Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Bila shaka atapata anachokitafuta bwana knife kule sio mchezo analindwa mpaka matunge (mganga )kaogopa unapoenda kulipa kisasi chimba makaburi mawili moja linaweza kukufaa mwenyewe
 
Sehemu ya 85

Siku ya pili, niliondoka na treni kuelekea Kigoma. Baada ya safari ya siku mbili njiani, hatimaye asubuhi ya siku ya Ijumaa, tulifika Kigoma.

Nilipowasili nyumbani, mke wangu Pili alinilaki kwa furaha na mapenzi makubwa. Alinikumbatia akanipa pole kwa maswahibu makubwa yaliyonikuta Dar es salam. Mwanamke huyo hakujua kabisa kama kulikuwa na uongo mkubwa katika yale aliyokuwa akiyajua.

Hakufahamu kabisa kama nilikuwa nimetoka kwa mganga huko Unguja kumvuta mpenzi wangu wa zamani Lawalawa, sanjari na kumroga Felix Kisu. Mwanaume aliyenindoa kwenye mchezo wa soka na kupoteza ndoto zangu zote maishani.

Mke wangu Pili, aliniuliza tena kwa kile kilichokuwa kimetokea, nami nikarudia kumuhadithia kwa kumdanganya kwa kiasi kikubwa, kwamba nilivamiwa na kuibiwa kiasi chote cha fedha ya biashara.

“Walikuumiza sana baba?” mwanamke huyo aliuliza kwa sauti ya upole na mapenzi makubwa. “Sana mke wangu, waliniumiza.” “Pole sana mume wangu.” “Ahsante.”

Aliniandalia maji ya kuoga na chakula. Nilipokwenda bafuni, nilibeba dawa nilizopewa kwa mganga huko Unguja, nikazichanganya kwenye maji, nikaoga dawa hizo kwa siri bila mke wangu kutambua lolote.

Usiku nilipopata nafasi ya kuchoma dawa za kunuiza, nilifanya hivyo kwa siri kubwa. Hakuna nilichokuwa nafikiria katika nyakati zote kama kumpata Lawalawa wangu.

Sikujali ningeonekanaje, sikujali lawama ambazo zingenifuata nyuma baada ya kumwacha mke wangu Pili.

Kitu pekee nilichokuwa nataka ni mpenzi wangu Lawalawa kurudi kwangu. Nilikuwa mwendawazimu kwa mwanamke huyo.

Nakumbuka, nilikaa nyumbani kwa wiki nzima tangu tukio la kuwanga kule Unguja lifanyike. Ndani ya kipindi chote sikuwa na taarifa zozote juu ya Felix kisu, sikujua kama uchawi niliomtumia ulijibu ama laa!. Sikujua kwa sababu sikuwa natambua maisha ya jamaa huyo kwa wakati huo.

Mbali ya hilo la Felix Kisu, kadhalika, niakeendelea kubaini kwamba, pamoja na kumroga Lawalawa ili kumrudisha mikononi mwangu ni vipi mwanamke huyo angesumbuka sana kunitafuta.

Ni kweli nyakati hizo kila mtu alikuwa na simu ya mkononi ila Lawalawa hakuwa na namba yangu, wala mimi sikuwa na yake.
 
Sehemu ya 86

Katika kufiriki fikiri mambo hayo, nikaona nina kila sababu ya kwenda nyumbani kwao, mjini Tabora.

Labda mwanamke huyo amekwisha ingia nchini, na pengine anahangika kunitafuta. Sasa kwa nini nisiende nyumani kwao Tabora kuonana naye? **** Usiku wa siku hiyo, baada ya chakula cha usiku. Nilizungumza na mke wangu Pili.

Nilimweka kitako usiku huo ili anipe pesa, nilimwongopea nahitaji pesa ya biashara, lakini ukweli ni kwamba nilitaka pesa itakayonisaidia kwenye harakati zangu za kumtafuta mpenzi wangu wa zamani. Lawalawa.

“Mke wangu nataka nirudi kwenye biashara, lakini kama ujuavyo, sina pesa hata kidogo,” nilimwambia. “Kweli mume? Kwa hiyo, ulikuwa una wazo gani?” “Nilitaka unisaidia kitu kimoja.” “Kipi hicho mpenzi?” “Unikopee kiasi cha pesa, kule kwenye kikundi chako cha vikoba.” “Kama shilingi ngapi?” “Laki tatu tu.”

“Hilo siyo tatizo mume wangu, kikubwa ni kupambana tu kwenye biashara hiyo ili uweze kurejesha kiasi hicho cha pesa. Sawa baba ?” “Sawa mke wangu.” Nilishangalia moyoni. Niliamini nikipata kiasi kile cha fedha kingenitosha kabisa kumpata Lawalawa wangu.

Hakuchukua muda. Siku tatu baadaye mke wangu alichukua mkopo kwenye kikundi chao cha akina mama. Shilingi laki nne. Akanipatia pesa yote. Mrembo huyo akinisihi niwe makini na biashara ili niweze kurejesha pesa hiyo ya mkopo.

“Unanijua Pili. Tutarudisha pesa yote kama inavyotakiwa.” Nilimwondoa wasiwasi mke wangu. Moyoni nilibaki na ukweli. Haraka haraka niliandaa mipango ya safari ya mjini Tabora, kwao na Lawalawa. Na siku chache badaye nikaondoka na treni.

Niliondoka huku nyuma mke wangu Pili akijua naelekea Dar kwenye biashara yangu ya dagaa, ambayo nilikuwa nikifanya siku zote. Masikini ya Mungu, mwanamke huyo anipendaye, hakujua lolote lile nililokuwa nikilifanya.

Usiku wa saa saba, tuliingia mjini Tabora, kwa kuwa ilikuwa ni usiku mkubwa nilitafuta nyumba ya kulala wageni na kupumzika hadi asubuhi. Kulipokucha nikajiweka sawa kwenda nyumbani kwao Lawalawa.

Nilichukua tax hadi Ipuri, nikateremka hatua chache kutoka nyumbani kwa Lawalawa. Nikazipiga hatua kulifuata geti. “Ngo, ngo, ngo!” niligonga mlango. Ukimya ulikuwa umetawala.
 
Sehemu ya 87

“Ngo, ngo, ngo!” niligonga mlango. Ukimya ulikuwa umetawala. “Ngo, ngo, ngo!” niligonga tena.
Nikasikia mchakacho wa hatua za mtu akisogea getini. “Nani wewe!” sauti ya kike ilisikika.

Mungu wangu!. Ilikuwa ni sauti ya Lawalawa. Mapigo ya moyo yalienda kasi. “Dawa ya mganga imefanya kazi? Huyu Lawalawa kweli ametoka huko mashariki ya mbali alikokuwa ameolewa na karudi Tanzania, nguvu za dawa hizi kweli? Ama kaja kwa mambo yake mengine tu?” Nilijiuliza kimoyomoyo. “Nani wewe?” Lawalawa aliendelea kuuliza akiwa ndani. “Mimi!” hatimaye nikamjibu.

Mlango ukafunguliwa. Macho kwa macho na Lawalawa. Kwa pamoja tukabaki tukitizamana kwa sekunde kama nne ama tano, kisha chotara huyo akanirukia na kunikumbatia kwa furaha. “Ajibu!!...Ajibu jamani Ajibu!!” aliniita huku akiwa amenishika kwa nguvu. “Naam mpenzi.” “Ajibu mume wangu mpenzi, ulikuwa wapi miaka yote hiyo?” “Nilikuwepo Lawalawa”

Alitoka mwilini mwangu, akaniangalia usoni kwa hisia kali. Machozi ya furaha yakajikusanya machoni mwake. “Karibu ndani baba, pita ndani mpenzi wangu.”

“Ndani kwenu!!” niliongea kwa wasiwasi.
Nilitambua mwanamke huyo alikuwa akiishi na baba yake, sasa vipi anikaribishe mimi mpenzi wake ndani ya nyumba ya mzee wake. Adabu gani hiyo? “Ndio pita, usigope?” alisema. Akanishika mkono na kunipeleka ndani.

“Wewe Lawalawa humwogopi baba yako, si mke wa mtu wewe?” “Njoo...Pita usiogope.” Binti alizidi kunivutia. Tukaingia ndani sebuleni. Nilimkuta baba mmoja mzee sana, alikuwa hajiwezi kutokana na uzee, aliketi sofani huku akionekana kuchoka kwa kutafunwa na maradhi ya utu uzima.

Alikuwa ni mwarabu, ngozi ya mwili wake ilikuwa ikining’inia mwilini, nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufi, zilionesha kunyonyoka kwa kukosa afya. Macho yalimtumbukia ndani na midomo ilimtepeta.

Alikuwa na umri kati ya miaka 90 ama 95. Alikuwa ni kikongwe aliyebahatika kuwa hai. “Huyu ni baba yangu,” alinitambulisha, akaendelea. “Baba huyu anaitwa Ajibu, ndiye mwanaume niliyekuwa nakwambia habari zake,” alimwambia yule mzee, sikujua aliposema ‘Ndio mwanaume niliyekuwa nakwambia habari zake’ aliwahi kumweleza nini baba yake.

TUKUTANE KESHO.
 
Huyo ajibu ananiudhi kusema ukweli shunie mpe adhabu kabla hadithi haijafika mbali huyu mbwa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom