Rushwa ya wawekezaji wageni yapofusha viongozi serikalini
Ndyesumbilai Florian na Ramadhan Semtawa
BAADHI ya viongozi katika serikali ya Tanzania ni miongoni mwa watu wanaoelezwa kupofushwa na rushwa inayotolewa na makampuni makubwa ya uwekezaji kutoka nchi 30 maarufu duniani ili kupindisha sheria na kanuni, ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Transparency International (TI) imefichua.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa TI, walengwa wakuu katika mtego huu wanaelezwa kuwa ni viongozi wa serikali, mashirika yake ambao hongo imewalevya, hivyo kuwalainisha kupitisha miradi, zabuni, uwekezaji au biashara.
Katika orodha hiyo, (nakala tunayo), hata hivyo, makampuni kutoka Ufaransa, Italia na India, ndiyo yanadaiwa kuongoza kwa uchafu huo wa kuchochea rushwa.
Orodha ya nchi hizo 30, inaongozwa na Uswisi iliyopewa alama 7.81 (kati ya 10 za juu), ingawa India ni ya mwisho ikiwa na alama 4.62. Mataifa tajiri, Uingereza iko katika nafasi ya sita ikiwa na alama 7.36, Marekani, nafasi ya 10 (pointi 7.22) ikifuatiwa na Japan (7.10).
Barani Afrika, imo Afrika Kusini yenye alama 5.61, ikiwa katika nafasi ya 24 huku ikiwa ya kwanza kwa bara la Afrika. Nchi hiyo, pia ni mwekezaji mkubwa miradi mbalimbali iliyoko Tanzania.
Nchi kama vile, India na China ambazo zimetokea kuwa washirika wakuu wa kibiashara na uchumi wa nchi za Afrika, ripoti ya shirika hilo la kimataifa la kupambana na rushwa inafichua na kueleza kwamba mikataba mingi ya kibiashara baina ya makampuni ya nchi hizo na nyinginezo imeoza kwa rushwa.
Wakati hali ikiwa ni hivyo, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), zinaonyesha kwamba baadhi ya nchi zilizotajwa ndani ya ripoti ya TI kwa kuchochea ufisadi zimo katika nchi kumi bora zinaoongoza kwa kuwekeza vitegauchumi vyao katika sekta mbalimbali nchini.
Nchi hizo ambazo zinaongozwa na Uingereza nyingine ni pamoja na India, China, Italia, Ujerumani, Marekani, Uholanzi, Canada, Afrika Kusini na Kenya.
Kati ya nchi hizo, Uingereza imewekeza nchini katika miradi 527 ambayo ni pamoja na sekta ya kilimo, India miradi 120 na China 123.TI, kwa upande mwingine inaeleza wasiwasi wake kuhusu rushwa hii ya kiwango cha kimataifa, inayozihusu sekta mbalimbali zikiwamo za uwekezaji, biashara inavyozidi kuongezeka na hata kutishia uhai wa nchi hizo kiuchumi.
Orodha hiyo ya nchi 30 zinazoongoza, hasa kwa makampuni yake kuhonga ili kupata zabuni au kazi nyinginezo, TI inasema inaonyesha kukiukwa kwa sheria na taratibu za kimataifa.
Taarifa hiyo inayoitwa Transparency International 2006 Bribe Payers Index (BPI), inaelezwa kuwa ni ya utafiti na uchunguzi wa aina yake ambayo haijawahi kufanyika.Ripoti hiyo ya Oktoba 4, inaeleza kuwa imeyachunguza makampuni zaidi ya 400 kutoka nchi 30 zikiwamo zenye viwanda au zile zinazoongoza kwa usafirishaji na uuzaji nje bidhaa.
Kwa bahati mbaya, nchi tajiri kama vile, Uingereza, Marekani, nazo zimeorodheshwa kwamba makampuni yake ni miongoni mwa yale yenye rekodi mbaya."Imekuwa kawaida kwa makampuni kutoka nchi hizi tajiri kutoa hongo, hasa kwa nchi zinazoendelea ili kupata kazi," inaeleza TI ambayo imetoa alama 10 zikiwa ni za juu kwa makampuni ya nchi hizo 30. Licha ya mataifa tajiri, lakini TI inaeleza pia wasiwasi wake kuhusu kujiingiza kwa makampuni kutoka mataifa yanayokuja juu kibiashara kwa ngazi ya kimataifa, yaani India, China na Russia.
Lakini kwa upande wa China na nchi hizo zinazoitwa 'wafalme wajao' kibiashara, shirika hilo linaeleza kuwa hata juhudi za kupambana na rushwa na ufisadi zimeshindikana kiasi cha kuwa mzigo wakati vitendo hivyo vinapohamishiwa nje ya mipaka ya nchi hizo.
Makampuni hayo yanahonga na hivyo kukwamisha juhudi za serikali za nchi maskini katika kupambana na maovu kama rushwa, kujenga misingi ya utawala bora, matokeo yake nchi hizo zinazama zaidi katika lindi la umaskini, anaeleza Mwenyekiti wa TI, Huguette Labelle.Walengwa wakuu wa mtego, TI inaeleza kuwa ni pamoja na maofisa wa serikali, makampuni na wengineo ambao kwa namna oja au nyingine wanahusika katika kufanikisha miradi.
Katika uchunguzi wake ambao ulihusisha wafanyabiashara zaidi ya 11,000 kutoka nchi 125 kuhusu mtazamo huu wa hongo na rushwa katika kupata zabuni, wengi walionyesha wasiwasi wao kuhusu jinsi makampuni kutoka India yanavyohusika katika mtego huu.Katika hatua ya kushangaza, TI inaeleza kuwa wafanyabiashara wengi kutoka Afrika waliohojiwa wakati wameyataja akampuni kutoka Ufaransa, Italia kama ambayo yamebobea kwa kuchochea vitendo hivyo.
Ni unafiki mkubwa kuona makampuni kutoka nchi zilizoendelea yakiendelea kutembeza hongo karibu katika nchi zote ulimwenguni, huku serikali za nchi zao zikiyafumbia macho au kuendelea kutoa mashinikizo kwa nchi maskini zijenge utawala bora," anaeleza mwenyekiti huyo. Ripoti hiyo, pia inazituhumu nchi zote ambazo makampuni yake yanatuhumiwa katika kushiriki maovu hayo kwa kushindwa uchukua hatua thabiti na za kutosha kuzuia rushwa hiyo ya kimataifa, anaeleza Mtendaji Mkuu wa TI, David Nussbaum.
Anaongeza: Kwa hakika rekodi ya mataifa hayo kuhusu vita dhidi ya rushwa na ufisadi katika sekta ya biashara kimataifa inasikitisha kuisoma.Sote tunajua kwamba sheria na kanuni zipo, lakini ama hazitumiki au haziheshimiki kabisa, anaeleza.Sheria za kitaifa zimetungwa ili kupambana na rushwa na ufisadi kwa nchi moja moja, kutokana na kubuniwa na Umoja wa Mataifa (UN)na zimeridhiwa, lakini ugumu ni kwenye utekelezaji wake, anaongeza.Nchi nyingine ambazo zinatajwa kubobea bali ya China na Russia ni Uturuki na Taiwan.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TI kwa Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati, Casey Kelso, anaeleza kuwa rushwa imekuwa ikitumiwa kama kishawishi cha kupata zabuni na nafasi za kibiashara.Kelso anayatetea makampuni hayo kuwa hayatoi tu rushwa au hongo au kuichochea rushwa, isipokuwa kwa kushindwakuvifichua au kuvikemea vitendo vya rushwa katika nchi zao vinapofanyika. TI Bripe Payers Index 2006: the rankings
Katika hatua nyingine, wakati TI ikieleza msimamo huo, mchumi kutoka Benki ya Dunia analionya bara la Afrika ikiwamoTanzania kuhusu ongezeko la makampuni ya India na China yanayowezeka katika ardhi yao.
Mchumi huyo, Harry Broadman, katika kitabu chake: Africa's Silk Road: China and India's New Economic Frontier, anaeleza kuwa licha ya ongezeko la makampuni ya nchi hizo kuwekeza katika sekta mbalimbali katika Afrika, lakini kukosekana kwa uwiano ulio sawa kibiashara, Afrika inaumia zaidi.
Kitabu hicho alichokitoa mwezi uliopita, mchumi huyo anazieleza China na India kuwa zinaelekea kuzipokonya nafasi ya kibiashara Ulaya na Marekani katika kuwekeza na kufanya biashara Afrika.Hata hivyo, anaonya mchumi huyo kuwa nchi hizo zinakabiliwa na changamoto zaidi kutokana na kufanya biashara namataifa hayo ambazo baadhi yake kodi ziko juu, hasa kwa bidhaa zinazoingizwa katika masoko yake.
Broadman anaeleza kuwa ingawa kumekuwako na ongezeko la bidhaa kutoka Afrika kwenda Asia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hali iliyofanya bara la Asia kuwa mshirika mkubwa wa tatu kibiashara na Afrika hadi kufikia asilimia 27 na kuziacha Ulaya yenye asilimia 32 na Marekani asilimia 29, bado hali si shwari.Anaeleza kuwa kwa kipindi hicho, rasilmali kutoka India na China zilizowekezwa Afrika ziliongezeka kwa China uwekezazenye thamani ya dola 1.18 bilioni hadi Juni mwaka huu.
Uchunguzi katika makampuni 450 ya Kichina na India katika nchi za Afrika Kusini, Tanzania, Ghana na Senegal, mchumi huyo anaeleza kuwa yamewekeza katika sekta mbalimbali, ikiwamo za mafuta, maliasili, ujenzi, viwanda na kadhalika.
spacer.gif ¨"Lakini, ukifanya uchunguzi kwa sasa, inachouza Afrika huko India na China ni malighafi au maliasili tu," anaelezaBroadman.
Katika kitabu hicho ambacho mchumi huyo alikizindua wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia uliofanyika Singapore, ambao ulizungumzia pia jinsi ya kuwasaidia watu 300 milioni wanaokabiliwa na umaskini katika Afrika, anaeleza pia bara hilo linahitaji miujiza ili kujinasua katika umaskini kama ilivyofanyika kwa watu milioni 400 barani Asia miaka 25 iliyopita.Wasiwasi wake ni kuhusu uwekezaji kama njia ya kuleta matumaini kwa Afrika hasa kwa kuendelea kuwapo kwa vikwazokama vile uhusiano usio sawa wa kibiashara baina ya maeneo hayo mawili.
Kwa mfano, anaeleza mchumi huyo kwamba China na India zinazotoza viwango vikubwa vya kodi kwa bidhaa kutoka Afrika, jambo linalozizuia nchi hizo kupenya katika soko hilo.Kwa mujibu wa mchumi huyo, biashara ya nje ya Afrika kuelekea Asia ni asilimia 1.6 ya biashara ya bara hilo (Asia) ulimwenguni.
Hata hivyo, mchumi huyo anaeleza kuwa dhana ya ushirikiano wa kusini-kusini, kupitia uwekezaji katika Afrika, huenda ikabadili hali hiyo.
Mchumi huyo anaona kuwa kuendelea kuzalishwa kwa bidhaa katika nchi hizo za India na China ambazo zina soko kubwa Afrika, kutokana na kuwa za bei ya chini, machoni mwa wachumi wa Afrika zinaonekana kuwa zinadumaza soko la ndani.
Anaeleza wasiwasi ambao unakubaliwa na wafanyabiashara wazawa, kwamba bidhaa hizo zinashindana na zile zinazozalishwa katika nchi hizo, ikiwamo Afrika Kusini.