SEHEMU YA 25
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo mdomo wangu ulivyozidi kuwa mchungu mpaka kufikia hatua ya kuwaomba maji.
Baada ya sekunde ishirini nikaletewa maji yakiwa katika kikombe kilichokuwa kichafu, nilipoyaangalia maji yale, sidhani kama kulikuwa na watu ambao walikuwa wakinywa maji yale katika dunia hii.
Maji hayakuwa masafi hata kidogo, maji yalikuwa machafu mno. Nikabaki nikiyaangalia maji yale.
Mdomo ulikuwa mchungu na nilikuwa nikihitaji sana kunywa maji, ila maji ambayo nilikuwa nimeletewa mahali pale, yalikuwa ni maji machafu sana, sikujiuliza zaidi, nikayanywa maji yale huku nikifumba macho yangu.
Hayo ndio maisha ambayo walikuwa wakiishi watu wa hapo Zahor, walikuwa wakiishi maisha ya tabu sana.
Yale majani ambayo kwangu nilikuwa nikiyaona kuwa machugu, kwao yalionekana kuwa matamu kama pizza ama baga, maji yale ambayo nilikuwa nikiyaona kuwa machafu, kwao yalionekana kuwa masafi sana kama ya Mlima Kilimanjaro.
Hatukuendelea zaidi na safari, tulichokitaka ni kukaa mahali pale japo kwa siku moja zaidi. Vichwani mwetu hatukujua kile ambacho kingeweza kutokea mahali pale, kama tungelewa kile ambacho kingetutokea kesho yake asubuhi, nadhani tungeondoka kijijini hapo jioni hiyo hiyo.
*
*
*
Je, nini kitaendelea?