Simulizi: Niliyoyaona Darfur yanatisha

Simulizi: Niliyoyaona Darfur yanatisha

SEHEMU YA 20

Nilichokifanya huku nikijivisha ujasiri, nikamwambia Majeed achukue kamera na kuanza kazi mahali hapo. Nikaanza kuongea huku Majeed akinirekodi, kwa kuniangalia harakahara, sikuonekana kuongea nikiwa na amani, lakini ukweli nilikuwa na hofu sana.

Kitendo changu cha kuyainamia mafuvu yale nilikiona kuwa cha ujasiri sana. Mafuvu ambayo yalikuwepo mahali pale yalikuwa ni mafuvu ya tofauti tofauti.

Kulikuwa na mafuvu ya watoto wadogo na pia kulikuwa na mafuvu ya watu wakubwa. Eneo hilo lilionekana kutokuwa na amani katika kipindi cha nyuma, kuna watu ambao waliteketezwa kwa kupigwa risasi mahali hapo.

Mafuvu yalikuwa mengi mahali hapo, kwa idadi ya haraka haraka ya kuhesabu huku nikiwa na hofu, yalikuwa yakifikia hata mia tatu. Watu wengine ambao tulikuwa tukisafiri pamoja katika farasi wale walibaki wakiniangalia katika kipindi hicho ambacho nilikuwa nikitengeneza makala yangu.

Tulikaa mahali pale kwa takribani dakika arobaini na tano na ndipo tukaendelea na safari yetu. Moyoni nilikuwa na majonzi makubwa, hofu ilizidi kuongezeka na kujua huko tulipokuwa tukienda ilikuwa ni hatari.

Nikaanza kujiuliza maswali mengi kwamba kama pale mwanzo wa kuingia Al Junaynah kulikuwa na mafuvu mengi kiasi kile, vipi huko katikati ya mji huo ambao mapigano yalikuwa makubwa zaidi? Kila nilichokuwa nikijiuliza nilikosa jibu kabisa.
 
SEHEMU YA 21

Kamera yangu ya picha za kawaida ilikuwa imetumika kwa kupiga picha zaidi ya kumi huku zikiwa zimebakia picha sitini hata kabla ya mkanda kuisha.

Kwa wakati huo, kichwa changu kilikuwa na mawazo mengi sana, nilikuwa nikijifikiria juu ya mambo ambayo ningeweza kukutana nayo katikati ya mji wa Darfur.

Kumbukumbu za mafuvu yale ambayo ulikutana nayo ziliniogopesha kupita kawaida, amani ikaanza kupotea moyoni mwangu huku ujasiri ambao nilikuwa nao ukianza kuyeyuka.

Tuliendelea kwenda na wale farasi, sehemu ambayo tulikuwa tukipita ilikuwa jangwa moja kubwa, hakukuwa na nyumba nyingi sana.
Hapa labda ningependa kuzungumza kitu kimoja.

Kwa sababu asilimia tisini ya nchi ya Sudan ilikuwa ni jangwa basi lilikuwa ni jambo la kawaida sana kukutana na wakinamama njiani wakiwa wamebeba mitungi ya maji huku wakitembea kwa mwendo mrefu kutokana na maji kuwa ya shida sana katika nchi nyingi zilizokuwa na majangwa.

Tukafika sehemu moja ambayo kulikuwa na miti zaidi ya ishirini ikiwa imesimamishwa kwa kuchomekwa mchangani.

Nilibaki nimeduwaa huku nikiwa nimeikodolea macho miti ile.
Sikutaka kuendelea na safari, nilichokifanya ni kuwaambia watu ambao nilikuwa nao kwamba nilitaka kuona ni kitu gani ambacho kilitokea mahali pale mpaka miti ile kuchomekwa mchangani.

Kama kawaida yao, wote wakawa wabishi, hawakutaka kukubaliana nami kwamba twende kule na kuiona miti ile. Nilipoona wanakataa, nikawakumbusha kwamba mimi ni mwandishi wa habari niliyekuwa na wajibu wa kufahamu vitu vingi kuhusu.

Kuwa mwandishi wa habari katika nchi kama ya Sudan kulikuwa na uzuri wake, watu walikuwa wakikusikiliza sana, hii ilitokana ni kwa sababu waliamini kama wewe mwandishi ungekuwa unaelezea mambo mengi yaliyotokea katika nchi hiyo basi ingekuwa rahisi kwenda kwenye vyombo vya habari na kutangaza na hatimaye kupata msaada kutoka katika nchi za Magharibi.
 
SEHEMU YA 22

Nikaruka kutoka katika farasi na moja kwa moja kuanza kuelekea katika sehemu ile ambayo ilikuwa na miti ile huku nikiongozana na Majeed huku wale watu wengine wakiwa wanatusubiria.

Nilichokifanya ni kuchukua kamera yangu na kuanza kupiga picha huku tukizidi kuisogelea miti ile.

Hatua ishirini hata kabla hatujaifikia miti ile, macho yetu yakatua katika maganda mbalimbali ya risasi ambazo zilikuwa zimekwishatumika. Mwili wangu nilihisi kusisimka.

Maganda yale yalikuwa mengi pale chini. Sikuacha kitu chochote kile, nikaanza kupiga picha maganda yale ya risasi na kuanza kusogea kule kulipokuwa na miti ile.

Kama ilivyokuwa njiani na ndivyo ilivyokuwa pale, mafuvu ya watu yalikuwa yakionekana katika miti ile mchangani jambo ambalo lilizidi kuniongezea hofu zaidi. Sudan kwangu ikaonekana kuwa kama jehanamu, nilikuwa nikihofia kupita kawaida kiasi kwamba wakati mwingine nilikuwa nikitetemeka waziwazi.

“Haya ni mafuvu ya watu ambao walikuwa wamefungwa katika miti hii, pale tulipoyaona maganda ya risasi ndipo ambapo wapigaji risasi walipokuwa wamesimama na kuwalenga huku wakiwa wamewafunga katika miti hii,” Majeed aliniambia.

Sidhani kama kuna siku ambayo niliumia kama kipindi kile, nilimwangalia Majeed na bila kutegemea, machozi yakaanza kunitoka. Moyoni niliumia kupita kawaida kiasi, kichwa changu kikaanza kutengeneza picha ya watu waliokuwa wamefungwa katika miti ile na kumiminiwa risasi.

Kitu ambacho kilikuwa kimeniumiza zaidi ni kwamba katika mafuvu yale pia kulikuwa na mafuvu ya watoto, hali ilionyesha kwamba hata watoto nao walikuwa wamefungwa katika miti ile na kumiminiwa risasi.

Hiyo ndio hali niliyokutana nayo, sikutaka kuendelea kujiuliza, hapo hapo Majeed akaanza kunirekodi huku nikiielezea hali iliyokuwa imetokea mahali pale.
 
we jamaa unatupiga kamba lakini bas sababu ni story just go on
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom