SoC01 Stashahada kiwe kigezo au sifa ya lazima kwa Walimu wa Shule za Sekondari

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Jun 3, 2021
544
558
Taifa kuwa na elimu bora ni pamoja na kuwa na walimu mahiri wenye misingi ya ualimu na maadili ya kazi hiyo. Mbali na kazi ya kufundisha lakini pia mwalimu ni mlezi. Hivyo tunatarajia watoto wetu wakipelekwa shule wapate elimu bora pamoja na kulelewa kimaadili kwa ajili ya kuandaa taifa la kesho lililo imara.

Katika pita pita zangu nikiwa katika mihangaiko ya kutafuta tonge, nilibahatika kukaimu ofisi ya mkurugenzi wa shule moja hapa mjini kwa muda wa miezi kadhaa. Muda huu nikiwa nimekaimu nafasi hiyo ndipo nilipogundua kuwa kuna haja ya walimu wa sekondari wapitie kwanza chuo cha mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya stashahada kabla hawajajiunga na vyuo vikuu kwa ajili ya shahada ya ualimu.

Nilibaini kuwa walimu wenye stashahada ya ualimu wana maadili na nidhamu ya kazi na ni wachapakazi zaidi kuliko walimu wenye shahada. Hata katika upande wa nidhamu, walimu wenye stashahada wanaongoza katika hilo ukilinganisha na wale ambao walipohitimu kidato cha sita wakaenda moja kwa moja kujiunga vyuoni kwa ajili ya shahada.

Sikuridhika na majibu niliyoyapata, nikajaribu kulioji hilo kwa baadhi ya wadau wa elimu na wao wakalithibitisha hilo kwa asilimia kubwa sana.

Walimu wengi wenye shahada ambao hawajapitia vyuo vya stashahada huwa ni shida katika kutekeleza majukumu yao ya kazi. Wengi wao wamejawa na kiburi kisicho na kichwa wala miguu kisa ni hiyo shahada waliyonayo. Kubwa zaidi baadhi yao hata uwezo wa kufundisha hawana.

Jambo hili likanipelekea kufikiria kama ningekua na mamlaka basi ningeweka kuwa ni jambo la lazima kwa walimu pindi wanapohitimu kidato cha sita lazima wapiti vyuo vya stashahada kabla hawajajiunga katika vyuo vikuu kwa ajili ya shahada. Kwani inaonesha huko kwenye vyuo vya stashahada walimu wanapikwa na kunolewa vizuri sana.

Na katika kuliendea hilo ningeweka utaratibu kusomea uwalimu wanafunzi wanapangwa moja kwa moja na wizara au idara husika kama ilivyo katika kupangiwa shule kwa kidato cha tano. Hivyo walimu wa madaraja yote wangepatikana, wale waliopata daraja la kwanza, la pili na hata la tatu wangepelekwa kwenye vyuo vya stashahada.

Kisha baada ya kuhitimu stashahada hapo sasa mtu ndio awe huru kuendelea na kingine anachotaka kukisomea katika elimu ya juu. Hili lingesaidia kupata walimu mahiri na wenye uzalendo wa kufanya kazi kwa kujituma.

Kwa kuwa sina mamlaka, lakini nina haki ya kushauri; nashauri stashahada iwe ni sifa ya lazima kwa walimu wa sekondari.



DustBin
 
Back
Top Bottom