Chenge, Kigoda kupitia mkataba jengo la UVCCM
2008-09-11 10:55:55
Na Mary Edward, Dodoma na Simon Mhina Dar
Kilio cha Nape Nnauye juu ya mkataba wa jengo jipya la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kimesikika ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho na sasa mkataba huo umeundiwa Timu ya watu watatu kurekebisha kasoro zilizopo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Feruz, aliiambia Nipashe jana usiku kwamba Timu hiyo itaundwa na wajumbe wa Kamati Kuu, Andrew Chenge, Pindi Chana na Dk. Abdallah Kigoda.
Alisema kazi ya Timu hiyo ni kushirikiana na UVCCM kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mkataba huo na kuendelea kushauri hatua kwa hatua za utekelezaji wa mradi huo.
Hata hivyo, Feruz alisema Kamati Kuu haitapitia tena mkataba huo, bali itakuwa ikipewa taarifa ya maendeleo yake.
``Kazi ya kusaini mkataba huo ipo ndani ya uwezo wa UVCCM,`` alifafanua.
Alisema suala la kusainiwa kwa mkataba huo liko ndani ya uwezo wa UVCCM na kwamba kilichokuwa kimesainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Edward Lowassa, si mkataba wa ujenzi bali ni makubaliano ya awali (MoU).
Alitaja baadhi ya kasoro zilizogundulika kuwa ni kutokueleza madaraka ya bodi ya wakurugenzi kwa pande zote mbili; kutokuweka wazi mchakato mzima wa uendelezaji wa jengo hatua kwa hatua; na kutokuweka wazi hatua za kusuluhisha migogoro endapo itajitokeza.
Feruz pia alisema mkataba huo hausemi sababu za kuvunjwa kwa mkataba kama ikibidi.
Mkataba huo umekuwa chimbuko la mvutano ndani ya UVCCM kiasi cha kusababisha mwanasiasa kijana na machachari, Nape, kufukuzwa uanachama wa umoja huo Jumapili iliyopita.
Nape alifukuzwa unachama na Baraza Kuu la UVCCM baada ya kutuhumiwa kuvunja kanuni za umoja huo.
Feruz alisema kwamba Timu hiyo itakuwa endelevu kwa ajili ya kushirikiana na UVCCM kushauri maendeleo ya mradi huo.
Pia alisema kwamba Kamati Kuu imegundua kuwa mradi huo una manufaa kwa UVCCM kwa kuwa utaifanya jumuiya hiyo kujitegemea.
Alisema Kamati Kuu imeona ni vema jumuiya hiyo kuingia ubia kwa vile haina uwezo wa kuliendeleza eneo hilo wala kuliendesha. ``Kama hawataingia ubia basi eneo lile lingeendelea kuwa wazi tu bila faida,`` alisema.
Kwa mujibu wa mkataba huo, UVCCM itamiliki asilimia 25 na wabia asilimia 75.
Hapo awali, Nape alionyesha wasiwasi wake kuhusiana na mkataba huo kutokuwa na ukomo na kiasi kidogo cha faida ambayo inatarajiwa kupatikana.
Hata hivyo, Feruz alisema Kamati Kuu imeridhia mkataba huo kuwa endelevu kwa ubia kwa pande zote mbili.
Kuhusu suala la Nape kufukuzwa uanachama wa UVCCM, alisema Kamati Kuu imesema kwamba haiwezi kuingilia maamuzi ya Baraza Kuu la UVCCM, lakini Nape ana uhuru wa kukata rufaa kwa umoja huo au hata CCM kama hakuridhika na maamuzi.
* SOURCE: Nipashe