Makachero wa polisi wakichukua nyaraka kutoka kwa Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Murro (wa pili kushoto) wakati walipopekua gari lake katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaama jana.
Utata umeghubika tukio la kukamatwa kwa mshindi wa tuzo ya mwandishi bora kwa mwaka 2009, Jerry Muro, anayefanya kazi katika Shirika la Utangazaji wa Taifa (TBC).
Taarifa zinaeleza kuwa Muro alikamatwa jana asubuhi maeneo ya katikati ya jiji, baada ya askari polisi kulizingira gari lake na kumweka chini ya ulinzi, kisha kumpeleka Kituo Kikuu kwa mahojiano.
Inaelezwa kwamba Muro alifika katika eneo hilo baada ya kupigiwa simu na mtu asiyejulikana, akimtaarifu kuhusu kuwepo tukio lenye umuhimu kwa jamii, ambalo alistahili kuliandika na kulitangaza.
Wakati hayo yakijiri, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ameshindwa kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, licha ya kuthibitisha kushikiliwa kwa Muro.
Kova aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, maelezo ya ufasaha kuhusu kukamatwa kwa Muro, atayatoa leo kwa waandishi wa habari.
Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka polisi zilieleza kuwa baada ya kufikishwa Kituo Kikuu, Muro alidaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa mtu aliyetambulika kuwa ni Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.
Muro anadaiwa kuomba rushwa hiyo ili asaidie kushughulikia tatizo la kufukuzwa kazi kwa Mhasibu huyo, kulikofikiwa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Nipashe ilipofika Kituo Kikuu jana mchana, ilimshuhudia Muro akishikiliwa na polisi, huku gari lake aina ya Cresta GX 100 yenye namba T 545 BEH likilindwa na askari kanzu.
Habari za kipolisi zilidai kuwa, baada ya kufikishwa kituoni hapo, Muro alitakiwa kutoa maelezo kuhusu tukio la siku mbili zilizopita, la kumuomba rushwa Wage.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Wage anayedaiwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo aliiambia polisi kwamba alisahau mawani yake kwenye kiti cha mbele cha gari la Muro, na kwamba aliona pingu za polisi ndani ya gari hilo.
Kutokana na maelezo hayo, Muro alitakiwa kwenda kupekuliwa, lakini alipotakiwa kutoa ufunguo, Muro hakuuona, hali iliyomfanya aombe ruhusa ya polisi kuomba ndugu zake wamletee (ufungo) wa akiba kutoka nyumbani.
Kabla ya ufunguo kuletwa kituoni hapo, inadaiwa kuwa ufunguo wa awali ulionekana katika mazingira ambayo Muro hakuyajua, ndipo aliposhuka kutoka sehemu ya juu kituoni hapo, akiwa chini ya ulinzi wa polisi kwenda kupekuliwa gari lake.
Muro alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi, hakuonekana kushtushwa na tukio hilo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida alisema nipo hapa kikazi, si mnajua polisi wana ushirikiano mzuri na waandishi wa habari?
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuhusishwa na rushwa, Muro ambaye kuna taarifa kwamba aliachiwa huru kwa dhamana jana jioni, alijibu kwa ufupi, hakuna kitu kama hicho.
Kadhalika haikuweza kujulikana kwa nini Wage alivutika kwenda kushitaki kosa la rushwa polisi badala ya Takukuru ambao hutoa pesa za unga ambazo huwa kidhibiti 'murua'.
Muro amewahi kutayarisha vipindi vya televisheni vilivyotangazwa kupitia vituo viwili tofauti vya luninga, zikifichua uovu wa rushwa unaofanywa na polisi wa usalama barabarani, maarufu kama trafiki.
Kwa mara ya kwanza, Muro akiwa mfanyakazi wa ITV, alishirikiana na mpiga picha wake, Idrisa Magomeni, walifichua rushwa inayotolewa kwa trafiki katika maeneo ya kati ya mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.
Makala hiyo iliyochangia ushindi wa tuzo ya mwandishi bora, ilirushwa kupitia kipindi cha Ripoti Maalum cha ITV. Pia katika siku za hivi karibuni, Muro alishiriki kuandaa kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa kupitia luninga ya TBC1, ambapo askari wa usalama barabarani mkoani Iringa walionekana wakipokea rushwa.
Makala hizo zilizoonekana kutowafurahisha askari na maofisa kadhaa wa polisi, wahusika katika kadhia hiyo walifukuzwa kazi, ili kulinda heshima ya jeshi hilo.
Inadhaniwa pia kwamba habari hizo hazikuwafurahisha baadhi ya polisi na hivyo kumjengea maadui katika jeshi hilo.
CHANZO: NIPASHE