Simulizi: Niliyoyaona Darfur yanatisha

Simulizi: Niliyoyaona Darfur yanatisha

SEHEMU YA 37

“Atakuwa anajisumbua kwani ushahidi ninao kwamba ni yangu.”
“Ushahidi gani?”
“Majeed,” nilimjibu baba.

Kila siku macho yangu yalikuwa ni kuangalia BBC kwa kuamini kwamba ningeweza kuiona makala yangu lakini wala sikuiona.

Nilichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Penn kwa njia ya barua pepe lakini nae alikuwa kimya kabisa. Nikakata tamaa kwa kuona nilidhulumiwa ila baada ya mwezi mmoja mambo yakaanza kujipa.

Nilikuwa nimetumiwa barua pepe kutoka nchini Uingereza. Haikuwa kutoka kwa Penn bali ilikuwa imetoka kwa mkurugenzi wa kituo cha habari cha BBC ambaye alinitaka nielekee huko huku kila kitu kikiwa kimeandaliwa.

Nikawaambia wazazi wangu, nikamwambia mpenzi wangu, Myra na Hamza ambaye alinitengenezea kitambulisho. Kila mmoja akawa na furaha, baada ya wiki mbili nilikuwa ndani ya ndege ya British Airways nikielekea nchini Uingereza.

Ile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuelekea katika bara la Ulaya. Nilipofika huko, Penn pamoja na mwanaume mmoja walikuwa wamekuja kunipokea na hivyo kunipeleka hotelini.

Nilikaa huko huku usiku nikiwasiliana na wazazi wangu pamoja na Myra.

Baridi la nchini Uingereza lilikuwa kali sana ila nikavumilia na hatimae kesho kupelekwa katika jengo la BBC lililokuwa hapo London na kisha kuanza kufanyiwa mahojiano ya siri kidogo.

Kila mtu hakuamini kama nilikuwa nimeingia Darfur kama mwandishi wa habari na kutoka salama.

Siku ambayo MAKALA YANGU YA DARFUR ilipoanza kuonyeshwa, watu walikuwa wakilia, mambo ambayo yalikuwa yameonekana katika video ile yaliwatisha sana. Ndani ya wiki moja niliyokaa nchini Uingereza nikaonekana kuwa maarufu, watu wakaanza kunitafuta kwa ajili ya kufanya mahojiano binafsi pamoja nami.
 
SEHEMU YA 38

Mkurugenzi wa BBC, Bwana Patrick Pegg alihisi ningeweza kushawishiwa na kwenda kufanya kazi katika mashirika mengine na wakati wao wenyewe walikuwa wakinihitaji, wakanisainisha mkataba wa kufanya kazi hapo huku nikilipwa paundi elfu thelathini kwa wiki ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi milioni sitini na tano.

Mwaka huo ndio ulikuwa mwaka ambao nilipokea tuzo ya mwandishi bora duniani kutokana na makala hiyo niliyokuwa nimeiandaa kitu kilichoifanya nchi yangu ya Tanzania kutangazika sana.

Nililipwa kiasi kikubwa kwa sababu niliandaliwa kazi nyingi za kufanya nchi ya Iraq na Iran ambapo kulikuwa na mapigano yaliyokuwa yakiendelea.

Sikufa, nilifanya kazi zao zote na katika kipindi chote na mpaka sasa hivi imepita miaka nane na bado naendelea kufanya kazi mahali pale huku mke wangu, Myra akiwa amenizalia watoto watatu, Prince, Furaha na Magreth.

Mpaka nimefikia hatua ya kuandika kitabu hiki kifupi cha MAKALA YANGU YA DARFUR kuna watu wengi wamehuzunika na kulia, wameguswa na kile walichokiona, wanajeshi wa waasi walisababisha vidonda vingi mioyoni mwa watu wa Sudan na Afrika kwa ujumla.
Kuna wengine ambao walikamatwa na kuhukumiwa katika mahakama ya The Hague nchini Uholanzi lakini kuna wengine bado waliendelea kujificha mpaka leo hii.

Pamoja na yote, sikumsahau rafiki yangu, Majeed. Kwa kumuonyeshea kwamba tulikuwa pamoja, nikawa namlipia ada huku nikimtumia paundi elfu mbili mia tano mpaka pale alipomaliza masomo yake ila msaada wangu wa kifedha haukuisha kwani bila yeye, mambo yangekuwa magumu sana kwangu kukamilisha makala ile.

MWISHO.

Hii ni hadithi ya kutungwa japokuwa yale niliyoyaandika ndio yanayoendelea kutokea huko. Shukrani kwa walionifuatilia toka mwanzo mpaka mwisho. Niliiandika mwaka 2012, kipindi ambacho hata uandishi wangu ulikuwa bado mchanga.

Hayo ni maneno ya nyemo chilongani
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom