Mzee ES
Hizo info zipo. They know who took what. Ndio maana nimeuliza ni kwa nini TI wameondoka Tanzania? Huenda ikawa hawakupata ushirikiano wa serikali. Si unakumbuka ile ripoti ya Brian Cooksey kuhusu IPTL? Ilimlazimu aondoke nchini.
TI wameondoka nchini lini? Dr Cooksey naye mbona aliendelea kubaki licha ya sakata la IPTL akiendelea na utafiti wake TADREG?
Angalia na hii habari kutoka Mwananchi
Wanasiasa waongoza kwa rushwa
Na Mwandishi Wetu
WANASIASA wametajwa kuwa ni kundi la watu wanaoongoza kwa kujihusisha na rushwa duniani, ripoti ya Transparent International mwaka 2006 imeonyesha.
Ripoti hiyo (Global Corruption Barometer 2006), iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita, inaeleza kuwa, vyama vya siasa vinaongoza kwa kupata alama nne katika kipimo ambacho mwenye alama tano ndiye aliyebobea kwa rushwa.
Baada ya vyama vya siasa, Bunge linafuatia likiwa na lama 3.7 na kufuatiwa na wafanyabiashara/sekta binafsi waliopata alama 3.6.
Mtazamo wa wengi unaoonyeshwa katika ripoti hiyo unabainisha kuwa, wanasiasa wamebobea katika rushwa kubwa na pia wawakilishi katika vyombo vya kutunga sheria vya nchi mbalimbali, nao wamesahau majukumu yao na kukumbatia rushwa, hali inayofanya mdudu huyu kuwa hatari kabisa katika sekta za umma.
Ingawa Tanzania haikutajwa moja kwa moja na ripoti hiyo, lakini rushwa kwa wanasiasa, hasa nyakati za chaguzi, hugeuka kigezo muhimu cha kujihakikishia ushindi, eneo ambalo linatazamwa pia katika ripoti hii.
Nchini hapa, serikali iliwahi kupitisha sheria iliyohalalisha takrima katika kipindi cha uchaguzi, ambayo imetenguliwa na Mahakama Kuu baada ya wadau mbalimbali kuilalamikia na kutaka mahakama kuingilia kati baada ya kuichukulia kama rushwa.
Idd Simba, Mbunge wa zamani wa Ilala na mfanyabiashara maarufu, juzi alikaririwa na vyombo vya habari hapa nchini akisema kuwa rushwa inashindikana kutokomea kwa kuwa inawahusisha watu wenye madaraka makubwa serikalini.
Kauli hii ya Simba inaungana na ukweli unaobanishwa na ripoti hii ya Trasparency International, hasa kipengele hiki kinachowahusisha wanasiasa katika rushwa.
Kundi la wafanyabiashara katika ripoti hiyo ya TI linaelezwa kuwa linatumia rushwa kuziba mazingira ya kulipa kodi.
Polisi wamefuatia wakiwa na alama 3.5 na mahakama ikifuatia kwa kukamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 3.5. taasisi hizi zinahusishwa na rushwa katika kazi zake za kusimamia sheria za nchi.
Taasisi za mwisho katika upokeaji rushwa ni taasisi za dini ambazo zimepewa alama 2.8 na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yalipata alama 2.9.
Maeneo ya huduma za jamii kama elimu na afya yamegusiwa na ripoti hiyo, huku ikielezwa kuwa maeneo haya yanaawathiri zaidi raia maskini ambao hupaswa kutoa rushwa ili wapate huduma ambazo ni haki yao kisheria.
Sababu ya raia hawa kutoa rushwa inatokana na kukithiri kwa urasimu katika vitengo vya huduma mbalimbali za jamii, urasimu unaojengwa ili kurahisisha rushwa kutolewa au kutokana na kuwepo kwa huduma duni.
Kufuatia kuongezeka kwa rushwa, hasa barani Afrika na ulimwenguni kote, maisha ya familia mbalimbali katika bara hili yanaonyesha kuathirika zaidi ukilinganisha na familia katika mabara mengine.
Ukitupilia mbali tatizo la rushwa, bado maisha ya Afrika yanakabiliwa na kukosekana kwa huduma muhimu kama maji, afya na elimu, vita visivyokatika na pia ukosefu wa chakula katika nchi mbalimbali.
Ripoti hii inaonyesha pia kuwa, wananchi wengi hawana imani na serikali zao juu ya namna ya kupambana na rushwa na uchunguzi uliofanyika katika nchi za Marekani na Uingereza unaonyesha kuwa, wananchi wanaziona serikali zao kama taasisi zinazochochea rushwa na sio kupambana nayo.
Akizungumza na Mwananchi,
Mkurugenzi wa TI nchini, Willy Kitima, alisema utafiti huo ulifanyika kwa kutumia baadhi ya nchi kikanda, ambapo Afrika iliwasilishwa na Kenya, na baadhi ya watu walikuwa wanaulizwa ni makundi gani wanayodhani yanajihusisha na rushwa zaidi.
Mamlaka ya kupambana na rushwa nchini (Takuru) imekuwa ikilalamika mara kwa mara kushindwa kupambana na rushwa kutokana na kutokuwapo sheria zinazoilinda mamlaka hiyo na kuipatia nguvu.
Hata hivyo jana wakati wa sherehe za siku ya Maadili, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema sheria mpya ya rushwa itakayotoa mwanya zaidi kwa Takuru kufanya kazi zake vizuri zaidi, iko jikoni.
Eneo ambalo linalalamikiwa sana na mamlaka hiyo ni mikataba ya serikali na zabuni mbalimbali. Hili ni eneo linaloambatana na rushwa kubwa zinazoathiri taifa na kauli za serikali ya Tanzania mara nyingi zimekuwa zikikumbatia sheria za sasa ambazo zinataka mikataba mbalimbali inayotiwa saini na serikali kubakia siri kati ya viongozi wa serikali na wawekezaji.
Ripoti hii inaonyesha pia kuwa wengi wa wanaotoa rushwa hulenga katika kupata huduma za msingi ambazo ni haki yao kupata au kwa lengo la kupambana na urasimu wa serikali au ikiwa ni lengo la hofu ya sheria mbalimbali kandamizi dhidi yao.
Uzoefu unaonyesha pia kuwa, rushwa inawatafuna na kuwaumiza zaidi raia maskini hasa inapotokea kuwa baadhi ya kodi zinapunguzwa kwa walio na uwezo wa kuzilipa na kuziweka kwa wasio na uwezo wa kufanya hivyo.
Wakati huo huo, serikali jana ilizindua mkakati mpya wa kupambana na rushwa, mpango unaoipa taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini (Takuru) mbinu mpya za kupambana na kutokomeza tatizo hilo nchini.
Mkakati huo ujulikanao kama Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa (Nascap II), ulizunduliwa na Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein wakati wa maadhimisho ya siku ya maadili, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Mkakati huo ni mahususi kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kuratibu sekta binafasi, wizara na idara za serikali, serikali za mitaa na asasi zisizo za serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mpango huo wa miaka minne, unalenga kuongeza ushiriki wa asasi za kiraia, NGOs na sekta binafsi katika kupambana na rushwa ili kuongeza mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa.
Hata hivyo alisema jana kuwa pamoja na juhudi za serikali katika vita dhidi ya rushwa kuonyesha mafanikio, hasa kwa kupungua kwa kiasi kikibwa rushwa za wazi, bado kuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika taasisi zote zinazojishughulisha na vita hiyo.
Alisema pia kuna udhaifu katika usimamizi wa utawala bora kutokana na sheria zilizopitwa na wakati na ushirikishwaji mdogo wa vyama vya hiari na mamlaka za serikali za mitaa.
Alisema sheria mpya ya rushwa inaandaliwa, ili kuhakikisha kuwa Takuru inapewa uwezo mkubwa ikiwemo kushughulikia vitendo vya rushwa nje ya mipaka ya Tanzania na kushirikiana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizosaini Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Rushwa mwaka 2003, Tanzania ikiwa mojawapo.
Marekebisho hayo yanayotarajiwa kupelekwa bungeni Aprili mwakani, yanaingiza kifungu kinachowalinda watoa taarifa za rushwa pamoja na mashahidi wa kujitolea, wanaojitokeza katika vita hiyo.