Mwandishi Jerry Muro aingia matatani Dar
Boniface Meena na Sadick Mtulya.
SIKU chache baada ya kutoa habari zilizoanika rushwa zinazofanywa na askari wa kikosi cha usalama barabarani, mwandishi wa habari za uchunguzi, Jerry Muro ameingia matatani baada ya kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.
Muro, mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji (TBC) na ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kufichua aina tofauti za rushwa, anashikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ambayo imeeleza kuwa habari zaidi kuhusu mkasa wake zitatolewa leo.
Habari za kupambana na kero ya rushwa na ufisadi jana zilimwingiza mwandishi huyo mikononi mwa polisi.
Habari zaidi zinasema kuwa Muro, ambaye alishinda tuzo ya Mwanahabari Bora wa mwaka 2009 kutokana na habari yake ya rushwa inayofanywa na askari wa usalama barabarani, alikumbwa na mkasa huo jana majira ya saa 6:00 jijini Dar es Salaam.
Alikamatwa wakati akiwa hoteli ya Sea Cliff.
Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata, Muro alikamatwa baada ya kuwekewa mtego na polisi mara baada ya kuarifiwa na mfanyabiashara mmoja, ambaye jina halijawekwa bayana na polisi, kuwa mwandishi huyo amedai rushwa ya Sh10 milioni.
Habari zinadai kuwa mwandishi huyo alikamatwa muda mfupi baada ya kukabidhiwa fedha hizo.
"Muro alikuwa ameahidiana na mfanyabiashara mmoja kuwa angepewa Sh10 milioni kama hongo, lakini mfanyabiashara huyo alitoa taarifa polisi na ndio leo (jana) wamefanikiwa kumkamata. Walimkamata mara baada ya kupokea fedha hizo," alisema mtoa taarifa.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alikiri jeshi lake kumshikilia mwandishi huyo kwa mahojiano, lakini hakutaka kuelezea zaidi mkasa huo.
"Ni kweli yuko hapa na anahojiwa na mimi ndo ninapewa taarifa hivyo nitatoa taarifa kamili kesho (leo) saa 6:00,"alisema Kova.
Alisema kuwa Muro amekamatwa kutokana na tuhuma za kutaka kuchukua fedha kutoka kwa mlalamikaji ambaye hakumtaja jina lake.
Kukamatwa kwa mwandishi huo ni mwendelezo wa wimbi la matukio ya kukamatwa kwa waandishi mara baada ya kuripoti uozo katika taasisi za serikali. Mwaka 2004, mwandishi mwandamizi wa IPP, Zephania Musendo alikamatwa kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa kigogo wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru).
Alikamatwa baada ya kutoa habari mfululizo kuhusu uozo uliokuwa unaihusu taasisi hiyo, hasa migongano ya vigogo wa Takuru, ambayo kwa sasa imeongezewa majukumu na kuitwa Takukuru. Mwandishi huyo alitiwa hatiani mwaka 2005 na kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Mwaka 2002, mwandishi wa Mwananchi, George Maziku alikamatwa na polisi kwa madai ya ya kuingilia uhuru wa Bunge baada ya kuandika habari kuwa baadhi ya mabadiliko ya sheria yalilenga kukipa upendeleo chama tawala na kwamba suala la takrima lingechochea rushwa.
Maziku alihojiwa na polisi kwa saa kadhaa na baadaye kuachiwa bila ya kufunguliwa mashtaka.
Mwaka 1996, mwandishi wa IPP mkoani Ruvuma, Adam Mwaibabile alikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka za serikali. Mwandishi huyo alikuwa anachukiwa na uongozi wa mkoa kutokana na kuripoti uozo uliokuwa ukifanywa na viongozi wa juu wa serikali ya mkoa.
Inadaiwa alikutwa na nyaraka kutoka kwa mkuu wa mkoa ambayo ilikuwa ikimuelekeza mkurugenzi kutompa mwandishi huyo leseni ya biashara.
Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja, lakini juhudi za wanaharakati na wadau wa habari zilimrejesha mahakamani kupinga hukumu hiyo na akashinda na kuachiwa huru.
Katika taarifa yake iliyotingisha Jeshi la Polisi, Muro, wakati huo akiwa kituo cha televisheni cha ITV, alionyesha jinsi askari wa usalama barabarani wanavyoomba na kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa magari kwenye Barabara ya Morogoro.
Mapema mwaka huu akiwa TBC1, Muro alionyesha rushwa kama hiyo ya askari wa usalama barabarani mkoani Iringa wakiomba na kuchukua rushwa kutoka kwa madereva. Habari hizo mbili zilisababisha askari zaidi ya 20 kutimuliwa kazi.
Mbali na tuzo ya Mwandishi Bora wa Mwaka, Muro alitunukiwa pia tuzo mbili tofauti; moja ikihusu uandishi mzuri wa habari zinazohusu utawala bora na nyingine VVU na Ukimwi kwa upande wa televisheni.