Hatima ya Chenge wiki hii
*Serikali ya Jersey yajiandaa kutoa tamko
*Ni linalohusu kashfa ya rada,'vijisenti'
Na Mwandishi Wetu
WAKATI wiki hii limeingia kumi la mwisho kabla ya kujulikana hatma ya watuhumiwa wa wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu, tarifa ya uchunguzi wa kashfa nyingine nzito inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, inatarajiwa kuanikwa muda wowote kuanzia sasa.
Bw. Chenge amekuwa akichunguzwa na makachero wa Kitengo cha Kupambana na Makosa ya Ufisadi nchini Uingereza (SFO) kwa miezi kadhaa sasa, kuona iwapo alinufaika kwa namna yoyote na kamisheni iliyotolewa isivyo halali na kampuni ya uuzaji vifaa vya kijeshi na anga ya BAE Systems ya Uingereza iliyoiuzia rada Tanzania.
Mfanyabiashara wa kitanzania, Bw. Shaileshi Vithlani alikiri kupokea sh. bilioni 12 kama ada ya uwakala na pia 'hongo' kwa ajili ya vigogo kadhaa wa Tanzania alipobanwa na makachero wa SFO.
Uchunguzi zaidi wa SFO kuhusu maofisa wa Tanzania wanaoweza kuwa walinufaika na sehemu ya kamisheni hiyo, ulianza huku vigogo kadhaa wa Serikali akiwamo Bw. Chenge waliohusika kwa namna moja au nyingine katika mchakato wa ununuzi wa rada, wakichunguzwa. Wakati mkataba wa ununuzi huo ukisainiwa Bw. Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa maofisa hao wa Tanzania walihojiwa na kupekuliwa nyumba na mali zao jijini Dar es Salaam na baadaye kuitwa Uingereza ambako walibanwa zaidi katika mahojiano na makachero.
Kachero Helen Garlick, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi (Upelelezi) katika SFO, Majira imebaini kuwa alifika Dar es Salaam, akiwa na timu ya makachero wengine kuendesha sehemu ya uchunguzi huo.
Tangu SFO ilipoanza 'kumchimba' Bw. Chenge na kubaini kumiliki akaunti kwenye visiwa hivyo, Serikali ya visiwa vya Jersey ambako ndiko Chenge ilikobainika kuweka takribani pauni 500,000 (zaidi ya sh. bilioni moja), nayo ilianza uchunguzi wake mbali na ule wa SFO.
Katika mawasiliano yake na Majira kwa njia ya baruapepe juzi, Msemaji wa Waziri Mkuu wa Jersey, Bibi Cathy Keir alithibitisha kuwa kwa kipindi chote hicho, maofisa wa Serikali hiyo walikuwa wamepewa kazi ya kufuatilia uhalali wa akaunti ya Bw. Chenge.
"Suala hilo limekuwa likishughulikiwa na maofisa wetu wa sheria kwa muda sasa. Nitatoa tamko muda wowote wiki ijayo," alisema Bibi Keir katika baruapepe yake hiyo kutoka Jersey.
Awali katika mahojiano na Majira Jumapili, miezi kadhaa iliyopita, Serikali ya Jersey ilitangaza rasmi kuwa itachukua hatua kali dhidi ya Bw. Chenge ikiwamo kutaifisha fedha zote za akaunti hiyo ambayo kwa sasa imezuiwa, iwapo itabainika hakuzipata kihalali.
Katika taarifa hiyo, ilisema kwa mujibu wa sheria za visiwa hivyo, wana uwezo wa kufanya hivyo kama walivyowahi kutaifisha fedha za kiongozi wa zamani wa Nijeria, hayati Jenerali Sani Abacha.
Bw. Chenge mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia katika tuhuma hizo na kuzitaja fedha zilizoko Jersey kuwa ni 'vijisenti' tu.
Walipoulizwa kuhusu tuhuma hizo na hatua zilizofikia, maofisa wa kampuni ya BAE Systems waliendelea kusisistiza kuwa kwa sasa wanatoa ushirikiano kwa makachero wa SFO.
"BAE Systems inaendelea kutoa ushirikiano unaopaswa kwa wachunguzi kuhusu kashfa mbalimbali likiwamo suala la Tanzania. Kwa sasa hatuwezi kusema lolote zaidi," ilisema taarifa yao kwa gazeti hili.
source: majira