ILIPOISHIA
Wakati nakaribia kuchomoka ndani ya chocho ile nilikumbana na umati mkubwa wa watu waliosogea kwa kasi kunikaribia. Hofu ya kushushiwa kipigo iliuteka moyo wangu, uoga ukaingia mpaka kwenye viungo vya mwili wangu. miguu ikakosa nguvu za kuendelea kukimbia, nikajikuta nikisimama kama limbukeni nisiyeelewa nini cha kufanya....
ENDELEA
(Penye mbili sichagui, mwisho zikaniumbua,)
Sikuwa na namna zaidi ya kucheza mchezo wa pata potea kwa namna ya kutafuta kujiponya na balaa lililonikabili. Nikaanza kuita "mwizi mwizi" huku nikiunyoosha mkono yangu kuelekea ndani ya chocho ile; kama ishara ya kuelekeza wapi alipo mwizi halisi. Watu wa kwanza kufika eneo lile hawakudanganywa na janja yangu, wakaanza kunishambulia pasipo kujali ishara niliyotoa. Nilijitahidi sana kukwepa mapigo yao huku nikizidisha bidii kujitetea na kuonesha wapi aliko mwizi, “yupo kule! yupo kule! siyo mimi”. Bidii yangu ilizaa matunda, waliachana na mimi wakakimbilia ndani zaidi ya chocho ile, wakafuatiwa na msururu mkubwa wa watu waliofika kwa kuchelewa. Sikutaka kubaki tena eneo lile, niliitumia vizuri nafasi niliyoipata, nikatoweka kabisa ndani ya mazingira yale. Niliingia chuo mbiombio nisiamini kama nimeponyoka msala ule, nikiusifu mpango wangu ambao japo haukufaulu sana, lakini uliniponya na kipingo kizito ambacho kingenipata.
Ni baada ya kuingia chumbani ndipo niligundua uwepo damu iliyotapakaa mwilini mwangu. Hali hiyo iliniogofya sana, nikawaza labda niliumia wakati wa kujitetea dhidi ya raia walioanza kunishambulia. Hata hivyo sikuhisi maumivu yoyote mwilini, kuwa mzima mpaka dakika ile kilikuwa kitu mhimu sana kwangu. Nikaamua kuingia bafuni nijisafishe kabla rafiki zangu hawajafika na kunikuta katika muonekano ule ambao ungezalisha maswali mengi nisiyoweza kuyajibu. Nilijikagua zaidi ya mala moja lakini sikuona sehemu yoyote niliyoumia, mwili wangu ulikuwa salama kabisa bila mchubuko wowote ule. “Damu hii imetoka wapi” ndilo swali nililojiuliza. “Binti mlevi” ndilo jibu pekee lililonijia akilini. Lazima ingekuwa damu ya binti yule kwani ndiye mtu pekee niliyekumbana naye njiani. Nilithibitisha hilo kwa kuangalia namna damu ilivyojipakaza kwenye nguo zangu. Ilikuwa upande wa mbele tu, upande uleule alionipamia binti mlevi. Mawazo mengi yalipita kichwani mwangu, nikaanza kuukumbuka vizuri mkasa ulionikuta.
Nilimshukuru sana Mungu kwa kuniponya mikononi mwa raia wenye hasira kali, ambao bila shaka wangenipiga waniue kwa kunichoma moto. Mwili ulinisisimka baada ya kuwakumbuka wazazi wangu, nilimkumbuka mama; nikavuta picha ya namna gani angelia na kugalagala kuuona mwili wa mwanaye uliozungushiwa sanda na kuhifadhiwa ndani ya jeneza. Lakini mimi siyo mwizi, sijawahi kuwa mwizi hata siku moja; wala sina mpango wa kuwa mwizi. “Kwanini sasa akaniita mwizi, alitaka waniue?” swali hili halikunifanya kuwaza namna gani ilikuwa hivyo, bali nilijikuta nikimhurumia binti mlevi. Moyo wangu ulinishawishi kuamini kwamba kulikuwepo na mengi nje ya pazia ambayo sikuyajua kuhusu binti yule. Licha ya kwamba sauti yake ilikuwa inipeleke kuuawa, lakini moyo wangu haukumpokea kama muuaji. Ilinipata shauku, nikatamani kumjua kiundani zaidi. Nikawaza huenda aliuhitaji sana msaada wangu wakati tulipokutana.
Roho yangu ilinishawishi kuamini kwamba hakuyumba kwa sababu ya ulevi bali ni katika namna ya kujiokoa dhidi ya wale waliomuumiza na kumtoa damu. Suala la kumjua binti jasiri lilikuwa rohoni, nikapania kufanya juu chini mpaka nimfahamu. Vipi sasa ningemfahamu wakati sikumjua? wala sikuwahi kumuona sehemu yoyote? Sikuwa na uhakika kama ni mwanachuo au la! Niliona njia pekee ya kumfahamu binti mlevi ilikuwa kupitia tukio lilelile. Kwakua tukio lililotokea karibu na chuo, lazima litajulikana sana miongoni mwa wanachuo. Nikatalajia kusikia likizungumzwa na wanachuo wengi itakapofika kesho. Nilipanga kufanya uchunguzi wangu wa kimyakimya mpaka nimpate binti mlevi.
Hakuna siku nilijiona mwenye bahati kama siku hii. Kile nilichokitalajia kilitokea vilevile, nilichokiwaza kikaonekana na kila nilichokifanya kikanikubali pasipo upinzani wowote. Mpaka kufika majira ya mchana tayali nilikuwa nimeshapata taarifa za kutosha kumhusu binti mlevi na mabalaa yote yaliyomsibu. Tukio la jana usiku lilizungumzwa kwa ukubwa sana, zaidi ya vile nilivyotalajia. Uchunguzi kidogo nilioufanya ulinikutanisha na ukweli mgumu kuukabili, ukweli uliojificha nyuma ya mkasa wa binti mlevi. Tukio kama lile halikuwa la kwanza kutokea, lilikuwa sehemu ya mwendelezo wa matukio mengi ya namna ile. Matukio ya kukabwa, kubakwa na kuporwa yaliyowapata wanafunzi wengi wa kike waliokatisha mtaani majira ya usiku kama ilivyomtokea binti mlevi.
"Jina lake ni Agape, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza; anayesomea fani ya ususi na ushonaji. Usiku wa jana ulikuwa mbaya sana kwake, maana alikutwa na masahibu ambayo yamemfanya leo hii kuwepo ndani ya chumba cha daktari, akiyapambania maisha yake. Ilikuwa majira ya saa mbili na nusu za usiku, wakati akitoka chuo kwenda geto kwake; ndipo alikutana na kundi la vijana wahuni wa mtaani. Walimshambulia na kumkatakata kwa vitu vyenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake, wakamnyang’anya simu, laptop na vitu vingine alivyokuwa navyo ndani ya begi lake la mgongoni. Muda wote huo alikuwa kawekewa vitambaa kinywani vilivyomfanya kushindwa kupiga kelele, labda walipanga kumbaka kimyakimya maana mikono yake waliifunga kwa kamba ngumu. Mbio za miguu yake ndizo zilimponya dhidi ya ukatili wa kijinsia ambao vijana wale walitaka kumfanyia, alikimbia sana mpaka akafanikiwa kuwaacha wahuni wale ambao hawakujihangaisha kumkimbiza tena.
Wakati akikatisha chocho ya Windo alikumbana na kibaka mwingine ambaye naye alimkaba tena kwa lengo la kumuibia. Baada ya kumkagua na kukuta hana kitu chochote; akataka kumfanyia unyama uleule alionusurika kufanyiwa na vijana wahuni. Bado bahati ikawa upande wake, purukushani iliyotokea ilipelekea vile vitambaa alivyowekewa mdomoni kuchomoka, sasa akawa huru kuongea; hapo ndipo alipiga kelele za kuomba msaada. Kelele zile zilizomfanya kibaka kukimbia. Baadhi ya raia waliofika mapema eneo la tukio walifanikiwa kumuona kibaka yule akikimbia lakini hawakufanikiwa kumkamata kwa sababu aliwazidi ujanja. Mpaka sasa tunao mashahidi ambao wamethibitisha kuuona vizuri uso wa kibaka huyu ambaye ni mwizi wa pili. Upelelezi unaendelea, tunaamini tutampata mtu huyo mapema iwezekanavyo. Tutahakikisha amewataja wenzake wote na huo utakuwa ndio mwisho wa matukio ya ukabaji na uporaji ndani na nje ya eneo la chuo. Tunatoa rai kwa wahusika kujisalimisha mapema kwa uongozi wa chuo, ama wakae na kuusubiri mkono mrefu wa serikali uwakamate walipo, wakaadhibiwe kwa sheria kali mahakamani."
IMETOLEWA NA JESHI LA POLISI KANDA MAALIMU.
Niliisoma kwa uzuri taarifa hii iliyochapishwa kwa maandishi makubwa ya rangi nyekundu na kubandikwa kwenye ubao wa matangazo wa chuo. Ile shauku ya kumjua binti mlevi ilibadirika, ikawa hofu kubwa iliyonifanya kuogopa sana. Niliogopa si kwa sababu mimi ni mwizi, bali yale maelezo ya mwisho ndiyo yalinichanganya. Nikajua kama aliyeonekana ni mwizi wa pili, basi ningekuwa mimi. Ni mimi niliyekumbana na binti yule nikamdaka asianguke, ni mimi pia niliyekimbia baada ya binti yule kupiga kelele za kuomba msaada na ni mimi niliyeonwa na watu wa kwanza kufika eneo la tukio. Du! Nilijiona kukamatika sasa, ningewezaje kujitetea mbele ya watu waelewe kwamba sikuwa kibaka ama mwizi kama walivyoniona? Kilichoniogopesha zaidi ni baada ya kufikiwa na taarifa iliyozagaa chuoni, kwamba kuna kijana alionekana jana usiku, akiingia chuoni, kachafuka damu mwilini mwake. Taarifa hii ilisadikika kutolewa na walinzi wa getini ambao walithibitisha kumuona kijana huyo. “Aisee!! nitafanyaje sasa.” Niliwaza bila kupata jibu zuri la kuniepusha na balaa lililonikabili. Nikajiona nineyeenda kuadhibiwa kwa kosa ambalo sikulifanya. Sikuona kama nitaweza kupona kwa awamu hii iwe kama vile nilivyopona mikononi mwa raia wenye hasira. Taarifa hiyo ilinifanya kunyong’onyea sana, nikakosa amani moyoni. Nilimkwepa kila aliyenisogelea nikiamini anakuja kunikamata, kuna namna niliamini kwamba nimeshajulikana; kilichobaki ni wao kuamua kunikamata tu. Wangeshindwaje kumtambua kijana aliyeonekana kuchafuka damu hali ya kuwa getini kulikuwepo na kamera zilizoinasa vema sura ya kila aliyekatisha eneo lile? Lazima wangenipata tu. Hata hivyo sikuliunga mkono wazo la kujisalimisha kwa viongozi wa chuo, sikuwa tayali kuubali uhusika wa moja kwa moja katika tukio nisilolijua.
Kwa mala ya kwanza nilijitenga na marafiki zangu wakati wa chakula cha mchana, sikutaka wabaini mabadiliko ya hali yangu kwani wasingeshindwa kujua hilo. Nilitafuta sehemu tulivu iliyojitenga, nikakaa mwenyewe nikitafakari namna mambo yalivyoniharibikia ndani ya kipindi kifupi. Ile furaha niliyoihisi kuishi chuo ilitoweka mapema sana, nikatamani kutoweka eneo hilo mapema kabla sijaumbuka. “Mambow Mhanuzi!!” salamu hii ilinishtua sana kiasi nikataka nikimbie. Nilimtazama binti aliyenisalimia nisielewe kwa namna gani amepata ujasiri wa kunifata mpaka huku nilipo, amejuaje nipo huku? Japo nilimfahamu lakini sikuwa na mazoea naye kwa wakati huo, ni yeye tu ambaye malazote hulazimisha kuwa karibu yangu.
Jina lake ni Salome binti mwenye asili ya pemba, mweupe anayemiliki umbile la kipekee linalovutia macho ya kila mwanaume lijari. Siyo mrefu sana, yupo saizi ya kati, unene wake ni ule wa afya siyo ule wa kuzidiwa na mafuta mwilini. Hapo mwanzo uzuri wake ulinivutia sana, nikashawishika kuweka ukaribu naye mala ya kwanza tu nilipomuona. Kufuatia ile shauku niliyokuwanayo juu ya wanawake, nilifanikiwa kujiweka karibu naye. Nikamfanya kuwa rafiki yangu wa kike chuoni naye akanikubali na kunifanya rafiki yake wa kiume. Ukaribu wetu ulikuwa na kuongezeka kila siku, ikafikia hatua watu akaanza kulihisi penzi zito lililochipuka baina yetu. Wakati yeye akitarajia nipige hatua zaidi ndio wakati nilianza kuchukizwa na ukaribu ule. Nikajikuta nikimpotezea pasipo hata kumtamkia chochote kuhusu mapenzi. Sikuwahi kumtongoza wala kumtamkia chochote kuhusu mapenzi. Ule ukaribu wetu wa ghafla ukatoweka, nikalejea kuishi maisha ya kivyanguvyangu. Salome hakuwahi kunipotezea kama nilivyofanya mimi, alijitahidi sana kujiweka karibu kwa kunishirikisha mambo yake ambayo sikuwa na mda nayo tena.
Alisogea mpaka karibu yangu, akakaa pembeni yangu kimya pasipo kuongea chochote. Ujio wa Salome ulikivuruga kabisa kichwa changu, sikuwa tayali kuongea naye kwa wakati ule. nikaamua kunyanyuka ili niondoke eneo lile. “Najua unauchukia uwepo wangu hapa, hunipendi. Lakini mimi sipo kama wewe ambaye hujali chochote kuhusu wengine; nimekuona haupo sawa nikaamua nije nikujulie hari. Una shida gani Mhanuzi!” Maneno yake yalinifanya kusimama, nikageuka na kumuangalia namna alivyonikodolea macho yake makubwa kidogo yaliyozungukwa kwa kope zilizokolezwa kwa weusi wa kuvutia. Maneno yake yalikuwa mwiba mkali wa ukweli uliozijeruhi vibaya hisia zangu. Ni kweli sikuwa kwenye hali nzuri ya kumjibu binti huyu, lakini ule muonekano wa uso wake ulikuwa ujumbe uliotosha kizifikisha hisia zake, alihitaji kusikia neno langu kwa wakati huo. Nilijua hii ndiyo mala yangu ya mwisho kuonana na mrembo huyu kabla ya kukamatwa kwa tuhuma za wizi, uporaji, ukabaji na ubakaji; ambazo sikujua hatima yake ingekuwaje. Nikatamani kuongea neno lakini midomo ikawa mizito kutamka. Nikaishia kumuangalia tu mrembo huyu, naye aliniangalia kwa macho yake ya aibu ambayo hayakustahimili kutazamana kule, yalipepesa kabla ya kuangalia chini. Kuna namna nilijihisi hatia mbele ya Salome, hatia ya kuziamsha hisia zake kisha nikamtelekeza pasipo sababu yoyote.
Zile kumbukumbu za namna alivyowahi kuniomba nimsamehe kama kuna kitu kibaya alikitenda kilichofanya nimchukie; ziliushinda moyo wangu, nikalainika na kuwa mwepesi kama kalatasi mbele ya mrimbwende huyu. “Mbona huna amani, una tatizo gani?” niliisikia kwa ukaribu mkubwa sauti yake, sauti ya upole wa kubembeleza iliyoambatana na pumzi zake zenye joto tamu la kusisimua. Hayakuwa maneno matupu tu; ambayo yangeshindwa kuvunja mfupa, aliongea huku akinishika mikono yangu kama vile hakutaka niendelee kula mwenyewe bali anilishe yeye. Hali hiyo ilinifanya kujihisi kama mtoto aliyeonewa, na sasa nilitakiwa kumtaja aliyenionea mbele ya mama aliyenibembeleza kwa upendo mkubwa sana. “Utajionea mwenyewe,” nilitamka maneno hayo kisha nikajinasua mikononi mwake na kutoweka eneo lile. Ilikuwa lazima nifanye hivyo kuepusha kile ambacho sikutaka kinitokee mbele ya mtoto wa kike. Baada ya kuhisi ujio wa machozi machoni mwangu ambao nilishindwa kuudhibiti nikaamua niondoke, sikuwa tayali kujishuhudia nikitoa machozi mbele ya Salome. Ili iweje? nidhalilike. Sikuwa tayari kunyamazishwa kama mtoto mdogo.
Sikuwa tayali kuonesha mabadiliko yangu mbele ya mtu yeyote, niliigiza kuwa sawa kila nilipokutana na watu walionijua. Kilichotokea nilikifanya kuwa siri yangu ya moyoni ambayo sikuruhusu mtu yeyote aijue, nilifiificha siri hiyo hata mbele ya marafiki zangu. Baada ya kuachana na Salome nilirudi chumbani, nijiandae kwa ajili ya mafunzo ya jioni. Nilipoingia ndani niliwakuta marafiki zangu wote wametulia tuli kila mmoja akifanya mambo yake kwa ukimya. Hali hiyo ilinishangaza kidogo, sikuwa na kumbukumbu za kushuhudia kitu kama hicho. Yaani chumba kikose kelele muda kama huu, muda wa mchana tena watu wakiwa wameshiba. Hapo nikajua lazima kuna kitu kisicho cha kawaida kiliendelea, sasa kingekuwa nini? Wazo baya likanijia kichwani, nikawaza labda wameshazipata taarifa za uhusika wangu katika matukio ya jana usiku. Ndiyo maana wametulia kimya, kusubili nitaongea nini. Hilo liliniuma sana, nikaamua nipande kitandani nijipumzishe pasipo hata kujisumbua kuwaongelesha. “Za ndaaaani kabisa” hii ilikuwa sauti ya Lajoka aliyeongea kwa namna ya kupayuka kisha vikafatia vicheko vya wote waliokuwamo ndani. Sikuwa mgeni wa aina hii ya utani na ucheshi, lakini nilijiuliza nini kipya kinataka kuzungumzwa maana ukishasikia mtu kasema za ndani kabisa ujue kuna jipya anataka kulizungumza. Nilitulia tu kwani nilishajua nini kingefatia, taarifa zangu ndizo zingefatia. Lakini kuna kitu kimoja sikukielewa, iweje marafiki zangu wafurahishwe na kitu kile,” mbona wanacheka kama mazuri?”
“Bingwa wa kuigiza leo umejaa kwenye mifumo. Nilikwambia tangu zamani; lazima itajulikana tu. Sasa leo tumejua mpaka picha zako tunazo. Vipi, bado una kitu cha kujitetea au nikulipue?” Almanusula nidondoke baada ya kusikia maneno hayo, nikajua sasa nimekwisha; kila kitu kimeshajulikana. Niliamua kulala nikajifunika gubigubi nisitake kusumbuliwa na yeyote maana baada ya hapo ningesemwa mimi tu.
ITAENDELEA.
(Kila kitu kimeshakamilika, Simulizi ipo tayali. Ili kujua nini kiliendelea, tembelea uzi huu jioni ya kila siku kuanzia leo.)