Tanga, mafunzo ya huduma baada ya mimba kuharibika (CPAC) yamepunguza gharama za usafiri kwa wagonjwa

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Mafunzo ya huduma baada ya mimba kuharibika Comprehensive Post Abortion Care (CPAC) yanayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi zisizo za Kiserikali, Marie Stopes Tanzania yametajwa kupunguza gharama za usafiri kwa wateja katika kuitafuta huduma hiyo.

Mbali na kupunguza gharama pia mafunzo hayo yamechangia kuongeza ufanisi kwa baadhi ya watoa huduma katika Zahanati mbalimbali nchini na kwamba sasa huduma hiyo inapatikana ndani ya vituo vya afya kwa kila kata.
1.JPG
Akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari waliotembelea katika Zahanati ya Manga (Handeni) hivi karibuni, Mganga Mfawidhi wa Zahabati hiyo, Dk. Richard Juma amesema “Nilipopata mafunzo wateja (Wanawake wenye changamoto za kuharibikiwa na ujauzito) nimekuwa nikiwapatia huduma hiyo hapahapa Zahanati ya Manga, kupatikana kwa huduma hiyo kumepunguza gharama ya kumsafirisha mgonjwa kufikia vituo vya afya.

Ameongeza kuwa baada ya kupata mafunzo hayo alimshirikisha mhudumu wa Zahanati husika ngazi ya jamii: “Nilizungumza naye, akatumia elimu kwa ngazi ya jamii.”

Akizungumza kuhusu muitikio wa jamii baada ya huduma hiyo kuanza kutolewa Manga, Juma ameweka wazi: “Katika kila ripoti ya mwezi haijawahi kumalizika nikiwa sina mgonjwa.”

Akitolea mfano wa kisa cha mzazi aliyeharibikiwa na ujauzito, Juma anasema; “Alikuja mgonjwa aliyekuwa amezidiwa zaidi nilimpatia huduma ya kwanza na baadaye nikampeleka kituo cha afya kwa matibabu zaidi.

“Kitu ambacho nilitamani kiboreshwe ni vifaa ambavyo vingeweza kutusaidia katika kutoa huduma hizi haraka pamoja na watoa huduma kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara.
2.JPG
Akizungumzia changamoto alizokabiliana nazo kabla ya kupatiwa muongozo wa Serikali huduma ya utoaji mimba baada ya mimba kuharibika, alisema: “Kabla sijapata muongozo kweli kulikuwa na changamoto, wakati mwingine huduma inatolewa kwa lengo la kumsaidia mama au binti aliyekabiliwa na changamoto hiyo.

“Tunatamani nasi tutoe huduma kama zinazotolewa katika hospitali zetu kubwa ikiwemo Muhimbili na kwingineko.”

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Zahanati Manga hivi karibuni, Mhudumu Afya Ngazi ya Jamii Kijiji cha Manga, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Saum Masimba anasema pamoja na jukumu alilo nalo la kuihamasisha jamii kuhusu afya na usafi wa mazingira lakini pia analo jukumu la kutoa elimu kwa jamii ili iweze kushiriki mafunzo mbalimbali yanayoyohusu afya:

“Mimi kama mhudumu siwezi kufahamu mambo yote ila kinachonisaidia ni kuwa na muongozo wa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Muuguzi wa Shirika la Marie Stopes, Amina Mbwana amesema ushiriki wa Wanaume katika kushiriki mafunzo ya Afya ya Uzazi yanayotolewa katika vituo mbalimbali vya afya Handeni bado ni changamoto.
3.JPG
“Mwanzoni tangu nitoke Mtwara na kuwa mtoa huduma ya mikoba (Kilindi Outreach), tulipokuja mwanzoni kulikuwa na shida kidogo ya uelewa lakini kwa jinsi tunavyoendelea kutoa mafunzo muitikio ni mzuri kwa upande wa wanawake na mabinti.

“Ushiriki kwa wanaume ni changamoto, baadhi wanaamini kwamba ukitumia njia hii ya uzazi wa mpango ni uhuni, hivyo ushiriki kwa upande wa wanaume ni changamoto.”

Akizungumzia kundi la vijana katika kupatiwa mafunzo yanayohusu uzazi wa mpango anasema: “Vijana hususani katika uzazi wa mpango wapo vizuri, lakini tunashukuru ushiriki wa Serikali ni mkubwa kwa watumishi wake. Popote pale tunapokwama katika shughuli zetu za utoaji lazima Serikali itaingilia kati na kutusaidia, uhusiano wetu na serikali ni mzuri kwa kiwango kikubwa.”

Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake, Kituo cha Afya cha Mkata, Handeni, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Neema Komba ameshukuru wadau wa mashirika ikiwemo Marie Stopes inavyoshirikiana vyema na serikali katika kutoa mafunzo yanayohusu afya ya uzazi.

Neema takwimu za Mwaka 2022 ni 41% ya Wanawake wanaotumia njia ya uzazi wa mpango ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita, pamoja na kuwepo kwa changamoto kwa upande wa Wanaume lakini ukimuelimisha mtumiaji (mwanamke) anaelewa.

Jambo la muhimu ni uhamasishaji katika matumizi ya njia fupi za kupanga kwenda kwenye njia ndefu: “Kipindi hiki tunaona kwamba njia ya muda mrefu inampunguzia safari mteja ya kuja kumuona mtoa huduma mara kwa mara.”

Kwa upande wa huduma ya baada ya mimba kuharibika, Neema anasema “Mwanamke anapofikwa na changamoto ya aina hiyo huduma hiyo inafanyika kwenye vituo vya afya katika Wilaya ya Handeni tuna vituo tisa vinavyotoa huduma ya baada ya mimba kuharibika (post - abortion care).

Neema anaeleza kuwa: “Pamoja na jitihada zetu sisi Serikali lakini pia tunawashukuru kwa kuendelea kutuunga mkono katika kwa kampeni hizi za upatikanaji wa huduma bora ya afya ya uzazi na mtoto, mbali na Marie Stopes kuunga mkono jitihada hizi lakini pia wadau wengine wa serikali.


Chanzo: Mary Victor
 
Back
Top Bottom