TULIPOISHIA.
Mda huo nilikuwa nimeng’ata meno kwa nguvu, nikiugulia maumivu makali niliyoyapata baada ya kuchanwa ubavuni na chuma kizito kilichonidondokea. “Mhmm! Mhhmm! Mmhhm!” niliugulia maumivu makali yaliyosambaa mwili mzima. Nilianza kujihisi nguvu zikiniishia, nikashindwa hata kukwepa chuma kizito kilichonibamiza kichwani. Taratibu mwanga ulitoweka. Giza likatawala. Hata ile sauti ya maumivu iliyonitoka ikakoma...............
ENDELEA
(Saba nane au kenda, Nakosa lipi kutenda,)
SEHEMU YA PILI.
Baadhi ya watu huamini usingizi ni nusu ya kifo. Ndiyo maana husisitizwa zaidi kumuomba Mungu kabla ya kulala. Wanadai kuna uwezekano mkubwa ukalala mazima na usiamke tena. Mimi sikubaliani nao, wala sikiamini kabisa kitu hicho. Kama wangesema usingizi ni mazoezi ya kifo huenda ningekubaliana nao maana nusu humaanisha kisichotimilika au kutokukamilika. Usingizi si nusu ya kifo, ila nusu yenyewe ipo, nayo ni kupoteza fahamu kwa kuzimia au kuzilahi. Mtu aliyezimia yupo katika nafasi nzuri sana ya kukikabili kifo zaidi ya mtu aliyelala tu, japo kuzimia huja kama matokeo ya sababu mbalimbali. naongelea kuzimia kunakosababishwa na ajali. Yaani kupoteza fahamu kwa sababu ya majeraha yalisababisha kupotea kwa damu nyingi mwilini. Majeruhi anapopatwa na hali hii huingia katika hali mbaya inayoweza pelekea mauti yake, kama hatopata msaada wa haraka; aghalabu kuzuiliwa kwa upoteaji zaidi wa damu, pia kuongezewa damu safi na salama kufidia ile iliyopotea. Ili kukabiliana na upungufu wa damu mwilini, mgonjwa hushauriwa kupata kwa wingi vyakula vya protini vinavyosaidia kuzalisha damu mwillini.
Niliyasoma kwa umakini maandishi haya yaliyoandikwa katika kipeperushi nilichopatiwa na nesi aliyenihudumia kwa wakati wote. Sasa nilikuwa ndani ya chumba cha daktari, chini ya uangalizi mzito wa wauguzi na madaktari wabobevu. Nasema wabobevu siyo kuwapamba bure; wanastahiri kuitwa hivyo kutokana na kazi kubwa waliyoifanya kuokoa uhai wangu. Hii ilikuwa siku ya tatu tangia nilejewe na fahamu zangu, japo niliambiwa ilikuwa siku ya saba tangu nifikishwe hospitalini. Kuna wakati nilihisi maumivu makali katika mbavu zangu za kushoto, lakini sikuwa na cha kufanya kujitetea na kadhia hiyo. Nilikuwa nifungwa bandeji gumu lililoninyima uhuru wa kujigeuza vile nitakavyo, nimelazwa juu ya kitanda safi kilichoishikilia vizuri sehemu kubwa ya mwili wangu.
Asubuhi hii nilikuwa nimejipumzisha kitandani peke yangu. Sikuruhusiwa kuonana wala kuongea na mtu yeyote kwa wakati huu zaidi ya nesi muuguzi aliyekuwa nami kwa wakati wote. Nimeshamzoea sasa, nikambatiza jina la Nesi wangu maana muda wote alihangaika na mimi tu kama vile hakukuwa na wagonjwa wengine wanaoihitaji huduma yake. Kila watakapozuiliwa ndugu na marafiki zangu kufika pale nilipo, angekuja nesi huyu kuniomba nijiandae kwa ajili ya matibabu. Mala zote hunihudumia kwa kunipatia madawa makali sana ambayo huyachanganya kwenye mifumo ya matibabu iliyounganishwa mwilini mwangu. Angebaki nami kwa wakati wote, akinichangamsha kwa maongezi mepesi na stori za hapa na pale mpaka nitakapochukuliwa na usingizi. Nikija kuamka, najikuta ndani ya chumba kingine. Mbele yangu ningewaona baadhi ya ndugu na marafiki zangu nilio wafahamu vizuri, ndipo ningejua umeshafika mda wa kutazama wagonjwa. Baada ya kumaliza kile alichokuwa akikifanya, alisogea mpaka pale kitandani nilipolala; akakaa pembeni yangu. Sikufurahishwa na kitu hicho maana nilijua nini lengo la ujio wake, alitaka kunipigisha stori mpaka nitakapochukuliwa na usingizi mzito uliosababishwa na dawa nilizopewa. Stori zake hazikuwa shida kubwa kwangu, kibaya ilikuwa vile nitakavyopitiwa na usingizi mbele ya nesi yule mrembo niliyemuona kuwa saizi yangu kabisa. Huwa sifurahishwi na kitu hicho, yaani mimi nilale mbele ya mwanamke! Ili iweje. Siku hii niliamua kumueleza ukweli, nikamuomba aniache mwenyewe nipumzike.
Ni kama malalamiko yangu yalimfurahisha sana, aliangua kicheko cha chinichini huku akinitazama usoni kama anayeucheka uso wangu uliokunja ndita za hasira. Kicheko kilikolea, macho yake yalianza kutoa machozi, akaanza kuyapangusa kwa kutumia sehemu ya nyuma ya kiwiko cha mkono wake. Kitendo hicho kilinifurahisha, nikacheka kabla ya kuacha kufanya hivo baada ya kuhisi maumivu makali ubavuni mwangu. “Sikiliza nikwambie kitu mgonjwa wangu mzuri.” Kauli yake ilifuatiwa na maelezo marefu aliyoyatoa kuhusu saikolojia za magonjwa na wagonjwa kama mimi. Alinieleza ni kwa namna gani anaielewa vema saikolojia yangu, anajua nini kinanifurahisha na nini hakinifurahishi. Japo sikufurahishwa na maneno yake mengi ila naliipenda namna ya uongeaji wake, aliongea kwa namna iliyonivutia sana. Ubaya ni kwamba, akishaanza kuongea huwa hanipi tena nafasi ya kuzungumza. Mala zote huwa napitiwa na usingizi angali akiongea. “Kwa sasa unajihisi upweke mkubwa sana mgonjwa wangu, hata hivyo usijali, mimi nipo kwa ajili yako. Na wala usiniambie kwamba huutaki uwepo wangu kwani mimi ndiye nayekujua vizuri kwa sasa. Nakujua nje ndani zaidi ya mtu yeyote, hata mpenzi wako hanifikii. Halafuu! kuna kitu kimenivutia sana toka kwako, nimependezwa na namna unavyosinzia. Huwa unaonekana mzuri sana ukiwa umelala. Hata hivyo usiwaze sana, sitomwambia yeyote kuhusu hili, itakuwa siri yetu mimi na wee,,,,” sikuweza tena kuisikia sauti ya Nesi wangu. Nilipitiwa na usingizi mzito, usingizi tasa usiokuwa na njozi yoyote.
Mwanzoni nilihisi kama sauti kali zilizoyasumbua masikio yangu; baadae nikaelewa kumbe yalikuwa mazungumzo ya chinichini yaliyofanywa na watu walionizunguka. Nilipoyafumbua macho yangu sikuweza kuziona vema sura zao, ni mpaka pale nilipouzoea mwanga mkali uliokuwa ndani ya chumba kile ndipo nilianza kuwatambua mmoja baada ya mwingine. Nilimtambua mama Eliza mke wa mzee Gelo, Eliza mwenyewe na marafiki zangu watatu; Lajoka, Ally na Simoni. Wote walifurahi sana baada ya kuona nimeyafumbua macho, mama Eliza akawa wa kwanza kunijulia hali kisha yakafuatia maongezi marefu yaliyochangiwa na kila mmoja. Hali ile ilinifurahisha sana, nikajikuta nikichangamka kama vile niliyekuwa siumwi chochote. Muda ule mlango ulifunguka, nikamuona Nesi wangu aliyeongozana na watu wengine, ujio wao ulibadilisha hali ya hewa ya mle ndani. Wa kwanza alikuwa mkufunzi wangu niliyemfahamu vema, wengine ni wanafunzi wenzangu; baadhi yao niliwafahamu, wengine sikuwajua kabisa.
Macho yangu yalivutiwa na binti mmoja aliyekuwa miongoni mwa wageni wangu. Huyu si mwingine, ni Salome msichana tuliyejuana vizuri tangu siku ya kwanza kuonana. Sina uhakika kama tulikuwa wapenzi lakini kwa wakati huo tuliangaliana kwa namna ambayo ingekushawishi kuamini hivo. Alinitazama kwa macho yake ya upole; yaliyoonekana kutamani kulia, yakifurahia na kuogopeshwa na hali niliyokuwa nayo. Mwili ulinisisimka baada ya kumshuhudia akikipitisha kitambaa usoni mwake kuyafuta machozi yaliyoyang’arisha macho yake, kisha akaniangalia kwa namna iliyofikisha salamu ya pole aliyoitoa. Ama kweli nilipatwa na hisia za ajabu baada ya ujio wa Salome mpaka hali yangu ikabadilika, moyo wangu ulikiri kumpenda sana binti huyu. Mabadiliko hayo yalishuhudiwa vema na Lajoka ambaye hakujizuia kutabasamu kila aliponiona nikimtazama Salome. Nesi wangu alisogea pale nilipolala, akanikonyeza kwa namna aliyozoea kunifanyia wakati akakikunja kitanda changu kwa namna iliyonifanya sasa nikawa kama vile nimekaa japo haikuwa hivo; kuna vyuma vilinishikilia vizuri eneo la kifua changu.
Mkao ule uliniwezesha kugeuza vizuri eneo kubwa la mwili wangu, nikawaona vizuri watu wote waliofika kunijulia hali. Uwepo wao ulinifariji sana, nilijisikia vizuri kuwaona watu waliokaa kuniangalia kwa matumaini makubwa, bila shaka walitamani kuniona nikisimama tena nikiwa mzima. Uwepo wao ulinifanya nijihisi mwenye thamani kubwa duniani, ninayependwa na watu. Ni kweli kabisa, ninapendwa sana na watu wengi, mfano halisi ni Salome binti aliyezivutia hisia zangu tokea nilipomuona kwa mala ya kwanza. Ni ujinga wangu tu ulioyayumbisha mahusiano yetu, la sivyo tungekuwa mbali sana, huenda ningeshaliopoa tunda lake tamu lililojiotea katikati ya msamba wake. Wakati wao wakiendelea na maongezi ya hapa na pale, mimi nilijitia uvivu wa kushiriki maongezi yale, japo yalinilenga mimi. Niliweka umakini wangu juu ya kile kilichoyavutia macho yangu kwa wakati ule, Salome. Nilimungalia kwa macho ya hamu, nikitamani walau nipate hata dakika moja ya kuzungumza naye, nimueleze namna gani ameuteka moyo na hisia zangu. Kwa wakati huo hisia zangu zilinishangaza sana, yaani binti niliyewahi kumpotezea, nikamuona si lolote mbele yangu eti leo hii nilitamani awe karibu yangu. “Au ndiyo kama vile inavyokuwaga kwenye filamu, wahusika kutoweka wazi hisia zao kwa wale wawapendao mpaka dakika za mwisho za uhai wao.” Mawazo haya yalinifanya kuachana na ujinga wa kumuwaza Salome, nikahofioa kukutwa na matukio ya kwenye filamu. Nilipania kumueleza ukweli mrembo yule mala tu nitakapopata nafasi ya kufanya hivyo. Sikuona uzuri wa kuendelea kuchezea shilingi juu ya tundu la choo, vipi ikidondoka; nitaipataje?
Umakini wangu ukahama toka kwa Salome, nikaanza kutalii nikiyazungusha macho yangu juu ya sura za watu wote waliokuwa mbele yangu. Kila niliyemwangalia nilimtafakhari kwa namna nilivyomjua, nikampa heshima yake kwa kuja kunijulia hali. Macho yangu yalitua juu ya sura nyingine iliyouvuta umakini wangu, nikajikuta nikiitafakhari zaidi ya nilivyofanya kwa wengine. Huyu ni Eliza, binti kitindamimba cha mzee Gelo. Muda huo alikuwa bize akiichezea simu yake, mala kadhaa angeniangalia kwa namna ile aliyozoea kuniangalia. Kilichonivutia zaidi kwa binti huyu ni namna anavyojua kuigiza, yaani licha ya kuwepo kwa mazungumzo ya kufurahisha pale ndani lakini yeye hakujihangaisha nayo kabisa. Angezizungusha mboni za macho yake kwa awamu, mithili ya mshale wa saa kabla ya kuzilejesha tena kwenye mhimili wake ambao ni ile simu aliyoishikilia mkononi. Alikuwa mwepesi kunikwepa kila tulipokutanisha macho, angejidai kuangalia chini au kuigiza kuchezea simu. Haikutokea mala moja, ilikuwa zaidi ya mala mbili kiasi kwamba mimi mwenyewe nikajikuta nikiufurahia mchezo wa binti yule. Kila tukiangaliana, anakwepa. Anaigiza kuchezea simu au kuangalia pembeni kisha taratibu mithili ya kuku asiye na kumbukumbu angeanza kuniangalia tena, nikimtazama ananikwepa tena. Ikafika wakati nikaamua nimtegee mtego ili niiumbue janja yake, alipoigiza kuchezea simu nami nikajifanya kuangalia pembeni, kisha nikageuza macho haraka nikamfuma akiniangalia. Hapo alikubali kuwa kakamatika, akanitunuku zawadi safi ya tabasamu lake mwanana ambalo sikuwahi kuliona hapo kabla. Nililidhishwa sana na zawadi ile, kisha nikairudisha kama ilivyokuja. Amakweli leo nilijikuta nikipendezwa na michezo ya binti huyu tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Hata hivyo bado sikumuelewa sana binti huyu mkimya, asiyependa kamwe kuchangamana na wenzake; muda wote yupo kimya, huwezi kumkuta akiongea na watu. “Hata hivyo ni kazuri,” nilijisemea kimoyomoyo kisha nikaachana naye. Sasa nikaanza kishiriki mala moja moja katika maongezi yaliyokuwa yakiendelea.
Muda ulisogea kwa haraka sana, familia ya mzee Gelo walitaka kuondoka, wakahitaji kupata muda wa kuongea na mimi kabla hawajaondoka. Ikamlazimu nesi kuwaomba wote waliokuwa chumbani watoke, watupishe kwa muda kisha wangerudi baadae. Waliondoka wanafunzi wenzangu, walimu na marafiki zangu. Kilichonishangaza ni baada ya kugundua hata Eliza aliondoka. Chumbani tulibaki watu wawili tu, mimi na mama Eliza; hata Nesi wangu aliondoka baada ya kuhakikisha watu wote wameondoka. Nilipata wasaa mzuri wa kuongea na mama Eliza, akanieleza kila kilichotokea na kile kinachoendelea mpaka kufika dakika ile. Mama huyu ndiye alikuwa nyuma ya matibabu ya kibingwa niliyokuwa nikiyapata, amekuwa akifika hospitalini kila siku tokea siku ya kwanza alipopata taarifa za ajali iliyonipata wakati wa mafunzo. “Simu iliyopigwa nyumbani ilipokelewa na Eliza, kwa wakati huo mimi na baba Eliza hatukuwepo nyumbani. Yeye akawa mtu wa kwanza kufika chuoni kukutazama. Taarifa ya kilichokupata nilipewa na mwanangu wa kwanza, Josefu ambaye bila shaka hujawahi kumuona. Mpaka ninafika hapa nilikuta tayali umeshawekwa chumba cha daktari. Mshukuru sana Mungu kwa kukuweka hai mpaka leo maana hali yako ilikuwa mbaya sana, mpaka matabibu wanafika walikukuta katika hali ya kufa. Mungu kakuponya kwa sababu ya vilio na machozi ya wengi, yaliyomwagika kuulilia uhai wako. Wazazi wako, rafiki zako na wote waliopata taarifa za ajari iliyokukuta walikuombea, wale wote unaowajua na usiowajua. Huenda ni kwa sababu ya Eliza ndiyo maana Mungu aliuweka uhai wako, zikafanikiwa jitihada za matabibu mpaka leo ukawa hai hivyo ulivyo.” Nilitulia kwa umakini kusikiliza maneno mazito ya mama Eliza, aliyeongea mithili ya mchungaji kanisani, akinihubiria.
Aliendelea kunieleza namna mambo yalivyokuwa magumu kipindi chote nilipokuwa nimepotewa na fahamu. Kwamba ilifikia wakati akatamani kunisafirisha kwenda hospitali kuu ya taifa, ikashindikana baada wataalamu wa afya kushauri niendelee kutibiwa eneo lile. Isingekuwa vizuri kumsafirisha mgonjwa mahtuti kama nilivyokuwa, wakashauri niendelee kutibiwa palepale mpaka hali itakapotengamaa kidogo. Ushauri wa madaktari haukuwa mwisho wa jitihada zake, akaamua kuwaleta madaktari bingwa toka hospitali kuu ya taifa kuja kulichunguza kwa undani zaidi tatizo langu. Hawa ndio walionifanyia oparesheni ya kichwa na kifua, wakakiweka sawa kila kilichoharibiwa na ajali iliyonipata, hasa zile mbavu zangu zilizopanguka wakati wa ajali. Hata yule nesi wangu hakuwa muuguzi wa hospitali ya chuo, alitokea hospitali kuu ya taifa. Ujio wake ndani ya hospitali ya chuo ilikuwa kwa ajili yangu, kuniuguza mimi mtoto wa mkulima, mtoto wa dalali. “Nimeamua nikueleze yote hayo kwasababu afya yako imeanza kutengamaa. Sioni kama ni busara tena kuamua kitu chochote kinachokuhusu pasipo kukushirikisha. Sasa hari yako ni nzuri kidogo, tuliwaza tukuhamishie hospitali kuu ya taifa kwa uangalizi wa karibu zaidi, sijui wewe unasemaje hapo.” Melezo hayo yalinishangaza sana, nikaishukuru sana familia ya mzee Gelo kwa upendo wao kwangu na msaada mkubwa walioutoa kugharamikia matibabu yangu mpaka hapo nilipo. Bila wao sijui ningekuwaje mimi, labda ningeshakufa na kuzikwa; nikasahaulika.
Ukweli ni kwamba, kwa namna tukio lilivyotokea, ilikuwa vigumu sana kupona pasipo kupata matibabu ya halaka. Siyo matibabu tu ya kupewa vidonge na vipimo vya choo na mkojo ambayo hata kapuku mimi ningemudu kuyapata, bali matibabu ya kibingwa, toka kwa matabibu mahiri wanaoijua vema sanaa ya utabibu. Nilikumbuka kwa uzuri namna tukio lilivyotokea, namna nilivyobanwa ghafla na vyuma vilivyoniangukia na kuuchana upande wa kushoto wa ubavu wangu. Kilikuwa kitendo cha kufumba na kufumbua nikawa nimelowa damu iliyochuruzika kwa kasi kama vile ilikuwa ikishindana. Jitihada zangu za kijiokoa ndizo zilizidishia maumivu, nikahisi mvunjiko wa kitu kifuani kwangu kisha nikaangukiwa na chuma kizito kichwani, ukawa ndiyo mwanzo wa kutoweka kwa fahamu zangu. Nilimshukuru sana mama Eliza na mzee Gelo ambaye nilijulishwa kwamba hakuwepo nchini kwa zaidi ya wiki mbili sasa. Nilijiona kuwa na bahati ya kukubalika na familia ile yenye upendo wa ajabu. Niliukubali bila pingamizi uamuzi wao wa kunihamishia hospitali kuu ya taifa, nisingeweza kupingana na maoni ya watu walioijua vizuri hali yangu. Mama Eliza aliniaga, akaondoka. Wakabaki wanafunzi wenzangu na marafiki zangu ambao hawakukaa sana, nao wakaondoka kwa maana mda wa kutazama wagonjwa ulikuwa umeisha.
Ni kama vile wimbi la upweke lilipishana na wageni wangu wakati wakiondoka, walivyoufunga tu mlango, nikaanza kujihisi upweke wa ajabu uliombatana na mawazo mengi yaliyoniumiza kichwa changu. Haikupita hata dakika moja, nikauona mlango ukifunguka. Aliingia Nesi wangu akiwa na tabasamu la haja usoni mwake; mikono yake aliiweka nyuma kwa namna ya kukificha kitu alichokishikilia. “Otea nimeshika nini, otea.” Ilikuwa kauli yake ya kwanza mala tu aliponifikia..........
ITAENDELEA.
(Kila kitu kimeshakamilika, Simulizi ipo tayali. Ili kujua nini kiliendelea, tembelea uzi huu jioni ya kila siku kuanzia leo.)