Rushwa yamliza Idd Simba
na Dauson Harold
Tanzania daima
MWENYEKITI wa Jukwaa la Uchumi, Idd Simba, amesema taifa letu hivi sasa limegubikwa na rushwa kiasi kwamba vyombo vingi vya utawala vinaendeshwa kwa rushwa.
Alisema imefikia hatua kwamba hata huduma za msingi hutolewa kwa rushwa na akasema mahakama na hospitali zinaendeshwa kwa rushwa, na elimu hutolewa kwa ubaguzi kwa sababu ya rushwa.
Iddi Simba, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema hivi sasa hakuna Mtanzania asiyefahamu rushwa ni nini na kwamba kila mtu anajaribu kufatuta mwanya katika utaratibu wowote, ili atoe rushwa, ama kudai au kupokea.
Mfanyabiashara na mwanasiasa huyo aliyepata pia kuwa mbunge wa Ilala, alisema hayo jana katika mkutano uliokuwa ukizungumzia masuala ya rushwa, utawala bora na umilikaji wa njia kuu za uchumi wa nchi yetu.
Alisema sasa imefikia wapiga kura ndio wanaodai rushwa, na akasema hivi karibuni tutasikia watoto wa shule nao wanadai rushwa kwa wazazi, ili wakubali kwenda shule.
Kwa muda wa miezi kadhaa sasa, matukio ndani ya nchi yetu yametudhihirishia mengi ambayo wengi wetu tumekuwa tukiyasikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Hali ya uchumi ni mbaya sana.
Tukiendelea na shughuli kama kawaida, tutafika mahali ambapo hatutaweza kurekebisha chochote, na taifa litaangamia. Tutakuwa tumewakosea watoto wetu na wajukuu wetu. Tutakuwa tumelikosea taifa.
Hali ya uchumi ni mbaya kiasi kwamba idadi ya kutosha ya wananchi wamekwisha kusahau thamani ya maisha. Kuna Watanzania waliobanwa na ugumu wa uchumi mbovu kiasi cha kuuza uhuru wao wa kuchagua viongozi, alisema Simba.
Alisema kuwa mwananchi aliyefikia hapo ni dhahiri hana tena matumaini ya kupata maendeleo kwa kutumia uhuru na haki yake ya kikatiba, na kwamba kuna vijana wengi walio radhi kuuza miili yao bila kujali kuambukizwa virusi vya ukimwi ilimradi apate kuishi maisha ya starehe, mafupi kuliko maisha aliyonayo sasa.
Aidha, alisema wananchi wamekwishaamua kwamba ziko dhambi ambazo si dhambi tena, bali ndiyo njia ya maisha. Viongozi wa dini wanaita dhambi za aina hii kuwa ni dhambi za mfumo.
Aliendelea kueleza kuwa Watanzania wamekubali kubweteka na kuingizwa au kujiingiza katika mfumo unaowalazimisha kutenda dhambi na kusema kwamba anafahamu kwamba viongozi wa dini sasa kazi zao zimekuwa ngumu.
Alisema wako katika mchakato mpya wa kujaribu kubadili nchi kwa kujipa matumaini mapya na malengo ambayo japo ni makubwa, lakini yanatekelezeka.
Tunataka watu wetu wapate mwamko mpya wa kujikomboa katika utumwa uliokwishapata nguvu. Utumwa wa kuthamini mali kuliko watu. Utumwa wa kutumia binadamu wengine kupata na kupora rasilimali za taifa, badala ya kutumia rasilimali hizo kuongeza thamani ya maisha ya wananchi, alisema.
Alisema maisha ya amani, furaha na utulivu yamekwishapotea na kwamba tunastahili kuendesha maisha yatayotuwezesha kuutambua utukufu wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, maisha yenye urahisi wa kupata mahitaji muhimu.
Simba, alisema utumwa huu ni ule ambao umekuwa ukitukabili kwa karne kadhaa ukiitwa ubeberu, isipokuwa sura yake imebadilika kutokana na maendeleo ya kiteknolojia.
Teknolojia inayoendeshwa na wale wale waliotutawala kabla ya uhuru. Lazima tujiangalie wenyewe tujitambue sisi binadamu ni kitu gain? Na Tanzania ni kitu gain?
Je, ubinadamu wetu ni kitu gani na uzalendo ni kitu gain? Wengi wetu hawaoni viongozi wenye nyadhifa mbalimbali, lazima tujiulize tena ni nini maana ya kuwaongoza binadamu wengine. Je, utawala bora ni nini? alihoji Simba.
Alieleza kwamba baada ya uzoefu walioupata kwenye uongozi, wameelewa makosa yao ya kushindwa kujenga taifa lenye furaha na ustawi, badala yake wamejenga taifa ambalo bado limegubikwa na umaskini, maradhi na ujinga.
Machungu ya makosa haya ni makali sana kwa wananchi wote, lakini kwa ujasiri wetu wa kibinadamu tunaweza kutumia machungu hayo kuwa mafundisho yetu ya leo na kesho.
Hivi leo tunatambua pia jinsi gani sera zetu zinavyoendelea kujenga tabaka kubwa mno la mamilioni ya wasionacho, na tabaka dogo sana la walionacho. Hii ina maana kwamba malengo ya milenia tunayodhamiria kuyafikia mwaka 2025 yatakuwa ni ndoto tu.
Tukiangalia nchi yetu miaka 52 baada ya Vita ya Pili ya Dunia, tunaona kwamba uongozi wetu wenyewe umetushinda kulipa taifa matumaini mapya.
Wala hakuna ushahidi kwamba tukiendelea na sera za sasa za ubinafsishaji na wawekezaji kutoka nje, tutaweza kubadili hali hii ya kukatisha tamaa.
Rasilimali asili kama vile madini, bidhaa za misitu, mazao ya kilimo, haviwezi kugeuzwa kuwa utajiri na mtaji wa kutukomboa wazawa wa nchi hii, basi kuingia kwetu kwenye mfumo wa ubepari umekuwa kazi bure, alisema.
Kadhalika, alieleza kuwa yeyote anayefikiri au kuamini kwamba taifa letu linaweza kuendelezwa na kukombolewa na wawekezaji kutoka nje, anajidanganya na akasema ni lazima tuwe na mikakati madhubuti ya kuwamilikisha wazalendo uchumi wa nchi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba, aliyetoa mada ya utawala bora, alisema kuwa utawala bora ni ule unaoongozwa na sheria, kanuni na kufuata matakwa ya watu waliowachagua.