbili zikagombana basi litokee kundi la tatu liwe msuluhishi: “Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi patanisheni...Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki. (49:10).
(Kwa mafundisho hayo, mmoja wa wahusika wa tuhuma za matukio ya Oktoba 29, 2025, hawezi kuunda chombo cha upatanishi. Mwenyezi Mungu anasema “Patanisheni” hili ni kundi jingine, sio moja katika yale yanayogombana. Ufanisi wa maagizo ya aya hii unalazimisha mambo matatu kwa kundi la upatanishi;
1. Uchunguzi,
2. Kusuluhisha na-
3. Kutoa adhabu: “Na ikiwa moja ya makundi hayo linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu (liache dhulma)”(49:10).
Ikiwa mmoja katika watuhumiwa ataunda Kamati ya Uchunguzi na Kamati hiyo ikabaini muasisi wake ndio muhusika mkuu wa sababu za vita, ni kweli Bwaba huyo atakubali ripoti hiyi ya Kamati yake? Kamati nayo itaweza kumuadhibu Bwana wake?
MAPOKEO YA HOTUBA YA CHANDE
Hotuba ya Jaji Chande imepingwa vikali na wadau mbalimbali wakiwemo wasomi, wataalamu wa fani mbalimbali, wanasiasa, viongozi wa dini, wanaharakati na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi. Wadau hao wamesema kuwa taarifa ya Jaji Chande haina ukweli na uhalisia wa kile kilichotokea na imeficha ukweli wa matukio hayo kwa makusudi
Wamesema imekwepa kuwataja wahusika wa mauaji, na kuonesha matumizi makubwa ya silaha za moto dhidi ya wananchi wasio na silaha wakiwemo wale ambao hawakuwepo kabisa katika maandamano au vurugu. Wamedai imekwepa kutumia lugha halisi ya matukio hayo kama vile mauaji kuyaita “vifo visivyo vya kawaida” au “waliofariki” badala ya “waliouwawa”. Wanasema hotuba ya jaji Chande imekusudia kuwasafisha watuhumiwa wakuu na kuficha ukweli wa wanaopaswa kuwajibika. Aidha kwa upande wa Shura Maimamu Tanzania sisi tumeona yapo mambo makubwa ambayo hotuba ya Jaji Chande imeyathibitisha.
Hotuba imethibitisha chanzo halisi cha yale yaliyotokea Oktoba 2025. “Kwa mujibu wa uchunguzi, ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025 zilitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa”.4
Hotuba imekigawa chanzo hicho katika makundi mawili makubwa. Kundi la kwanza ni mambo yaliyotokana na Siasa na kundi la pili mambo ya Uchumi (pamoja na Serikali). Yale ya kiuchumi hotuba imeyapa anuani ya “MAFUTA” (PETROLI), na yale ya kisiasa imeyaita “KIBIRITI”.
Mfano na ufafanuzi huo wa hotuba ya Jaji Chande, umesaidia sana jamii kupata mwanga au uelewa katika jambo hilo. Ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kupima kati ya aliyeleta Petroli na aliyewasha Kibiriti, nani aliyekua na nia na aliye ratibu na kupanga vurugu na mauwaji yale. Tuangalie kwa ufupi uchambuzi wa hotuba ya Jaji Chande.
Sababu za kisiasa:
1. Madai ya Katiba Mpya.
2. Madai ya Kukosekana Demokrasia katika Siasa.
3. Madai ya Tume Huru ya Uchaguzi.
4. Madai ya Udhaifu wa Mfumo mzima wa Uchaguzi.
Sababu za kiuchumi alizozitaja:
1. Ukosefu wa Ajira.
2. Kukosekana kwa ustawi katika fursa za ajira na kiuchumi.
3. Kukosekana kwa mazingira stahiki katika biashara na uwekezaji.
4. Utitiri wa Tozo.
5. Utitiri wa Kodi.
6. Ubadhirifu wa Mali za Umma.
7. Kukithiri kwa Rushwa.
8. Mfumo usio stahiki wa utozaji na ukusanyaji wa Kodi.
9. Kuporomoka kwa Maadili.
10. Kushuka kwa Uzalendo.
11. Serikali kushindwa kutatua shida za Wananchi kwa wakati.
12. Utekelezaji hafifu wa Tume zilizoundwa.
13. Utekaji na Kupotezwa watu.
(Hayo ni maisha ya taifa hili kwa zaidi ya miaka 60 ya utawala wa serikali zote za chama kilichopo madarakani. Hapa ndipo penye fursa ya kuchemsha
4 4 Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba, 2025, Uk.11.
bongo, hivi aliye sababisha mambo hayo ni nani? Ni vyama vya vya siasa vya upinzani? Hotuba ya Jaji Chande imetuangazia wasifu wa taifa letu:
1. Taifa linaloporomoka Kimaadili.
2. Kushuka kwa Uzalendo.
3. Serikali kushindwa kutatua shida za Wananchi kwa wakati.
4. Utekaji na Kupotezwa watu.
5. Kushindwa kutengeneza ajira kwa raia wake.
6. Taifa lililokithiri utitiri wa Kodi na tozo.
7. Kukithiri ubadhirifu wa Mali za Umma.
8. Taifa lililokithi Rushwa.
9. Taifa lenye mfumo wa utozaji na ukusanyaji wa Kodi mbaya.
10. Taifa lenye utaratibu wa kutotekeza tafiti na ripoti za wataalamu (Tume zinazoundwa na mamlaka).
11. Taifa ambalo halina usawa katika fursa za ajira na kiuchumi.
12. Halina mazingira stahiki ya biashara na uwekezaji.
13. Madai sugu ya Katiba Mpya.
14. Kukosekana kwa Demokrasia katika Siasa.
15. Madai sugu ya Tume Huru ya Uchaguzi.
16. Madai ya Udhaifu wa Mfumo mzima wa Uchaguzi wa Viongozi.
Maelezo ya Jaji Chande yanathibitisha kwamba hata kama wale walio washa moto wa Oktoba 29, wasingefanya hivyo, maadamu madumu 16 ya PETROLI (tuliyayaona hapo juu) yametandawaa katika taifa letu, moto lazima utawaka (kama si leo kesho). Katika hotuba yake mbele ya Rais Jaji Chande ameyaita mambo hayo: Chanzo, Sababu, Asili, Chimbuko na Mzizi wa yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
MAPENDEKEZO YETU;
1. Tunamshauri Rais aitoe ripoti hiyo hadharani kwa sababu ilikua inachunguza haki za msingi za wananchi ikiwemo haki ya kuishi na haki ya kujua ni nani aliyesababisha vurugu na mauwaji makubwa ya Watanzania wenzetu. Raia wasio na hatia. Tume ya Jaji Chande ilipanga kuwasilisha ripoti kwa Rais na baadae kuitoa kwa Watanzania wote. Katika hotuba yake Jaji Chande alisema: “Nimetaja baadhi tu ya mapendekezo yaliyomo kwenye Ripoti; bila shaka wadau mbalimbali watapata fursa ya kuyasoma kwa kina ndani ya Ripoti”.5 Hata hivyo Mheshimiwa Rais amesema ripoti ni mali yake na kwa sababu hiyo Watanzania wamenyimwa haki ya kujua zaidi nini kilichopo ndani yake.
5 Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba, 2025, Uk.58.
2. Waliohusika na mauaji na madhara makubwa kwa Watanzania wenzetu wachukuliwe hatua za stahiki za kuwajibishwa. Tume ilieleza kuwa “imesikiliza vilio vya waliopoteza wapendwa wao, waliojeruhiwa, na waliopoteza mali. Waliona macho ya vijana waliokamatwa wakiuliza kwa wasiwasi mustakbali wao. Walikutana na familia ambazo hadi leo hazijaelewa ni nani aliyemuua mpendwa wao na kwa nini”. Pamoja na kusikia haya kutoka kwa waathirika, Tume nayo imeshindwa kuwajulisha waathirika hao ni nani waliohusika na mauaji ya ndugu zao.
3. Waathirika wote wa matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuata walipwe fidia kutokana na madhara waliyoyapata.
4. Tume itoe hadharani ulinganifu wa picha na video wanazodai zimetengenezwa na akili mnembe (AI) na zile inazodai kuwa ni za matukio ya Gaza ili Wananchi wathibitishe ukweli wa madai ya Tume. Aidha, itoe picha au maelezo ya madai ya waandamanaji waliokuwa na silaha/bunduki hizo ni aina gani na zimekamatwa kwa maelfu mangapi, zipo wapi kwa sasa?
5. Ufanyike uchunguzi huru utakaojumuisha vyombo/taasisi za Kimataifa ili kubaini ukweli na kuliponya Taifa. Pamoja na Tume kukana, ni ushahidi uliowazi kuwa; Tume imetegemea zaidi taarifa za Kamati za Ulinzi na Usalama na Vyombo vya dola. Kwa maoni yetu tume kufanya hivyo ilijipotosha kwa kujua au kutokujua kwani vyombo vya dola kwa raia ni watuhumiwa namba moja wa utekaji na mauaji yanayoendelea nchini. Kwa mfano moja ya Ushahidi wa tuhuma za wananchi ni taarifa iliyowahi kuwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ilielezwa ifuatavyo;
“Mheshimiwa Spika. Juni 12, 2017 mchana, Bi Ziada Salum wa Kitongoji cha Maparoni alikuwa nyumbani kwake akipika chakula cha familia, Jeshi la Polisi lilifika na kumchukua kwaajili ya kwenda kumhoji. Hivi leo ni miezi 11 tangu achukuliwe, hajarudishwa. Familia yake haijaarifiwa chochote, imekaa na matarajio kuwa ipo siku atarudi. Si Bi Ziada tu aliyechukuliwa na Polisi na kutokurudishwa mpaka leo bali wapo wengi. Mwezi huo huo wa Juni 26, 2017, kwa staili ya namna hiyo hiyo, kinamama wa familia moja, Rukia Muhohi na Tatu Muhohi, walichukuliwa na Jeshi la Polisi, na mpaka leo hawajarudishwa. Kwa hivyo basi, kwa maelezo hayo niliyoyatoa, kwa mujibu wa Kanuni ya 120 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu kadhia za Mauaji, Kupotea watu, Kupigwa Risasi na Kuteswa watu na vyombo vya dola”. Na ipo mifano mingi ya matukio ya namna hiyo.
6. Mapendekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume katika hotuba yake yafanyiwe kazi kwa uharaka mkubwa na kwa wakati ili kuliponya Taifa letu.
Tukio la maandamno ya Oktoba 29, 2025, hotuba ya Jaji Chande imelitaja kama moja ya vyanzo vya uvunjifu wa amani siku hiyo. Kwasababu hiyo imefanya uchambuzi mkubwa kuonesha madhara yake. “Tume” pia imetaja mambo 4, ya kisiasa na 13, ya kijamii, kama chanzo kikuu cha yaliyotokea Oktoba 29. Tulitaraji mambo hayo 4+13, kwa uzito wake pia Tume ingefanya uchambuzi mzito kueleza madhara yake.
Ingeeleza madhara ya taifa kutawaliwa na Rushwa, viongozi kuwa mafisadi wa mali za umma, kutowajibishwa mafisadi hata wale waliobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali. Madhara ya raia kutekwa, madhara ya kuwavunjia heshma Masheikh na Viongozi wa vyama vya upinzani kwa kuwabambikizia kesi za Ugaidi na Uhaini. Madhara ya serikali kushindwa kutatua shida za wananchi kwa muda mrefu, taifa kushindwa kujenga mazingira mazuri ya uchumi na uwekezaji na utitiri wa kodi usio na manufaa kwa raia maskini
Madhara ya serikali kuunda sera ya kugeuza hospitali za watu maskini zilizojengwa na kuendeshwa kwa kodi zao (Hospitali za serikali), kuwa vitega uchumi, madhara ya serikali kutoza mamilioni ya shilingi maiti ya wananchi maskini, na mengine yaliyotajwa moja kwa moja na hotuba hiyo.
7. Hatua stahiki za kujenga Taifa lenye misingi ya imara ya maadili kwa watumishi wa umma, uzalendo na kutenganisha kati ya siasa na utumishi wa umma ifanyike haraka. Tume imeeleza kuwa moja ya sababu za matukio hayo ni mmomonyoko wa maadili na kuondoka kwa uzalendo. Lakini ishara ya tuhuma hizo imewakwepa viongozi wa juu na kuelekezwa kwa Wananchi wa kawaida. Ipo mifano mingi inayodhihirisha Viongozi wengi wamepoteza sifa za kuwa Viongozi wa umma kutokana na vitendo vya kifisadi, kukosa maadili na kukiuka misingi ya utawala wa sheria.
8. Jaji Chande na Tume yake wamependekeza kuundwa kwa Tume nyingine ya uchunguzi wa kijinai. Tume ilieleza kuwa miongoni mwa sababu zilizopelekea kutokea ya Oktoba 29, “…ni utekelezaji hafifu wa mapendekezo ya tume zilizoundwa na serikali huko nyuma.” Kwa uzoefu wa Shura ya Maimamu, mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa huko nyuma si kwamba yanatekelezwa kwa uhafifu bali hupuuzwa kabisa na kuwekwa makabatini. Mapendekezo kama ya Tume ya Jaji Nyalali, Tume ya Jaji Kisanga, Tume ya Jaji Warioba, Tume ya Haki Jinai na Kikosi kazi cha Rais. Hiyo ni mifano ya wazi kuwa serikali iliyopo madarakani, haiko tayari kuleta ustawi mzuri wa maisha ya Watanzania kwa kujenga misingi imara ya mifumo ya haki, na utawala wa sheria.
Maoni yetu, kuunda Tume zaidi juu ya suala hili ni matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma katika nchi ambayo imezingirwa na madeni ya matrilioni ya shilingi. Tunaona kufanya hivyo ni hadaa za kisiasa zinazolenga kupoteza muda ili kutuliza joto la umma unaotaka uwajibikaji na mabadiliko ya mfumo wa utawala.
9. Tushindanishe hoja za kulijenga upya Taifa letu. Hoja zijibiwe kwa hoja (maoni kinzani yajibiwe kwa maoni bora zaidi) na si matusi, bunduki, kutekana, kulaaniana, kukamatana na kubambikiana kesi. Ukandamizaji wa raia duniani kote haujawahi kushinda na kuwa suluhisho la matatizo yaliyopo. Ni kuliahirisha tatizo na kulikomaza zaidi tatizo.
10. Kuhusu Maridhiano tunasema hayawezi kuwa ya ukweli. Kuna kila dalili za kuona kuwa waliopo madarakani hawaoni kama katika nchi yetu kuna matatizo ya msingi yanayohitaji kufanyiwa kazi. Baadhi ya Viongozi hawana Uzalendo na maadili, maslahi binafsi na ya makundi ndani ya watawala yamewekwa mbele. Hakuna tena siasa za ushindani wa Vyama kwa hoja, bali dola dhidi ya wanaoitwa Wapinzani wa watawala. Jaji Chande na Tume yake wanaona kama Wananchi pekee ndio wenye matatizo na watawala wana utakatifu wa kipekee wasiokuwa na dosari kwa yaliyotokea Oktoba 29.
Maoni yetu kabla ya maridhianao, ukweli wa masuala yote yaliyotokea Oktoba 29 yabainishwe wazi na hatua za uwajibikaji zichukuliwe, na haki itendeke na kuonekana ikitendeka. Kesi zote za kubambikiziwa zikiwemo zile za Ugaidi, Uhaini na Masheikh walio hukumiwa kunyongwa na kesi za kisiasa zifutwe na wahusika kuachiwa huru bila masharti yeyote. (Waislamu wamekuwa ni waathirika wakubwa wa kesi za kubambikizwa katika nchi yetu). Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu afutiwe mashtaka aliyonayo. Na hili linawezekana kama ilivyowezekana siku za nyuma kwa wanasiasa wengine.
11. Kuhusu Katiba Mpya; Mwenyekiti wa Tume ameeleza kuwa “Ni muhimu Katiba Mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030. Serikali iunde Kamati ya Wataalamu wa Katiba ambayo Itakuwa na: jukumu la kupitia Katiba iliyopo; rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba; Katiba Pendekezwa ya Mwaka 2014; ripoti za Tume, Kamati na Vikosi Kazi mbalimbali. Baada ya kufanya mapitio ya nyaraka hizo, Kamati ya Wataalam itapata maoni na michango ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba Mpya itakayopigiwa kura na wananchi (referendum)”.
Eneo hili Shura ina mapendekezo mawili yafuatayo;
Kabla ya Rasimu kupelekwa kwa Wananchi (kupigiwa kura ya maoni), pawepo na mkutano maalumu wa Wadau wakuu katika Siasa, taasisi za kidini, Asasi za kiraia, Wafanya biashara, wadau wa habari nchini, nakadhalika ili kujadiliana juu ya maeneo ya msingi ambayo hapo awali yalipelekea kuharibika kwa bunge la Katiba na rasimu kushindwa kuwafikia wananchi.
Pawepo na muafaka wa Kitaifa. Aidha pendekezo la pili ni kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa maana ya Huru, kisha ndioifa nyike kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya. Kura ya maoni itakosa uhalali wa kisheria na kisiasa bila ya kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Tumepitia dondoo za mapendekezo ya mchakato wa Katiba Mpya katika hotuba ya Jaji Chande, tunapendekeza utekelezaji wa dondoo hizo uanze na namba 5,6,7 ndipo utekelezaji wa pendekezo namba 4 ufanyike.
Hitimisho
Shura ya Maimamu Tanzania, inaamini kuwa Amani, Utulivu na Maendeleo vitapatikana na kustawi kwa kuwa na utawala unaozingatia sheria, na Kutenda Haki. Ukiukwaji wa haki nchini umechochea na kujenga chuki kubwa kati ya viongozi wa serikali na wananchi. Mageuzi ya kweli katika mifumo ya Utawala, Siasa, Uhuru wa Kiraia, uhuru wa Vyombo vya Habari na Asasi za Kiraia, Mageuzi makubwa ya muundo na utendaji wa jeshi la polisi, Uwajibikaji wa serikali na vyombo vyake kwa wananchi, kukomeshwa kwa vitendo vya rushwa na ufisadi, na mabadiliko ya kweli ya mfumo wa utoaji haki (Mahakama) ni nyenzo muhimu za kulirejesha Taifa letu katika UMOJA.
Tukamilishe Waraka wetu kwa maneno Matukufu ya Mwenyezi Mungu (SW): “Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu”. (05:02).
SHEIKH PONDA ISSA PONDA
KATIBU MKUU-SHURA YA MAIMAMU TANZANIA-0675839510.