Take home message: Nimekuwa nikijiuliza kila siku: Hivi, mtu mwenye akili timamu na raia mwema wa nchii au yoyote ni kwanini ununue Pingu?! Za nini?!!!!!!!
Sakata la Jerry Muro: Jeshi sasa lakuna vichwa
DUKA LA MZINGA LASEMA PINGU HAZIUZWI KWA RAIA
SAKATA la Mwandishi wa habari Jerry Muro, anayetuhumiwa kujihusika na vitendo vya kutaka fedha kwa nguvu pamoja na kukutwa na pingu, limezidi kufumuka baada ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kujadili sababu za kuingizwa katika kadhia hiyo huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiahidi kushughulikiwa kwa haraka.
Muro, mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji (TBC) na ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kufichua aina tofauti za rushwa, Jumapili iliyopita alikutwa na pingu katika gari alilokuwa akilitumia baada ya kukamatwa kwa kudaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.
Juzi, Muro aliwaonyesha waandishi risiti ya kumiliki pingu, alizodai kuzinunua katika duka la silaha la Mzinga lililo Upanga jijini Dar es Salaam, lakini hakuwa amewasilisha risiti hiyo kwa Jeshi la Polisi ambalo linaendelea kumpa muda wa kutafuta kidhibiti hicho.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, afisa habari na mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Mgawe Kapambala alisema wameshangazwa na suala la raia kuruhusiwa kununua pingu wakati hana matumizi nayo na kwamba tayari wamefanya vikao kujadili suala hilo.
"Sisi wenyewe tumeshangazaa baada ya kuona taarifa ile kwenye vyombo vya habari, lakini tunachojiuliza ni kwamba inakuwaje raia anauziwa pingu wakati hana matumizi nayo,â alisema Kanali Mgawe.
"Duka lile linauza hadi silaha za moto ndio maana tunashindwa kuelewa."
Kwa mujibu wa uchunguzi ambao gazeti dada la The Citizen liliufanya jana kwenye duka la silaha la Mzinga, raia hawaruhusiwi kununua pingu isipokuwa vyombo vya dola tu tena kwa shughuli maalum tu.
Mwandishi aliyejaribu kununua pingu kwenye duka hilo, aliambiwa: "Hatuwezi kukuuzia wewe kwa kuwa hautoki jeshini. Tunauza kwa polisi na magereza. Na silaha tunauza kwa watu kwa sababu maalum, lakini si pingu."
Suala la Muro pia liliibuka bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu.
Akijibu swali kuhusu mkasa huo wa Muro, Waziri Pinda alisema suala hilo litafanyiwa uchunguzi wa kina na kumalizwa kwa haraka kwa kuwa linaweza kusababisha mkanganyiko na kuzua hisia mbaya miongoni mwa wananchi.
Waziri mkuu alilazimika kulitolea maelezo hayo baada ya kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed kuhoji serikali inalifikiriaje juu ya sakata hilo.
Katika swali lake, Hamad alitaka kujua iwapo misukosuko anayopata Muro ambaye ni mwandishi wa kituo cha TBC1, kama ni sehemu ya misukosuko wanayopata waandishi wa habari wanaofuatilia mambo mazito duniani hasa barani Afrika.
Kabla ya kuuliza swali mbunge huyo alieleza ameshuhudiwa kwa muda mrefu waandishi wengi wa habari wanaofuatilia mambo mazito ya nchi, hupata misukosuko sehemu mbalimbali duniani hasa katika Bara la Afrika.
Na kabla ya majibu ya Waziri Pinda, Naibu Spika Anna Makinda alisema "bahati yako, halijaenda mahakamani".
Lakini katika majibu yake Waziri Mkuu Pinda alionyesha ugumu wa swali hilo akisema: "Hili suala lingekwenda mahakamani, jibu lingekuwa rahisi kweli."
Akaongeza:"Labda niseme kwanza kwamba, binadamu alivyoumbwa ni kiumbe mwenye mapungufu mengi tu, hata kama angekuwa ana sifa nyingine zote, tukubali tu kwamba atakuwa na mapungufu. Waziri mkuu anayo; Hamad anayo; kwa hiyo na waandishi wa habari vile vile wanayo mapungufu yao kama binadamu."
Alisema ndio sababu ziliwekwa sheria, kanuni na taratibu ili kusaidia kufanya mambo kwa kuzingatia sheria na kanuni.
"Sasa yaliyompata Jerry... niseme tu kwamba kama binadamu na kama mtumishi mwingine yoyote, ni jambo ambalo linawezekana kabisa. Yale anayotuhumiwa yanawezekana yakawepo, vile vile yasiwepo," alisema Pinda.
"Ndiyo maana kwa sababu hiyo inabidi uchunguzi ufanyike, tena wa kina ili kuweza kubaini ukweli wa yale wanayomtuhumu ni kiasi gani na kiasi gani si kweli."
Hata hivyo alisema tatizo ni namna jambo hilo lilivyoanza kushughulikiwa na vyombo husika vya usalama na Jerry mwenyewe. Alisema wote wamekimbilia kwenye vyombo vya habari na kujenga picha tofauti kwa wananchi.
"Tatizo ninalolitapa, Mheshimiwa Hamad, ni pengine namna jambo hili lilivyoanza kushughulikiwa... tumekimbilia kwenye vyombo vya habari sisi tunaochunguza, na yeye kama mtuhumiwa ametafuta vyombo vya habari na kuvitumia. Kwa hiyo sasa ujumbe tunaowapa wananchi kwa ujumla unaweza ukatuchanganya sana.
"Kwa hiyo mimi rai yangu ni kuwa uchunguzi fanyeni kama mnavyofanya uchunguzi mwingine wowote. Utakapofikia mwisho, itajulikana kama ni kesi ya kwenda mahakamani au hapana," alisema Pinda.
Katika swali lake la nyongeza Hamad, ambaye ni mbunge wa Wawi (CUF), alitaka kujua kama waziri mkuu anaweza kutumia nafasi yake kuhakikisha suala hilo linakwenda na kumalizika haraka.
Akijibu swali hilo Pinda alisema yeye binafsi hapendi suala hilo liendelee kwa muda mrefu kwa kuwa linaweza kuanza kuibua hisia zisizo nzuri kwa wananchi.
Alidokeza kuwa tayari amezungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ambao wamempa majibu ya uhakika kuwa suala hilo halitachukua muda mrefu kumalizika.
Wakati huo huo Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeeleza kuwa halitaki kulumbana na Muro kwa kujibizana kwenye vyombo vya habari na kuwataka wananchi kuliachia jeshi hilo lifanye kazi yake ili sheria ichukue mkondo wake mahakamani. Habari hii imeandikwa Exuper Kachenje, Dodoma, Sadick Mtulya, Patricia Kimelemeta, Boniface Meena na Festo Polea